Fadhila Za Kusuluhisha Waliokhasimiana - 2

Tukiendelea na fadhila za kusuluhisha waliogombana wakakhasimiana, na iwapo baada ya kusoma mada hii tutazithamini fadhila hizi, basi kila mmoja wetu atakimbilia kufanya hima ya kupatanisha ndugu zetu wa Kiislamu waliokhasimiana. Allaah سبحانه وتعالى  Amelichukia jambo hili kwani linavunja asili ya undugu wa Kiislamu kama Anavyosema :

 

((إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ إِخْوَةٌ فَأَصْلِحُوا بَيْنَ أَخَوَيْكُمْ))

 

((Hakika Waumini ni ndugu, basi patanisheni baina ya ndugu zenu))  [Al-Hujuraat: 10]

 

Na kwa jinsi jambo hili lilivyochukiza hadi kwamba Allaah سبحانه وتعالى Anakataa kupokea amali za watu waliokhasimiana mpaka wapatane, na hawasamehe watu hao: 

 

 عن أبي هريرة رضي الله عنه قال : قال رسول الله صلى الله عليه وسلم: ((تُعرض الأعمال في كل أثنين وخميس فيغفر الله لكل أمريء لايشرك بالله شيئاً، إلا إمرءاً بينه وبين أخيه شحناء فيقول: اتركوا هذين حتى يصطلحا)) رواه مسلم

 

Imetoka kwa Abu Hurayrah رضي الله عنه kwamba kasema Mtume صلى الله عليه وسلم: Amali njema (vitendo vyema) hutandazwa kila Jumatatu na Alkhamiys, kisha Allaah Humghufuria kila mtu asiyemshiriki kitu Allaah, isipokuwa mtu aliyekuwa baina yake na baina ya ndugu yake uhasama, Husema: Waacheni hawa wawili mpaka wapatane)) [Muslim]

 

Kwa hiyo ni hatari kubwa kwa waliogombana kuwa wanapoteza umri wao bure kutenda mema na hali kumbe havipokelewi vitendo hivyo hadi  wapatane.

 

 

 

Njia za kupatanisha Watu

 

 

 

1-Kwanza tia nia kuwa unafanya kupata Radhi na ujira mkubwa kutoka kwa Allaah سبحانه وتعالى, na muombe Allaah سبحانه وتعالى Akuwafikie jambo hili. 

 

2-Msikilize kila mmoja malalamiko yake. 

 

3-Ukishajua sababu ya ugomvi, watajie hatari ya kuhasimikiana kama Anavyosema Allaah سبحانه وتعالى na Mtume صلى الله عليه وآله وسلم .

 

4-Tafuta wakati na sehemu munaasib kwa wote wawili.

 

5-Ikibidi kusema uongo, inafaa katika jambo hili kwa kutaka kumridhisha mmojawao ili kuleta suluhisho kama alivyoruhusu Mtume صلى الله عليه وآله وسلم katika Hadiythi:

 

((لَيْسَ الْكَذابُ الَّذِي يُصْلِحُ بَيْنَ النَّاسِ فَيَنْمِي خيرا أو يقول خيرا))  رواه البخاري ومسلم

 

((Si muongo yule anayesuluhusha watu kwa kusema uongo, kwani anaarifu mema au anasema mema [kwa lengo la kusuluhisha]))  [Al-Bukhariy na Muslim]

 

6-Fanya uadilifu, usipendelee hata kama mmoja ni jamaa yako wa karibu au unampenda zaidi.  Amesema Allaah سبحانه وتعالى:

 

 

((...فَأَصْلِحُوا بَيْنَهُمَا بِالْعَدْلِ وَأَقْسِطُوا إِنَّ اللَّهَ يُحِبُّ الْمُقْسِطِينَ))

 

((…basi yapatanisheni kwa uadilifu. Na hukumuni kwa haki. Hakika Allaah Anawapenda wanaohukumu kwa haki)) [Al-Hujuraat: 9]

 

Na Anasema tena Allaah  سبحانه وتعالى :

 

((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ كُونُواْ قَوَّامِينَ بِالْقِسْطِ شُهَدَاء لِلّهِ وَلَوْ عَلَى أَنفُسِكُمْ أَوِ الْوَالِدَيْن  وَالأَقْرَبِينَ  إِِن يَكُنْ غَنِيًّا أَوْ فَقَيرًا فَاللّهُ أَوْلَى بِهِمَا فَلاَ تَتَّبِعُواْ الْهَوَى أَن تَعْدِلُواْ وَإِن تَلْوُواْ أَوْ تُعْرِضُوا فَإِنَّ اللّهَ كَانَ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرًا ))

 

((Enyi mlioamini! Kuweni wenye kusimamisha uadilifu, mtowao ushahidi kwa ajili ya Allaah, ijapokuwa ni juu ya nafsi zenu, au wazazi wawili na jamaa zenu. Akiwa tajiri au masikini Allaah Anawastahikia zaidi. Basi msifuate matamanio, mkaacha kufanya uadilifu. Na mkiupotoa au mkajitenga nao basi Allaah anajua vyema mnayoyatenda)) [An-Nisaa: 135]

 

 

7-Wakishapatana In shaa Allaah  omba du'aa Allaah سبحانه وتعالى Awaendeleze masikilizano na mapenzi baina yao na muombe pia Akutakabalie juhudi yako.

 

 

Tunamuomba Allaah سبحانه وتعالى   Atunufaishe kwa yale tunayojifunza na Atuajaalie miongoni mwa wale wanaosikiliza kauli (nyingi) wakafuata zile zilizo njema. Aamiyn.

 

 

 

 

 

 

Share