Zipi Sifa Za Sumayyah – Shahidi Wa Kwanza Mwanamke Katika Uislamu

SWALI:

 

a, alailkum, ningependa kujua historia ya bibi sumaiyya, na nasaba yake katika uislamu na ana sifa zipi? Ntashukuru nikijibiwa. wasal alaikum


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani kwa swali lako kuhusu sifa za Bi Sumayyah bint Khabbaat (Radhiya Allaahu ‘anha).

Bibi huyu alikuwa ni mtumwa wa Abu Hudhayfah bin ‘Abdillaah al-Makhzuumiy. Na bwana wake alimsifu kuwa alikuwa mwanamke mwenye akili na fahamu nzuri sana.

 

Bibi huyu aliolewa na bwana aliyehamia Makkah kutoka Yemen kwa jina, Yaasir (Radhiya Allaahu ‘anhu). Yaasir alijenga urafiki na kuwa chini ya himaya ya Abu Hudhayfah. Baada ya kupita muda Yaasir alimuoa bi Sumayyah. Ndoa hiyo ilikuwa ni nzuri na kukapatikana masikilizano mazuri baina ya wanandoa hao. Walipata mtoto wa kwanza waliomuita ‘Ammaar, na baadaye wakapata ‘Abdullaah na Haarith.

 

Abu Hudhayfah alikuwa ni mtu mkarimu, mwenye huruma na mwenye kuwapenda. Kwa minajili hiyo akaiacha familia huru na akawa ni mwenye kuwasaidia kila wakati kwa hali na mali.

 

Kwa akili muruwa aliyokuwa nayo Sumayyah (Radhiya Allaahu ‘anha) hakuchelewa kusilimu pindi Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipoanza kuutangaza Uislamu. Panasemwa kuwa Sumayyah (Radhiya Allaahu ‘anha) alikuwa mtu wa saba katika kusilimu jambo ambalo lilimpatia hadhi kubwa. Kusilimu kwake kulikuwa kwa dhati na Iymaan yake ilikuwa ni kubwa na kila alipopata misukosuko na mitihani alisimama imara kabisa juu ya hilo.

 

Familia hii ya Sumayyah (Radhiya Allaahu ‘anha) iliposilimu ilipata mitihani na mateso kwa ule udhaifu wao wa kinasaba kama walivyopata Waislamu wengine waliokuwa wenye nasaba duni au watumwa. Kwa ajili hiyo, Sumayyah, Yaasir na ‘Ammaar (Radhiya Allaahu ‘anhum) walilengwa na Maquraysh katika kupatiwa adhabu. Wakati mmoja Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akipita sokoni akaikuta familia hiyo ya watu watatu ikiadhibiwa kwa adhabu kali sana. Hakuwa na la kuwafanya isipokuwa kuwapatia hima kwa kuwaambia: “Subirini, enyi familia ya Yaasir kwani mashukio yenu ni Peponi”.

 

Abu Jahl, adui wa Allaah ndiye aliyekuwa akimuadhibu sana Sumayyah bint Khabbaat (Radhiya Allaahu ‘anha), lakini Summayah (Radhiya Allaahu ‘anha) hakuyumba yumba katika Iymaan yake bali alibakia katika uimara na istiqaamah (msimamo). Abu Jahl alijaribu sana kutumia nguvu na kumtisha ili aritadi lakini alikataa hayo bila ya kusita. Abu Jahl hakukubali ule ukweli kuwa mwanamke huyu mwenye Iymaan anaweza kumpuuza yeye kiasi hicho, na kwa hasira kali aliyokuwa nayo iliyojaa kifuani mwake alimdunga mkuki, hivyo kufa kwa kipigo hicho.

 

Na hivyo, akawa Muislamu wa kwanza kuuliwa kwa ajili ya Dini yake wakati wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kufa kwake shahidi ndicho kilichowapatia wengine ujasiri wa kuweza kusimama imara dhidi ya maudhi, mateso, kejeli na kuipita mitihani waliyokuwa wakikumbana nayo kutoka wka maadui.

 

Familia hii ilijitolea mhanga kwa ajili ya Uislamu, hivyo kuuliwa katika kuitetea Dini. Baba na mama, mama akiwa ndiye wa kwanza, sio katika familia tu bali kwa wakati wote mpaka ulimwengu utakapomalizika. Walijitolea mhanga ili waweze kuisimamisha haki na ukweli na pia kupata thawabu za Kesho Akhera.

 

Hao ndio waliotangulia kwa wema na wakatupatia sisi mfano mzuri wa Muislamu mwema na mzuri, mwenye akili, elimu na busara na kuwa na Iymaan ya kweli na matunda yake.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share