Wakati Mgumu Katika Historia Ya Kiislamu (Jinsi Ya Kuisoma Historia)

 

Wakati Mgumu Katika Historia Ya Kiislamu (Jinsi Ya Kuisoma Historia)

 

Imefasiriwa Na:

 

 Muhammad Faraj (Rahimahu-Allaah)

 

Alhidaaya.com

 

 

Namna Ya Kuisoma Historia

 

Tunapoisoma historia ya kiislamu, lazima tuisome kama vile tunavyosoma vitabu vya hadithi za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kwa sababu tunaposoma hadithi za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) huwa tunatafuta ukweli iwapo hadithi hizo ni sahihi au si sahihi.

 

Na hatuwezi kutambua ikiwa hadiyth ni sahihi au si sahihi bila ya kuwajuwa wapokezi wa hadithi hiyo (narrators) pamoja na matni (maneno) yake, na hii ni kwa sababu katika elimu ya hadithi maulamaa wamechukuwa juhudi kubwa ya kuchunguza habari za wapokezi wake na wakaweza kuwajuwa yupi muongo na yupi mkweli miongoni mwao, yupi mwenye kusahau na yupi anayependa kuongeza maneno yake (kutia chumvi), kisha wakazichunguza hadithi na kuzidurusu na hatimaye wakaweza kupambanua baina ya hadiyth sahihi na dhaifu pamoja na zile za uongo zilizopachikwa tu. Na kwa ajili hiyo wakaweza kuzisafisha hadithi za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kwa kuzibainisha zile za uongo zilizochomekwa na zile zilizo dhaifu.

 

Lakini tunaposoma vitabu vya historia (Taariykh), si rahisi mtu kuweza kutambua yote hayo, na hii ni kwa sababu utakuta ndani yake maelezo mengi yaliyoandikwa bila kutajwa majina ya wapokezi (narrators), tofauti na ilivyo katika vitabu vya elimu ya hadiyth. Na mara nyingi maelezo hayo yanaambatanishwa na majina ya wapokezi yasiyokuwemo na yasiyojulikana katika vitabu vya elimu ya wapokezi wa hadithi. Kwa ajili hiyo si rahisi kujuwa iwapo wapokezi hao walikuwepo kweli, na kama walikuwepo kweli si rahisi pia kujuwa juu ya mwenendo wao kama walikuwa wakweli waaminifu au waongo wenye kupenda kuandika kila wanachosikia nk. Na kwa ajili hiyo ni vigumu sana mtu kuweza kutoa uamuzi juu ya maelezo hayo iwapo ya kweli au ya uongo.

 

Kwa hivyo katika kuisoma historia mambo ni magumu zaidi kuliko ilivyo katika kusoma vitabu vya elimu ya hadithi, lakini hii isitufanye kuyarahisisha mambo, bali ni wajibu wetu kuutafuta ukweli na kujuwa wapi tuitafute historia yetu. Mtu anaweza kusema:

 

"Ikiwa tutavichambua vitabu vya historia na kuzitoa hadiyth zisizo sahihi, basi maelezo mengi juu ya historia yetu yatapotea na kubaki machache tu".

 

Lakini sisi tunamjibu kwa kumwambia kuwa; la, hayatopotea maelezo mengi, kwani yapo mengi katika maelezo ya historia yaliyoandikwa kwa isnadi zake, na hayo yamo katika vitabu vya historia mfano wa kitabu cha Atw-Twabariy na pia yamo ndani ya vitabu vya hadithi kama vile  Al-Bukhaariy na Musnad ya Imam Ahmad na Sunan At-Tirmidhiy au vitabu vilivyoandikwa na Ibni Abi Shaybah au katika vitabu vya tafsiri vinavyoandikwa ndani yake isnadi za kila riwaya kama vile tafsiri ya Ibni Jariyr na tafsiri ya Ibni Kathiyr na mara nyingine katika vitabu vinavyoandikwa juu ya matukio maalum kama vile vita vilivyotokea baada ya kufa kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) n.k.

 

Na kama utashindwa kuupata ukweli, basi uamuzi utabaki pale pale kuwa imani yetu ni kuwa haitupasi kuwatuhumu Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum) kwani Allaah Subhanahu wa Ta’aalaa amewasifia na kuwatakasa. Kwa ajili hiyo tukikutana na maelezo yoyote yale yanayowatuhumu Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum) kwanza kabisa tunatizama isnadi ya wapokezi wa maelezo hayo (narrators), na kama isnadi ni sahihi, basi kabla ya kuwatuhumu tutizame kwanza tafsiri ya riwaya hizo na zinaleta maana gani? Ama ikiwa isnadi yake ni dhaifu, basi AlhamduliAllaah, na kama riwaya hiyo haina isnadi yoyote, basi tunarudi katika asili yetu nayo ni imani yetu kuwa Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum) ni watu waadilifu kama tutakavyoona kila tukiendelea mbele namna gani Allaah amewatakasa watu hawa.

Kwa hivyo tunapoisoma historia hatuna budi kuisoma kwa kuichambua vizuri kama tunavyofanya wakati tunaposoma vitabu vya elimu ya hadiyth na hasa katika historia ya Swahaba wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

Tusome Vitabu Vilivyoandikwa Na Nani?

 

Wengi siku hizi wanapendelea kusoma vitabu vya historia  vilivyotungwa katika zama hizi zetu, vitabu ambavyo waandishi wake wanajishughulisha na upambaji wa maelezo au kusimulia habari zinazopotosha ukweli au yote mawili mfano wa vitabu vya ‘Abbaas Al Aqaad aliyeandika juu ya Ustadi ‘Abqariyaat’, au vitabu vilivyoandikwa na Khaalid Muhammad Khaalid ‘Khulafaa rasuul’ na ‘Rijaal haula rasuul’ au vya Taaha Husein ‘Mawqifat al Jamal’ au vya Georgie Zeidan ‘Taariykh tamadunil Islam’ au vingine vya mfano huo. Watungaji hawa wanapoandika juu ya historia hujishughulisha na uandishi na upambaji wa visa vilivyomo ndani yake bila kujali kama visa hivyo ni sahih au si sahihi, muhimu kwao ni kukuandikia kisa kizuri kinachovutia. Kwa hivyo suali linarudi pale pale. ‘Nisome vitabu vilivyoandikwa na mwandishi gani?’

 

Ikiwa unao uwezo wa kuwachambua wapokezi (narrators) na na kuwajuwa wakweli na waongo miongoni mwao, basi soma kitabu cha Imam Atw-Twabariy, kwani yeye ni bingwa miongoni mwa waandishi wa Taariykh (historia), ama ikiwa huna uwezo wa kuwachambua wapokezi, basi soma kitabu cha Al Bidaya wal Nihaya kilichoandikwa na Ibn Kathir au kitabu cha Taariykh al Islam kilichoandikwa na Imam Al Dhahabi au kitabu kilichoandikwa na Abu Bakr bin al Arabi kiitwacho ‘Al Awasim minal Qawasim’, na hiki ni miongoni mwa vitabu vizuri sana vilivyoandika juu ya wakati huu mgumu.

 

 

Tujitahadharishe Na Nini?

 

Tunaposoma vitabu vya historia lazima tujitahadharishe tusije tukachukuliwa na rai ya mtungaji, kwani inatupasa tuwe waadilifu huku tukisoma, na hatuna budi kuziangalia riwaya zenyewe na si kuangalia rai ya muandishi, na hatuna budi pia kuwa na mambo mawii akili mwetu huku tukisoma vitabu vinavozungumza juu ya historia ya Swahaba wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhis-sallam).

 

La kwanza: ni kuwa na itikadi kuwa Swahaba wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni viumbe bora kupita wote baada ya Rusuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhim-sallam) na hii ni kwa sababu Allaah Subhanahu wa Ta’aalaa amewasifia na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) pia amewasifia na akatuabainishia katika hadithi nyingi kuwa kuwa umma ule ulikuwa ni umma bora kupita zote baada ya Manabii (Swalla Allaahu ‘alayhim -salam).

 

Jambo La Pili: inatupasa tuelewe kuwa Swahaba wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hawakukingwa na kufanya makosa (si Maasumin), ndiyo sisi tunaitakidi kuwa hawawezi kufanya makosa katika jambo lolote walokubaliana nalo wote kwa pamoja (Ijamai), na hii ni kwa sababu Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikwishatuambia kuwa umma huu hauwezi kukubaliana wote kwa pamoja katika jambo la upotofu (upotevu), lakini unapowachukulia kama watu binafsi, wao hawakukingwa na kufanya makosa, kwani walokingwa ni Manabii wa Allaah peke yao, ama wengine wasiokuwa wao sisi hatuamini kuwa yupo yeyote aliyekingwa na kufanya makosa (asiyefanya makosa).

 

Kwa hivyo hatuna budi kuamini kuwa Swahaba ni umma bora kupita umma zote na hatuna budi kuamini kuwa wao wanaweza kufanya makosa.

 

Kwa hivyo itakapokujia riwaya (maelezo) ambayo ndani yake mna lawama juu ya Swahaba basi usikimbilie kuikataa na pia usiikubali moja kwa moja mpaka kwanza uitizame vizuri. Utakapoona kuwa isnadi ya riwaya hiyo ni sahihi basi ujuwe kuwa hii ni katika yale mambo ambayo hawakukingwa nayo, ama ikiwa isnadi ya riwaya hiyo ni dhaifu, basi unarudi katika itikadi yetu ya asili nayo ni kuwa Swahaba ni watu wema.

 

Ama sifa ambazo Allaah Amewasifia Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum) ni katika aya ifuatayo;

 

مُّحَمَّدٌ رَّسُولُ اللَّـهِ ۚ وَالَّذِينَ مَعَهُ أَشِدَّاءُ عَلَى الْكُفَّارِ رُحَمَاءُ بَيْنَهُمْ ۖ تَرَاهُمْ رُكَّعًا سُجَّدًا يَبْتَغُونَ فَضْلًا مِّنَ اللَّـهِ وَرِضْوَانًا ۖ سِيمَاهُمْ فِي وُجُوهِهِم مِّنْ أَثَرِ السُّجُودِ ۚ ذَٰلِكَ مَثَلُهُمْ فِي التَّوْرَاةِ ۚ وَمَثَلُهُمْ فِي الْإِنجِيلِ كَزَرْعٍ أَخْرَجَ شَطْأَهُ فَآزَرَهُ فَاسْتَغْلَظَ فَاسْتَوَىٰ عَلَىٰ سُوقِهِ يُعْجِبُ الزُّرَّاعَ لِيَغِيظَ بِهِمُ الْكُفَّارَ ۗ وَعَدَ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ مِنْهُم مَّغْفِرَةً وَأَجْرًا عَظِيمًا﴿٢٩﴾

Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) ni Rasuli wa Allaah. Na wale walio pamoja naye ni wakali zaidi dhidi ya makafiri; wanahurumiana baina yao. Utawaona wakirukuu na wakisujudu wakitafuta fadhila na radhi kutoka kwa Allaah. Alama zao dhahiri zi katika nyuso zao kutokana na athari za sujudu. Huo ni mfano wao katika Tawraat, na mfano wao katika Injiyl kama mmea umetoa chipukizi lake, likautia nguvu kisha likawa nene, kisha likasimama sawasawa juu ya shina lake, liwapendezeshe wakulima, ili liwatie ghaidhi makafiri. Allaah Amewaahidi wale walioamini na wakatenda mema miongoni mwao maghfirah na ujira adhimu. [Al-Fat-h: 29]

 

Katika aayah hii Allaah Amewasifia Swahaba wa Nabiy wote kwa pamoja. Kwa hivyo asili ya itikadi yetu ni kuwasifia, na imepokelewa hadithi sahihi ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) isemayo;

 

"Msiwatukane Swahaba wangu, lau kama mmoja wenu atatoa dhahabu ukubwa wake mfano wa jabali la Uhud, basi haitofikia gao lao wala hata nusu yake." [ Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Hizi pia ni sifa ambazo Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amewasifia Swahaba wake (Radhwiya Allaahu ‘anhum), na tutaelezea kwa ufafanuzi zaidi tutakapoufikia mlango nilioutenga katika kitabu hiki niloupa jina la ‘Uadilifu wa Swahaba’.

 

Kitabu muhimu kupita vyota katika elimu ya tarekh ni kile kilichoandikwa na Imam Atw-Twabariy na wengi wananukuu kutoka katika kitabu hicho. Ahlu Sunnah wananukuu kutoka katika kitabu cha ‘Taariykh Atw-Twabariy’, na Ahlul Bida’a (wanofuata madhehebu a ki Shia) pia wananukuu kutoka katika kitabu cha Taariykh Atw-Twabariy. Ahlu Sunnah wanatoa hoja zao katika kitabu cha Taariykh Atw-Twabariy na Ahlul Bida’a wanatoa hoja zao kutoka katika kitabu cha Taariykh Atw-Twabariy.

 

 

Kwa Nini Kitabu Cha Taariykh Atw-Twabariy Kinapendekezwa Kuliko Vingine?

 

Kwa sababu nyingi zikiwemo zifuatazo:

 

1.     Kitabu cha Atw-Twabariy kimeandikwa wakati ulio karibu zaidi na matukio yenyewe.

 

2.     Imam Atw-Twabariy anahadithia pamoja na isnadi (majina ya wapokezi wa hadithi hizo).

 

3.    Utukufu wa Imam Atw-Twabariy pamoja na haiba na heshima yake kutokana na daraja yake ya elimu.

 

4.      Vitabu vingi vya historia vinanukuu kutoka kwake.

 

Kwa ajili hiyo na sisi tunapotaka kuisoma historia inatubidi tukiendee kitabu hicho cha Atw-Twabariy moja kwa moja. Lakini kama nilivyosema ni kuwa Ahlus Sunnah wananukuu kutoka kitabu hicho kiitwacho ‘Taariykh Atw-Twabariy’, na Ahlul Bida-a nao pia wananukuu kutoka katika kitabu hicho cha Taariykh Atw-Twabariy. Sasa vipi tutaweza kusawazisha baina ya hii na ile?

 

Tulikwishaelezea hapo mwanzo kuwa uzuri wa kitabu hiki cha Taariykh Atw-Twabariy ni kwamba hakiandiki juu ya hadithi isipokuwa lazima kitataja majina ya wapokezi wa hadithi hiyo (isnadi). Ahlus Sunnah wao wanachukuwa hadiyth zilizo na isnadi sahihi katika kitabu hicho lakini Ahlul Bida-a wao wanachukuwa zilizo sahihi na zisizo sahihi, muhimu zikubalieni na matamanio ya nafsi zao.

 

 

Taratibu Alizotumia Imam Atw-Twabariy Katika Kuandika Kitabu Chake Cha Taariykh

 

Imam Atw-Twabariy Allaah amrehemu ametupumzisha sana katika jambo hili kutokana na utangulizi wa kitabu chake hicho, yareti wale wanaokisoma kitabu hiki cha Taariykh wangesoma utangulizi huo.

 

Anasema Imam Atw-Twabariy katika utangulizi wake:

 

"Ajue msomaji wa kitabu chetu hiki kuwa yote niliyoyaelezea humu yanatokana na maelezo niliyoyapokea kutoka kwa wasimulizi wa habari na nimejiwekea masharti ya kuandika isnadi (mlolongo wa majina ya wapokezi) ya yote yale walionihadithia. Iwapo ndani ya kitabu changu hiki zimo habari zozote nilizozisimulia juu ya waliotangulia zisizompendeza msomaji au zitakazomuudhi msikilizaji, na habari hizo zikawa siyo sahihi, basi atambuwe msomaji au msikilizaji huyo kuwa habari hizo hazikutokana na sisi, isipokuwa sisi tumezifikisha vile vile kama tulivyofikishiwa".

 

Nadhani Imam Atw-Twabariy kwa utangulizi wake huu amekutupia mzigo wewe msomaji, kama kwamba anakwambia;

 

"Ukikuta ndani ya kitabu changu hiki habari zisizokufurahisha au zisizokubalika, basi tizama kutoka kwa nani tumezipokea habari hizo. Na kama nilivyoahidi kuwa nitaandika majina ya wale walionipa habari hizo, kwa hivyo ukiona kuwa wale niliopokea kutoka kwao habari hizo ni watu wa kuaminika, basi zikubali, la kama si wa kuaminika basi usizikubali".

 

Utaratibu huu ndio uliofuatwa na wengi kati ya waandishi wa vitabu vya elimu ya hadithi. Iwapo mtu atarudia na kusoma vitabu vya hadithi, ukivitowa vitabu vya Al-Bukhaariy na Muslim, kwa sababu waandishi wa vitabu hivyo viwili wameahidi kuandika hadiyth zilizo sahihi tu ndani yake. Lakini vitabu vingine kama vile Attirmidhy au Abu Daud au Addaraqutniy au Addarimiy au Musnad ya Imam Ahmad au kitabu chochote kingine katika vitabu vya elimu ya hadiyth, utaona kuwa waandishi wake wanakutajia mlolongo wa majina ya wapokezi wa hadithi hizo (isnadi) kwa sababu wao hawakutoa ahadi ya kuandika hadiyth zilizo sahihi peke yake, na kwa ajili hiyo wakawa wanakuandikia isnadi na unachotakiwa wewe ni kuziangalia isnadi hizo. Ikiwa wapokezi ni watu wanoaminika utazikubali, ama ikiwa si watu wa kuaminika, basi usizikubali.

 

Kutokana na utangulizi wake, Atw-Twabariy hakutoa ahadi ya kuandika yale yaliyo sahihi peke yake, isipokuwa ametoa ahadi ya kuandika majina ya wale ambao kutoka kwao amepokea maelezo hayo. Ikiwa mambo yenyewe ni kama hivyo, basi Imam Atw-Twabariy hakutoa ahadi (ya kuandika hadithi zile sahihi tu). Na katika kitabu chake, Attabari amenukuu habari nyingi kutoka kwa mtu mmoja aitwae Luut bin Yahya, maarufu kwa jina la ‘Abu Makhnaf’.

 

Imam Atw-Twabariy amenukuu kutoka kwa Luut bin Yahya huyu, riwaya mia tano na themanini na saba. Na riwaya hizi zinaelezea kuanzia wakati alipofariki Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumalizikia wakati wa ukhalifa wa Yazid bin Muawiya, na huu ndio wakati nitakaozungumza juu yake katika kitabu chetu hiki, zikiwemo habari za Saqiyfat Bani Saaidah, kisha cha Shuura, sababu zilizowafanya Khawarij wachukuwe msimamo dhidi ya ‘Uthmaan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) na hatimae kuuliwa kwake, ukhalifa wa ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu), vita vya ‘Al Jamal’, vita vya ‘Siffin’, kuhukumu, (Tahkiym), vita vya Naharawan, ukhalifa wa Mu’aawiyay (Radhwiya Allaahu ‘anhu), kuuliwa kwa Al-Husayn (Radhwiya Allaahu ‘anhum). Katika yote haya utazikuta riwaya zilizosimuliwa na Abi Makhnaf, riwaya ambazo Ahlul Bida-a ndiyo wanaozitegemea sana na kuzishikilia.

 

Na si Abu Makhnaf peke yake mwenye riwaya za uongo, isipokuwa tu, Abu Makhnaf ni mashuhuri kupita wenzake, lakini wapo wengine waongo kama yeye kama vile Al Waaqidiy ambaye katika elimu ya hadithi anajulikana kuwa ni muongo ambaye hadiyth zake hazikubaliwi, juu ya kuwa yeye ni mjuzi wa riwaya nyingi na mtaalamu wa historia, isipokuwa si mtu mwaminifu wa kufikisha habari.

 

Wa tatu ni Seif bin ‘Umar At Tamimi ambaye pia ni mtaalamu wa historia maarufu, isipokuwa naye pia si muaminifu wa kufikisha habari na anajulikana kuwa ni mtu muongo na hadiyth zake hazikubaliwi. Yupo mwingine pia aitwae Al Kiliy ambaye ni muongo mashuhuri, na kwa ajili hiyo mtu inampasa achunge asije akazikubali riwaya zilizosimuliwa na watu wa aina hii.

 

Turudi kwa Abu Makhnaf na tutazame ‘ulamaa wamesea nini juu yake. Ibni Maiyn ambaye ni mwanachuoni maarufu wa elimu ya wapokezi wa hadithi amesema;

'Abu Makhnaf si mwenye kuaminika'.

Na Abu Hatim amesema;

'Abu Makhnaf hazikubaliwi riwaya zake'.

Na Imam Ad Daraqutny amesema;

'Abu Makhnaf ni dhaifu'.

Imam Adhahabi amesema;

'Mwingi wa habari na mtungaji wa maneno asiyeaminika'.

 

Na wewe unapokifungua kitabu cha Taariykh ya Atw-Twabariy na ukakumbana na riwaya inayowalaumu Swahaba wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kisha ukaona kuwa Atw-Twabariy amezinukuu habari hizi kutoka kwa Abu Makhnaf, basi ni juu yako kuziweka upande habari hizo. Kwa nini? Kwa sababu ni riwaya iliyosimuliwa na Abi Makhnaf. Na Abu Makhnaf huyu amekusanya riwaya nyingi zenye mambo ya Bida-a ndani yake na za uongo.

  

Njia Zinazotumiwa Na Waletao Habari Katika Kuipaka Matope Historia

 

1).     Uzushi na maneno ya uongo.

Wanatunga kisa fulani, mfano wa kisa walichokitunga juu ya Bibi ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anha) kwamba eti alisujudu kwa ajili ya kumshukuru Allaah aliposikia habari za kifo cha ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu). Bila shaka hiki ni kisa cha uongo.

 

2).  Kuongeza maneno au kupunguza kwa nia ya kuleta sura mbaya.

Huenda kisa cheyewe kikawa ni sahihi, kwa mfano kisa cha tukio la Saqiyfat bani Sa’ad. Kisa hiki kilitokea kweli mara baada ya kufariki kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) walipokutana Abu Bakr na ‘Umar na Abu ‘Ubaydah upande mmoja, na upande wa pili alikuwa Al Khabab bin Mundhir na Sa’ad bin ‘Ubaadah na wengineo katika watu wa Madiynah (Radhwiya Allaahu ‘anhum). Waandishi hao wakaongeza maneno yao kama nitakayokuja kuelezea kila tukiendelea mbele. Wameongeza kwa nia ya kuharibu sifa za Swahaba wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

3).     Kufasiri visivyo sahihi hadithi za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Nako ni kuyafasiri maneno ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama wanavyotaka wao ili yakubaliane na matamanio yao na itikadi zao.

 

4).     Kudhihirisha lugha mbaya au makosa.

Kisa kinakuwa cha kweli, lakini wao wanakielezea huku wakitilia mkazo pale

Sahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alipofanya makosa kwa nia ya kuyabainisha makosa hayo huku wakiyaficha mema yao bila kuyabainisha.

 

5).     Kutunga mashairi kwa ajili ya kuyapa nguvu matukio ya kihistoria.

Wanatunga mashairi kisha wanayanasibisha na ‘Aamiri wa Waislamu ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhwiya Allaahu ‘anhu) au wanayanasibisha na Mama wa Waislamu Bibi ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa), au wanayanasibisha na Az-Zubayr bin Awaam au Talha (Radhwiya ‘anhumaa) kwa ajili ya kumtuhumu mmojawapo katika ya Swahaba, kama walivyotunga shairi la kumkashifu Bibi ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) kisha wakalinasibisha na Ibni ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu).

 

6).     Kutunga barua za uongo

Kama tutakavyoona In shaa Allaah katika kisa cha kuuliwa kwa ‘Uthmaan (Radhwiya Allaahu ‘anhu), jinsi barua za uongo zilivyoandikwa, kisha akasingiziwa ‘Uthmaan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa yeye ndiye aliyeziandika, na namna gani zilivyoandikwa barua za uongo na kunasibishwa na Bibi ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) na nyingine zikaandikwa na kusingiziwa ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa ndiye aliyeziandika na Talha na Az-Zubayr (Radhwiya Allaahu ‘anhu), haya ukiacha kuhesabu barua na vitabu kama kitabu kiitwacho Nahjul Balagha kilichoandikwa na kunasibishwa na ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhwiya Allaahu ‘anhu) pamoja na kitabu kiitwacho Al Imamah walichokinasibisha na Imam Ibni Qutaybah.

 

 

Juhudi Za Mashia Katika Kuingiza Uongo Na Kuipa Sura Mbaya Historia Ya Kiislamu

 

Walio mashuhuri kupita wote katika historia kwa uzushi na kwa uongo ni Mashia, na hii ndiyo maana maulamaa wanawapigia mifano kwa kusema:

 

'Muongo kuliko Rafidhiy (Shia)”, na hii inatokana na wingi wa kusema uongo kwao'.

Anasema Al A-amash;

'Niliwahi kuishi na watu waliokuwa wakijulikana kwa jina la ‘waongo’.

Anasema Shurayh Al-Qaadhiy:

'Naipokea elimu kutoka kwa yeyote nitakayeonana naye isipokuwa Mashia, kwa sababu wao wanatunga hadithi za uongo kisha wanaigeuza hadithi hiyo kuwa dini yao'.

Anasema Imam Shafi:

'Sijapata kuona wenye kusema uongo kuliko Mashia'.

 

Kusudi langu ni kuwa ingawaje makundi mengine pia yanasema uongo lakini hawa ni mashuhuri sana kuliko wengine katika kueneza habari zisizo za kweli na kutunga hadithi za uongo.

 

 

Taratibu Za Kuhakikisha Ukweli Wa Hadithi Kwa Ahlus Sunnah – Wakati Gani Zilianza?

 

Zilianza baada ya kutokea vita vya wenyewe kwa wenyewe (fitan).

Muhammad bin Siriyn (Rahimahu-Allaah) ambaye ni miongoni mwa ‘ulamaa wakubwa wa Taabi iyn amesema:

 

'Watu hawakuwa wakiuliza juu ya isnadi za hadithi walizokuwa wakizisikia, mpaka pale ilipotokea ‘fitna’ (vita vya wenyewe kwa wenyewe), wakaanza kusema; ‘Tutajieni majina ya wale mlopokea hadithi hizi kutoka kwao’, Ikawa watu wanaangalia majina ya wapokezi wa hadithi zinazosimuliwa na watu wa Ahlus Sunnah na kuzikubali riwaya zao, na wanapoangalia majina ya wapokezi wa Ahul Bida-a, wanazikataa riwaya zao'.

[Haya yamo katika utangulizi wa kitabu cha Sahih Muslim].

Na hii ni kwa sababu watu wanapokea riwaya kutoka kwa wanoaminika, na Ibni Siyrin ni mmojawapo wa wakubwa wa maulamaa wa At-Tabiiyn aliyewahi kuishi na baadhi ya Swahaba na akaishi pamoja na maulamaa wakubwa wa Taabiiyn na wadogo wao, na kwa sababu fitna zilizotokea ndiyo maana kukatokea makundi ya Shia na Khawarij na Qadiriyah.

 

 

Kuja Kwa Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam)

 

Siku ya Jumatatu tarehe 12 mwezi wa Rabiul Awwal (ipo khitilafu juu ya siku aliyozaliwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)), Allaah aliwatunukia walimwengu wote zawadi kubwa sana kwa kuzaliwa kwa bwana wa viumbe vyote na kiongozi wao Muhammad bin ‘Abdullaah bin ‘Abdul Mutwalib Al-Haashimy kutoka katika kabila la ki Quraysh. Alizaliwa akiwa yatima hana baba na alipotimia miaka sita mama yake akafariki na akachukuliwa na babu yake ‘Abdul Mutwalib, na miaka miwili baadaye babu yake akafariki na akachukuliwa na ammi yake Abu Twaalib.

 

Alipotimia miaka arubaini Allaah alimpa utume ili awe mwenye kuleta bishara njema na mwenye kuonya, akausimamia ujumbe wake kama unavyostahiki kusimamiwa na akafikishi yale Allaah alomuamrisha ayafikishe kwa ajili ya kuwatowa watu katika giza na kuwaingiza katika nuru. Wakubwa wa kabila lake wakamfanyia uadui na wakawatendea wafuasi wake kila aina ya udhia, wakamfuata makundi ya watu walioiuza dunia yao kwa ajili ya aakhirah, wakapigana jihadi katika njia ya Allaah kwa mali zao na kwa nafsi zao, wakainusuru (dini ya) Allaah na Nabiy wake.

 

Allaah Anasema:

 

لِلْفُقَرَاءِ الْمُهَاجِرِينَ الَّذِينَ أُخْرِجُوا مِن دِيَارِهِمْ وَأَمْوَالِهِمْ يَبْتَغُونَ فَضْلًا مِّنَ اللَّـهِ وَرِضْوَانًا وَيَنصُرُونَ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ ۚ أُولَـٰئِكَ هُمُ الصَّادِقُونَ﴿٨﴾

Wapatiwe (pia) mafuqara Muhaajiriyn ambao wametolewa kutoka majumbani mwao na mali zao wanatafuta fadhila na radhi kutoka kwa Allaah na wananusuru (Dini ya) Allaah na Rasuli Wake hao ndio wakweli. [Al-Hashr:  8]

 

Akaendelea Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kuwalingania watu muda wa miaka kumi na tatu mpaka Allaah alipomuamrisha kuhamia Madiynah, mji ambao Allaah ameutia nuru kwa kumjaalia Nabiy wake kuhamia huko. Wakahamia huko pia Swahaba wake (Radhwiya Allaahu ‘anhum) na kuacha mali zao na watoto wao nyuma yao, yote hayo kwa ajili ya kutaka radhi za Allaah.

 

Alipowasili Madiynah akapokewa vizuri na watu wa mji huo, waliomnusuru na kumsaidia. Wakawasaidia wale waliohama pamoja naye, wakagawana nao mali zao na nyumba zao na hata wake zao, kwani watu wa Madiynah wenye wake wawili au zaidi walikuwa wakiwaambia watu wa Makkah:

 

'Chagua mmoja kati ya wake zangu yule unayemtaka ili nimtaliki kisha nikuozeshe wewe'.

 

Allaah Anasema:

 

وَالَّذِينَ تَبَوَّءُوا الدَّارَ وَالْإِيمَانَ مِن قَبْلِهِمْ يُحِبُّونَ مَنْ هَاجَرَ إِلَيْهِمْ وَلَا يَجِدُونَ فِي صُدُورِهِمْ حَاجَةً مِّمَّا أُوتُوا وَيُؤْثِرُونَ عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ وَلَوْ كَانَ بِهِمْ خَصَاصَةٌ ۚ وَمَن يُوقَ شُحَّ نَفْسِهِ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ﴿٩﴾

Na wale waliofanya maskani yao hapa (yaani Madiynah) na wakautakasa Uislamu (wao barabara) kabla ya kuja hao (Muhajir huko Madiynah) na wakawapenda hao waliohamia kwao, wala hawapati (hawaoni) dhiki nyoyoni mwao kwa hayo waliyopewa (hao Muhajiri), na wanawapendelea kuliko nafsi zao ingawa wenyewe wana hali ndogo. Na waepushwao na ubakhili wa nafsi zao hao ndio wenye kufaulu kweli kweli. [Al-Hashr: 9]

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akaendelea na da’awah yake nje ya mji wa Madiynah na hatimaye bara ya Arabu yote mpaka ilipofika siku ile tukufu ambayo Allaah Alimfungulia Nabiy wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mji mtukufu wa Makkah (alipouteka mji wa Makkah) na watu wake wakaingia katika dini ya Kiislamu na baada ya hapo bara ya Arabu yote ikawa chini ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Baada ya kuwalingania watu pamoja na kupigana jihadi muda upatao miaka ishirini na mitatu, ikamfikia qudra ya lazima kwa kila mtu inayosadikishwa na kauli ya Allaah isemayo:

 

وَمَا مُحَمَّدٌ إِلَّا رَسُولٌ قَدْ خَلَتْ مِن قَبْلِهِ الرُّسُلُ ۚ أَفَإِن مَّاتَ أَوْ قُتِلَ انقَلَبْتُمْ عَلَىٰ أَعْقَابِكُمْ ۚ وَمَن يَنقَلِبْ عَلَىٰ عَقِبَيْهِ فَلَن يَضُرَّ اللَّـهَ شَيْئًا ۗ وَسَيَجْزِي اللَّـهُ الشَّاكِرِينَ ﴿١٤٤﴾

Na Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) si yeyote isipokuwa ni Rasuli tu. Wamekwishapita kabla yake Rusuli. Je, akifa au akiuawa mtageuka nyuma ya visigino vyenu (mrudi ukafirini)? Na atakayegeuka nyuma ya visigino vyake, basi hatomdhuru Allaah kitu chochote. Na Allaah Atawalipa wenye kushukuru. [Aali ‘Imraan: 144]

 

Dunia ilikuwa kama kwamba imeingia giza totoro kutokana na tukio hili. Na kwa nini isiwe hivyo wakati Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:

 

"Atakayekutwa kati yenu na msiba, basi akumbuke msiba wake kwangu (wa kifo changu), kwani huo ndio msiba mkubwa zaidi". [Atw-Twabaqaat al-Kubraa na imesahihishwa na Shaykh Al-Albaaniy].

 

Haukupata kutokea msiba mkubwa wakati wowote ule tokea iumbwe dunia kuliko msiba wa kifo cha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam). Na huyu Bibi Faatwimah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) binti wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) wakati baba yake alipokuwa akijiwa na sakrati l mauti alikuwa akisema:

 

"Baba yangu! ameitikia mwito wa Rabb wake, baba yangu! Jannah (Pepo) ya Firdausi makazi yake, baba yangu! kwa Jibril tunafikisha pole yake". Anas bin Maalik (Radhwiya Allaahu ‘anhu) naye alisema:

 

"Siku ile Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipoingia mji wa Madiynah, kila kitu kilikuwa kikitowa mwangaza, ama siku ile aliyofariki kila kitu kiliingia giza, na tulipokuwa tukipangusa mikono yetu michanga baada ya kumzika tulihisi nyoyo zetu zimenyongeka (kwa sababu wahyi umeshakatika na hautoshuka tena baada yake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)".

 

Ibni Majah katika ‘Kitaabul Janaaiz – mlango wa ‘Wafaatun Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Baada ya kifo cha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), Abu Bakr alimwambia ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhum);

'Twende tukamtembelee Ummu Ayman'.

Walipowasili kwake, Ummu Ayman alilia sana, wakamuuliza;

'Kwa nini unalia hivyo wakati atakayopata Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kwa Rabb wake ni bora zaidi?'

Akajibu;

'WaAllaahi ninalia si kwa sababu sielewi kuwa yaliyoko kwa Allaah ni bora zaidi kwa Nabiy wake, isipokuwa kinachoniliza ni kukatika kwa wahyi kutoka mbinguni'.

Maneno hayo yaliwaliza sana Abu Bakr na ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhuma) [Muslim]

 

Na hivi ndivyo nafsi hii njema ilivyohamia kwa Rabb wake.

 

 

Ukhalifa Wa Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu ‘Anhu)

 

Mara baada ya kutangazwa kufariki kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Abu Bakr alikwenda moja kwa moja mpaka mahali alipolazwa, akaufunua uso wake na kumbusu juu ya kipaji cha uso wake baina ya macho yake, kisha akasema:

 

'(Nakufidia) Kwa baba yangu na mama yangu, unapendeza ukiwa hai au umekufa'.

Kisha akaufunika uso wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), akanyanyuka na kupanda juu ya membari na kusema:

 

'Kama yupo aliyekuwa akimuabudu Muhammad, basi Muhammad kesha kufa, ama kama mlikuwa mkimuabudu Allaah, basi Allaah yuhai na hafi'. (kisha akaisoma kauli ya Allaah ifuatayo):

 

وَمَا مُحَمَّدٌ إِلَّا رَسُولٌ قَدْ خَلَتْ مِن قَبْلِهِ الرُّسُلُ ۚ أَفَإِن مَّاتَ أَوْ قُتِلَ انقَلَبْتُمْ عَلَىٰ أَعْقَابِكُمْ ۚ وَمَن يَنقَلِبْ عَلَىٰ عَقِبَيْهِ فَلَن يَضُرَّ اللَّـهَ شَيْئًا ۗ وَسَيَجْزِي اللَّـهُ الشَّاكِرِينَ ﴿١٤٤﴾

Na Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) si yeyote isipokuwa ni Rasuli tu. Wamekwishapita kabla yake Rusuli. Je, akifa au akiuawa mtageuka nyuma ya visigino vyenu (mrudi ukafirini)? Na atakayegeuka nyuma ya visigino vyake, basi hatomdhuru Allaah kitu chochote. Na Allaah Atawalipa wenye kushukuru. [Aali-‘Imraan: 144]

 

Watu wakawa wanalia na wengine wakawa wanatembea mitaani huku wakiikariri aya hiyo. Anasema Anas (Radhwiya Allaahu ‘anhu):

 

"Ilikuwa kama kwamba hatujapata kuisikia aya hiyo isipokuwa wakati ule (kama kwamba tunaisikia kwa mara ya mwanzo)".

[Al-Bukhaariy] – kitabu cha Fadhila za Swahaba.

Juu ya kuwa Qur-aan ilikwisha kamilika kabla ya kufa kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kabla ya kufariki kwake, lakini aya hii ilikuwa kama ni mpya kwao, kama kwamba hawakupata kuisikia kabla ya siku hiyo kutokana na mshituko waloupata kwa kifo cha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).

 

Al-’Abbaas bin Abdul Mutwalib na ‘Aliy bin Abi Twaalib na Az-Zubayr bin Al-‘Awaam (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) ndio waliofanya kazi ya kumuosha na kumkafini Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na kumshughulikia mpaka aliposaliwa, na hii ni kwa sababu Al-’Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ni ‘Ami yake Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ni mtoto wa ammi yake Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Az-Zubayr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ni mtoto wa shangazi lake Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na kwa ajili hiyo wao ndio waliostahiki zaidi kujishughulisha na hayo.

 

 

Saqiyfat Bani Saa’idah

 

Wakati Al-’Abbaas na Ali na Az-Zubayr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) walipokuwa wakijishughulisha na kumtayarisha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), baadhi ya watu wa Madiynah walikutana mahali panapoitwa Saqiyfat Bani Saa’idah, na nitakielezea kisa hiki kwanza kama kilivyoelezwa katika kitabu cha Taariykh cha Imam Atw-Twabariy namna kilivyoelezwa na Abi Makhnaf ‘muongo’, kisha nitakielezea kama kilivyoelezwa na Imam  Al-Bukhaariy, kisha pima wewe mwenyewe baina ya riwaya mbili hizi ili uweze kuujuwa uongo ulio ongezwa na Abu Makhnaf. Huenda mengi katika uongo huo uliozidishwa ukawa katika wakati wetu huu ni jambo lililokwisha kubalika miongoni mwa watu, na haya tutakuja kuyaona pale tutakapozungumza juu ya tukio la Shuura.

 

Anasema Imam Atw-Twabariy (Allaah Amrehemu):

 

Ametuhadithia Hisham bin Muhammad kutoka kwa Abi Makhnaf, (kuwa) amesema: Nimehadithiwa na ‘Abdullaahi bin ‘Abdur-Rahmaan bin Abi Amru bin Abi Amrah Al Ansari kuwa Nabiy alipofariki, watu wa Madiynah walikusanyika (mahali panapoitwa) Saqiyfat bani Saa’idah wakasema;

“Baada ya Muhammad tumchaguwe Sa’ad bin Ubada awe kiongozi wetu”.

Mmoja wao akainuka na kusema:

“Kwa panga zenu waarabu wote wamekufuateni, na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amefariki akiwa ameridhika nanyi na akiwa amefurahika nanyi (kwa hivyo) musiiache fursa hii wakaja kuichukuwa watu wengine”.

Wote wakajibu;

“Rai yako ni sawa”.

Mmojawao akasema;

“Wakikataa wahajiri wa KiQuraysh tutawaambia ‘Aamiri mmoja atoke kwao na ‘Aamiri mmoja atoke kwetu”.

Akasema Sa’ad bin ‘Ubaadah;

“Huu ni udhaifu wa mwanzo”.

 

Kisha zikamfikia habari ‘Umar bin Al-Khatwaab kuwa baadhi ya watu wa Madiynah wamekusanyika Saqiyfat bani Saa’idah wakisema: ‘Amri mmoja kutoka kwetu na ‘Aamiri mmoja kutoka kwenu’. Alipewa habari hizo na mmojawapo katika watu wa Madiynah. Akenda moja kwa moja mpaka kwa Abu Bakr na kumueleza juu ya jambo hilo, akamwambia:

 

“Ndugu zetu katika watu wa Madiynah ‘Al Ansar’, wamekusanyika na wanasema hivi na vile, tuwaendee huko haraka sana”.

‘Umar na Abu Bakr walipokuwa wakiondoka wakakutana na Abu ‘‘Ubaydahh wakamwambia:

“Twende pamoja”.

Wakaondoka watatu hao na kuelekea mahali walipojikusanya watu wa Madiynah. Anasema ‘Umar:

“Nilikuwa nimekweshajitayarishia maneno ya kusema, na nilipokuwa nikijitayarisha kusema, Abu Bakr akaniashiria kuwa ninyamaze na akaanza Abu Bakr kusema;

“AlhamduliAllaah”, kisha akampwekesha Allaah, kisha akasema;

“Hakika Allaah amemleta Muhammad…..”

Kisha akaitaja khutba ndefu iliyotolewa na Abu Bakr na kwamba alisema ndani ya khutba hiyo kuwa watu wa Makkah ‘Muhajirin’ ndio wanaostahiki kuwa Makhalifa.

Akasema Al Habaab bin Mundhir;

“Enyi watu wa Madiynah! Mumiliki wenyewe amri yenu, kwani watu wako chini ya kivuli chenu na hawezi yeyote kujaribu kwenda kinyume nanyi na watu hawatofuata isipokuwa rai yenu, nyinyi ndio wenye nguvu na wenye mali na wenye idadi kubwa ya watu na wenye ulinzi, na kama wakikataa kukufuateni basi watoweni nje ya mji (wenu) huu. Waongozeni nyinyi katika mambo haya, kwani nyinyi waAllaahi ndiwo wenye haki kuliko wao, kwa sababu kwa panga zenu wameingina katika dini hii walioingia wale wasiokuwa na dini. Mimi ndiye mwenye kuistahikia zaidi na mwenye uwezo mkubwa zaidi wa kulibeba jukumu hili kuliko wengine”.

‘Umar na Abu ‘‘Ubaydahh wakamwambia Abu Bakr:

“Tandaza mkono wako tufungamane nawe”, walipokuwa wanataka kufungamana naye, akawatangulia Bashir bin Sa’ad (mtu wa Madiynah) na akawa yeye mtu wa mwanzo kufungamana naye, na hivi ndivyo watu walivyofungamana na Abu Bakr.

Anasema (Abu Makhnaf):

“Akainuka Usayd bin Hudhair aliyekuwa miongoni mwa viongozi wa kabila la Aus waliokuja kufungamana na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam)  katika ‘Fungamanao la Aqaba la pili’ kabla ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kuhamia Madiynah, akasema:

“WaAllaahi ikiwa uongozi juu yenu watauchukuwa watu wa kabila la Khazraj mara moja tu, basi haitoondoka tena fadhila yao hiyo juu yenu”.

(Abu Makhnaf anamaanisha hapa kuwa Usayd alimuonea husda Sa’ad bin ‘Ubaadah anayetokana na kabila la Khazraj kwa kuteuliwa na watu wa Madiynah kuwa kiongozi wa Waislamu”.

(Aus na Khazraj ni makabila mawili makubwa ya watu wa Madiynah)

Sa’ad akasema:

“WaAllaahi kama ningelikuwa na nguvu za kujinyanyua, basi ungelisikia kutoka kwangu mngurumo utakaokujeruhi wewe na sahibu zako, kisha waAllaahi ningelikufukuzia kwa kaumu ambayo wewe ulikuwa ukiwafuata tu na wala hawakufuati, niondoweni mahali hapa”.

Wakamnyanyua na kumuingiza nyumbani kwake, akaachwa kwa muda wa siku nyingi kisha akasema:

“Ama waAllaahi mpaka nikuvurumishieni mishale niliyoibeba ndani ya mfuko wake, na niipake rangi (damu) meno yake (mishale hiyo), kisha nikupigeni kwa upanga wangu kisha nikupigeni vita mimi na watu wa nyumba yangu pamoja na watakaonitii katika watu wa kabila langu”.

Anasema (Abu Makhnaf):

“Sa’ad akawa hasali sala yao wala hasali Ijumaa pamoja nao, anahiji lakini hafuatani nao, akaendelea katika hali hiyo mpaka alipofariki Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu)”.

 

Hii ni riwaya kama ilivyoelezewa na Abu Makhnaf juu ya tukio la Saqiyfat Bani Saa’idah, na sasa someni riwaya iliyosimuliwa na Imam Al-Bukhaariy juu ya kisa hiki, kisha linganisheni.

Anasema Imam Al-Bukhaariy:

“Nimehadithiwa na Ismail bin ‘Abdullaah, nimehadithiwa na Suleiman bin Bilal kutoka kwa Hisham bin Uruwah amesema: Amenambia Uruwah bin Az-Zubayr kuwa ‘Aaishah mke wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema;

“Hakika alipofariki Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) watu wa Madiynah walijumuika kwa Sa’ad bin Ubada mahali panapoitwa Saqiyfat bani Saa’idah, wakasema;

“‘Aamiri mmoja atoke kwetu na ‘Aamiri mmoja atoke kwenu”.

Abu Bakr na ‘Umar na Abu ‘‘Ubaydahh wakawaendea, na ‘Umar alipotaka kuhutubia akanyamazishwa na Abu Bakr, na ‘Umar alikuwa akisema;

“WaAllaahi kwa kufanya vile sikuwa na nia nyingine isipokuwa nilitaka kusema maneno yaliyonipendeza niliyokwishayatarisha na nikaogopa Abu Bakr asije akashindwa kuifikisha fikra hiyo, lakini Abu Bakr akaweza kuifikisha vizuri kupita mtu yeyote, na akasema katika maneno yake;

“Ma ‘Aamiri watoke kwetu na Ma Waziri watoke kwenu”.

Akasema Khubab bin Mundhir:

“WaAllaahi hatukubali. Kwetu atoke ‘Aamiri na kwenu atoke ‘Aamiri”.

Abu Bakr akasema;

“Sivyo hivyo, sisi ni Ma Amri na nyinyi ni Ma Waziri, wao (MaQuraysh) ndio waarabu wa kati kwa kati kupita wote na watukufu kupita wote, Fungamaneni na ‘Umar au Abu ‘Ubaydahh”.

‘Umar akasema;

“Bali tutafungamana na wewe, kwani wewe ndiye bwana wetu na mbora wetu na unayependwa zaidi na Rasuli wa Allaah kuliko sisi. Kisha ‘Umar akauchukuwa mkono wake na akafungamana naye, na watu wote wakafungamana naye”.

[Sahihul Al-Bukhaariy] katika mlango wa Fadhail al Swahaba

 

 

Hii ni riwaya ya Imam Al-Bukhaariy, kama unavyoiona kuwa ni fupi na ndogo na huu ndio uhakika wa mambo yalivyokuwa katika Saqiyfat bani Saa’idah. Ama yale aliyozidisha Abu Makhnaf kama mlivyosikia kwamba eti Sa’ad bin ‘Ubaadah alisema;

“Nitapigana vita na nyinyi…” na kwamba eti hakuwa akihiji wala kuswali pamoja nao wala hakuwa akisali Ijumaa pamoja nao wala hakuwa akifuatana nao, na kwamba Al Khabaab bin Mundhir alimjibu Abu Bakr, pamoja na nyongeza nyingine (yoote hayo ni uongo mtupu), kwani tukio la Saqifa halikuchukuwa zaidia ya nusu saa, na tazameni namna gani walivyokifanya kisa hicho kuwa kikubwa kuliko kinavyostahiki.

Ama kuhusu Sa’ad bin ‘Ubaadah, imepokelewa hadithi katika Musnad ya Imam Ahmad kutoka kwa Humaid bin Abdur Rahman kuwa amesema;

“Alizungumza Abu Bakr na wala hajaacha sifa zozote katika zile walizoteremshiwa watu wa Madiynah ndani ya Qur-aan au zile alozitaja Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) asizitaje (Amezitaja sifa zote za watu wa Madiynah). Akasema;

“Mnakumbuka kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema; “Na lau kama watu wote watafuata njia zao katika mabonde na mitaa, na watu wa Madiynah watafuata njia nyingine, basi mimi ningefuata njia watakayopita watu Madiynah”.

Kisha baada ya hayo Abu Bakr akamwambia Sa’ad bin ‘Ubaadah;

“Na wewe unakumbuka ewe Sa’ad kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) (siku moja) ulipokuwa umekaa alikwambia: “Maquraysh ndio watakao ongoza amri hii, na watu wema wanawafuata wema wao na waovu wanawafuata waovu wao”.

Baada ya kusikia maneno hayo Sa’ad akasema;

“Umesema kweli! Sisi ni Ma Waziri na nyinyi Ma ‘Aamiri”.

Riwaya hii imesimuliwa na Ahmad katika Musnad yake kwa isnadi sahihi iliyonyanyuliwa (mursal) na Humaid bin ‘Abdur-Rahmaan bin ‘Awf (Radhwiya Allaahu ‘anhu), na ingawaje riwaya hii imenyanyuliwa, lakini ina nguvu zaidi kuliko riwaya za muongo yule – Abu Makhnaf.

 

 

Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu ‘Anhu)

 

Jina lake ni ‘Abdullaah bin ‘Uthmaan bin ‘Aamir bin Amru bin Ka’ab bin Sa’ad bin Tiym bin Murrah bin Kaab bin Luayyi bin Ghalib bin Fihr, na Fihri huyu ndiye Quraysh.

Amesema ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhwiya Allaahu ‘anhu);

“Allaah ameteremsha jina la Abu Bakr (la) Asw-Swiddiyq kutoka mbinguni”.

Atw-Twabaraaniy hadithi nambari 1/55 na ameitaja hadithi hii pia Al-Haafidh Ibn Hajar katika Al-Fatah 7/11.

 

 

Kusilimu Kwake

 

Kutoka kwa Abu Dardaa (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema;

“Nilikuwa nimekaa kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akatokea Abu Bakr akiwa ameshika (na kuinyanyua) ncha ya nguo yake hata goti lake likawa linaonekana, akasema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam):

“Ama sahibu yenu (anaonesha) kesha kasirishwa”.

Abu Bakr akatoa salamu kisha akasema;

“Ilikuwa baina yangu na ‘Umar jambo, nilimfanyia haraka, kisha nikajuta, nikamuomba anisamehe akakataa, nikakujia wewe”.

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema;

“Allaah akughufirie ee Abu Bakr (akasema hivyo mara tatu)”.

Kisha ‘Umar naye akajuta, akenda mpaka nyumbani kwa Abu Bakr na kuuliza;

“Abu Bakr yupo?”

Wakasema;

“Hayupo”.

Akenda kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na uso wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ukawa umebadilika rangi kwa ghadhabu, mpaka Abu Bakr akamuonea huruma ‘Umar, akapiga magoti mbele ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kusema;

“Ee Rasuli wa Allaah, waAllaahi mimi ndiye niliyemkosea (mara mbili)”.

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema;

“Allaah alinituma kwenu (na nyote) mkanambia muongo, (isipokuwa) Abu Bakr alisema; ‘nakusadiki’, akaniliwaza kwa kwa hali na mali, sasa nyinyi mtamuacha sahibu yangu (akasema hiyvo mara mbili)”.

Tokea siku hiyo Abu Bakr hakukasirishwa tena na mtu.

Al-Bukhaariy mlango wa Fadhila za Swahaba

Na kutoka kwa ‘Amaar bin Yaasir (Radhwiya Allaahu ‘anhuma) amesema;

“Nilimuona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akiwa hakufuatana na zaidi ya watu watano na wanawake wawili na Abu Bakr”. [Al-Bukhaariy]

 

 

Kuhajiri Kwake

 

Kutoka kwa Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema;

“Nilikuwa na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) pangoni, nikanyanyua kichwa changu, nikajikuta nipo karibu na miguu ya watu (makafiri). Nikasema; “Ee Rasuli wa Allaah mmoja wao akitupa jicho lake chini atatuona”.

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema;

“Nyamaza ewe Abu Bakr, (sisi) wawili na AAllaah wa tatu wao”.

Al-Bukhaariy kitabu cha sifa za watu wa Madiynah, mlango wa Hijra ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na Swahaba zake. Hadithi nambari 3922.

Muslim kitabu cha wa sifa za Maswahaba hadithi nambari 1.

 

 

Fadhila Zake

 

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema;

“Nilimsikia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akisema;

Atakayetoa viwili vya aina moja katika njia ya Allaah (mfano ngamia wawili au mbuzi wawili au dirham mbili n.k.), ataitwa kwenye milango ya Jannah (Peponi) huku akiambiwa; “Ee mja wa Allaah, hii ni kheri (yaani njoo uingie Peponi kupitia mlango huu). Aliyekuwa katika watu wenye kuswali (kwa wingi) ataitwa kupitia mlango wa Swaalah, na aliyekuwa katika watu wa Jihadi ataitwa kupitia mlango wa Jihadi, na aliyekuwa mtoaji wa Sadaka (mwingi wa kutoa Sadaka) ataitwa kupitia mlango wa Sadaka na aliyekuwa katika watu wa Swawm (mwingi wa kufunga) ataitwa kupitia mlango wa Swawm au mlango wa Ar-Rayaan”.

Abu Bakr akasema;

“(Nimefahamu kuwa) Si lazima mtu aitiwe kupitia milango yote hiyo (muhimu aingie Peponi tu).

Kisha Abu Bakr akauliza;

“Yupo atakayeitwa kupitia milango yote hiyo ee Rasuli wa Allaah?”

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema;

“Naam – yupo na nataraji utakuwa miongoni mwao ewe Abu Bakr”.

 Al-Bukhaariy kitabu cha ‘Fadhila za Swahaba’, hadithi nambari 3666

 

Kutoka kwa Anas bin Malik (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema;

“Aliupanda Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Abu Bakr na ‘Uthmaan (mlima Uhud), ukatikisika mlima, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema;

“Tulia (ee) Uhud, kwa sababu juu yako yupo Mtume na Asw-Swiddiyq na mashahidi wawili (watakaokufa shahid)”.

 Al-Bukhaariy kitabu cha ‘Fadhila za Swahaba’ hadithi nambari 3675

 

Kutoka kwa ‘Amru bin Al-‘Aasw (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema;

“Nilimuuliza Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): mtu gani unayempenda zaidi kupita wote?”

Akanambia;

“‘Aaishah”.

Nikamuuliza tena:

“Yupi katika mwanamume (unayempenda zaidi)?”

Akanambia:

“Baba yake”.

Nikamuuliza:

“Kisha nani?”

Akanambia:

“‘Umar bin Al-Khatwaab”.

 Al-Bukhaariy katika kitabu cha Fadhila za Swahaba hadithi nambari 3662

Muslim mlango wa Fadhila za Swahaba hadiyth nambari 8

Kisha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

 

"Katika watu walonisaidia sana kwa hali na mali ni Abu Bakr, ingelikuwa naweza kumchagua Khalil (rafiki), basi angekuwa Abu Bakr, lakini ni ndugu katika Uislamu na kupendana. Milango yote iliyoelekea msikitini ifungwe isipokuwa mlango wa Abu Bakr".

Al-Bukhaariy kitabu cha Fadhila za Swahaba hadithi nambari 3654

 

 

Kuwa Kwake Pamoja Na Nabiy (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam)

 

Kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Amru (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alipoulizwa juu ya jambo gani ovu kupita yote alowahi kutendewa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na washirikina, akasema.

“Nilimuona ‘Uqbah bin Abi Mu’it akimuendea Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) wakati akiwa anasali, akamzungushia nguo yake shingoni pake na kumkaba nayo rohoni pake kwa nguvu sana, akatokea Abu Bakr na kumsukumilia mbali na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kisha akasema:

“Oh! Mtamuua mtu kwa sababu anasema Rabb wangu ni Allaah? Na kwa yakini yeye amekujieni kwa dalili waziwazi zitokazo kwa Rabb wenu”

Al-Bukhaariy kitabu cha Fadhila za Swahaba hadithi nambari 3678

 

 

Dalili Za Kupewa Ukhalifa Kutoka Kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)

 

Kutoka kwa ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anha) amesema;

“Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alipokuwa akiumwa alinambia;

“Muamrishe Abu Bakr asalishe watu”.

 Al-Bukhaariy katika kitabu cha ‘Adhani’ mlango wa ‘Ahlul ilm wal fadhal ahaqu bil Imamah’, hadithi nambari 678

 

Kutoka kwa Jaafar bin Mut’im amesema:

“Alikuja mwanamke mmoja kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akamuarisha arudi siku nyingine, akauliza:

“Nisipokukuta (nifanyeje)?” (kama kwamba anamuuliza ‘ukifa nimuendee nani?”

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akamwambia:

“Usiponikuta mwendee Abu Bakr”.

 Al-Bukhaariy kitabu cha Fadhila za Swahaba hadithi nambari 3659

Muslim kitabu cha Fadhila za Swahaba hadithi nambari 10

 

Kutoka kwa ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) amesema:

“Alinambia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alipokuwa akiumwa: “Niitie Abu Bakr na ndugu yako ili nimwandikie maneno kwani mimi naogopa asije akatamani mwenye kutamani kisha akasema: “Mimi ndiye ninayestahiki zaidi na Allaah hamkubali mwengine na Waislamu hawamkubali mwengine isipokuwa Abu Bakr”.

Muslim kitabu cha Fadhila za Swahaba hadithi nambari 11

Al-Bukhaariy kitabu cha ‘Kuumwa’ mlango wa ‘Anachoruhusiwa mgonjwa kusema anapoumwa hadiyth nambari 5666

 

 

Mambo Muhimu Yaliyotokea Wakati Wa Ukhalifa Wa Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘Anhu)

 

a- Jeshi La ‘Usaamah

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa keshatayarisha jeshi chini ya ongozi wa ‘Usaamah (Radhiya Allaahu ‘anhu) litakalokwenda kupigana vita nchi ya Sham, na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alifariki dunia kabla ya jeshi hilo kuondoka Madiynah, na jambo la mwanzo alofanya Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ni kulipeleka jeshi hilo la ‘Usaamah. Na katika kulipeleka jeshi hilo la ‘Usaamah, ilikuwa pigo kubwa kwa wanafiki waliortadi waliodhania kuwa baada ya kufa kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) Uislamu utadhoofika na kutoweka, na katika kulipeleka jeshi hilo pia kulinyanyua nguvu za irada ya Waislamu.

  

b- Vita Vya Walortadi

Walortadi ni wale waliotoka katika Uislamu baada ya kufa kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi sallam) na wengi wao ni wafuasi wa Musailima l Kadhab (Nabiy wa uongo) na Taliha al Aswad na Sajaaj, na vilipiganwa vita vikali sana na vilivokuwa vikali zaidi ni vita vilivyojulikana kwa jina la ‘Mapambano ya bustanini’ (Maarakatul hadiqah) dhidi ya Musailimah l Kadhab katika mji wa Yamama na Waislamu wakashinda

ushindi mkubwa kabisa.

 

c- Vita Dhidi Ya Walokataa Kutoa Zakaah

Waliokataa kutoa Zakaah ni wale walikuwa wakidhania kuwa zile pesa za Zakaah walizokuwa wakimpa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kuwa ni kodi na kwamba baada ya kufa kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) hapana haja tena ya kuilipa kodi hiyo.

Imetolewa na Al-Bukhaariy kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa amesema:

“Alipofariki Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na Abu Bakr akawa khalifa walikufuru waliokufuru katika waarabu na ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akasema (kumwambia Abu Bakr): Vipi tutapigana vita na watu wanaoitamka shahada ya laa ilaaha illa Allaah wakati Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: ‘Nimeamrishwa nipambane na watu mpaka watamke Laa ilaaha illa Allaah, na atakayeitamka itahifadhika kwangu mali yake na nafsi yake na hesabu yake iko kwa Allaah?

Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akasema:

"WaAllaahi nitapambana na kila anayefarikisha baina ya Sala na Zakaah kwa sababu Zakaah ni katika haki ya mali. WaAllaahi kama watakataa kunipa mbuzi mdogo waliyekuwa wakimpa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ningepigana nao kwa kukataa kwao huko”.

Sahih Al-Bukhaariy kitabu cha Zakaah mlango wa ‘Kuwajibika kwa Zakaah’ hadithi nambari 1399

 

 

Kutekwa Kwa Miji Ya Uajemi (Iran)

Abu Bakr alipeleka majeshi yake katika nchi ya Uajemi (Iran) yakiongozwa na Al Muthanna bin Al Haritha, kisha akampeleka Khaalid bin Waliyd na akamfuatilia na Al Qaa qaa bin ‘Amru At-Tamimiy.

 

 

Kutekwa Kwa Miji Ya Sham

Abu Bakr alimchaguwa Khaalid bin Said bin Al-’Aasw kuwa mkuu wa majeshi yake aliyoyapeleka katika nchi ya Sham, akapambana na majeshi ya Warumi na alipotaka msa’ada kutoka kwa Abu Bakr, akampeleka Al Waliyd bin Utbah na Ikrimah bin Abu Jahal na Amru bin Al-’Aasw na Abu ‘Ubaydah ‘Aamir bin Al-Jaraah na yeye ndiye aliyechukuwa uongozi wa majeshi baadaye.

Yakasonga mbele majeshi ya Waislamu mpaka yakaweza kuuteka mji wa Yarmuk, kisha Abu Bakr akampeleka huko Khaalid bin Waliyd na Allaah akawapa ushindi.

 

 

Itaendelea In shaa Allaah

 

 

Share