Anataka Amuache Mke Ili Apate Radhi Za Baba

SWALI:

 

Mimi nimeowa mke miaka mitatu sasa tumejaaliwa mtoto mwaka mmoja sasa.  Matatizo ni kuwa baba hakuridhia mimi kumuoa huyo mke na kwa hivyo amenikasirikia hata jambo lolote na mimi hata akiwa mgonjwa ananifukuza nikienda kumuangalia. Na amesema njia ya pekee nikataka suluhu ni nimuache huyo mke niowe mke mwengine. Mke mwenyewe hatujakosana tangu kumuoa na alhamdullilah kwa nimjuavyo anatekeleza mambo ya dini na akikosea yuko tayari nikimrekebisha ana swali inavyotakikana wala hajamkosea mzee wangu heshima. ila tu mzee wangu hajakuwa na uhusiano mzuri na familia yake hasa tangu wanikubalie ni muoe mtoto wao hivyo hawasemi japo ni jirani. Na pia kabla ya kumuoa mzee wangu alikuwa amemuoza my step brother kwa dadake mke wangu. Lakini baadaye ndio akasema hangetaka mimi ni owe hulo. Dhamira yangu ilikuwa kupata mke alie na tabia za kiislam wala nilikuwa sijatembea naye ama mwengine yeyote. Sasa je nimuache mke ili nipate radhi za baba ama ni vipi.

 


 

 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukran kwa swali lako kuhusu babako kutaka umuache mkeo ambaye hajakukosea.

Hakika ni makosa Kiislamu kwa mtu yeyote yule kumtaka mwanamme amuache mwanamke kwa sababu ambazo si za kishari’ah.

Hilo ni jambo ambalo halifai na pia ni makosa na dhulma kwa mwanamme kumuacha mkewe bila ya sababu yoyote ile. Hivyo, linalotakiwa ni wewe kubaki na mkeo kwa njia nzuri huku ukitafuta mbinu ya kuweza kurudisha uhusiano wako mwema na baba yako.

 

Radhi za baba haziwezi kutoka kwako kwa jambo ambalo unafanya kumridhisha Allaah Aliyetukuka kama hilo la kubaki na mkeo wa halali kwa njia nzuri. Njia nzuri ni kutafuta watu ambao wanaweza kuzungumza na baba yako kama ni ‘ami zako, wajomba, Imaam, Shaykh au mtu yeyote aliye karibu nawe. InshaAllaah kwa kutumia njia hiyo huenda akarudi nyuma na kukutambua wewe kama mtoto wake na kumtambua mkeo.

 

 

Tafadhali bonyeza kiungo kifautacho upate manufaa zaidi:

 

 

Mtoto Kukosa Radhi Za Wazazi Kwa Sababu Ya Kuchagua Mwenyewe Mke

 

 

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share