‘Aqiydah Ya Imaam Sufyaan Ath-Thawriy (Aliyefariki 161H)

Isnadi Ya ‘Aqiydah Hii

1 - Muhammad bin ‘Abdir-Rahmaan bin al-’Abbaas bin Abdir-Rahmaan Abu Tahiyr al-Baghdadiy al-Mukhallas. Ni Shaykh, na Muhaddith, ni mwandamizi na mkweli. Khatwiyb alisema: “Ni mwaminifu.” Adh-Dhahabiy amesema: “Hii (‘Aqiydah) imehakikishwa kutoka kwa Sufyaan na Shaykh al-Mukhallas ni mwaminifu (Allaah Awarehemu wote)” [Tadhkiratul-Huffaadh, 1/206- 207].

Alizaliwa Shawwal mwaka wa 305H na alifariki katika Ramadhaan mwaka wa 393H. [Adh-Dhahabiy, Siyar A’laam an-Nubalaa, 16/478-480; Taarikh Baghdaad, 2/322-323; Shadharaatudh-Dhahab, 3/144]

2 - Shu’ayb bin Muhammad bin Rajiyan. Adh-Dhahabiy alimtangaza kuwa ni mtu mwaminifu. [Tadhkirah, 1/207]

3 – ‘Aliy bin Harb al-Mawsiliy, Abu’l-Hasan: Imaam, na muhaddiyth, mwenye kuaminika na mjuzi. Alizaliwa katika mwaka wa 175H. Abu Hatiym amesema: “Ni mkweli.” Daraqutniy alisema: ‘‘Ni mwenye kuaminika” Alifariki katika mwaka 265H [Adh-Dhahabiy, Siyar A’laam an-Nubalaa, 12/251-253, al-Jarh wat-Ta’diyl, 6/183, Taariykh Baghdaad, 11/418-420; Twabaqaat al-Hanabilah, 1/223; Shadharaatudh-Dhahab, 2/150]

4 - Shu’ayb bin Harb: Imaam, kiigizo bora, mcha Mungu, ni Shaykh wa Uislamu, Abu Swaalih al-Mada’ini. An-Nasaaiy amesema: “Muaminifu.”, Na Ibn Ma’iyn na Abu Haatim wamesema: “Mkweli na mwenye kuaminika” Alifariki katika mwaka wa 196H inasemekana pia katika mwaka wa 197H (Allaah Amrehemu). [Adh-Dhahabiy, As-Siyar, 9/188-191; Twabaqaat Ibn Sa’ad, 7/320, al-Jarh, 4/342, Al-Miyzaan, 2/275; Tahdhiyb at-Tahdhiyb, 4/350; Shadharaatudh-Dhahab, 1/349]

 

Matini (Maandiko) Ya ‘Aqiydah Hii

Muhammad bin ‘Abdir-Rahmaan bin al-’Abbaas alitueleza akisema: “Abul-Fadhl bin Muhammad bin Shu’ayb Rajiyaan amesema: “‘Aliy bin Harb al-Mawsiliy alituhadithia - katika mwaka wa 257H- akisema: “Mimi nimemsikia Shu’ayb bin Harb akisema:

 

Nilimwambia Abu ‘Abdillaah Sufyaan bin Sa’id ath-Thawriy: “Nisimulie Hadiyth kutoka katika Sunnah ambayo Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Atanifaidisha nayo, ili wakati nitasimama mbele ya Allaah (Jalla Jalaaluh) na Akaniuliza kuhusiana nayo (hiyo Hadiyth), Akisema: ‘‘Kutoka wapi umepata hii Hadiyth?

 

Mimi nitasema: ‘‘Ee Mola wangu, Sufyaan ath-Thawriy ndiye aliyenisimulia Hadiyth hii na mimi niliichukua kutoka kwake.

Hivyo basi mimi nitaokolewa na (kisha) wewe uulizwe hiyo Hadiyth.

Hivyo Sufyaan akasema: ‘‘Ewe Shu’ayb, ama kweli hii ni dhamana na dhamana gani kama hii?

Andika:

Kwa jina la Allaah, Mwingi wa Rehma mwenye kurehemu.

Qur-aan ni maneno ya Allaah. Haikuumbwa. Ni asili kutoka Kwake na Kwake Yeye ndiko itarudi. Yeyote yule asemae zaidi ya haya ni kafiri.

Na Iymaan [ya Muislamu] inasadikishwa kwa maneno, matendo na Niyah. Inaongezeka na kupungua. Inaongezeka kwa vitendo vya utiifu na inapungua kwa matendo ya maovu. Hakuna maneno yanayokubaliwa ila mpaka yaambatane na vitendo, na hakuna vitendo vinavyokubaliwa ila mpaka viambatane na Niyah (nzuri), na hakuna Niyah ispokuwa ikiwa itaafikiana na Sunnah.

 

Shu’ayb akasema: ‘‘Ewe Abu ‘Abdillaah, ni kipi kiafikianacho na Sunnah?

Akasema: “Kuwapa kipaumbele Mashaykh wawili: Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) na ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu).

 

Ewe Shu’ayb uliyoandika hayatokuwa na faida kwako mpaka umuweke ‘Uthmaan (Radhiya Allaahu ‘anhu) na ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) mbele ya wale waliokuja baada yao.

 

Ewe Shu’ayb bin Harb, uliyoandika mwenyewe hayatokuwa na faida kwako mpaka ushuhudie kwa watu wote kwamba wao ni wa Peponi au motoni, wameokolewa watu kumi kutokana na ambavyo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alivyoshuhudia, na wote ni kutoka kabila la Quraysh.

 

Ewe Shu’ayb bin Harb, uliyoandika mwenyewe hayatokuwa na faida kwako mpaka ushikilie kwamba kupangusa juu ya khuffayn (soksi za ngozi) ni bora kwako kuliko kuzivua wakati unaosha miguu.

 

Ewe Shu’ayb uliyoandika hayatokuwa na faida kwako mpaka uwe ni mwenye kusema “BismiLlaahi Rahmaaniyr-Rahiym” kimya (kwa sauti hafifu) katika Swalah, kufanya hivyo ni bora zaidi kwako kuliko kuisema kwa sauti.

 

Ewe Shu’ayb bin Harb, uliyoandika hayatokuwa na faida kwako mpaka uwe mwenye kuamini Qadar (Matakwa ya Allaah), mema na mabaya, matamu yake na machungu yake. Yote [yatayokukuta] ni kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala).

Ewe Shu’ayb bin Harb, Ninaapa kwa Allaah wasemayo Qadariyyah siyo kabisa Asemayo Allaah, au wasemayo Malaika, au wasemayo Mitume, au wasemayo watu wa Peponi na wa Motoni, au asemayo ndugu yao (Qadariyyah), Ibliys (Allaah Amlaani).

 

 

Allaah (‘Azza wa Jalla) Anasema:

Je! Umemwona aliyefanya matamanio yake kuwa ndiye mungu wake, na Allaah Akamwacha apotee pamoja na kuwa ana ujuzi, na akapiga muhuri juu ya masikio yake, na moyo wake, na akambandika vitanga machoni mwake? Basi nani atamwongoa huyo baada ya Allaah? Hamkumbuki?’’ [Al-Jaathiyah 45: 23]

 

Na (Jalla Jalaaluh) Anasema tena:

“Wala nyinyi hamtataka isipokuwa atake Allaah Mola wa walimwengu wote” [At-Takwiyr 81: 29]

 

Na Malaika walisema:

“Wakasema: Subhanaaka, Wewe umetakasika! Hatuna ujuzi isipokuwa kwa uliyo tufunza Wewe. Hakika Wewe ndiye Mjuzi Mwenye hikima.” [Al-Baqarah 2: 32]

 

Na Muusa (‘Alayhis Salaam) alisema:

“umpoteze umtakaye na umhidi umtakaye” [Al-A’araaf 7: 155]

 

Na Nuuh (‘Alayhis Salaam) alisema:

“Wala nasaha yangu haikufaini kitu nikitaka kukunasihini, ikiwa Allaah Anataka kukuachieni mpotee. Yeye ndiye Mola wenu; na kwake mtarejeshwa” [Huud 11: 34]

 

Na Shu’ayb (‘Alayhis Salaam) alisema:

“Wala haiwi kwetu sisi kuirejea mila hiyo, ila akitaka Allaah, Mola wetu. Ujuzi wa Mola wetu umeenea katika kila kitu.” [Al-A’araaf 7: 89]

 

Na watu wa Peponi watasema:

“AlhamduliLlaah! Kuhimidiwani kwa Allaah, ambaye Aliyetuhidi kufikia haya. Wala hatukuwa wenye kuhidika wenyewe ingelikuwa Allaah hakutuhidi.” (Al-A’araaf 7: 43)

 

Na watu wa Motoni watasema:

“Mola wetu! Tulizidiwa na uovu wetu na tukawa watu tuliopotea” [Mu-minuun 23: 106]

 

Na ndugu yao, Ibliys akasema:

“Akasema: Mola wangu! Ilivyo kuwa umenitia makosani, basi nahakikisha nitawazaini hapa duniani na nitawapoteza wote,” (Al-Hijr 15: 39)

Ewe Shu’ayb, uliyoandika hayatokuwa na faida kwako mpaka ushikilie kuwa: Swalah inaswaliwa nyuma ya kila mtu mwema au mtu mwenye dhambi; ushikilie kuwa Jihaad itakuwepo mpaka siku ya Qiyaamah; ushikilie kuwa uvumilivu ni kitu muhimu sana chini ya bendera ya (yaani chini ya uongozi) wa mtawala sawa akiwa ni mtu dhalimu au mwema.

Shu’ayb akasema: “Kwa hiyo nikamwambia Sufyaan: Ewe Abu Abu ‘Abdillaah, ni katika Swalah zote?

Akasema:

“Hapana, ni Swalah ya Ijumaa na Swalah ya ‘Iyd mbili. Swali Swalah hizi nyuma ya mtu yeyote utakayemkuta. Lakini katika Swalah zingine zote (yaani za faradhi) uko na hiari katika jambo hilo. Usiswali nyuma ya yeyote ila tu yule ambaye unamuamini na ambaye unamjua vizuri ni katika Ahlus Sunnah Wal Jama’aah.

 

Ewe Shu’ayb bin Harb, wakati utakaposimama mbele ya Allaah (‘Azza wa Jalla) na Akakuuliza juu ya hii Hadiyth, basi sema:

 

“Mola wangu, Sufyaan bin Sa’iyd ath-Thawriy ndiye aliyenihadithia hii Hadiyth, kisha mimi nitajenga urafiki kati yangu mimi na Mola wangu (Subhaanahu wa Ta’ala). [al-Lalika’iy, Sharh Usuul I’tiqaad Ahlis-Sunnah Wal Jama’ah, 1/151-154. Adh-Dhahabiy, Tadhkiratul-Huffaadh, 1/206-207]

 

Tanbihi

1 - Imaam Atw-Twabariy alisema:

“Qur-aan ni maneno ya Allaah na tanzil yake (yaani ufunuo wake), haikuumbwa katika hali yoyote inaweza kuwa imeandikwa au wakati ilipokuwa ikisomwa, katika mahali popote inaposomwa, kama jinsi ilivyopatikana katika mbingu au juu ya ardhi, hata hivyo inaweza kuwa imehifadhiwa kama ilivyoandikwa katika Lawhul-Mahfuudh au katika nakala za watoto wa shule za Qur-aan, au ilipoandikwa juu ya jiwe na kuandikwa juu ya karatasi au majani, kama kuihifadhi katika moyo, au kusemwa na ulimi. Yeyote yule atakayesema kinyume na haya, au akadai kuwa Qur-aan ambayo tunaisoma na ndimi zetu, na ambayo tumeandika katika Msahafu, au ambaye ataamini katika moyo wake au ambaye ataficha aina ya imani kama hiyo katika moyo wake, au ambaye atakiri kwa ulimi wake, basi yeye ni kafiri ambaye damu na mali yake ni halali na ambaye atakuwa mbali na Allaah na Allaah yuko mbali naye.” [Atw-Twabariy, Sarihus-Sunnah, 24-25].

 

Ibn ‘Abbaas (Radhi za Allaah zimshukie) kasema (kuhusiana na Aayah):

“Qur-aan ya Kiarabu isiyo na upogo, ili wamche Mungu.” (Az-Zumar 39: 28): “Haikuumbwa”. (Sharh Usuulul-I’tiqaad, 2/217)

 

Al-Laalikaiy alisema:

“Sa’iyd bin Naswiyr alisema: Nilimsikia Ibn Uyaynah akisema: Nini ambacho huyu dawih (Bishr al-Marisi) anachosema “Ewe Abu Muhammad bin Abu Imraan, (anasema) Qur-aan imeumbwa?: Akajibu: amedanganya. Allaah (‘Azza Wa Jalla) Anasema:

“Fahamuni! Kuumba na amri ni Zake” [Al-A’araaf 7/54)

Kwa hiyo “viumbe” ni uumbaji wa Allaah, na amri ndiyo Qur-aan.

 

Na Imaam Ahmad bin Hanbal na Nu’aym bin Hammaad, Muhammad bin Yahya ad-Dihli, ‘Abdus-Salaam ‘Aaswim bin ar-Raaziy, Ahmad bin Sin’aan al-Waasitwiy na Abu Haatim ar-Raaziy wamesema vivyo hivyo.” [Sharh Usuul I’tiqaad 2/219]

 

‘Aliy bin al-Hasan al-Haashimiy alisema:

“Mjomba wangu alinihadithia: Nilimsikia Waki bin al-Jarrah akisema: Mtu yeyote atakaedai kuwa Qur-aan imeumbwa basi atakuwa amedai kuwa kitu kutoka kwa Allaah kimeumbwa. Hivyo nikamwambia:

Ewe Abu Sufyaan, unasemaje hili? Akasema: “Kwa sababu Allaah (‘Azza wa Jalla) Anasema: “Lakini imekwisha kuwa kauli iliyotoka kwangu...” [As-Sajdah 32: 13] hakuna kitu cha Allaah ambacho kimeumbwa” [Sharh Usuul I’tiqaad 2/219] Habari zaidi kuhusu mada hii inaweza kupatikana kutoka katika vitabu hivi:

 

As-Sunnah cha Imaam ‘Abdullaah, 2/18; Sharh Usuulul-I’tiqaad, 2/216, 3/378-385; Sarihus-Sunnah cha Imaam Atw-Twabariy,, 24-29; Al-Hujjah cha Asbahaaniy,, 1/334-359, 2/198; Ash-Shari’ah cha Al-Ajuurriy, 75-96, al-Asmaa was-Swifaat cha Al-Bayhaqiy, 1/299- 422; Sharhu Atw-Twahaawiyyah, 107-127.
 

2 – Imaan inajumuishwa na maneno na vitendo na kupungua na kuongezeka kwake ni moja ya mambo ambayo ummah umekubaliana kwalo. [Atw-Twabariy, Sarihus-Sunnah, 42-45; Al-Ajuurriy, Ash-Shari’ah, 103-118; Ibn Abi ‘Aaswim, As-Sunnah, 449-451; Al-Laalikaiy, Sharh Usuulul-I’tiqaad, 4/830, 5/890-964, Al-Bayhaqiy, al-I’tiqaad, 174-185)

 

3 - Ummah umekubaliana kuwa mbora zaidi katika Maswahaba wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ni Asw-Swiyddiyq, Abu Bakr (Radhi za Allaah zimshukie), kisha Al-Faaruuq, ‘Umar bin al-Khattwaab (Radhi za Allaah zimshukie), kisha Dhun-Nuurayn (mwenye nuru mbili); ‘Uthmaan bin ‘Affaan (Radhi za Allaah zimshukie), kisha Amiyrul Mu-uminiyn, na Imaamul Muttaqiyn, ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhi za Allaah zimshukie). [Atw-Twabariy, Sarihus-Sunnah, 38-39).

 

Shaykhul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

“Kwa kuendelea, Abu Bakr (Radhi za Allaah zimshukie), kisha ‘Umar (Radhi za Allaah zimshukie), kisha ‘Uthmaan (Radhi za Allaah zimshukie) na ‘Aliy (Radhi za Allaah zimshukie) haya ni mashauri walikubaliana Wanavyuoni wote wa Waislamu na miongoni mwa wale viongozi katika elimu na Dini miongoni mwa Maswahaba, Tabi’iyn, kisha waliokuja baada yao... na Imaam Maalik amenukuliwa na Ijmaa’ (makubaliano) ya watu wa Madiynah juu ya suala hili akisema: “Sijakutana na mtu yeyote miongoni mwa wale wengine ambao wanaongoza wenyewe wakiwa na mashaka juu ya uongozi wa Abu Bakr (Radhi za Allaah zimshukie) na ‘Umar (Radhi za Allaah zimshukie).” [Majmuu’ al-Fataawa, / 421-428), Ibn Hajar, Fat-hul-Baariy, 7/16; Al-Laalikaiy, Sharh Usuulu’l-I’tiqaad, 7/1363-1372)

 

4 - Ibn Abil-‘Izz (Aliyefariki 792H) amesema:

“Hatusemi juu ya mtu yeyote maalum miongoni mwa watu wa Qiblah kuwa yeye ni mtu wa Peponi au wa Motoni, isipokuwa yule ambaye mkweli mwaminifu (Mtume wa Allaah) katueleza juu yao, kwamba ni miongoni mwa watu wa Peponi, kama vile wale kumi waliobashiriwa Pepo (Allaah Awaridhie wote). Na kama tutasema: “Yeyote ambaye Allaah Atamuingiza Motoni miongoni mwa watu ambao walitenda madhambi makubwa atakuwa anastahiki kuingia huo Moto, na kwamba atatolewa nje ya Moto ikiwa atakuwa miongoni mwa wale ambao wanastahiki kuombewa Shafaa’, basi tunasimamia kwa kutosema ni mtu maalum. Hivyo hatuna ushahidi wa yeye kama ataingia Peponi, wala kama ataingia Motoni ila tu kutokana na dalili kwa sababu ukweli wa mambo umefichikana na anachofia mtu hakijulikani na yeyote kati yetu.

 

Hata hivyo tuna matumaini mazuri kwa wale waliofanya matendo mazuri na tunakuwa na hofu kwa wale waliofanya maovu. Na Salaf (Wema waliotangulia) walikuwa na kauli tatu katika suala la kushuhudia Pepo kwa mtu fulani: Kauli ya kwanza ni kwamba pepo haishuhudiwi na mtu yeyote isipokuwa Mitume, na imenukuliwa kutoka kwa Muhammad bin al-Hanafiyyah na al-Awza’iy.

Kauli ya pili ni kwamba Pepo inashuhudiwa kwa kila muumini ambaye maandiko yametajwa juu yake, na hii ni kauli ya Wanavyuoni wengi na Ahlul Hadiyth (watu wa Hadiyth).

Kauli ya tatu ni kwamba Pepo inashuhudiwa juu ya (wote) na ambaye waumini wameshuhudia juu yake kwa hilo (Sharh ‘Aqiydatit-Twahaawiyyah, 378)

 

5 – Nao ni: Abu Bakr (Radhi za Allaah zimshukie), ‘Umar (Radhi za Allaah zimshukie), ‘Uthmaan (Radhi za Allaah zimshukie), ‘Aliy, Twalhah bin ‘UbaydiLlaah (Radhi za Allaah zimshukie), Az-Zubayr bin Al-Awwaam (Radhi za Allaah zimshukie), Sa’ad bin Abi Waqqaas (Radhi za Allaah zimshukie), Zayd bin Sa’iyd bin ‘Amr bin Nufayl (Radhi za Allaah zimshukie), ‘Abdur-Rahmaan bin ‘Awf (Radhi za Allaah zimshukie), Abu ‘Ubaydah bin al-Jarraah (Radhi za Allaah zimshukie).

 

6 - Sunnah ya kufuta juu ya khufu (soksi za ngozi) wakati wa kuosha miguu imekuja kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kwa mapokezi mengi (mutawaatir).

Raafidhah (Mashia) wanapinga hii Sunnah iliyo Mutawaatir. Kwa hiyo tunawaambia: “Wale ambao walisimulia Wudhuu kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) katika maneno na matendo na wale ambao wamejifunza Wudhuu kutoka kwake, wakafanya Wudhuu kipindi cha maisha yake na akawaona wafanyavyo na kuwasadikisha kwa hilo. Kisha wakasimulia hili kwa wale waliokuja baada yao, kwa idadi kubwa zaidi kuliko wale waliosimulia mapokezi haya, kwa sababu Waislamu wote walifanya Wudhuu wakati wa maisha yake na hawakujifunza Wudhuu isipokuwa kutoka kwake (Mtume) na kitendo hichi hakikufungamana nao wakati wa zama za Ujahiliya - na walimuona akifanya Wudhuu mara kadhaa ambayo hakuna yeyote ila Allaah (Jalla Jalaaluh) ndiye anaweza kuhesabia.

Na pia walisimulia kutoka kwake uoshaji wa miguu miwili katika kila kitu ambacho Allaah Anapenda miongoni mwa Hadiyth” [Sharhu At-Twahaawiyyah, 386-387]
 

7 - Hili ni moja ya masuala madogo ya utekelezaji na tofauti imetokea kwa heshima na ni miongoni mwa Wanavyuoni wa ummah. Hili latokana na ripoti za yanayokinzana ambazo zipo kuhusiana nayo. Na hata kama isnadi ya kusema ‘BismiLlaah...’ kimya ni sahihi zaidi, bado ni kunabaki moja ya matatizo ambayo hayashikamani na ‘Aqiydah. [Sharhus-Sunnah, 3/54; Fathul-Bariy, 2/226-229]
 

8 - Al-Qadar ni elimu (ujuzi) wa Allaah wa tangu hapo kabla ya ambayo yatayotokea kutoka miongoni mwa matendo ya waja Wake, nini watachochuma, na kuibuka kwa vitendo hivyo kutokana na Alichoamrisha, ametakasika yeye kutokana na kutokamilika, na viumbe Wake ndiyo hawakukamilika, mema na mabaya yao. Hivyo, Qadar ni kitu ambacho kwa ajili ya mambo manne kimethibitishwa: Jambo la kwanza ni kutokana na elimu ya Allaah juu ya mambo kabla ya hayajatokea. Jambo la pili ni kutokana na maandiko ya (elimu hio). Jambo la tatu ni kuwa hakuna jambo laweza kutokea au laweza kuja katika kuwepo ila ni kutokana na matakwa Yake, hivyo basi chochote akitakacho hutokea na chochote Asichokitaka hakitokei. Jambo lanne ni kuwa uumbaji wa Allaah – mkamilifu ni Yeye kutokana na upungufu wa matendo na kuwaleta kwake katika kuwepo.

[Sharh Usuulul-I’tiqaad, 3/534, Al-Bayhaqiy, Al-I’tiqaad, 132; Ajurriy, Ash-Shari’ah, 149-168; Atw-Twabariy, Sarihus-Sunnah, 34-36; Al-Bukhaariy, Ar-Radd ‘Alal-Jahmiyyah, 39-42; Majmuu’ Al-Fataawa, 2/152, 8/484-488; Sharhut-Twahaawiyyah, 383-399]
 

9 - Imaam Atw-Twahaawiy alisema:

“Tunashikilia ya kuwa Swalah nyuma kila mtu mwenye mwema na hata mwenye dhambi kutoka katika watu wa Qiblah (Waislamu), na pia kuwaswalia miongoni mwao wanaokufa.

Kisha mfafanuzi wa hii ‘Aqiydah, Ibn Abi Al-‘Izz kasema: “Jua - (Allaah Akurehemu), kwamba inaruhusiwa kwa mtu kuswali nyuma ya mtu ambaye ana uzushi wa ufasiki (fisq) inayojulikana kwa makubaliano ya Wanavyuoni. Na si miongoni mwa masharti ya kumfuata Imaam, na haifai mtu kumchunguza Imaam na kumuuliza haswa:

“Nini unachoamini? Badala yake, ataswali nyuma ya mtu ambaye msimamo wake haujulikani. Na hili (inatumika) hata kama atabidi kuswali nyuma ya mtu wa Bid’ah ambaye analingania na kuita watu katika hizo Bid’ah zake au faasiq anayetenda madhambi yake wazi na ambaye ni Imaam kateuliwa hapo haitokuwa rukhsa kuswali nyuma yake, ispokuwa tu kama atakuwa ni Imaam wa Swalah ya Ijumaa, Swalah ya ‘Iyd mbili na Swalah wakati wa Hajj katika ‘Arafah na Swalah mfano wake. Maamuma wataswali nyuma yake na hii ndiyo mtazamo wa jumla wa Masalaf na wa Makhalaf (Wanavyuoni waliotangulia na waliofuatia). Na mtu yeyote atakayeacha kuswali Swalah ya Ijumaa nyuma ya Imaam ambaye ni mfanya madhambi huyu ni mzushi katika mtazamo wa Wanavyuoni wengi. Na ni sahihi kuwa ataswali pamoja na Imaam na kwamba hatokuwa na haja ya kuzirudia, kwa sababu Maswahaba (Allaah Awawie radhi) walikuwa wakiswali Swalah ya Ijumaa na mara kwa mara wakiswali nyuma ya kiongozi mwenye madhambi na walikuwa hawazirudii Swalah zao.” [Sharhut-Twahaawiyyah, 373-377]

 

 

10 – Akizungumzia kuwarudi Maraafidhah (Mashia) kwa kusema kwao:

“Hakuna Jihaad katika njia ya Allaah mpaka aliyechaguliwa kutoka katika kizazi cha Muhammad atokeze na mlinganiaji kutoka mbinguni anadi: “Mfuateni”. Uongo wa maneno haya yako wazi kabisa zaidi na dhahiri yasiyohitaji hata kuelezwa kwa Dalili. [Sharhut-Twahaawiyyah, 387-388]

11 – Habari zaidi kuhusiana na mada hii inaweza kupatikana katika: Sharh Usuulul-I’tiqaad, 7/1229-1233, Al-Bayhaqiy, Al-I’tiqaad, 242-246; Ibn Abi ‘Aaswim, As-Sunnah, 508-511

 

Share