Maana Ya Hadiyth Dhwa'iyf

 

Maulamaa wanasema kuwa: Hadiyth dhaifu ni ile isiyokuwa na sifa zinazokubalika. Na wengine wakasema kuwa Hadiyth dhaifu ni ile isiyostahiki kuitwa Sahihi wala Hasan (njema).

Zipo aina nyingi ya Hadiyth dhaifu zikiwemo:

 

 

Mursal:

Nazo ni zile zilizonyanyuliwa moja kwa moja kutoka kwa Taabi'iy mpaka kwa Mtume  صلى الله عليه وآله وسلم.  

 

Taabi'iy ni Muislamu aliyeishi wakati wa Maswahaba رضي الله عنهم   akawaona lakini hajamuona Mtume صلى الله عليه وآله وسلم.

Kwa mfano Tabi'iy aseme:

“Mtume wa Mwenyezi Mungu  صلى الله عليه وآله وسلم amesema…”

Wakati yeye hajawahi kuonana na Mtume صلى الله عليه وآله وسلم.

 

Maulamaa wamekhitalifiana juu ya kuzitumia Hadiyth za aina hii katika makundi manne:

1.     Imaam Abu Haniyfah na Imaam Maalik na baadhi ya wanavyuoni wanasema kuwa Hadiyth hizi zinafaa kutumika.

 

2.     Imaam An-Nawawiy akieleza juu ya Jamhuur kubwa ya Maulamaa na pia akimnukuu Imaam Ash-Shaafi'iy anasema kuwa Hadiyth za aina hii zinaweza kutumika kama ni hoja lakini si hoja ya moja kwa moja (ya kutegemewa).

 

3.     Imaam Muslim anasema: “Hadiyth Mursal kwetu sisi na kwa wengi kati ya wanavyuoni si hoja hata kidogo.”

 

4.     Wengine wakasema kuwa inaweza kuwa hoja pale tu ikiwa imepokelewa kutoka kwa Tabi'iy mkubwa, kisha Hadiyth hiyo iwe imefanyiwa kazi na Swahaba yeyote au na wanavyuoni wengi.

 

 

Munqatwi'i:

Hizi ni zile Hadiyth zilizokatika Isnadi zake, yote sawa kukatika huko kuwe mwanzo au mwisho wa majina ya wapokezi

 

 

Al-Mudallas:

Nazo ni zile Hadiyth ambazo muelezaji aeleze kuwa amehadithiwa na mtu aliyeishi katika zama moja kisha ikathibiti kuwa hawajapata kuonana. Au ahadithie kama kwamba amehadithiwa na mtu huyo wakati ukweli ni kuwa hakuhadithiwa na mtu huyo, kwa mfano aseme:

“Amenihadithia fulani.” Au: “Nilimsikia fulani.” Wakati ingekuwa sahihi kama angesema:

“Amesema fulani.” Au: “Kutoka kwa fulani.”

 

Maulamaa wanasema kuwa Mudallis (muelezaji wa Hadiyth hizi) hazikubaliwi riwaya zake hata kama aliwahi mara moja tu katika maisha yake kusema uongo katika Hadiyth.

 

Wengine akiwemo Imaam Ash-Shaafi'iy wakasema kuwa: “Ni zile Hadiyth alizodallis tu hazikubaliki, lakini zile alizozielezea kwa njia sahihi zinakubalika.”

 

 

Mudhwtwarib:

Nazo ni zile Hadiyth nyingi zinazogongana. Hadiyth aina hii zimedhoofishwa kwa sababu ya kugongana kwake na kutokuwa thaabit.

 

 

Munkar:

Nazo ni zile zilizohadithiwa na ‘Dhaifu’ (mtu asiyeaminika) kisha zikakhitilafiana na Hadiyth zilizohadithiwa na Thiqah (mtu mwenye kuaminika).

 

 

Al-Mudhwa'af:

Nazo ni zile Hadiyth zilizodhoofishwa na baadhi ya Maulamaa kutokana na udhaifu wa wapokezi wake, wakati baadhi nyingine ya Maulamaa wakasema kuwa ni sahihi.

 

 

Al-Matruuk:

Nazo ni zile zilizohadithiwa na mtu anayetuhumiwa kwa uongo katika Hadiyth au hata katika mazungumzo yake. Au anayetuhumiwa kuwa ni Faasiq wa maneno au vitendo. Matruuk pia ni yule mwenye kusahau sana au mwenye kukosea sana.

 

 

Wakati Gani Hadiyth Dhaifu Inakuwa Na Nguvu?

Hadiyth dhaifu inapata nguvu pale tu ikiwa rawi wake (mwenye kuhadithia) anatuhumiwa kuwa ameanza kusahau sahau. Ni Sharti awe Thiqah hatuhumiwi kwa Uongo wala kwa Ufaasiq wala kwa kusahau sana. Kisha Hadiyth alozungumza juu yake ziwe zimepokelewa kwa njia nyingi sana, na hapo inapanda darja na kuwa ‘Hadiyth Hasan.’

 

Na hii ni kwa sababu imepokelewa kwa njia zinazokubalika tena kwa njia ya rawi asiyetuhumiwa kwa uongo au kwa sababu ovu za kumdhoofisha.

 

 

Kuzifanyia Kazi Hadiyth Dhaifu:

Maulamaa wamekhitalifiana katika hukumu za kuzifanyia kazi Hadiyth za aina hii katika makundi matatu:

 

1.     Wapo wanaosema kuwa Hadiyth hizi hazifai kuzifanyia kazi kabisa, yote sawa iwe katika kuamrisha mambo ya Fadhila au katika Hukmu. Na hii ni kauli ya Yahya bin Ma'iyn na Abu Bakr bin Al-'Arabiy na pia Al-Bukhaariy na Muslim.

 

2.     Wengine wakasema kuwa Hadiyth hizi zinaweza kufanyiwa kazi.

 

3.     Na wengine wakasema kuwa Hadiyth hizi zinaweza kufanyiwa kazi katika mambo ya Fadhila na katika kuwaidh watu tu. Na kwamba zisitumike katika kutoa hukmu au katika ibada, tena ziwe zimekamilisha baadhi ya masharti kama vile asituhumiwe mmojawapo wa wapokezi wake kwa uongo au ufasiki n.k. Na pia udhaifu wa Hadiyth usiwe mkubwa sana, na pia mtu anapoelezea Hadiyth ya aina hii awajulishe watu kuwa ina udhaifu ndani yake. 

 

Anasema Dr. Muhammad Al-‘Ajjaaj Al Khatwiyb katika kitabu chake ‘Al-Mukhtaswar Al-Wajiyz fiy 'Uluum al-Hadiyth:

“Mimi naunga mkono rai ya mwanzo inayosema kuwa Hadiyth dhaifu zisifanyiwe kazi kabisa. Zipo Hadiyth za kutosha zilizo sahihi katika mambo ya fadhail na mawaidha kiasi ambapo haina haja ya kuingiza Hadiyth zenye shaka zinazoweza kuwa ni maneno ya uongo aliyozuliwa Mtume wa Mwenyezi Mungu صلى الله عليه وآله وسلم.”         

Pia Fadhail na Tabia njema ni katika mambo muhimu sana katika dini kwa hivyo haina haja kuzitumia Hadiyth dhaifu kwa ajili yake.”

 

Rai ya Dr. Muhammad Al-‘Ajjaaj ni bora zaidi kwa sababu mtu atawezaje kuiamini Hadiyth iliyosimuliwa na Mudallis, mtu mwenye kubadilisha majina ya Mashaykh au ya miji akijua kuwa anawadanganya wasikilizaji wake, au muongo ‘Kadhaab’ anayependa kuwadanganya watu katika mambo ya kidunia ambaye hatoshindwa kuwadanganya katika mambo ya dini.

Na vipi mtu ataweza kuifanyia kazi Hadiyth Mudhtwarib inayogongana na Hadiyth Swahiyh au Hadiyth Matruuk iliyodhoofishwa kwa ajili ya tabia ovu za msimulizi kwa ajili ya uongo na ufasiki n.k.

 

Na Allah Anajua zaidi

 

 

Share