Takbiyrah Ya Ihraam Ni Yenye Kutangulia Au Du’aa Ya Kufungulia Swalaah (Inayoitwa Na Wengine Tawjiyh)?

SWALI:

 

sheikh assalaam alaykum kama nilivyotangulia mwanzo kuomba radhi kwa kuingia bila kurusika ktk uwanja huu wa maswali, sheikh ningeomba unifahamishe kidogo, hivi unapomaliza kukimu swala kwanza unapiga takbira ihram au unasoma dua ya kufungulia swala ndipo unapiga takbir na hivyo ambavyo ni sahihi ni ktk swala ya fadhi au pia na taraweih najua kuwa ni rakaa mbili mbili unaswali je ukiinuka rakaa ya tatu inakuwaje alhidaaya naomba majibu yenu japo kwa ufupi ili nijuwe kama nakwenda sahihi.


 

JIBU: 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. 

Shukrani kwa swali lako kuhusu Takbiyrah ya kuanza Swalaah na Du’aa yake, ipi inatangulia mwanzo.

Awali ya yote ni kukufahamisha ndugu yetu kuwa uwanja wa maswali na kuuliza ni huru na uwazi kwa kila mmoja wetu. Hivyo, haina haja kuomba samahani kwani hujafanya kosa lolote nasi tunakukaribisha kwa moyo mkunjufu katika tovuti hii. 

Pili, Swalaah ya faradhi au Sunnah ina mfumo wake maalumu kama alivyo tufundisha Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kama alivyotuambia:

Swalini kama mlivyoniona nikiswali” (al-Bukhaariy).

Katika Swalaah yoyote ile unafaa uanze na Takbiyrah ya kuanzia Swalaah ambayo inakujuza kuwa tayari umeingia katika Swalaah kisha ndio unaweza kusoma du’aa ya kufungulia hiyo Swalaah. Haiwezekani kufanya kinyume na hivyo na hakuna ushahidi sahihi wa hilo. 

Ikiwa unainuka kutoka katika Tahiyyaatu kwa kuwa unaswali Swalaah ya rakaa tatu au nne, utainuka na kusoma Suratul Faatihah baada ya kupiga Takbiyrah ya kunyanyuka. Ama katika Swalaah ya taraawiyh kila baada ya rakaa mbili unatoa salaam na unanyanyuka na kuanza kama ulivyoanza mwanzo kwa Takbiyrah ya Ihraam na kasha du’aa ya ufunguzi na kuendelea na Swalaah yako kama kawaida. 

Zaidi unaweza kusoma mambo yanayohusu Swalaah katika kitabu kizuri chenye mafunzo sahihi ya Swalaah kama ilivyofundishwa na Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kilichopo katika kiungo hiki hapa chini: 

Sifa Ya Swalah Ya Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam)

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

Share