Adhabu Za Kaburi Katika Qur-aan Na Hadiyth

 

SWALI:

Ningependa kuelemishwa kuhusu adhabu ya kaburi kwa Quran na hadithi.

jazakumullahJIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako zuri. Huenda swali hili limekuja kwa sababu ya kupatikana baadhi ya Waislamu wenye muelekeo wa kutoamini adhabu ya kaburi ndio suala hili likaletwa kwetu. Hawa ni watu ambao wanatilia shaka Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa sababu moja au nyingine. Na huenda wakaona adhabu hiyo haieleweki wala haingii katika akili ya mwanadamu kwa mawazo yao.

Hata hivyo, Qur-aan na Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) zipo wazi kabisa katika suala hili. Hebu tutizame dalili zifuatazo:

  1. Allaah Aliyetukuka Anasema: “Basi Allaah Akamlinda na ubaya wa hila walizozifanya. Na adhabu mbaya itawazunguka watu wa Firauni. Wanaonyeshwa Moto asubuhi na jioni. Na itapofika Saa ya Qiyaama patasemwa: Waingizeni watu wa Firauni katika adhabu kali kabisa!” (40: 45 – 46). Hii Aayah iko wazi kabisa kuwepo kwa adhabu ya kaburi kabla ya Siku ya Qiyaama.

  2. Allaah Aliyetukuka Anasema: “Nani dhalimu mkubwa kuliko yule anayemzulia uongo Allaah, au anayesema: Mimi nimeletewa wahyi; na hali hakuletewa wahyi wowote. Na yule anayesema: Nitateremsha kama alivyoteremsha Allaah. Na lau ungeliwaona madhalimu wanavyokuwa katika mahangaiko ya mauti, na Malaika wamewanyooshea mikono wakiwaambia: Zitoeni roho zenu! Leo mtalipwa adhabu ya fedheha kwa sababu ya mliyokuwa mkiyasema juu ya Allaah yasiyo ya haki, na mlivyokuwa mkizifanyia kiburi Ishara Zake” (6: 93). Hotuba hii ni kwa madhalimu wanapokuwa katika mauti, wakijulishwa kuwa wataadhibiwa siku hiyo hiyo ya kuaga dunia kwao. Lau kama adhabu ingeakhirishwa mpaka Siku ya Qiyaama, hawangeambiwa: “Leo mtalipwa”. Hii ni dalili kuonyesha ipo adhabu ya kaburi.

  3. Allaah Aliyetukuka Anasema: “Na hakika waliodhulumu watapata adhabu nyengine isiyokuwa hii, lakini wengi wao hawajui” (52: 47). Aayah hii inaonyesha kuwa adhabu ya kwanza ni ile ya kaburini, kwani haitakuwa sawa kuifasiri kuwa ni adhabu katika maisha haya kwani madhalimu wengi hawaadhibiwi hapa duniani.

  4. Allaah Aliyetukuka Anasema: “Na katika mabedui walio jirani zenu wamo wanafiki; na katika wenyeji wa Madiynah pia wapo waliobobea katika unafiki. Wewe huwajui. Sisi tunawajua. Tutawaadhibu mara mbili, kisha watarudishwa kwenye adhabu kubwa” (9: 101). Adhabu ya kwanza katika Aayah inahusu adhabu ya hapa duniani na ya pili ni adhabu ya kaburi. Kisha Allaah Aliyetukuka Anasema: “Kisha watarudishwa kwenye adhabu kubwa”, ina maana ya adhabu ya Siku ya Qiyaama.

Dalili katika Sunnah kuhusiana na adhabu ya Kaburi ni kama zifuatazo:

  1. Imeripotiwa kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipita karibu na makaburi mawili akasema: “Hawa watu wawili wanaadhibiwa lakini si katika madhambi makubwa (kuacha). Mmoja wao hakuacha kujikinga na mkojo, ilhali wa pili alikuwa akisambaza uvumi” (al-Bukhaariy na Muslim).

  2. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Nimeteremshiwa wahyi kuwa watu wako watatiwa katika mtihani sawa na mtihani wa ad-Dajjaal, makaburini mwenu. Lau haingekuwa kwa sababu ya kwamba mtaacha kuzika wafu wenu makaburini kwa kusikia adhabu humo ambayo naisikia, hakika ningefanya nanyi muisikie” (Muslim).

  3. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema tena: “Mmoja wenu anapomaliza tashahhud ya mwisho aombe ulinzi wa Allaah kwa mambo manne: Adhabu ya moto (wa jahannam); adhabu ya kaburi; mtihani wa maisha na kifo; na shari ya mtihani wa Masihi ad-Dajjaal” (Muslim).

Ni muhimu kuhimiza hapa kuwa Hadiyth zote hizi ni sahihi zilizopokewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa isnadi zilizo sahihi na wapokezi wenye kutegemewa. Ifahamike kuwa yeyote asiyeamini basi yuko katika hatari kubwa. Shaykh wa Uislamu, Ibn Taymiyyah, amesema: “Zipo Hadiyth sahihi nyingi zinazothibitisha kuwepo kwa adhabu na raha kaburini kwa anayestahiki. Pia kusualiwa (kuulizwa) kaburini na Malaika wawili ni hakika na kweli”.

Jambo hili la ghaybu ni muhimu kila Muislamu awe ni mwenye kuliamini bila tashwishi yoyote ile. Hilo tuelewe kuwa lipo mbali na kuweza kuelewa na mwanaadamu mwenye mapungufu mengi.

Na Allaah Anajua zaidi

Share