Adabu Za Swawm

 

Adabu Za Swawm

 

Imekusanywa kutoka Kitabu Cha Fiqhus-Sunnah

 

Alhidaaya.com

 

 

Kula Sahuwr (Daku)  

 

Imependekezwa kula sahuwr (daku) na hakuna madhambi kwa yule ambae hakufanya hivyo. Anas (Radhwiya Allaahu 'anhu) amehadithia kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Kuleni daku, kwani ndani yake kuna baraka” [Al-Bukhaariy na Muslim].

 

Sababu ni kuwa kula daku kunampa nguvu mwenye Swawm, kunamfanya awe mkakamavu, na kuifanya Swawm kuwa ni nyepesi kwake.

 

 

Ni Nini Kinachotimiza Sunnah ya Kula Sahuwr (Daku).

 

Sunnah hii itatimizwa kwa kula kiasi kidogo au kikubwa cha chakula, au hata japo kwa kunywa funda la maji. Abuu Sa’iyd Al-Khudriy (Radhwiya Allaahu 'anhu) amehadithia kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Sahuwr (Daku) ni mlo uliobarikiwa, hivyo usiupuuze japo kwa fundo la maji, Kwani Allaah na Malaika wanamswalia yule mwenye kula sahuwr” [Ahmad]

 

 

Wakati wa kula Sahuwr (daku)

 

Wakati wa kula Sahuwr (daku) ni baina ya usiku wa manane na alfajiri. Inakuwa ni vizuri zaidi kuichelewesha (yaani, karibu zaidi ya alfajiri kwa kadri inavyowezekana). Zayd bin Thaabit (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amehadithia: “Tulikula Sahuwr (daku) pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kisha tukanyanyuka kuswali. Akaulizwa: ‘Ni kiwango gani (baina ya viwili hivyo) daku na Swalah?’ Akajibu: ‘[Ni kiasi cha kusoma] Aayah khamsini’ ” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Shaka Katika Kuingia Wakati Wa Alfajiri

  

Iwapo mtu atakuwa na shaka kama wakati wa Alfajiri umeshaingia au la, anaweza kuendelea kula na kunywa mpaka atapopata uhakika kuwa Alfajiri imeingia. Asitegemeze kitendo chake kwenye shaka au dhana. Allaah ('Azza wa Jalla) Amezifanya dalili za kuingia alfajiri kuwa ziko wazi kabisa na wala hazina utata. Allaah Amesema:

 

 وَكُلُوا وَاشْرَبُوا حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَكُمُ الْخَيْطُ الْأَبْيَضُ مِنَ الْخَيْطِ الْأَسْوَدِ مِنَ الْفَجْرِ ۖ 

“Na kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa alfajiri katika weusi wa usiku.” [Al-Baqarah: 187]

 

Mtu mmoja alimwambia Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhu): “Ninakula mpaka ninapodhani kuwa wakati wake (yaani daku) umemalizika na ninaacha. Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhu) akabainisha: “Endelea kula mpaka uwe na uhakika na wakati wake” Abu Daawuud aliripoti kuwa Ahmad bin Hanbal amesema: “Iwapo huna uhakika kama wakati wa alfajiri umeingia au la, basi kula mpaka uwe na uhakika kuwa umeshaingia.”

 

 

Kufanya Haraka Kufutari

 

Imependekezwa mtu kukimbilia kufutari wakati wa kuchwa kwa jua. Sahl Ibn Sa’ad (Radhwiya Allaahu 'anhu) amehadithia kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Watu wataendelea kuwa katika kheri madhali watakuwa wanaharakisha kufutari” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Imependekezwa kufutari kwa tende zenye idadi ya witri (isiyogawika kwa mbili) au, kama hapana, basi kwa kunywa maji. Anas (Radhwiya Allaahu 'anhu) amehadithia: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  alikuwa akifungua kwa tende mbivu (laini), na anapokosa basi huwa anafungua kwa tende kavu, na anapokosa huwa anafungua kwa maji” [Abu Daawuud, Al-Haakim na At-Tirmidhiy]

 

Sulaymaan ibn ‘Amr (Radhwiya Allaahu 'anhu) amehadithia kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Anapokuwa katika Swawm mmoja wenu, basi afungue Swawm yake kwa tende. Akikosa tende, basi afungue kwa maji, kwani maji ni tohara” [Ahmad na At-Tirmidhy]

 

 

Du'aa

 

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Watu watatu du’aa zao hazitokataliwa; mwenye swawm hadi atakapofungua, Imaam muadilifu, na mwenye kudhulumiwa” [At-Tirmidhiy]

 

 

Kujiepusha Na Kufanya Tendo Lolote Ambalo Si Muwafaka Kwa Swawm

 

Swawm ni tendo la ‘ibaadah linalomkaribisha mtu kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ameifaradhisha ili kuisafisha nafsi na kuizowesha katika matendo mema. Mtu mwenye swawm ni lazima ajilinde dhidi ya tendo lolote linaloweza kusababisha kupoteza faida za Swawm yake. Kwa kufanya hivyo, Swawm yake itamuongezea kumjua Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na Allaah Anasema katika Qur-aan: 

 

 يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ ﴿١٨٣﴾

“Enyi mlioamini! Mmefaradhishiwa Swawm, kama walivyofaradhishiwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kuwa na taqwa.” [Al-Baqarah: 183]  

 

Swawm si kujizuilia kula na kunywa tu, bali pia kujizuilia na jambo jengine lolote ambalo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amelikataza. Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) amehadithia kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Swawm si kujizuia na kula na kunywa tu, bali pia (kujizuia) na maneno ya kipuuzi na mazungumzo machafu. Anapotukanwa mmoja wenu au kuudhiwa, anatakiwa aseme: “Mimi niko katika Swawm mimi niko katika Swawm.” [Ibn Khuzaymah, Ibn Hibbaan na Al-Haakim]

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) pia amesema: “Allaah hana haja na Swawm ya yule asiyejizuia na maneno ya uongo na matendo yake [Al Bukhaariy]

 

Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) ameeleza kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  amesema: “Huenda mwenye Swawm asipate ujira wowote wa kukaa kwake na njaa, na huenda yule mwenye kusimama kisimamo cha usiku (kuswali) asipate chochote kwa kusimama kwake ila kuacha kulala.” [An-Nasaaiy, Ibn Maajah na Al-Haakim]

 

 

Kupiga Mswaki

 

Imependekezwa kwa mtu aliye katika Swawm kupiga mswaki. Hakuna tafauti iwapo atapiga mswaki mwanzo au mwisho wa siku. Imehakikishwa kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipiga mswaki huku akiwa katika Swawm.

 

 

Share