Wameoana Zaidi Miaka Kumi Lakini Mume Hampi Haki Zake

SWALI:

 

ASLKM, NINA MUME AMBAE TUNA MIAKA MINGI TUNAISHI KWA BAHATI MBAYA AU NZURI SASA NI ZAIDI YA MIAKA 10 HAKUNA BAINA MIMI NA YEYE KUISHI KAMA MUME NA MKE HALAFU NIMEMGUNDUA KUWA ANAISHI KWA CHANGU MAANA TANGU ANIOWE HANITAZAMI KWA CHOCHOTE MWISHO NI HIVI KARIBUNI ALIUZA NYUMBA YAKE AKASAFIRI HATA SENTI MOJA HAKUNIACHIA NA WALA KUNIULIZA KUMALIZIKIWA NDIO AKAJUWA KUNITAFUTA NA KUJILETA NYUMBANI HIYO KULA BASI MPAKA KWA VITA ANATAKA MIMI PIA NILIPE, NINI SHAURI YENU KWA HAKIKA MAPENZI HAKUNA TENA KWA SOTE WAWILI LAKINI MWENZANGU ANAJUWA KINACHOMUWEKA KWANGU

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani kwa swali lako kuhusu ndoa yako yenye mashaka na mume ambaye hakupi haki.

Hakika suala lako ni dogo sana kwa njia ambayo unatakiwa uwe wazi kabisa kwa wapili wako.

 

Linalotakiwa ni anapokuja nyumbani kwako umkalishe na mzungumze kama watu wazima wenye kujua mambo. Swali ambalo unafaa umuulize ni je, anataka muendelee kuishi pamoja au hapana? Hapo utapata jibu la mara moja ndio au hapana. Ikiwa jibu ndio, swali la pili litakuwa mbona hunitazami kwa kunitimizia mahitaji yangu? Ikiwa anayumba yumba katika kujibu inafaa uitishe kikao baina yako, mumeo, na wawakilishi wenu (wazazi au jamaa wa karibu). Na katika kikao hicho unatakiwa uwe wazi kabisa kwa yaliyo na yanayo tokea baina yenu. Kikao hicho baada ya kutazama haki basi kitamuamuru aweze kutimiza majukumu hayo ya kukutazama.

 

 

Ikiwa hakuna natija yoyote ile itabidi upeleke malalamiko yako kwa Qaadhi au kwa Shaykh mwadilifu. Hapo atashurutishwa akutazame na ikiwa hatofanya hivyo basi Qaadhi atawaachisha na hamtakuwa tena mume na mke. Muislamu hakubali kudhulumiwa wala hadhulumu. Uislamu umetupatia njia kwa kila jambo na hili lako pia. Kwa hiyo, suluhisho la tatizo lako ni kujaribu kufuata hayo maelekezo na InshaAllaah Allaah Atakufanyia lenye kheri nawe.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share