Allaah Hushuka Kwenye Mbingu Ya Dunia Theluthi Ya Mwisho Ya Usiku

 

www.alhidaaya.com

 

Imaam Maalik anaeleza kuhusu kushuka kwa Allaah jwa maelezo yenye vipengele vinne:

1.     Kushuka ni jambo lenye kufahamika vizuri.

2.     Namna halisi ya kushuka kwa Allaah haijulikani kwetu.

3.     Imani ya jambo hilo ni jambo la Waajib.

4.     Kutafuta undani wake ni hambo la uzushi (bid’ah).

 

Shaykh Al-Islaam Ibn Taymiyyah amezungumzia maelezo kwa kirefu -kuhusu shubuhaat za watu wa Jahmiyyah- kwenye kitabu chake “Sharh Hadiyth an-Nuzuul” karibu na mwisho wa kitabu hicho (uk. 320 na kuendelea mbele) na katika msingi wa jambo hili ni kuwa swali kama hilo huja pale wakati mtu anapofikiria na kuoanisha namna au aina ya kushuka kwa Allaah na kuufananisha na kule kushuka au kuteremka kiumbe. Na wakati mtu anapoanza kufikiria hivyo ndipo mashaka na utata unapoanza. Kama alivyosema Imaam Maalik kuhusiana na Istiwaa (kuwa kwa Allaah juu ya ‘Arsh) na alivyosema Abu Ja’afar At-Tirmidhiy (Faqiyh wa Baghdaad) kama alivyonukuliwa na Imaam Adh-Dhahabiy katika ‘Al-‘Uluww’ (uk. 231), kuhusiana na ‘kushuka’:

“Kushuka (nuzuul) ni jambo lenye kufahamika (ma’aquul), na namna yake (kayf) haifahamiki (majhuul), na kuamini jambo hilo ni Waajib, na kuliulizia ni uzushi (bid’ah).”

 

Na kifupi, tunajua ya kwamba:

- Allaah huteremka bila ya kuondoka kutoka kwenye ‘Arshi, yeye hubakia juu ya ‘Arshi.

- Allaah huteremka bila ya kuwa chini ya pepo zake, kama watangu wema waliotangulia (Salaf) mbele ya Allaah waliwaambia Majahmiyyah waliotilia shaka jambo hili la Allaah kuteremka:

“Tunamuamini Mola ambaye Anafanya Atakalo.”

- Kwa watu wote ulimwenguni na pembe zote za dunia, juu ya kuwa na tafauti za masaa mchana na usiku, kuteremka kwa Allaah ni katika robo ya tatu ya usiku wao na hatuwezi kujua jambo hili Allaah Analifanya vipi -kama ambavyo hatujui namna Allaah Atawafanyia hesabu wanaadamu wote siku ya Qiyaamah kwa wakati mmoja.

 

Ibn Taymiyyah akasema tena:

“Ama huko kuteremka kwa Allaah si kama kuteremka kwa waja wa Allaah yaani binaadamu, kwa hivyo si kwamba haiwezekani kwa Allaah kufanyika hilo (la kushuka) kwa wakati mmoja kwa viumbe wengi… na hili ni kama vile wakati wa Hesabu Atakapowahesabia waja Wake Siku ya Hesabu. Atawahesabia wote kwa muda na wakati mmoja, na wote watakuwa pekee na Yeye tu, kama ambavyo mtu anapokuwa mwenyewe pekee na mwezi katika usiku unaong’aa, na Atathibitisha Aayah Zake, na kila mmoja atakapokuwa anafanyiwa Hesabu, mwenziwe aliye pembeni yake hatojua hilo. [uk. 334].

 

Kisha Ibn Taymiyyah akatoa Hadiyth kadhaa kuhusiana na hilo, mojawapo ni Hadiyth inayozungumzia Allaah Anapomjibu mja Wake pale anaposoma Suratul Faatihah akiwa katika Swalah. Allaah Anasema, “Mja Wangu ananisifu Mimi’’ na kuendelea… na jambo hili ni kwa kila mtu ambaye yuko kwenye Swalah (Allaah Anamjibu), kwa wakati mmoja, na hivyo ndivyo Allaah Anawaona watu wote kwa mara moja na akawakidhia haja zao wote  kwa mara moja. Na ndio hivyo hivyo hali ya kushuka Kwake Allaah -basi ikiwa tutaondosha ile shaka ya vipi (namna) Allaah huteremka ambayo tumekatazwa nayo, nayo ni ile ya kutaka kufananisha ushukaji Wake Allaah na ule ushukaji au uteremkaji wa kiumbe- basi tutakuwa hatuna tena shaka ya kuteremka huko kwa Allaah hivyo tutakuwa tumethibitisha bila ya tashbiyh wala tamthiyl na bila ya shaka yoyote  juu ya hilo.

 

Na yote haya yanamtosheleza Mu-umin ambaye amezikubali sifa zote za Allaah Alizojipa mwenyewe Allaah bila takyiif wala ta’atwiyl wala tamthiyl.

 

Hapa Tutaona Athar Ya Imaam Maalik (Rahimahu Allaah) Kuhusiana Na Haya

Ametuhadithia Yahya bin Yahya At-Tamiymiy na Ja’afar bin ‘Abdillaah na wengine miongoni mwao walisema:

Tulikuwa pamoja na Imaam Maalik akatokea mtu mmoja akamuuliza? Ewe Aba-Abdillaah! Allaah aliyetukuka ‘Istawaa’ (yuko juu) kwenye ‘Arshi Yake (kwa namna inayolingana na Utukufu Wake Yeye mwenyewe Allaah) (Twaahaa 20: 5). Je, vipi Yeye Allaah Amestawi ‘Istawaa’? Imaam Maalik aliinamisha kichwa chake chini kwa muda mrefu mpaka akalowa na jasho. Kisha akasema:

 “Al-Istiwaa (kuwa Kwake juu ya ‘Arshi) ni jambo ma’aquul (linajulikana); ‘Vipi’ ni majhuul (hakujulikani/hakuwaziki); na kuamini hilo ni Waajib (lazima); na kuuliza au kuhoji hilo ni bid’ah (uzushi); na nina hofu kuwa wewe si zaidi ila mzushi.” Kisha akaamrisha mtu huyo atolewe kwenye darsa lake.

[Shaykh Al-Albaaniy (Rahimahu Allaah) amesema Hadiyth hii ni sahihi.
(Tazama Mukhthasar Al-Uluww cha Imaam Adh-Dhahabiy (Rahimahu ALlaah) iliyopitiwa na Shaykh Naaswir (Rahimahu Allaah). Uk. 131]

 

 

 

Yafuatayo Ni Maelezo Kutoka Kitabu ‘Kitaabul ‘Ilm Cha Shaykh Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahu Allaah) Uk. 47-48

 

“Mola wetu huteremka mpaka wingu wa kwanza katika kila robo tatu ya usiku na husema, “Ni nani ananiita Nimuitike wito wake? Nani anayenihitaji kwa haja Nimkidhie haja yake? Nani anayenitaka msamaha Nimsamehe”. [Al-Bukhaariy].

 

Hadiyth hii ilisimuliwa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na inajulikana wazi. Hakuna katika Maswahaba wake Mtume hata mmoja aliyehoji au kuleta kipingamizi kwa kumwambia Mtume. “Vipi Allaah huteremka na je huacha ‘Arshi Yake au hapana? Na wala hakukuwa na maswali mfano wa hayo kutoka kwa Maswahaba. Hata hivyo, tunaona watu wakizungumza na kuuliza maswali kama, “Iweje Yuko juu ya ‘Arshi na kisha tena Ashuke chini kwenye mbingu ya chini kabisa? Na maswali ya upinzani mfano wa hilo! Lakini hapo hapo utawaona watu hao wakiwa wanaikubali Hadiyth hiyo na wanakubali kuwa Allaah Yuko juu ya ‘Arsh, na kupanda au kuwa juu ni kule kunakolingana na Utukufu Wake, na hushuka Yeye (Aliyetukuka) Anavyotaka mwenyewe, na hayo yanavunja na kuondosha mashaka yao ambayo yanawachanganya na kuwatatiza kwa yale ambayo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amewafahamisha wao kumhusu Mola wao.

 

Kwa hivyo ndugu Muislamu ni wajibu wetu kukubali yale Allaah (Taa’ala) na mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) waliyotujulisha nayo yanayotokana na yale tusiyokuwa na ujuzi nayo (Ghayb) kwa moyo wetu wote na kuyatii kikamilifu, na kisha tusiwe ni wenye kupinga kwa kuendekeza yale ya kutokana na akili zetu yaliyotawaliwa na hisia zetu na ufahamu wetu wa kifalsafa. Kwani mas-alah ya Ghayb, yako mbali na upeo wa fahamu zetu. Na mifano kuhusiana na haya ni mingi, na sihitajii kurefusha kuitaja.

 

Kwa nafasi ya Mu-umin anapoletewa Hadiyth kama hii ni kuikubali kikamilifu kwa kusema Allaah na Mtume Wake wamesema kweli, kama Allaah Alivyosema:

آمَنَ الرَّسُولُ بِمَا أُنزِلَ إِلَيْهِ مِن رَّبِّهِ وَالْمُؤْمِنُونَ ۚ كُلٌّ آمَنَ بِاللَّـهِ وَمَلَائِكَتِهِ وَكُتُبِهِ وَرُسُلِهِ لَا نُفَرِّقُ بَيْنَ أَحَدٍ مِّن رُّسُلِهِ ۚ وَقَالُوا سَمِعْنَا وَأَطَعْنَا ۖ غُفْرَانَكَ رَبَّنَا وَإِلَيْكَ الْمَصِيرُ ﴿٢٨٥﴾

 

“Mtume ameamini yaliyoteremshwa kwake kutoka kwa Mola wake, na Waumini vile vile. Wote wamemuamini Allaah, na Malaika Wake, na Vitabu Vyake na Mitume Wake. Hatutofautishi baina ya yeyote katika Mitume Wake, na (Waumini) husema: Tumesikia na tumetii. Tunakutaka maghfira Mola wetu! Na marejeo ni kwako.” [Suratul Baqarah 2: 285].

 

Share