Ikiwa Maulidi Hayafai Vipi Mashekhe Wengine Wanayakubali?

 

 

SWALI:

 

MIMI NI MPENZI WA ALHIDAYA NAOMBA NIULIZE SUALI. NIMEPATA TAARIFA YA KUA TUSISHEREHEKEE MAULID NA KWAMBA KWA WAISLAM NI VIBAYA. JEE HAWA MASHEHE WAKUBWA WA ZANZIBAR WAMEPATA WAPI USHAHIDI WA MAULID HATA IKAWA WANATUSHAJIHISHA JUU YA KUSHEREHEKEA MAULID?   

 

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kusherehekea Mawlid.

Si mashaykh wa Zanzibar tu wanaosherehekea Mawlid bali hata Mashaykh wa miji na nchi nyingine. Hata hivyo, katika Uislamu matendo ya Mashaykh hata wakiwa wakubwa namna gani huwa yanapimwa kwa kipimo cha Qur-aan na Sunnah; yakiwa yamekubaliana nayo huchukuliwa, na yakiwa yamepingana nayo hutupiliwa mbali.

Machimbuko ya msingi ya Muislamu kufuata ni Qur-aan na Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Kwa ajili ya hiyo, ndio tunakuta kuwa Maimaam wanne wakubwa wamekuwa na misemo ifuatayo:

 

1.     Imaam Abu Haniyfah alikuwa anajua na kuielewa mipaka yake, kwa hiyo, aliwafahamisha wanafunzi wake na wale wote watakaofaidika na ufahamu wake wa kina wa Uislamu kuwa upambanuzi wa mwisho kwa haki na batili ni Qur-aan na Sunnah; chochote kinachokwenda pamoja navyo ni haki na sawa na kinachokwenda kinyume ni batili. Mwanafunzi wake, Muhammad bin al-Hasan, ameripoti kuwa alisema, “Ikiwa nimetoa hukumu inayopingana na Kitabu cha Allaah na Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ikatae hukumu yangu”. Pia imenukuliwa kuwa aliashiria hakika ya msingi wa kufuata, ikiwa yeyote anataka kufuata Madh-hab yake kama alivyotarajia kufuatwa, ni kule kukubali Hadiyth sahihi. Imaam Ibn ‘Abdil-Barr ameripoti kuwa Imaam Abu Haniyfah alisema, “Ikiwa Hadiyth itapatikana kuwa sahihi, basi hiyo ni Madh-hab yangu”.

 

2.     Imaam Maalik alihimiza ile hakika kuwa anaweza kukosea na kuwa hukumu pekee ambazo zinafaa kutumiwa ni zile ambazo hazina ukinzani na Qur-aan na Hadiyth. Ibn ‘Abdil-Barr ameripoti kuwa Maalik wakati mmoja alisema, “Hakika ni kuwa mimi ni mwanaadamu, ninakosea na wakati mwengine ninasibu; hivyo chunguzeni vilivyo rai zangu, kisha chukueni yale yanayokubaliana na Kitabu na Sunnah, na yakataeni yote yanayopingana navyo”. Kauli hii ni dalili ya dhahiri kuwa Qur-aan na Hadiyth vilipewa kipaumbele juu ya vitu vyengine vyovyote na mwanachuoni huyu mkubwa ambaye hakuwa na Niyyah ya kuwa rai zake zifuatwe pasi na kuchunguzwa.

 

 

3.     Imaam ash-Shaafi‘iy alitilia mkazo sana nukta muhimu kuhusu rai za kibinafsi dhidi ya Sunnah. Alisema, “Waislamu (wa wakati wangu) walikuwa na rai zinazokubaliwa na wote kwa pamoja kuwa yeyote anayepata Hadiyth sahihi ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) haruhusiwi kuipuuza kwa kufadhilisha rai ya mwengine yeyote”. Nukta hii inagonga kabisa katika kiini cha Taqliyd, ambayo moja kati ya nguzo zake ni kukataa Sunnah kwa kufuata rai ya Madh-hab.

 

4.     Imaam Ahmad alikuwa wazi kabisa katika kutahadharisha dhidi ya Taqliyd, kama ilivyo dhahiri katika kauli yake ifuatayo iliyonukuliwa na Ibn Qayyim, “Musifuate hukumu zangu, zile za Maalik, ash-Shafi‘iy, al-Awzaa‘iy au ath-Thawriy kimbumbumbu. Chukueni (hukumu zenu) kutoka sehemu walizochukua wao”. Hivyo hivyo, katika kauli yake nyengine iliyonukuliwa na Ibn ‘Abdil-Barr, alisema, “Rai za al-Awzaa‘iy, Maalik na Abu Haniyfah ni maoni yao tu na kwangu mimi yote ni sawa, lakini kigezo cha uhakika kwa ukweli na uongo kipo katika Hadiyth”.

 

Hakika ni kuwa Mashaykh wenye kusoma na kusherehekea Mawlid hawana dalili katika Qur-aan wala Sunnah ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) bali ni kinyume chake ndio sawa.

 

Sherehe hizo zilianzishwa na maadui wa Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) huko Misri kuwafanyia mwanzo sherehe za wafalme wao wakati wa siku ya mazazi. Baadaye kukawa na sherehe za mazazi ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na wengineo kama ‘Aliy, Faatwimah, Hasan na Husayn (Radhiya Allaahu ‘anhum).

 

Na kwa zaida kuhusu Mawlid tazama makala kadhaa katika ALHIDAAYA.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share