Mama Kaacha Gari, Wameuza Kwa Milioni 4 Nao Ni Ndugu Watatu Mmoja Ni Mwanamke; Vipi Wagawane?

SWALI:

 

ASALAM alaikum  ndugu zangu katika iman

 

swali langu sisi tupo ndugu watatu mimi msichana mmoja na kaka zangu wakubwa wawili aliyefariki mama yetu ameacha gari tumeliuza sasa ndugu zangu wanasema tugawane pesa sawa kwa sawa na mimi nataka nichukue theluthi tu maana mimi ni mwanamke na hela yenyewe ni milioni 4 je nichukue ngapi wao wanataka hata kunipa yote wananipenda sana ila mimi nataka kama sheria inasema nipate theluthi sihitaji zaidi inshaalah

 

wabilah taufic


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani zetu kwa swali lako kuhusu urathi wa mama yenu aliyeaga dunia.

Mwanzo tunamuomba Allaah Aliyetukuka Amuweke mama yenu pema pamoja na wema, nasi pia atupe istiqaamah ya kufuata maagizo Yake ili tuwekwe sehemu hiyo ya Pepo.

 

Ama tukija katika swali lako inaonyesha waliobakia ni nyinyi tu watatu (ndugu). Hili lilivyoeleweka ni kwamba mama yenu hana wazazi walio hai wala mume. Ikiwa hali ni hiyo basi mgao wenu utakuwa kama ifuatavyo:

1.   Kaka wa kwanza atapata 2/5 ya pesa hiyo yaani milioni 1.6.

 

2.   Kaka wa pili naye atapata 2/5 ya pesa hiyo yaani milioni 1.6.

 

3.   Na wewe utapata 1/5 ya pesa yaani laki nane (800,000).

 

Wewe huwezi kupata thuluthi ya mirathi kwa kuwa wapo ndugu wa kiume wawili. Lau ungekuwa umebakia wewe na ndugu mmoja wa kiume basi ungepata hivyo.

 

Ama ikiwa ndugu zako wanataka kukuachia pesa zote kwa hiari yao hakuna tatizo kwani sasa ni zao na wamekupa wewe dada yao.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share