Wasichana Kujitengeneza Sehemu Zao Za Siri Kabla Ya Kuolewa Na Kujitazama

 

Wasichana Kujitengeneza Sehemu Zao Za Siri Kabla Ya Kuolewa Na Kujitazama

 

Alhidaaya.com

 

SWALI:

 

Assalam Aleykum Warahmatullahi, jee kujiangalia sehemu ya siri kwa madhumuni ya kujitengeneza yafaa? Mfano kama wasichana wa kinyarwanda na kiganda huwa kabla ya kuolewa huwa wanavuta sehemu yao ya siri kwa madhumuni ya kuwa wakiolewa huwa wanastarehesha waume zao zaidi. Huwa kuna dawa ya mitishamba wanatumia na lazima katika kutumia ile dawa watajiangalia uchi wao. Jee, yafaa. Mimi nimeshauriwa kuvuta lakini nataka kujua kama ni makosa.

 

Shukran jazakallahu kheir.

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

 

Hakika hayo ni mambo ya kushangaza, na kwa Muislamu hayafai kuyafanya kwani ni mambo ambayo hayana maana hata kidogo na kama ni kwa ajili ya kumstarehesha mume, basi kuna njia nyingi za asili za kumstarehesha mume na si za kubadili maumbile na mwanamke kugeuka kituko na hata kuwa na maumbile yanayoweza kudhaniwa ni ya kiume.

 

 

Pia kuna masuala ya msingi ya kujiuliza kwa mwanamke wa Kiislamu mwenye kushawishika kuingia kwenye upuuzi wa kimila kama hizo ambazo hazioani na kufanana na Uislamu, nayo ni kujiuliza je, ana hakika kufanya kwake hivyo ni kweli kutamridhisha huyo mume ambaye yeye bado hajampata? Je, akipata mume ambaye ataudhika na maumbile kama hayo na ikapelekea yeye kupewa talaka itakuwaje? Na ikiwa ana uhakika maumbile hayo yatamridhisha mume, swali atakuwa amejuaje? Kawasiliana kwanza naye? Kapanga naye? Kajulishwa kuwa ndio anapenda hivyo? Majibu ni kuwa yote hayo ni makosa na ni haraam kwa mwanamke kuwa na mawasiliano na mwanaume kabla ya ndoa na pia kuzungumza masuala ya ndani kama hayo.

 

 

Isitoshe mila kama hizo zinapelekea wanawake wengi kuwa na matamanio na kuanza kufanya uzinifu na hata wanapoolewa wanakuwa wanashawishika kwenda nje ya ndoa ikiwa waume zao ima hawawatimizii wanavyotaka wao, au ikiwa waume zao hawavutiki na maumbile kama hayo.

 

 

Hivyo, tunakushauri dada katika Uislamu, jiepushe na hizo mila za kipuuzi na ridhika na maumbile uliyoruzukiwa na Allaah na jitunze na kujiheshimu na utapata mume bora ambaye anayetaka mke bora mwenye tabia njema za Kiislamu.

 

 

Jiepushe na kuwa katika usalama na Dini yako na heshima yako.

  

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share