Kisa Cha Swahaba Tha’labah Ni Cha Kweli?

 

SWALI:

 

AMANI IWE KWENU WAELIMISHAJI INSHAALLAH MOLA ATULIPE MAZURI DINIANI NA AKHERA. SWALI LANGU NI KWAMBA NIMESIKILIZA MAWAIDHA MENGI LAKINI SIJABAHATIKA KUJUA HATIMA YA BWANA SAALABA BAADA YA KUAMBIWA ATOE MALI NA AKAKATAA KAMA KUNA SEHEMU NAOMBA UNIFAMISHE NIWEZE KUFUNGUA NIJUE MWISHO WAKE NA KAMA HAKUNA JAPO KWA MAELEZO NIJULISHE KUPITIA E MAIL YANGU HAKIKA NIMEVUTIWA NA KUTAKA KUJUA MWISHO WAKE. WABLAH TAUFIK

 

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani zetu kwa swali lako kuhusu mtu aliyekuwa akiitwa Tha’labah.

Aayah inayozungumzia mtu aliyekataa kutoa Zakaah kwa ajili ya unafiki wake hata baada ya kumuahidi Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni ile ya Suratut Tawbah (9), ambayo kwayo Allaah Aliyetukuka Anatuambia: “Na miongoni mwao wapo walio muahidi Allaah kwa kusema: Akitupa katika fadhila yake hapana shaka tutatoa sadaka, na tutakuwa katika watendao mema. Alipowapa katika fadhila yake wakaifanyia ubakhili na wakageuka, na huku wakipuuza. Basi akawalipa unafiki kuutia nyoyoni mwao mpaka Siku watapo kutana Naye, kwa sababu ya kuwa walimkhalifu Allaah katika yale waliyo muahidi, na kwa sababu ya kusema kwao uwongo” (75 – 77).

 

Kuhusiana na aayah hizi mufassirina wametofautiana kuhusu jina la huyu mnafiki ambaye baadaye alitaka kutoa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Abu Bakr, ‘Umar na ‘Uthmaan (Radhiya Allaahu ‘anhum). Na huyo bwana akawa ni mwenye kuaga dunia wakati wa ‘Uthmaan (Radhiya Allaahu ‘anhu).

 

Mufasirina wengine wanasema kuwa huyo bwana alikuwa anaitwa Tha’labah bin Haatwib na Aayah hizi ziliteremshwa kwa ajili yake. Hata hivyo haiwezekani hilo kwa kuwa bwana huyo alikuwa ni Swahaba aliyehudhuria vita vya Badr na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwashuhudilia waliohudhuria Badr kuwa ni wenye Iymaan na waliosamehewa madhambi yao. Ikiwa ni hivyo vipi Tha’labah atakataa kutoa Zakaah.

 

Wengine wanasema kuwa wapo Tha’labah wawili mmoja ni huyo tuliyemtaja juu na wa pili ni yule aliyekuwa mnafiki na ndiye aliyekusudiwa hapa.

 

Ama adhw-Dhwahhaak amesema: Aayah hizi ziliteremshwa kwa wanafiki nao ni Nabtal bin al-Haarith, al-Jadd bin Qays na Mu’attib bin Qushayr.

 

Kwa muhtasari kisa hicho hakiwezi kuwa kimetokea kwa Tha’labah bin Haatwib (Radhiya Allaahu ‘anhu) lakini kilitokea kwa asiyekuwa yeye kwa mnafiki au wanafiki kama walivyoyatajwa majina yao hapo juu.

 

Maelezo mazuri na marefu zaidi ya uchambuzi wa suala hilo, utalisoma hapa kwenye kiungo kifuatacho:

 

 

Kisa Kinachonasibishwa Na Swahaba Tha'alabah Bin Haatwib Kuhusu Kukataa Kutoa Zakaah

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share