Masiyh Dajjaal

Masiyh Dajjaal

 

Imetarjumiwa Na: ‘Naaswir Haamid

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

Maana ya neno Masiyh (Masiya):

 

 

Kuna zaidi ya maoni hamsini ya kiwanazuoni yenye maana ya Masiyh. Wanasema kwamba neno hili linatumika sehemu zote kwa Aliyemkweli [Masiyh wa Kweli, yaani (Yesu)] na mpotoshaji aliye muongo [dhidi ya ‘Kristo’ ama Dajjaal]. Masiyh ndiye Mkweli, ‘Iysaa bin Maryam (Yesu mwana wa Mariyamu), Masiyh wa uongofu, aliyewaponya wale waliozaliwa vipofu ama viguru, na kuwafanya wafu kuwa hai kwa uwezo wa Allaah.

 

Masiyh wa kuigiza (al-Masiyh ad-Dajjaal) ni muongo anayewaongoza watu kwenye uovu, Masiyh wa upotovu atawadanganya watu kwa namna alizojaaliwa, kama vile kuteremsha mvua, kuihuisha ardhi na kuifanya kuchipua mimea, na ‘miujiza’ mengineyo.

 

Kwa hivyo, Allaah Amewaumba Masiyh wawili, ambao mmoja wao ni tofauti kwa mwengine.

 

 

Wanazuoni wanasema kwamba sababu ya kwanini Dajjaal akaitwa Masiyh ni kwasababu moja kati ya macho yake ni mamsuuh (kimaana ni ‘lililo futika’; lililo tandazika au lililo kwaruzika, yaani atakuwa ni kipofu wa jicho moja ama halifanyi kazi). Au imesemwa kwamba ni kwasababu atakagua au kuzuru ardhi yote (yamsah) kwa siku arobaini... Maelezo ya awali ndio sahihi zaidi, kwasababu ya yale yaliyosemwa ndani ya Hadiyth iliyopokelewa na Muslim kutoka kwa Anas bin Maalik, aliyesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:  “Dajjaal atakuwa kipofu (mamsuuh) katika jicho lake moja, na baina ya macho yake kutaandikwa ‘kaafir’...”

 

 

Maana Ya Neno Dajjaal:

 

Neno Dajjaal limetolewa kutoka kwenye maneno “Dajjala al-ba’iir (amemtia alama ngamia)”, ikimaanisha pale wanapopaka kwa lami.

 

Mzizi wa [neno la Kiarabu la] dajala linamaanisha mchanganyo. Neno dajala linatumika kumaanisha kwa makusudi kuchanganya mambo na kuwa mbabaifu na mtatanishi. Dajjaal ni yule anayezungumza kwa ubabaifu, anayesema uongo mwingi na kuwadanganya watu wengi.

 

Neno “Dajjaal” limekuja kuwa ni sifa anayopewa muongo, mwenye jicho moja, Masiyh muongo. Dajjaal anaitwa hivyo kwasababu ataficha ukafiri wake mbele za watu kwa kuwaambia uongo, kuwachanganya na kuwababaisha.

 

Maelezo Kuhusu Dajjaal, Na Hadiyth Zilizosimuliwa Zinazomhusu Yeye:

 

Dajjaal atakuwa ni mtu miongoni mwa watoto wa kiume wa Aadam. Atakuwa na sifa nyingi ambazo zimeelezwa ndani ya Hadiyth nyingi kuwafafanulia watu kuhusiana naye na kuwaonya kuhusiana na uovu wake. Kwa hivyo pale anapokuja, Waumini wataweza kumtambua na hawatapotoshwa kutokana naye; watazitambua sifa zake ambazo Aliye Mkweli (Nabiy Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuelezea. Sifa hizi zitamtenganisha na watu wengine, ili kwamba hakuna mtu atakayelaghaiwa naye isipokuwa wale walio kuwa wajinga na uoni wao umeshaamuliwa (wapotofu). Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Atujaalie kuwa salama na wenye upambanuzi.

 

Baadhi Ya Sifa Hizi Ni:

 

Atakuwa ni mtu kijana mwenye ngozi ya wekundu, mfupi, nywele nyingi za mawimbi, uso mpana, na kifua kilichotanuka, kipofu au mlemavu (mamsuuh) wa jicho moja. Jicho halitanyanyuka wala kuzama, na litakaa kama ni zabibu inayoelea.

 

Jicho lake la kushoto litakuwa na kipande cha nyama chembamba kilichoota pembezoni mwa jicho lake. Kumeandikwa baina ya macho yake mawili “Kaaf, faa na raa’ (K-F-R)”, kwa herufi (za Kiarabu) zisizoshikana. Au “Kaafir”, kwa herufi zilizounganishwa. Zitasomeka kwa kila Muislamu, mwenye kujua ama asiyejua kusoma.

 

Sifa zake nyengine ni kwamba atakuwa tasa, hatozaa mtoto.

 

Zinafuatia Baadhi Ya Hadiyth Sahiih Ambazo Zinataja Sifa Zake Zilizoelezwa Hapo Juu. Hadiyth Hizi Zinafanya Kuwa Ni Sehemu Ya Ushahidi (Daliil) Kuhusiana Na Kutokea Kwa Dajjaal:

 

Kutoka kwa ‘AbduLlaah bin ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu), aliyesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:  “Wakati nikiwa nimelala, nilijiona nikifanya tawaaf kuizunguka Ka’bah, ambapo nilimuona mtu anayengara akiwa na nywele ndefu, akiwa amesimama baina ya watu wawili, na maji yakidondoka kutoka kichwani mwake. Nikauliza, “Huyu ni nani?” Wakasema, “Mwana wa Maryam.” Baadaye nikageuka na kumuona mtu mwenye ngozi ya wekundu, mwili uliojaa, akiwa na nywele za mawimbi, kipofu kwenye jicho lake la kulia, na jicho lake likionekana kama zabibu inayoelea. Nikauliza, “Huyu ni nani?” Wakasema, “Huyu ni Dajjaal.” Mtu ambaye amefanana naye sana ni Ibnu Qatan.” [Imepokewa na Al-Bukhaariy; Ibn Qataan alikuwa ni mtu kutoka Banu Mustalaq kutoka Khuzaa’ah].

 

 

Pia imepokewa kutoka kwa Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amelitaja (jina la) Dajjaal kwa watu na kusema:  “Allaah Hana jicho moja, lakini Masiyh wa uongo (al-Masiyhud-Dajjaal) ni mwenye jicho moja (chongo), kipofu na mlemavu kwenye jicho lake la kulia, na jicho lake likionekana kama ni zabibu inayoogelea...” [Imepokewa na Al-Bukhaariy].

 

 

Kwenye Hadiyth refu iliyopokewa na an-Nawwaas bin Sam’aan (Radhiya Allaahu ‘anhu) inasema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimtaja Dajjaal (wakati wa) asubuhi moja. Mara nyengine akimuelezea kwamba ni mtu asiye muhimu na mara nyengine akimuelezea kwamba ni mtu aliye muhimu hadi kufikiria kwamba alikuwa kwenye sehemu ya shada la miti ya tende...” Moja kati ya sifa za Dajjaal alizozielezea zilikuwa: “Atakuwa ni mtu kijana mwenye nywele zilizopindana pindana (pilipili), akiwa na jicho lenye kuogelea. Ni kana kwamba anaonekana kufanana na ‘Abdul-‘Uzza bin Qataan.” [Imepokewa na Muslim].

 

 

Imepokewa kutoka kwa ‘Ubaadah bin as-Swaamit (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Nimekuelezeni mengi mno kuhusu Dajjaal na kwamba (bado) ninahofia hamutafahamu. Atakuwa ni mwenye jicho moja, jicho lake likiwa halijatokeza nje wala halijazama. Iwapo mutapata utata kuhusiana naye, basi kumbukeni kwamba Mola wenu sio mwenye jicho moja.” [Abu Daawuud. Hadiyth hii ni sahihi – Swahiyhul-Jaami’ as-Swaghiyr]

 

 

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:  “... ama kwa Masiyh muongo, atakuwa ni mwenye jicho moja, akiwa na ubapa wa uso ulio mpana na mwenye kifua kipana, na atakuwa ni mwenye kibiongo...” [Ahmad]

 

 

Hudhayfah (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Dajjaal atakuwa ni mwenye jicho moja, kipofu na mlemavu kwenye jicho lake la kushoto, akiwa na nywele nyembamba. Atakuwa pamoja naye pepo na moto, lakini moto wake utakuwa ni pepo na pepo yake itakuwa ni moto.” [Muslim]

 

 

Kwa mujibu wa Hadiyth ya Anas (Radhiya Allaahu ‘anhu), Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:  “Hakuna Rasuli aliyeletwa isipokuwa aliwatahadharisha watu wake kuhusu (mtu) aliye na jicho moja (na aliye) muongo. Yeye ni mwenye jicho moja, lakini Mola wenu sio mwenye jicho moja, na baina ya macho yake kutaandikwa ‘Kaafir’” [Al-Bukhaariy].

 

 

Kwa mujibu wa simulizi nyengine:

 

“Baina ya macho yake kumeandikwa ‘kaaf Faa Raa’.” [Muslim].

 

 

Kwa mujibu wa Hadiyth iliyopokewa na Hudhayfah:  “Haya yatasomeka na kila Muumini, aliyesoma ama asiyesoma (anaye/asiye jua kusoma na kuandika).” (Muslim).

 

Kwa maana iliyo wazi, maandishi haya yatakuwa ni sahihi, na ukweli kwamba baadhi yao watayaona wakati wengine hawatayaona, na kwamba wasiojua kusoma watayasoma, (kwao) sio (jambo) lenye kutatiza. “Hii ni kwa sababu Allaah Anawajaalia watu kuelewa kitu kwa kukiangalia, kama Anavyopenda na wakati Anaopenda. Hivyo, Muumini atayaona haya kwa ukaribu, hata kama sio msomi, na kaafir atashindwa kuyasoma, hata kama ni msomi. Kwa ishara moja, Muumini ataiona kwa ushahidi wa karibu hali ya kuwa kafiri hatauona. Allaah Atajaalia Muumini kuelewa bila ya yeye kuwa ni msomi, kwa sababu kwa wakati huo, mambo ya maajabu yatakuwa yanatokezea.” [Fat-hul-Baariy cha Ibn Hajar al-‘Asqallaaniy, 13/100].

 

 

An-Nawawi amesema: “Maelezo sahihi kuhusiana na wale waliosoma kadhia hii ni kwamba maandiko haya yachukuliwe kwa maana halisi, kama ni maandishi ambayo Allaah Atayatengeneza kuwa ni dalili, moja kati ya ushahidi bora wa kwamba (Dajjaal) ni kafiri na ni muongo, ili kufichua uongo wake. Allaah Ataionesha ishara hii kwa kila Muislamu, aliyesoma na asiyesoma, na Ataificha kwa kila mtu Ambaye Ameshamuhukumu kupotoka na Anayetaka kumjaribu. Hakuna sababu kwa nini hili lisiwezekane.” [Sharh an-Nawawiy li Swahiyh Muslim, 18/60]

 

 

Sifa zake nyengine zimetajwa ndani ya Hadiyth ya Faatwimah bint Qays (Radhiya Allaahu ‘anha), kwenye kisa cha aj-Jassaasah, ambayo Tamiym ad-Daariy (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema: “Hivyo tukakimbilia kuelekea katika nyumba ya mtawa, ambapo tulimuona mtu wa maajabu tusiyepata kumuona, akiwa amefungwa na minyororo tusiyopata kuiona. [Muslim].

 

 

‘Imraan bin Huswayn (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema: Nilimsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:  “Tokea kipindi cha kuumbwa Aadam hadi Saa itakapoanza, hakutakuwa na uumbaji mkubwa kuliko wa Dajjaal.” [Muslim].

 

 

Dajjaal hatokuwa na mtoto yeyote, kama ilivyoelezwa ndani ya Hadiyth ya Abu Sa’iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ‘anhu), ambaye ameeleza lile lililotokezea baina yake na Ibn Sayyaad, aliyemwambia: “Je hujamsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema kwamba hatakuwa na mtoto yeyote?...” Abu Sa’iyd alisema: ‘Nikasema: ‘Ndio...” [Muslim).

 

 

Kutokana na simulizi zilizonukuliwa hapo juu, tunaweza kutambua kwamba baadhi yake zinamuelezea jicho lake la kulia kama ni lenye upofu au ulemavu, na baadhi zikimuelezea jicho lake la kushoto kama ni lenye upofu au ulemavu. Tanbihi zote ni sahihi. Baadhi ya wanazuoni walijaribu kuzijumuisha simulizi hizi. Al-Qaadhi ‘Iyaad amesema: “Macho yake yote mawili ya Dajjaal yatakuwa ni (yenye) ulemavu, kwa sababu simulizi zote ni sahihi. Jicho lake la kulia litakuwa ni lile ambalo limechubuka (mamsuuh) na lisilofanya kazi, lisiloweza kuona, kama ilivyosimuliwa ndani ya Hadiyth ya Ibn ‘Umar. Na jicho lake la kushoto litakuwa ni lile ambalo limefunikwa na ugozi mwembamba, na pia litakuwa halifanyi kazi.”

 

 

Hivyo atakuwa ni mwenye ulemavu kwenye macho yake yote la kulia na jicho lake la kushoto; kila jicho litakuwa ni pofu, yaani, lisilofanya kazi, kwa sababu neno la Kiarabu lililotumika ndani ya Hadiyth, a’war, linatumika kuelezea chochote ambacho hakifanyi kazi na haswa linatumika kwa kuelezea macho yasiyofanya kazi. Jicho moja litakuwa halifanyi kazi na jicho jengine litakuwa ni lenye ulemavu (bovu).”

 

An-Nawawiy amekubaliana na mjumuisho huu ulioshauriwa na al-Qaadhi ‘Iyaad, na al-Qurtubiy pia amekubaliana nao.

 

 

Sehemu Ambayo Dajjaal Atatokezea:

 

Dajjaal atatokezea upande wa mashariki, sehemu za Khurasaan, kutoka miongoni mwa Mayahudi wa Kisfahani. Kisha atatembea sehemu mbali mbali duniani na hatoacha mji isipokuwa ameuingia, isipokuwa kwa Makkah na Madiynah, ambayo hatoweza kuingia kwa sababu Malaika wanailinda.

 

 

Kwa mujibu wa Hadiyth ya Faatwimah bint Qays (Radhiya Allaahu ‘anha), Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema kuhusiana na Dajjaal: “Atatokezea upande wa bahari ya Syria au kutoka sehemu za bahari ya Yemen... Hapana, inawezekana upande wa mashariki...” – na aliashiria pande za mashariki.  [Muslim).

 

 

Abu Bakr as-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuambia:  “Dajjaal atatokezea kutoka ardhi ya upande wa mashariki inayoitwa Khurasaan.” [at-Tirmidhiy. Ameisahihisha al-Albaaniy, Swahiyh al-Jaami’ as-Swaghiyr].

 

 

Anas (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Dajjaal atatokezea kutoka miongoni mwa Mayahudi wa Kisfahani, na pamoja naye watakuwepo Mayahudi sabini elfu, wakiwa wamevalia mataji.” [Ahmad].

 

 

Sehemu Ambazo Dajjaal Hatoingia Kamwe:

 

 

Amezuiliwa Dajjaal kuingia Makkah au Madiynah pale atakapotokezea mwishoni mwa Saa (uhai wa dunia), kwa sababu Hadiyth zilizo sahihi zimepokewa kwa uthibitisho huo. Kwa namna zilivyo sehemu nyenginezo, ataziingia moja baada ya nyengine.

 

Katika Hadiyth ya Faatwimah bint Qays (Radhiya Allaahu ‘anha), amesema: “[Atasema Dajjaal:], ‘Ni karibuni nitaruhusiwa kutokezea. Kisha nitatokezea na kutembea pembe za dunia kwa siku arobaini, na sitoacha mji wowote bila ya kuuingia, isipokuwa kwa Makkah na Madiynah, ambayo nitazuilika kuiingia kwa sababu kila nikijaribu kuingia, kutakuwepo Malaika aliye na panga lisilo na ala (lililo wazi) mkononi, akinizuia kuingia. Kwenye kila mlango kutakuwa na malaika wakiihami.’” [Muslim]

 

 

Pia imesimuliwa kwamba Dajjaal hatoingia Msikiti wa Sinai, au Masjidul-Aqsaa (uliopo Jerusalem). Imaam Ahmad amepokea kwamba Junaadah bin Umayyah al-Azdiy amesema:  “Nilikuja kwa mtu kutoka miongoni mwa Swahaba wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumwambia: ‘Nielezee Hadiyth ambayo umeisikia kutoka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu Dajjaal.’ Aliitaja Hadiyth hiyo, na kusema: ‘Atakaa miongoni mwenu kwa siku arobaini, ambazo ndani yake atakwenda katika kila pembe (ya dunia) isipokuwa kwa Misikiti minne: Masjidul-Haraam (Makkah), Msikiti wa Madiynah, (Msikiti wa) Sinai na Masjidul-Aqsaa.’”

 

 

 

Wafuasi Wa Dajjaal:

 

 

 

Wengi miongoni mwa wafuasi wa Dajjaal watakuwa wanatoka miongoni mwa Mayahudi, Wafursi na Waturuki, na mchanganyiko wa watu wengine, zaidi ni Mabedui na wanawake.

 

Imaam Muslim amepokea ndani ya Swahiyh yake kutoka kwa Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:  “Wafuasi wa Dajjaal kutoka miongoni mwa Mayahudi wa Kisfahani watafikia idadi ya sabini elfu, wakivaa maguo mazito na zenye mistari.” Kwa mujibu wa simulizi iliyopokewa na Imaam Ahmad: “Mayahudi sabini elfu, wakiwa wamevalia mataji.”

 

 

Kwa mujibu wa Hadiyth ya Abu Bakr iliyonukuliwa hapo juu: “Atakuwa na wafuasi wenye sura kama ngao zinazong’ara.” [at-Tirmidhiy].

 

 

Kwa mnasaba wa Mabedui kuwa wafuasi wa Dajjaal, hili ni kutokana na kwamba wengi miongoni mwao ni majahili. Kwa mnasaba wa wanawake, hii ni kutokana na kwamba wao tayari ni wenye kushawishiwa, na kwa sababu wengi wao ni majahili. Imesimuliwa kwamba Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema: Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:  “Dajjaal atakuja kwenye ziwa hili la Marriqanaat – bonde lililopo Madiynah – na wengi wao watakaotoka pamoja naye watakuwa ni wanawake, hadi itafikia mtu kumuendea mama mkwe wake, mama yake, binti yake, dada yake na shangazi yake, na kuwafunga pamoja (mfano kamba) barabara kwa kuhofia kwamba watatoka pamoja naye.” [Ahmad].

 

 

Fitnah Za Dajjaal:

 

Fitnah za Dajjaal zitakuwa ni za daraja ya juu tangu kuumbwa kwa Nabii Aadam ('Alayhis Salaam) hadi Saa itakapoanza. Hii ni kwa sababu ya miujiza mitukufu ambayo Allaah Atamuumba pamoja naye, ambayo itazifanya akili za watu kupigwa na butwaa na kuishangaa.

 

 

Imesimuliwa kwamba atakuwa na pepo na moto pamoja naye, lakini pepo yake itakuwa ni moto na moto wake utakuwa ni pepo. Atakuwa na mito ya maji na milima ya mkate. Ataiamuru mbingu kushusha mvua, na itanyesha, na ataiamuru ardhi kuchipua mimea nayo itatii. Hazina za ardhi zitafuatana pamoja naye, na atatembea kwa kasi, kama vile mawingu yanavyopeperushwa na upepo. Na atafanya matendo mengi makubwa mno. Yote hayo yametajwa ndani ya Hadiyth zilizo sahihi. Imaam Muslim amepokea ndani ya kitabu chake Swahiyhu Muslim kwamba Hudhayfah (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:  “Dajjaal atakuwa na jicho moja, pofu kwa upande wake wa kushoto, na atakuwa na nywele nyembamba. Atakuwa na pepo na moto pamoja naye, lakini pepo yake itakuwa ni moto na moto wake utakuwa ni pepo.” [Muslim].

 

 

Muslim pia amepokea kwamba Hudhayfah (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Ninajuwa ni kipi ambacho Dajjaal atakuja nacho pamoja naye: atakuwa na mito miwili yenye kututurika (maji). Mmoja utaonekana kwa uwazi kama ni maji na mwengine utaonekana wazi kama ni moto uwakao. Iwapo yeyote kati yenu atayaona hayo, basi na achague mto wenye kuonekana kama ni moto, kisha mwaachie afumbe macho yake na ainamishe kichwa chake na anywe kutoka humo, kwani utakuwa ni (wenye) maji baridi.” [Muslim].

 

 

Ndani ya Hadiyth ya an-Nawwaas bin Sam’aan kuhusu Dajjaal, imesimuliwa kwamba Swahaabah ameuliza: “Ee Rasuli wa Allaah, ni kwa muda gani atakaa ardhini?” Alisema: “Siku arobaini: siku moja kama ni mwaka, siku moja kama ni mwezi, siku moja kama ni wiki, na siku zilizobaki kama ni siku zenu...” Waliuliza: “Ni kwa kasi gani atatembea ardhini?” Alisema: “Kama mawingu yanavyopeperushwa na upepo. Atakuja kwa baadhi ya watu na kuwalingania, na watamuamini na kumkubalia. Kisha ataiamuru mbingu kunyesha mvua, na ardhi kuchipua mimea, na ng’ombe wao watarejea kwao jioni, vinundu vyao vikiwa ni virefu, na viwele vyao vimejaa maziwa, na mbavu zao zimetanuliwa (kwa nyama). Kisha atakuja kwa watu wengine na kuwalingania, lakini watamkana. Hivyo atawaacha na watakumbana na ukame, wakiwa hawana mali yao yoyote mikoni mwao. Atapita (sehemu zenye) maangamizi na atasema: ‘Leteni hazina zenu!’ – na hazina zitamfuata kama ni bumba (kundi) la nyuki. Kisha atamuita mtu ambaye ni kijana madhubuti, na kumchoma panga na kumkata vipande viwili, kisha (ataviweka vipande mbali mbali) umbali wa mpigaji upindi na shabaha yake. Kisha atamuita, na kijana huyo atakuja mbele akiwa na tabasamu, mwenye uso unaong’ara.” [Muslim].

 

 

 

Al-Bukhaariy amepokea kutoka kwa Abu Sa’iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba mtu huyu ambaye Dajjaal atamuua atakuwa ni miongoni mwa watu [Waumini] bora, ambaye atatoka kwenda kwa Dajjaal kutoka mji wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na atasema kumwambia Dajjaal: ‘Ninashuhudia kwamba wewe ni Dajjaal ambaye Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuambia.’ Dajjaal atasema (kuwaambia watu): “Munaonaje iwapo nitamuua mtu huyu na kumrudisha akiwa hai, je mutakuwa na mushkeli wowote?” Watasema: “Hapana.” Hivyo atamuua, kisha kumrudisha kwenye uhai. Kisha (yule mtu aliyeamini) atasema: “(Naapa) Kwa Allaah, sijapata kuwa na uhakika zaidi kuhusiana na wewe kuliko nilivyo hivi leo.” Dajjaal atajaribu kumuua lakini hatoweza kufanya hivyo. [Al-Bukhaariy].

 

 

 

Kwa mujibu wa Hadiyth ya Umaamah al-Baahiliy (Radhiya Allaahu ‘anhu), Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema kuhusiana na Dajjaal:  “Sehemu ya fitnah yake ni kwamba atamwambia Bedui: ‘Je unafikiri kwamba iwapo nitamfufua baba na mama yako kwa ajili yako utanishuhudia kwamba mimi ni mola wako?’ Atasema: ‘Ndio.’ Hivyo majini mawili yatajitokeza kwake katika sura ya baba na mama yake, yakisema: ‘Ewe mwanangu, mfuate kwani yeye ndiye mola wako.” [Imepokewa na Ibn Maajah. Imethibitishwa usahihi wake na Shaykh Al-Albaaniy, Swahiyhul al-Jaami’ as-Swaghiyr].

 

 

 

Kinga Dhidi Ya Fitnah Za Dajjaal:

 

 

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameufunza Ummah wake kuhusiana na yale ambayo yatawakinga dhidi ya fitnah za Masiyh wa uongo (al-Masiyhud-Dajjaal). Ameuacha Ummah wake kwenye njia ambayo ipo wazi, na hakuna anayepotea nayo isipokuwa kwa yule aliyeangamia. Hakuacha kitu chochote kizuri bila ya kukitaja kwa Ummah wake, au ovu lolote bila ya kuwatahadharisha dhidi yake. Miongoni mwa vitu alivyotutahadharisha dhidi yake ni fitnah ya Dajjaal, kwa sababu ya fitnah yake kubwa ambayo Ummah utakutana nayo hadi Saa itakapofika. Kila Rasuli aliutahadharisha Ummah wake dhidi ya Dajjaal mwenye jicho moja, lakini Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa ni Rasuli pekee aliyeutahadharisha Ummah wake zaidi kuhusiana naye. Allaah Alimfahamisha (Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) sifa nyingi za Dajjaal ili apate kuwatahadharisha Ummah wake. Hakuna shaka yoyote Dajjaal atatokezea ndani ya Ummah huu, kwa sababu huu ndio Ummah wa mwisho, na Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ndiye hitimisho la Mitume.

 

 

 

Zinafuatia Baadhi Ya Miongozo Ambayo Nabiy Mteuzi (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam) Alizifafanua Kwa Ummah Wake Ili Kwamba Ujiepushe Dhidi Ya Fitnah Hii Kuu, Ambayo Tunamuomba Allaah Atukinge Na Atupatie Hifadhi:

 

 

(i) Kushikamana na Uislamu, kuwa na imani thabiti na kujifunza Majina na Sifa Nzuri zilizo Bora za Allaah Ambazo hazipatikani kwa mwengine yeyote. Mtu atambue kwamba Dajjaal atakuwa ni binaadamu aliye hai mwenye kula na kunywa, na kwamba Allaah Yupo mbali kabisa na hilo; Dajjaal atakuwa na jicho moja lakini Allaah Hana jicho moja; hakuna yeyote atakayemuona Mola wake hapa duniani hadi afariki, lakini Dajjaal atakapotokezea ataonekana na watu wote, Waumini na vivyo hivyo makafiri.

 

 

(ii) Kuomba hifadhi ya Allaah kutokana na fitnah za Dajjaal, haswa ndani ya Swalaah (maombi). Hii imesimuliwa ndani ya Hadiyth zilizo sahihi, kama vile iliyosimuliwa na Ummul-Muuminiin ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha), aliyesema kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiomba ndani ya Swalaah zake:

 

 

للّهُـمَّ إِنِّـي أَعـوذُ بِكَ مِـنْ عَذابِ القَـبْر، وَأَعـوذُ بِكَ مِـنْ فِتْـنَةِ المْسيحِ الدَّجّـال، وَأَعـوذُ بِكَ مِـنْ فِتْـنَةِ المْحْـيا وَالمْمـات. اللّهُـمَّ إِنِّـي أَعـوذُ بِكَ مِنَ المْأْثَـمِ وَالمْغْـرَم

 

Allaahumma inniy a’uwdhu Bika min ‘adhaabil qabri, wa a’uwdhu bika min fitnatil Masiyhid-dajaal wa a’uwdhu bika min fitnatil mahyaa wal mamaat, Allaahumma inniy a’uwdhu bika minal ma-athami wal maghrami

 

Ee Allaah!  Hakika mimi najikinga Kwako na adhabu ya kaburi, na najikinga Kwako na fitna ya Masihid-dajjaal, na najikinda Kwako na fitna ya uhai na (fitna) ya mauti, Ee Allaah, hakika mimi najikinda Kwako kutokana na dhambi na deni  [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

Na pia,

 

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:  “Pindipo mmoja wenu anaposoma Tashahhud, basi na aombe hifadhi ya Allaah kwenye mambo manne, na aseme:  

 

للّهُـمَّ إِنِّـي أَعـوذُ بِكَ مِـنْ عَذابِ القَـبْر، وَمِـنْ عَذابِ جَهَـنَّم، وَمِـنْ فِتْـنَةِ المَحْـيا وَالمَمـات، وَمِـنْ شَـرِّ فِتْـنَةِ المَسيحِ الدَّجّال

Allaahumma inniy a’uwdhu Bika min ‘adhaabil qabri, wa min ‘adhaabi jahannam, wamin fitnatil mahyaa wal mamaati, wamin sharri fitnatil-Masiyhid-dajjaal

 

Ee Allaah hakika mimi najikinga Kwako na adhabu za kaburi, na adhabu ya Jahannam, na fitna ya uhai, na (fitna) ya kufa, na shari ya fitna ya Masihi-dajja [al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

 

(iii) Kuhifadhi Aayah kutoka Suuraatul-Kahf. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuhimiza kuzisoma Aayah za mwanzo za Suuratul-Kahf dhidi ya Dajjaal. Kwa mujibu wa baadhi ya simulizi, Aayah za mwisho za Suurah hii zimetajwa. Hii inamaanisha kwamba kusoma Aayah kumi za mwanzo au kumi za mwisho. Miongoni mwa Hadiyth zilizosimulia kuhusiana na hili ni Hadiyth refu iliyopokewa na Muslim kutoka kwa an-Nawwaas bin Sam’aan, ambayo amesema:  “Yeyote miongoni mwenu anayemuona (Dajjaal), basi na asome Aayah za mwanzo za Suuratul-Kahf.”

 

 

 

Muslim amepokea kutoka kwa Abud-Dardaa kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:  “Yeyote anayehifadhi aayah kumi za mwanzo za Suuratul-Kahf atakingwa kutokana na Dajjaal” –  yaani kutokana na fitnah zake. Muslim amesema: “Shu’bah amesema: ‘kutoka mwisho wa al-Kahf.’ Hammaam amesema: ‘kutoka mwanzoni mwa al-Kahf.’” [Muslim]

 

An-Nawawiy amesema: “Hoja ya hili ni kwa sababu mwanzoni (mwa Suurah hii), kumetajwa maajabu na alama, na yeyote anayezikubali, hatahadaiwa na fitnah za Dajjaal. Na mwishoni mwa Suurah, Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema (maana ya maneno):

 

أَفَحَسِبَ الَّذِينَ كَفَرُوا أَن يَتَّخِذُوا عِبَادِي مِن دُونِي أَوْلِيَاءَ ۚ إِنَّا أَعْتَدْنَا جَهَنَّمَ لِلْكَافِرِينَ نُزُلًا ﴿١٠٢﴾

Je, wanadhania wale waliokufuru kwamba wanaweza kuchukua waja Wangu kuwa walinzi badala Yangu? Hakika Sisi Tumeandaa Jahannam kwa ajili ya makafiri kuwa mahala pa kuteremkia. [Suwrah Al-Kahf: 102 – Hadiyth imerekodiwa katika Sharh Muslim (6/93)]

 

 

 

Hii ni moja ya sifa muhimu za Suuratul-Kahf. Kuna Hadiyth ambazo zinahimiza kuisoma, haswa siku za Ijumaa. Al-Haakim amepokea kutoka kwa Abu Sa’iydul-Khudriy (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: 

“Yeyote anayeisoma Suuratul-Kahf siku ya Ijumaa, itakuwa ni mwangaza kwake kutoka Ijumaa moja hadi nyengine.” [Al-Mustadrak, 2/368. Imesahihishwa na al-Albaaniy kwenye Swahiyhul-Jaami’ as-Swaghiyr].

 

 

 

Hakuna shaka yoyote kwamba Suuratul-Kahf ina umuhimu mkubwa, yenye Aayah bora, kama vile kisa cha Watu wa Pango, kisa cha Muusa na al-Khidhr, na kisa cha Dhul-Qarnayn na kujenga kwake ukuta kuwazuia Ya’juuj na Ma’juuj, ushahidi wa kufufuliwa na kupulizwa Baragumu, na maelezo ya wale ambao matendo yao ni maovu zaidi, wale ambao walidhani kwamba wameongoka ingawa ukweli ni wapotofu na vipofu.

 

Kila Muislamu atie himma ya kuisoma Suurah hii, na kuihifadhi na kuikariri kuisoma, haswa siku bora ambayo jua linachomoza (Magharibi), nayo ni Ijumaa.

 

 

(iv) Kumkimbia Dajjaal na kujiweka mbali naye. Njia bora ni kuishi Makkah na Madiynah, na sehemu ambazo Dajjaal hatoingia. Pale Dajjaal atakapotokezea, Waislamu wajiweke mbali sana naye, kwa sababu atasababisha wasiwasi (kutokana) na maajabu makubwa atakayokuwa nayo, ambayo Allaah Atajaalia yafanyike kwenye mikono yake ili kuwajaribu wanaadamu. Kuna mtu atakuja kwake, akidhani kwamba yeye ni Muumini madhubuti, kisha (hatimaye) atamfuata Dajjaal. Tunamuomba Allaah Atupe sisi na Waislamu wote hifadhi kutokana na fitnah hii.

 

 

Kutoka kwa ‘Imraan bin Huswayn (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:  “Yeyote anayemsikia Dajjaal, basi na ajiweke mbali naye, kwani (itafikia) mtu atamjia (Dajjaal) na kudhani kwamba yeye (Dajaal) anasema ukweli kwa sababu ya maajabu yaliyofikishwa kwake.” [Imaam Ahmad, Abu Daawuud na al-Haakim]

 

 

Kifo Cha Dajjaal:

 

Dajjaal atafariki mikononi mwa Masiyh ‘Iysaa bin Maryam ('Alayhis Salaam), kama ilivyooneshwa ndani ya Hadiyth Swahiyh. Dajjaal atatokezea ardhini na atawakumba wafuasi wengi, akisambaza fitnah zake kwa mapana na marefu. Hakuna mtu atakayekimbia fitnah yake isipokuwa wachache miongoni mwa Waumimi. Kwa hatua hiyo, ‘Iysaa bin Maryam ('Alayhis Salaam) atashuka katika mashariki ya mnara wa Damascus, na waja Waumini wa Allaah watamzungukia. Atawaongoza kwa Dajjaal, (Dajjaal) ambaye wakati anaposhuka ‘Iysaa ('Alayhis Salaam) atakuwa anaelekea Baytul-Maqdis (Jerusalem). ‘Iysaa ('Alayhis Salaam)  atakutakana naye katika lango la Ludd (Lod), sehemu iliyomo ndani ya Palestine karibu na Baytul-Maqdis. Pale Dajjaal atakapomuona, ataanza kuyayuka kama vile chumvi inavyoyayuka ndani ya maji. Lakini ‘Iysaa ('Alayhis Salaam) atasema kumwambia: “Nina kazi na wewe, hutonikimbia.” Kisha atapambana naye na kumuua kwa ala yake. Wafuasi wake (Dajjaal) watakimbia, (hata hivyo) watakimbizwa na Waislamu, ambao watawaua, na miti na mawe yatasema, ‘Ewe Muislamu, Ewe mja wa Allaah, kuna Yahudi nyuma yangu – njoo na umuue!’ – (wataweza kujificha) mbali ya (mti wa) gharqad (miashoka), kwani ni mmoja kati ya miti ya Mayahudi.

 

 

 

Zinafuatia Baadhi Ya Hadiyth Zilizopokewa Kuhusu Kifo Cha Dajjaal Na Wafuasi Wake:

 

Muslim amepokea kwamba ‘AbduLlaah bin ‘Amr (Radhiya Allaahu ‘anhuma) amesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:  “Dajjaal atatokezea miongoni mwa Ummah wangu na atakaa kwa siku arobaini... Kisha Allaah Atamleta ‘Iysaa bin Maryam, anayeonekana kama ‘Urwah bin Mas’uud, na atapambana naye na kumuua.” [Muslim]

 

 

Imaam Ahmad na at-Tirmidhiy wamesimulia kwamba Majma’ bin Jaariyah al-Answaariy (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema: Nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:  “Mwana wa Maryam atamuua Dajjaal langoni mwa Ludd.” [Ahmad, At-Tirmidhiy]

 

 

Muslim amepokea katika Hadiyth refu kutoka kwa an-Nawwaas bin Sam’aan (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuhusu Dajjaal, ambayo kuna kisa cha kushuka kwa ‘Iysaa na kumuua kwake Dajjaal kinatajwa. Ndani ya Hadiyth hii Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “... Kila kaafir atakayenusa harufu ya (‘Iysaa ['Alayhis Salaam]) atakufa, na harufu yake itasambaa umbali wa namna atakavyoweza kuona. Kisha atamtafuta (Dajjaal) hadi atamkuta kwenye lango la Ludd, ambapo atamuua.” [Muslim]

 

 

Imaam Ahmad amepokea kwamba Jaabir bin ‘AbdiLlaah (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:  “Dajjaal atatokezea enzi ambazo utiifu wa Diyn ni wa chini na elimu imepungua... Kisha ‘Iysaa bin Maryam atashuka kabla ya mawio na kuwaita watu, akisema: “Enyi watu, ni kipi kinachowazuia kutoka na kupambana dhidi ya muovu huyu muongo?” Watasema, ‘Mtu huyu ni jini’, kisha wataondoka. Pale watakapokutana na ‘Iysaa bin Maryam, muda wa Swalaah ukawadia na iqaamah ikakimiwa, na itasemwa kwake: ‘Nenda mbele (kuongoza Swalaah) Ewe Roho ya Allaah.’ Atasema: “Muacheni Imaam wenu aende mbele na kuwaongozeni katika Swalaah.” Watakapomaliza kuswali alfajiri, watatoka kwenda kukutana naye (Dajjaal) na watamuona muongo (mkubwa), ataanza kuyeyuka kama chumvi ndani ya maji. ‘Iysaa atapambana naye na kumuua. Hadi miti na mawe yataita: ‘Ewe Roho ya Allaah, hapa kuna Yahudi!’ Na hakuna yeyote mwenye kumfuata yeye (Dajjaal) atakayebaki, wote watauliwa.” [Ahmad]

 

 

Pale (Dajjaal – laana za Allaah ziwe juu yake) atakapouliwa, fitnah yake zitafikia kikomo. Allaah Atawaokoa wale walioamini kutokana na uovu wake na kutokana na uovu wa wafuasi wake, katika mikono ya Roho na Neno la Allaah: ‘Iysaa bin Maryam ('Alayhis Salaam) na wafuasi wake Waumini.

 

 

Shukrani na Rahmah zote ni za Allaah.

 

 

 

 

 

Share