'Aqiydah Iwe Mwanzo

 

‘Aqiydah Iwe Mwanzo

 

Shaykh Swaalih Al-Fawzaan (Hafidhwahu Allaah)

 

Alhidaaya.com

 

 

Jambo la kwanza, kubwa, na la msingi katika kulingania watu kumtii Allaah, na kwa nini ‘Aqiydah iwe mwanzo.

 

 

Aqiydah ni lazima ije mwanzo kwa sababu, kinachozusha mgawanyiko na maangamizi katika ulimwengu wa Kiislamu ni kukosekana ‘Aqiydah iliyo sahihi.

 

 

Kwa Nini ‘Aqiydah Liwe Jambo La Mwanzo?

 

 

1-Hakika ‘Aqiydah lazima ije mwanzo kwa sababu ni msingi wa Da’wah ya Rusuli wote kama Allaah ('Azza wa Jalla)  Alivyotuma Risala Yake  kupitia kwa Rusuli Wake. Anasema Allaah ('Azza wa Jalla)  kupitia ulimi wa kila Rasuli Aliyemtuma kwa watu wake:

 

  يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّـهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرُهُ ۖ

Enyi kaumu yangu! Mwabuduni Allaah, hamna mwabudiwa wa haki ghairi Yake.  [Huwd: 84]

 

2-‘Aqiydah lazima ije mwanzo kwa ajili ya kuepusha kubakia Motoni (Jahannam) milele na kujiepusha na adhabu hiyo. Hamkusikia maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ ۚ وَمَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدِ افْتَرَىٰ إِثْمًا عَظِيمًا ﴿٤٨﴾

Hakika Allaah Haghufurii kushirikishwa; lakini Anaghufuria yasiyokuwa hayo kwa Amtakae. Na yeyote atakayemshirikisha Allaah basi kwa yakini amezua dhambi kuu. [An-Nisaa: 48]

 

 

Kumshirikisha Allaah ('Azza wa Jalla) ni dhambi kubwa ambayo inampelekea mja kutoka nje ya Tawhiyd (kumpwekesha Allaah), na Tawhiyd ni msingi sahihi wa ‘Aqiydah.

 

 

3-‘Aqiydah lazima iwe mwanzo vilevile kwa sababu kumshirikisha Allaah ('Azza wa Jalla)  ni dhambi kubwa ambayo ni madhara kwetu kama Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anavyosema:

 

إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيم

Hakika shirki ni dhulma kubwa mno!” [Luqmaan: 13]

 

 

4-‘Aqiydah lazima ije mwanzo kwa sababu, kinachozusha mgawanyiko na maangamizi katika ulimwengu wa Kiislamu ni kukosekana ‘Aqiydah iliyo sahihi na watu kufuata ‘Aqiydah zisizo sahihi.

 

 

Ndio maana ‘Aqiydah nyingi za Waislamu zimejaa ufisadi kwa mambo ya shirk kubwa. Mfano utakuta watu wanatufu (wanazunguka) kwenye makaburi na kuwaomba maiti waliomo ndani ya makaburi hayo wawasaidie haja zao na kudhania kuwa kufanya hivyo watapata kukidhiwa  mahitaji yao na shida zao.

 

 

Na kwa hali hiyo, watu kama hawa wamerudi nyuma kiwakati, wanajirudisha katika wakati wa Jaahilliyah (zama za ujinga kabla ya Uislamu). Na wanajifanya kama hawajasikia maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)   

 

إِن تَدْعُوهُمْ لَا يَسْمَعُوا دُعَاءَكُمْ وَلَوْ سَمِعُوا مَا اسْتَجَابُوا لَكُمْ ۖ وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ يَكْفُرُونَ بِشِرْكِكُمْ ۚ وَلَا يُنَبِّئُكَ مِثْلُ خَبِيرٍ ﴿١٤﴾

 Mkiwaomba, hawasikii maombi yenu, na hata wakisikia, hawatakuitikieni.  Na Siku ya Qiyaamah watakanusha ushirikina wenu, na wala hakuna atakayekujulisha vilivyo kamaMwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika. [Faatwir: 13-14] 

 

Na sisi tunawakataza kufuata uzushi wa Masufi ambao wameweza kuueneza kwa watu wa kawaida wasio na elimu, hadi kwamba takriban nchi mbalimbali zimekuwa zikiongozwa na kutawaliwa na uzushi wa hawa Masufi na bid’ah zao kama vile Mawlid. Na hata uzushi wa aina mbalimbali kama kuwaiga Makafiri katika sherehe zao na sikukuu zao, achilia mbali uzushi mbalimbali wanaoufanya katika Dini ambao umegawa nchi zao na kuziweka mbali na Qur-aan na Sunnah.

 

 

Kwa haya machache ndugu yangu mpendwa, tumejaribu kuwaonyesha ukweli kwamba ‘Aqiydah ni jambo la muhimu na la mwanzo katika maisha yako na ‘Aqiydah inapaswa daima iwe mwanzo.

 

 

Na Allaah Anajua Zaidi

 

 

 

Share