Allaah Ni Mpangaji Wa Vifo Je, Anapouawa Mtu Huwa Kapunguziwa Muda Wa Kuishi?

 

Allaah Ni Mpangaji Wa Vifo Je, Anapouawa Mtu

Huwa Kapunguziwa Muda Wa Kuishi?

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Aslm alkm

 

Je Allaah (m'mungu) hupanga Muda wa Kifo? Je mtu anapouwawa anakuwa amempungzia muda wa kuishi? Na kama hapana kwa nini wanasema anayeua nae auwawe?

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Hii ni hukumu iliyotolewa na Allaah Aliyetukuka kwa waja Wake kwa maslahi yetu wenyewe.

 

Kufanya hivyo ni kuweka nidhamu ya kimaisha ili asione mtu anaweza kufanya lolote bila kuchukuliwa hatua. Hii inapunguza sana uhalifu na kuleta maslahi ya watu dunaini.

 

Na bila shaka Allaah Aliyetukuka Ambaye ndiye Mjuzi wa kila kitu pamoja na kujua muda wa mwanaadamu kuishi hapa duniani ndiye mwenye kuleta uhai na kifo, kwani Yeye ndiye Rabb. Allaah Aliyetukuka Anasema:

الَّذِي خَلَقَ الْمَوْتَ وَالْحَيَاةَ لِيَبْلُوَكُمْ أَيُّكُمْ أَحْسَنُ عَمَلًا ۚ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْغَفُورُ﴿٢﴾

Ambaye Ameumba mauti na uhai ili Akujaribuni ni nani kati yenu mwenye ‘amali nzuri zaidi. Naye ni Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Mwingi wa kughufuria. [Al-Mulk: 2]

 

Na Anasema pia,

إِنَّ اللَّـهَ عِندَهُ عِلْمُ السَّاعَةِ وَيُنَزِّلُ الْغَيْثَ وَيَعْلَمُ مَا فِي الْأَرْحَامِ ۖ وَمَا تَدْرِي نَفْسٌ مَّاذَا تَكْسِبُ غَدًا ۖ وَمَا تَدْرِي نَفْسٌ بِأَيِّ أَرْضٍ تَمُوتُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ عَلِيمٌ خَبِيرٌ ﴿٣٤﴾

Hakika Allaah Ana elimu ya Saa (Qiyaamah), na Anateremsha mvua na Anajua yale yaliyomo katika tumbo la uzazi, na nafsi yoyote haijui nini itachuma kesho, na nafsi yoyote haijui itafia katika ardhi gani, hakika Allaah ni Mjuzi wa yote, Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika. [Luqmaan: 34].

 

Kwa hiyo, Allaah Aliyetukuka ndiye mwenye kupanga muda na mahali pa kufia mwanaadamu.

Mtu anapouawa kwa sababu ya kuua, au kuuliwa katika vita au kuuawa kwa sababu nyengine yoyote ile ina maana ya kuwa muda wake wa kuishi umemalizika na sio kuwa muda umepunguzwa. Na anayesema kuwa mwenye kuua auawe ni Allaah Aliyetukuka sio mwengine.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share