Mambo Yanayobabaisha Katika Kumpwekesha Allaah Kwenye 'Ibaadah (Tawhiyd)

  

 

Muhammad Faraj Saalim As-Sa’iy 

 

Inasikitisha kuona kuwa hadi wakati huu, bado wapo Waislamu wenye itikadi isiyokuwa sahihi na wenye kusema maneno ambayo huenda yakawatia katika shirki.

Watu wa aina hiyo wengi wao nia zao ni nzuri, na ni katika watu wamchao MwenyeziMungu sana, wanasali na kufunga na kutimiza nguzo zote tano za kiislamu. Lakini itikadi zao hizo pamoja na kuvuka kwao mipaka katika kuwasifia na kuwatukuza watu wema au Mtume katika Mitume ya Allaah ('Alayhis Salaam Ajmaiyn), huwafanya kutoa kauli zinazoweza kuwatia katika shirki na kuwatoa katika Tawhyid ambayo juu yake diyn hii tukufu imesimama.

Allaah Anasema:

{{Usimshirikishe Allaah, maana shirki ndiyo dhulma kubwa.}} [Luqmaan: 13]

Na Akasema:

{{Hakika Allaah Hasamehe (dhambi ya) kushirikishwa na kitu, lakini (Yeye) husamehe yasiyokuwa hayo kwa amtakaye.}} ]Annisaa: 116]

Kabla ya kuendelea mbele, ni bora tufafanue kidogo nini maana ya Tawhiyd.

Tawhiyd, ambayo kinyume chake ni Shirki; maana yake ni "kupwekesha" au kuelekeza ‘ibaadah zote mahali pamoja tu. Nako ni kwake Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Tawhiyd inakanusha aina yoyote ya kumshirikisha Allaah.

Diyn ya Kiislamu ndiyo diyn pekee ulimwenguni inayohubiri Tawhiyd. Kwasababu diyn nyengine zote zinamnasibisha Allaah na washirika wengine.

Ma’ulamaa wameigawa elimu hii ya Tawhiyd sehemu tatu, nazo ni:

  1. Tawhiyd Ar-Rubuubiyyah
  2. Tawhyid Al-Uluuhiyyah
  3. Tawhiyd Al-Asmaa Was-Swifaat

 

1.    Tawhiyd Ar-Rubuubiyyah

Nayo ni kuamini kwamba Allaah.  Allaah Ndiye aliyeumba kila kitu bila ya msaidizi. Itikadi hiyo pekee haimuingizi mtu Peponi, kwasababu washirikina wa Makkah wote walikuwa wakiamini kwamba Allaah ndiye Aliyeumba kila kitu bila ya msaidizi.

Allaah Anasema:

{{Ni nani anayekuruzukuni kutoka mbinguni (kwa kuleta mvua) na katika ardhi (kwa kuotesha mimea)? Au ni nani anayemiliki masikio (yenu) na macho na nani amtoae mzima katika mfu na kumtoa mfu katika mzima? Na nani atengezaye mambo yote? Watasema (washirikina wa Makkah) "Allaah".}} [Yuunus: 31]

Hata Ibliys aliyelaaniwa na Mwenyezi Mungu, alikuwa anayo Tawhiyd hii.

Mwenyezi Mungu Anasema:

{{Akasema Ibliys: Mola wangu! Basi nipe nafasi (nisife) mpaka siku watakayofufuliwa (viumbe vyote).}} [AlHijr: 36]

Kutokana na aayah zilizotangulia, utaona kuwa Makureishi waliokuwa wakiabudu masanamu, pamoja na Ibliys wao, walikuwa wakiamini kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Mola wao, na ndiye aliyeumba na ndiye Mwenye kumiliki kila kitu. Lakini imani yao hiyo hakuwasaidia kitu, kwa sababu ya kutoamini sehemu nyingine za Tawhiyd.

Kwa hivyo, hata kama utaamini kwamba Allaah Ndiye aliyeumba na ndiye mwenye kumiliki kila kitu, lakini ikiwa hujaamini sehemu ya pili na ya tatu ya Tawhiyd, basi imani yako hiyo haitokusaidia kitu.

 

2.    Tawhyid Al-Uluuhiyyah

Nayo ni kuamini kwamba ‘ibaadah zote lazima zielekezwe kwake tu Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala).

‘Ibaadah kama vile kusali, kuhijji, kuomba du’aa, kuchinja, kuweka nadhiri, kuhukumu n.k., zote hizo pamoja na nia ya mtu katika kutenda tendo lolote lile la kidunia au la kiakhera lazima zielekezwe kwake tu (Subhaanahu wa Ta’ala), na asiingizwe mshirika wa aina yeyote ndani yake.

Mwenyezi Mungu Anasema:

{{Sema: Hakika Swalah zangu, na ‘ibaadah zangu (zote nyengine) na uzima wangu na kufa kwangu; (zote) ni kwa Allaah Muumba wa walimwengu wote. Hana mshirika wake. Na haya ndiyo niliyoamrishwa na mimi ni wa kwanza wa waliojisalimisha (kwa Allaah).}}  [Al-An’aam: 162]

 

3.    Tawhiyd Al-Asmaa Was-Swifaat

Nayo ni kuamini na kukubali kila kilichoandikwa katika Qur-aan Tukufu na katika Hadiyth zilizo sahihi za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) zikielezea sifa tukufu za Allaah au majina Yake matukufu, bila ya kukisia kisia, wala kuchelewesha, wala kubadilisha maana yake.

Kwa mfano unapokutana na kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo: {{Mkono wa Allaah uko juu ya mikono yao.}} [Al-Fat-h: 10] Kubadilisha neno mkono tukasema nguvu, tutakuwa tumebadilisha maana.

Na Shaytwaan anapojaribu kutaka kukuchezea kwa kutaka ufananishe au ugeuze maana ya sifa, au majina ya Allaah kumbuka kauli Yake (Subhaanahu wa Ta’ala):

{{Hakuna chochote mfano Wake.}} [Ash-Shuura: 11]

 

Shirki

Shirki katika lugha ya Kiarabu maana yake ni Ushirika. Nako ni kumjaalia mmoja au zaidi, awe na sehemu kubwa au ndogo, katika jambo lolote lile aloshirikiana na mwenziwe au wenziwe.

Kumshirikisha Allaah katika kuamini kwamba anaye mshirikia katika kuumba chochote kile (Tawhiyd Ar-Rubuubiyyah) au kuamini kwamba yuko mwenye uwezo au sifa kama zake (Tawhiyd Al-Asmaa Was-Swifaat), au kuamini kwamba ‘ibaadah ya aina yoyote ile, inaweza ikaelekezwa au kupitia kwa mwengine asiyekuwa Allaah (Tawhyid Al-Uluuhiyyah), basi huko ni kwenda kinyume na mafundisho ya diyn yetu tukufu ya Tawhiyd na kumkadhibisha Allaah, na kwa sababu hii, dhambi yake haisameheki [kwa ukubwa wake].

Mwenyezi Mungu Anasema:

{{Allaah Ameshuhudia ya kwamba hakuna aabudiwaye kwa haki ila Yeye tu.}} [Al-‘Imraan: 18]

Na akasema:

{{Jua ya kwamba hakuna aabudiwaye kwa haki ila Allaah.}} [Muhammad: 19]

 

Tofauti Baina Ya Shirki Na Kufru

Shirki inahitilafiana na kufru. Kwani kuna shirki nyengine hazikupeleki kwenye kufru, kama vile Shirki ndogo (Ash-Shirkul-Asghar) au Shirki iliyojificha (Ash-Shirkul-Khafiy).

Pia kutenda au kutamka neno la shirki bila kujua, hakumpeleki mtu katika kufru. Isipokuwa mara tu baada ya kutambua, inampasa Muislam akiache kitendo hicho haraka sana.  Dalili ya maneno haya ni Hadiyth zifuatazo:

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), aliulizwa juu ya watu ambao wanapokuwa mbele ya wenzao hujionyesha kuwa ni watu wema na wanapokuwa peke yao hufanya kinyume na hayo. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwakufurisha watu wa aina hiyo, bali alisema: ((Ninachokuogopeeni sana ni Shirki ndogo.)) Maswahaabah wakauliza: "Ni nini hii Shirki ndogo, ewe Mtume wa Allaah?" Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Riya (kujionyesha).)) [Imepokewa na Imaam Ahmad]

Dalili nyengine ni pale Swahaabah mmoja alipomwambia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Kama alivyotaka Allaah na ulivyotaka. Maa shaa Llaahu wa shi-ita.” Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: ((Umenigeuza kuwa mshirika wa Allaah? Sema: 'Alivyotaka Allaah peke Yake' Qul Maa shaa-Llaahu wahdahu.)) [Imepokewa na Imaam Ahmad, Addarmy na Ibni Maajah]

Zipo dalili nyingi juu ya maudhui haya, lakini hapa nitamaliza kwa kutoa dalili ifuatayo:

Siku moja Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwasikia baadhi ya watu wakisema: "Njooni tuombe, tuelekeze du’aa zetu kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).” Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipowasikia, akawaambia: ((Nani huyu mnafiki? Du’aa hazielekezwi kwangu, bali zinaelekezwa kwa Allaah.)) [Imepokewa na Imaan Ahmad na At-Twabaraaniy]

Ingawaje maneno yaliyotamkwa hapo juu na baadhi ya Maswahaabah, yalikuwa na dalili ya shirki ndani yake; lakini Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwahukumu waliotenda au kutamka maneno hayo kuwa ni makafiri. Bali aliwasahihisha itikadi yao, na hii ni kwasababu ya kutokujua kwao kosa lao, kisha akawafahamisha hatari ya makosa hayo.

Kwa hivyo mwenye itikadi kama hiyo ya kumuomba Mtume katika Mitume ya Allaah ('Alayhis Salaam Ajmaiyn) au Waliy katika Mawaliy wa Allaah n.k., hatuhumiwi kuwa ni kafiri. Isipokuwa mtendaji au msemaji wa kauli kama hizi ikiwa anafanya inda na kushikilia, pamoja na kuendelea kutenda au kutamka maneno mfano wa haya kwa inadi na kutakabari tu, basi hapo ndipo anapokuwa katika hatari ya kuingia katika kufru.

 

Je, Inajuzu Kumuomba Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam)?

Suala sasa linakuja: "Jee inajuzu kuelekeza du’aa yako kumuomba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)?"

Jawabu: "Haijuzu".

Kwa sababu Mtume mwenyewe (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amebainisha aliposema: ((Du’aa ndiyo ‘ibaadah.)) [Imepokewa na Imaam Ahmad na Imaam At-Tirmidhiy]

 

Nini ‘Ibaadah?

Anasema Ibnul-Qayyim Al-Jawziy (Rahimahu Allaah): "’Ibaadah ni jina lililokusanya kila Anachokipenda Allaah na kuridhika nacho ikiwa ni kitendo au kauli, zilizojificha au zilizodhihirika.”

Kwa hivyo kitendo chochote kinachokukaribisha kwa Allaah kama vile kusali, kufunga, kuhijji, kutoa Zakkah, kutoa Swadaqah, kusoma Qur-aan, kuomba du’aa n.k. ni ‘ibaadah.

Ushahidi kwamba du’aa ni ‘ibaadah unatokana na kauli yake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) iliyotajwa hapo juu; aliposema katika Hadiyth sahihi iliyosimuliwa na Imaam Ahmad pamoja na Imaam At-Tirmidhiy: ((Du’aa ndiyo ‘ibaadah.))

Kwa hivyo atakayemuomba yeyote asiyekuwa Allaah iwapo ni Malaika mtukufu, au Mtume katika Mitume ya Allaah ('Alayhis Salaam), au Waliy katika mawaliy wa Allaah au jinni au kiumbe chochote kile kihai au kilichokufa, atakuwa amekwisha fanya kitendo cha ushirikina.

Allaah Anasema:

{{Na kama Allaah Akikugusisha dhara, basi hakuna yeyote awezaye kuiondoa isipokuwa yeye (Mwenyewe). Na kama Akikutakia khayr, basi hakuna awezaye kurudisha fadhila Zake. Huzifikisha kwa amtakaye katika waja Wake. Naye ni Mwingi wa kusamehe, Mwingi wa Rahmah.}} [Yuunus: 106-107]

Na Akasema:

{{Sema: (Ewe Muhammad) "Mimi sikumilikiini kukudhuruni wala kukuongoeni".}} [Al-Jinni: 21]

Na pia Akasema:

{{Sema: "Sina mamlaka ya kujipa nafuu wala ya kujiondolea madhara ila apendavyo Allaah, na lau kama ningalijua ghayb ningejizidishia mema mengi wala isingalinigusa dhara, mimi si chochote ila ni muonyaji na mtoaji wa habari njema kwa watu."}} [Al-‘Aaraaf: 188]

Ukizichunguza aayah nyingi, utaona kwamba Allaah Anamwambia Mtume wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): sema, waambie, wafahamishe, wajuulishe kwamba hakuna awezae kudhuru au kunufaisha isipokuwa Allaah, na kwamba hapana ajuae ghayb isipokuwa Allaah  tu. Lakini kinachosikitisha ni kwamba bado wapo wasiotaka kufahamu wala kuambiwa.

Inafaa mtu ajiulize suali hili: "Je Mtume mwenyewe (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwahi kudai au kutufundisha kwamba du’aa zielekezwe kwake?"

Bila shaka hakupata hata siku moja kudai hayo, bali kauli zake zote ni dalili ya kuyakanusha hayo. Ndiyo maana siku ile Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipopanda mnyama pamoja na Ibni ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhu) akamwambia:

((Ewe kijana, mimi ninakufundisha maneno: Muhifadhi Allaah naye atakuhifadhi, muhifadhi Allaah siku zote atakuwa na wewe, ukiomba du’aa umuombe Allaah ukitaka msaada umuombe Allaah  na ujue ya kwamba Ummah wote ukikusanyika ili wakunufaishe na kitu basi hawawezi kukunufaisha ila kwa kile ambacho Allaah ameshakuandikia, na wakikusanyika ili wakudhuru kwa jambo, basi hawawezi kukudhuru ila kwa kile ambacho Allaah  keshakuandikia; kalamu zimekwishanyanyuliwa na wino umekwishakauka juu ya karatasi.)) [Imepokewa na At-Tirmidhiy]

Hakumwambia Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba: "Ukiomba du’aa niombe mimi, na ukitaka msaada niombe mimi." Bali alimwelekeza kule kule kwa Mwenye Nguvu, Mwenye Uwezo Allaah  (Subhaanahu wa Ta’ala).

Anasema Imaam Ibn Al-Qayyim Al-Jawziy (Rahimahu Allaah) katika kitabu chake kiitwacho Zaad al-Maad, ukurasa wa tatu:

"Ninashuhudia kwamba Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameletwa na Mola wake kama Mitume mingine, akiwa kiongozi wa wamchao Allaahh  ni rahmah kwa walimwengu. Akawaongoza watu katika njia iliyo sahihi na iliyonyooka. Allaah akawafaradhishia waja wake kumtii Mtume huyu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kumuheshimu, kumpenda na akajaalia njia ya kuelekea kwenye Pepo yake ni moja tu, nayo ni kufuata njia yake Mtume huyu mtukufu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Akajaalia kudhalilika na kudharaulika kumfikie kila atakayekwenda kinyume na Mtume huyu mtukufu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Na akajaalia kudhalilika na kudharaulika kwa kila atakayekwenda kinyume na amri yangu na atakayejifananisha na kundi keshakuwa pamoja nao.)) [Imepokewa na Imaam Ahmad]

Kwa hivyo watadhalilika waliomuasi na wataheshimika watakaomtii na kumfuata Mtume huyu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Allaah  Anasema:

{{Na musilegee wala musihuzunike maana nyinyi ndio mtakaokuwa juu ikiwa mnaamini kweli.}} [Aali-‘Imraan: 139]

Na Akasema:

{{Na utukufu hasa ni wa Allaah na Mtume wake na wa Waislamu.}} [Al-Munafiquun: 8]

 

Kutosheleza Na Kufuata

Anaendelea kuelezea Imaam Ibnul-Qayyim katika kitabu chake hicho akisema: Alllaah Anasema:

{{Ewe Mtume wa Allaah! Allaah  Anakutosheleza wewe na wale waliokufuata katika hao walioamini.}} [Al-Anfaal: 64]

Na Akasema:

{{Na kama wakitaka kukuhadaa basi Allaah Atakutoshelezea. Yeye ndiye aliyekusaidia kwa nusura yake na kwa waliokuamini.}} [Al-Anfaal: 62]

Anaendelea kueleza Ibnul-Qayyim kwamba; katika aayah hizi Allaahh Anamjuulisha Mtume wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba Allaah pekee anamtosheleza yeye pamoja na waliomfuata, na kwamba hawahitajii msaada wa yeyote mwengine isipokuwa wake Subhaanahu wa Ta’ala.

Katika aayah nyengine Akasema:

{{Wale ambao watu waliwaambia 'Watu wamekukusanyikieni kwa hivyo waogopeni" Lakini (maneno hayo) yakawazidishia imani (Waislamu) wakasema “MwenyeziMungu anatutoshea. Naye ni mlinzi bora kabisa”.}} [Al-‘Imraan: 173]

Ukiichunguza aayah hii utaona kuwa Waislamu hawakusema "Anatutosheleza Allaah  na Mtume wake". Bali walisema: "Allaah anatutosha. Naye ni mlinzi bora kabisa".

Na ukiichunguza kauli ya Mwenyezi Mungu katika Suuratut-Tawbah aayah ya 59 Aliposema:

{{Na kama wangeyaridhia yale aliyowapa Allaah  na Mtume Wake, na wakasema: “Anatutoshea Mwenyezi Mungu, karibuni Allaah Atatupa katika fadhila zake na Mtume wake (pia), hakika sisi tunaelekea kwake".}}  [At-Tawbah: 59]

Tizama jinsi Allaah  Alivyomnasibisha Mtume wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika kutoa’. Akatumia neno (Alllaah  Atatupa katika fadhila zake na Mtume wake) kama katika kauli nyengine aliposema:

{{Na anachokupeni Mtume basi pokeeni.}} [Al-Hashr: 7]

Lakini katika neno ‘kutosha’, utaona kwamba amejinasibisha Yeye peke yake Subhaanahu wa Ta’ala. Hakusema: ‘Anatutoshea Allaah  na Mtume wake’ bali amesema: Anatutoshea Allaah’. Akakamilisha kwa kauli yake: ‘Hakika sisi tunaelekea kwa Allaah’. Akajaalia ‘kuelekea’ kuwe kwake tu, kama Alivyosema katika Suuratun-Nashrah:

{{Basi ukishamaliza (kulingania), shughulika (kwa ‘ibaadah). Na jipendekeze-elekea-kwa Mola wako.}} [Nashrah: 7-8]

Kwa hivyo, kutegemea, kutosheleza, kuelekea ni kwake Allaah tu peke yake. Pia kusujudu, kuweka nadhiri, kuapa, yote haya yanaelekezwa kwake tu Subhaanahu wa Ta’ala. Ushahidi wa haya ni kauli yake Mwenyezi Mungu:

{{Je Allaah  hamtoshei mja wake?}} [Zumar: 36]

Kwa hayo tunatambua kuwa, kumshirikisha Allaah katika ‘ibaadah zake zozote zile, na kiumbe chochote kile baada ya kuzijua dalili zilizotangulia na zilizowazi kabisa, ni jambo lililo baatwil na la ufisadi.

Kwa ufupi, Allaah Anatutaka tumtegemee Yeye tu na Kumuomba Yeye tu, pamoja na kuelekeza ‘ibaadah zetu zote kwake Yeye tu, na Anatutaka tumfuate Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ndipo utakapopatikana ushindi na utukufu na kusaidiwa na Allaah pamoja na maisha mema hapa duniani na Akhera.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliapa akasema:

((Hatoamini mmoja wetu mpaka mapenzi yake kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yawe makubwa kupita mapenzi ya nafsi yake, na ya watoto wake na ampende Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuliko watu wote.))

Na Allaah Akaapa Akasema:

{{Naapa kwa haki ya Mola wako. Wao hawawi wenye kuamini (kweli kweli) mpaka wakufanye hakimu katika yale wanayokhitilafiana, kisha wasione uzito nyoyoni mwao juu ya hukumu uliyotoa na wanyenyekee kabisa.}} [An-Nisaa: 6]

Katika aayah hii, Allaah Anatukataza kufuatwa amri isiyokuwa Yake Subhaanahu wa Ta’ala au ya Mtume wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Muislamu hana hiari ya kuchagua, kufuata au kutofuata baada ya kuijua hukumu ya Allaah au ya Mtume wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Bali Muislamu, lengo lake lote pamoja na mapenzi yake yote, yawe katika kufuata amri za Allaah  na za Mtume wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Mwisho wa maneno ya Ibnul-Qayyim (Rahimahu Allaah).

 

Wasiylah

Nini maana ya Wasiylah?

Majibu:

Wasiylah katika lugha ya Kiarabu, maana yake ni njia au sababu inayoweza kukufikisha utakapo.

Na asili yake ni kauli yake Mwenyezi Mungu katika Qur-aan aliposema:

{{Enyi mlioamini mcheni Mwenyezi Mungu na tafuteni njia ya kumfikilia.}} [Al-Maaidah: 35]

Na katika Hadiythul-Qudusy Mwenyezi Mungu Anasema:

((Hatojikurubisha kwangu mja wangu kwa jambo nilipendalo kuliko yale niliyomfaradhishia. Na mja wangu angali anaendelea kujikurubisha kwangu kwa ‘ibaadah za Sunnah mpaka nimpende...)) [Imepokewa na Al-Bukhaariy]

Amma katika lugha ya diyni (katika Fiqhi), neno 'Wasiylah' pia huwa na maana ya amali njema anayoitanguliza mja kwa Mola wake, kabla hajaomba du’aa au pamoja na du’aa ili du’aa yake ikubaliwe.

Katika kujisogeza huku kwa Mola wao, baadhi ya Waislamu wakavumbua njia zisizo za kishari’ah ambazo badala ya kuwasogeza karibu na Mola wao, huwa zinawabaidisha Naye. Kuna Wasiylah inayompeleka mtu katika shirki, na nyengine inampeleka mtu katika uzushi (bida’ah).

 

Mambo Yanayowababaisha Watu

Kujikurubisha Kwa Jaha (Heshima) Ya Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam)

Kwanza kabisa; nini maana ya Jaha:

Jaha, katika lugha ya Kiarabu maana yake ni hishima. Mwenyezi Mungu Anasema juu ya Nabii ‘Iysa ('Alayhis Salaam):

{{Jina lake ni Masyih ‘Iysa, mwana wa Maryamu, mwenye hishima katika dunia na Akhera Wajihan fiddunya wal aakhirah.}} [Aali ‘Imraan: 45]

Na juu ya Nabii Muusa ('Alayhis Salaam), Mwenyezi Mungu Anasema:

{{Naye alikuwa mwenye hishima mbele ya Mwenyezi Mungu Kaana ‘inda Llaahi wajiyhaa.}}  [Al-Ahzaab: 69]

Bila shaka (Jaha) hishima ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mbele ya Mola wake ni kubwa kabisa. Lakini kumuomba Mwenyezi Mungu akukubalie jambo lako kwa hishima ya Mtume wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) badala ya kumuomba akukubalie kwa nguvu Zake Mwenyezi Mungu au kwa uwezo Wake au kwa ukarimu Wake n.k. huku ni kuyakimbia yale majina na sifa Zake tukufu Subhaanahu wa Ta’ala.

 

Kujikurubisha Kwa Baraka Za Mawalii

Nako ni kujisogeza kwa Mwenyezi Mungu kwa njia ya kwenda makaburini (makaburi ya mawalii) au njia zilizo kama hizo.

Hapana anayepinga kuwepo kwa Mawalii wa Mwenyezi Mungu, pamoja na makarama yao pale walipokuwa hai. Qur-aan na Sunnah zimezungumzia juu ya yote hayo. Lakini kwenda makaburini na kuwaomba maiti hao ili kupitia kwao uweze kuondolewa shida zako na Mola wako, jambo hilo halijuzu kabisa na pana hatari ya kukuingiza katika kumshirikisha Mwenyezi Mungu na kiumbe.

 

Kujisogeza Kwa Du’aa Iitwayo ‘Wasiylah’

Kuna baadhi ya watu hujisogeza kwa kusoma ‘Wasiylah’ - nayo ni du’aa maarufu iitwayo Asw-Swalaatu-Nnaariyah. Husomwa mara 4,444 ili kuondoa shida au dhiki. Inasemekana kwamba mmoja katika watu wema alioteshwa na kufundishwa du’aa hii.

Swalah yenyewe inasomwa hivi:

"Allahumma swalliy swalaatan kaamilah, wa sallim salaaman taammah ‘alaa Sayyidina Muhammad, alladhiy tanhallu bihil ‘uqad, watanfarij bihil kurab, watanqadhiy bihil hawaaij...” mpaka mwisho wake.

Maana yake ni: "Mola wangu Swali Swalah iliyokamilika na umsalimie salaam iliyotimia Bwana wetu Muhammad, ambaye kwake yeye fundo zinafunguka na dhiki zinaondoka na haja zinatimia…” mpaka mwisho wa du’aa.

Ukiichunguza Swalah hii, utaona kwamba badala ya kuelekeza du’aa kwa Mwenyezi Mungu, inaelekezwa kwa Mtume wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na kumpa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) sifa za Mwenyezi Mungu. Hasa pale inaposemwa ‘kwake yeye fundo zinafunguka na dhiki zinaondoka’, na huku ni kumpa kiumbe sifa za Mwenyezi Mungu.

Baadhi ya Ma’ulamaa wamesema laiti pale paliposemwa , alladhiy tanhallu bihil ‘uqad na maana yake ni ‘kwake yeye fundo zinafunguka’ pangesemwa tanhallu bihal ‘uqad; hapo maana yake inabadilika na kuwa ‘kwa kumswalia na kumsalimia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ndiyo dhiki na shida zinaondoka’; na kwa vile kumswalia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni ‘ibaadah ambayo Mwenyezi Mungu Ametuamrisha.

Mwenyezi Mungu Anasema:

{{Inna Allaaha wa Malaaikatahu yuswalluuna ‘alan Nnabiy, yaa ayyuha lladhiyna aamanuu swalluu ‘alayhi wa salliimu tasliyma.

Hakika Mwenyezi Mungu na Malaika Wake wanamteremshia rahmah Mtume. Basi enyi Waislamu mswalieni (Mtume) na muombeeni amani.}} [Al-Ahzaab: 56]

Na kwa vile inajuzu kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu kwa ‘ibaadah iliyo sahihi, kwa hivyo inajuzu kujikurubisha Kwa kumswalia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Amma kuielekeza du’aa yako kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) moja kwa moja au kumpa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) sifa katika sifa za Mwenyezi Mungu, hiyo haijuzu.

 

Kujisogeza Kwa Mwenyezi Mungu Kwa Amali Njema

Inajuzu kujisogeza kwa MwenyeziMungu (Kutawassal) kwa amali njema. Kwa mfano, mtu aseme:

"Ewe Mola wangu siku moja nilifanya jambo fulani jema, na sikulifanya jambo hilo ila kwa ajili ya kutaka ridhaa yako tu, kwa hivyo kwa ajili ya kitendo changu kile chema nakuomba unikubalie du’aa yangu hii".

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitufundisha hayo katika Hadiyth iliyopokewa kutoka kwa Al-Bukhaariy na Muslim. Hadiyth hiyo imo katika kitabu cha Imaam An-Nawawiy kiitwacho Riyaadhus-Swaalihiyn (Hadiyth nambari 13) juu ya wale watu watatu walioingia pangoni kisha jiwe kubwa sana likaanguka na kuifunga njia yao ya kutokea. Kila mmoja wao aliomba kwa amali njema yake na Mwenyezi Mungu Akawafungulia njia yao.

 

Toba Ya Aadam ('Alayhis Salaam)

Kuhusu usemi wa baadhi ya watu kwamba Nabii Aadam ('Alayhis Salaam) alipotubu aliomba asamehewe kwa Jaha ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hadiyth zilizoegemewa katika kuithibitisha hoja hii ni zile ambazo Ma’ulamaa wa Hadiyth wamezitaja kuwa ni maudhui (za uongo na hazina msingi wowote).

Qur-aan imekweshatujulisha juu ya du’aa aliyoiomba Aadam ('Alayhis Salaam). Mwenyezi Mungu Anasema:

{{Na Mola wao akaweta (akawaambia): "Je sikukukatazeni mti huu na kukwambieni ya kwamba Shaytwan ni adui yenu aliye dhahiri.” Akasema (Aadam): "Mola wetu! Tumedhulumu nafsi zetu na kama hutusamehe na kuturehemu, bila shaka tutakuwa miongoni mwa wenye khasara".}} [Al-‘Aaraf: 22-23]

Natumai inafahamika hapa kwamba; Aadam na mkewe ('Alayhimas Salaam) waliomba toba moja kwa moja kwa Mola wao bila kupitia njia nyingine.

 

Hadiyth Ya Kipofu

Kipofu mmoja alimwendea Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: "Niombee du’aa ili Mwenyezi Mungu anijaalie niweze kuona.” Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: ((Ukitaka nitakuombea na kama ukitaka subiri, kwani hiyo ni khayr kwako.)) Yule kipofu akasema: "Bora niombee ili nipone". Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuamrisha atawadhe vizuri na aswali raka’ah mbili kisha aombe ifuatavyo: ((Mola wangu mimi nakuomba na ninaelekea kwako pamoja na Mtume wako, Mtume wa Rahmah, Ewe Muhammad mimi naelekea Kwa Mola wangu pamoja nawe katika haja yangu hii ili ikubaliwe. Mwenyezi Mungu mkubalie du’aa yake kwa ajili yangu.)) [Imepokewa na At-Tirmidhiy na Ahmad]. Hadiyth inaendelea: "Baada ya kuomba du’aa hii mtu yule akapona".

 

Jawabu

Baadhi ya watu imewakanganya Hadiyth hii, wakaona kwamba labda inajuzu kuomba kwa baraka au kwa Jaha ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hasa kwa vile kipofu yule alitumia neno: "Atawassal ilayka binabiyyika Muhammad, nabiyyi rahma".  Maana yake ni: "Ninajisogeza kwako pamoja na Mtume wako Muhammad, Mtume wa Rahmah".

Ukiichunguza, utaona kwamba; tawassul hii imepangika kwa mambo mengi, na haiwi sahihi ila baada ya kupatikana kwa mambo hayo, na baadhi ya mambo hayo hayawezi kupatikana hivi sasa baada ya kufa kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Mambo yenyewe ni haya yafuatayo:

a.     Iwapo wakati huu mtu ataomba aseme:

"Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, muombe Mola wako anikidhie haja yangu".

Kauli yake hiyo itakuwa ni batwili na ya upotevu. Kwasababu Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hamsikii wala hamuoni na wala hatoweza kumuombea kama alivyoombewa kipofu yule.

 

b.     Iwapo mmoja wetu atasema:

"Mola wangu ninakuomba na ninaelekea kwako pamoja na Mtume wako.”

Mtu huyo atakuwa muongo, maana Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hayupo ili aelekee naye na aombe du’aa pamoja naye. Kwasababu maneno hayo husemwa na aliyesimama na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mfano wa yule kipofu.

Kwa hivyo tawassul hiyo haifai, kwasababu ya kukosekana kwa nguzo muhimu, nayo ni du’aa ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa muombaji wa wasiylah.

 

Hadiyth Ya Kuomba Mvua

Hadiyth ifuatayo pia imewakanganya baadhi ya watu. Hadiyth hiyo inasema hivi:

’Umar bin Khattwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu), alikuwa akimuomba Al-‘Abbaas Ammi yake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakati wa ukame na mvua ilikuwa ikinyesha.

Hadiyth inaendelea:

‘Umar bin Khattwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa wakati wa ukame akimuomba Al’Abbaas Ibn ‘Abdul-Muttwalib na kusema:

"Mola wetu tulikuwa tukikuomba kupitia kwa Mtume wetu na ukituletea mvua, na sasa tunakuomba kwa njia ya Ammi yake ili utuletee mvua - Walikuwa wakinyeshewa mvua". [Imepokewa na Al-Bukhaariy]

Wamebabaika kwa kudhani kuwa kwa vile ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisema:

"Sisi tulikuwa tukikuomba kupitia kwa Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na ukituletea mvua". Wakaona kuwa huu ni ushahidi kwamba ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa akitawassal kwa jaha ya ‘Ammi yake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kwa hivyo, haina lazima sisi kumuomba Mwenyezi Mungu. Na kwa vile hapo mwanzoni ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa akitawassal kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kwa nini basi na sisi tusiuombe kwa njia ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)?

Jibu:

Kule kutawassal kwa Maswahaba wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kulikuwa ni kwa kumuomba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) awaombee du’aa. Naye Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiomba, na du’aa yake ilikuwa ikikubaliwa. Hadiyth hiyo kwa ukamilifu inasema hivi:

"Siku moja Mabedui walimuendea Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumtaka awaombee du’aa ili mvua inyeshe, maana hata wanyama wao walikuwa wakifa kwa ukame. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akanyanyua mikono yake juu na kuomba, kabla ya kuishusha chini, mvua kali ilinyesha."

Shaykh Abuu Bakar Al-Jazairiy katika kuisherehesha Hadiyth hii katika kitabu chake kiitwacho “Itikadi ya Muislam” Aqiydatul-Muumin alisema:

Maswahaabah hawakuwa wakiomba kwa kuelekeza du’aa zao kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mwenyewe, au kwa dhati yake au kwa jaha yake kama wanavyofikiria.

Kwa sababu ingelikuwa ni hivyo basi ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) asingemoumba Al-‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhu) ili awaombee du’aa. Bali angeomba kwa Jaha ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye alikuwa amezikwa pale pale msikitini, karibu yake.

Lakini alielewa kuwa hivyo si sawa na sivyo alivyofundishwa na Mtume wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Ndiyo maana baada ya kufa kwake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), akaona ni vizuri kumtaka ‘Ammi yake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) awaombee, na alikuwa akiwaombea na kukubaliwa du’ah yao.

Na hii ni dalili kuwa inakubaliwa kumtanguliza mtu mwema ili aombe du’aa na wengine waitikie. Lakini haikubaliwi kumtanguliza maiti au asiyekuwepo na kusema: "Mola wetu tunatawassal kwako kwa jaha ya fulani".

Maana huyo atakayetangulizwa anatakiwa awepo na anyanyue mikono yake juu na kuomba, wakati maiti au asiyekuwepo hawezi kufanya hivyo."

Mwisho wa maneno ya Shaykh Abu Bakar Al-Jazairiy.

Tunamaliza kwa kauli yake Subhaanahu wa Ta’ala katika Suuratul-‘Imraan, aayah ya 79 Aliposema:

{{Haiwi kwa mtu ambaye Mwenyezi Mungu Amempa Kitabu na hukumu na Unabii aseme kuwaambia watu: "Kuweni wa kuniabudu mimi badala ya Mwenyezi Mungu (peke yake)" Bali (yeye atawaambia): "Kuweni wenye kuabudu Mwenyezi Mungu. Kwa sababu mnafundisha Kitabu na kwa sababu mnakisoma". Wala hatakuamrisheni kuwafanya Malaika na Manabii kuwa waungu. Je! atakuamrisheni ukafiri baada ya kuwa nyinyi Waislamu?}} [Al-‘Imraan: 79-80]

 

Share