Mwaliko Wa Futari Na Mtu Anayedanganya Ili Kupata Pesa Za Matumizi

 

SWALI:

 

ASSALAMU ALAYKUM WARAHMATULLAH WABARAKATUH MIMI LEO NIMEONA NIBORA NIULIZIE KUHUSU SUALA ZIMA LA UHALALI WA IFTAR ZETU TUKIZINGATIA NISIKU CHACHE ZIMEBAKI KUFIKIA MWEZI WETU MTUKUFU WA RAMADHANI. JE INAFAA KWA MUISLAM ANAEISHI NA MUME WAKE WA NDOA AMBAE ANAFANYA KAZI YAMSHAHARA AU YA KIBIASHARA LAKINI WANADANDANYA KWAMBA HAWAKO PAMOJA ILIWAPATIWE FEDHA ZA MATUMIZI, MTU WA NAMNA HII AKIKUITA KWAKE KWENDA KUFTAR INAFAA? NA HALI TUMETAKIWA TUITIKIE MWITO NA KAMA KAWIDA KATIKA MWEZI HUO WA RAMADHANI HUWA TUNAPENDA KUALIKANA SANA. NAOMBA MAELEKEZO JUU YA HILI KWANI KAMA UNAVYOONA MWEZI NDIO HUO HAPO UMEKARIBIA.


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukran kwa swali lako kuhusu kualikwa futari na mtu mwenye kudanganya ili apate fedha kutoka kwa serikali ya matumizi.

Hata hivyo, tunakuomba radhi kwa kuchelewa kujibu swali lako hadi Ramadhaan imekwisha kwani zamu ya swali lako ndio limefika na kulikuwa na maswali mengi sana yaliyotangulia.

 

Hakika udanganyifu si sifa kabisa ya Muislamu. Muislamu hafai kudanganya kwa sababu yoyote ile ima yawe ni maslahi kwake au mengineyo. Haswa katika mwezi wa Ramadhaan udanganyifu unakuwa ni dhambi kubwa zaidi kuliko miezi mingine kwa sababu ya utukufu wa mwezi huo.

 

Mwanzo, mtu mwenye kufanya hivyo anafaa apatiwe nasaha ili ajiondoe na dhambi hilo. Inatakiwa mtu wa aina hiyo awe ni mwenye kutubia, kujuta, kuweka azma ya kutorudia tena na kufanya mema kwa wingi.

 

Katika ule wakati ambao unachukua kumpatia nasaha vilevele kama una uhakika kuwa ana kipato kingine cha halali unaweza kwenda kwake huku ukiwa na dhana nzuri kuwa chakula hicho cha futari kimetokana na pato lake la halali.

 

Ikiwa katika hali ya kumnasihi, Muislamu huyo akawa anashindana na anaendelea kufanya kosa hilohilo tena kwa inadi au akawa anakuitikia kwa unayomnasihi lakini hapo hapo ukawa unaona hafanyi jitihada zozote za kuacha uongo wake na kuchuma chumo la haramu, basi inatakiwa umkate na kumsusia kuonyesha uchukivu wa kitendo chake kibaya. Na ni vizuri kama jambo hilo litafanywa na watu wengi kwa pamoja ili mtu huyo ajue amesuswa na kutengwa na hivyo kutanabahi na kujirudi. Kwani wengi wetu hawamuogopi Allaah bali huogopa watu.

 

Ama suala la mtu kudanganya serikali kuwa haishi na mkewe na kuwa wametendana au kuwa huyo si mkewe, hilo ni jambo baya na ovu na kishari’ah pia uongo kama huo na mtu kumkana mkewe kuwa si mkewe ni katika mambo yanayowatendanisha kishari’ah. Hayo ni mambo ya dhulma na udhaliishaji mkubwa wa Uislamu kwa Waislamu walioko Ulaya ambao huyafanya hayo kwa tamaa ya kipato na maisha rahisi. Ni aibu kubwa pia na fedheha kwa Waislamu pindi mke huyo anapokuwa na mimba au kuzaa na huku anajulikana hana mume! Kadhalika ni mambo yenye kuwafukuza mbali wasio Waislamu na Uislamu.

 

Tafadhali bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi:

 

Nasaha Kwa Wakimbizi Wanaoishi Kusema Hawajaoana Ili Wapate Ruzuku Ya Serikali

 

Pesa Anazopata Kwa Kuongopa Serikalini Zinafaa Kutumika Kwa Matumizi yake na kufanyia Mambo Ya Kheri?

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share