Zingatio: Dini Mseto

 

Naaswir Haamid

 

Mitume ishirini na tano ambao wametajwa katika Qur-aan, Aliowaleta Mola wetu Mtukufu, wote walikuwa na muongozo mmoja tu, nao ni kuusimamisha Uislamu kwa haki inayostahiki kusimamishwa. Nako ni kujikubalisha kwa amri za Mola pamoja na kushuhudia kwamba hakuna Mola Apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah na wala Hana mshirika.

 

Taariykh ya Uislamu haikupatapo hata siku moja kuandika kwamba Mitume hawa walishirikiana na makafiri katika ibada. Wala hakuna uthibitisho wa kuonesha kuwepo muingiliano wa elimu baina ya misingi ya Uislamu na ukafiri. Hizo ni njia mbili tofauti, wala hazitakuwa na mfanano wowote hadi mwisho wa dunia hii.

 

Basi kwa wale wanaosema kwamba Uislamu upo sawa na dini nyengine, haswa zile zinazosemwa kuwa ni dini za Kitabu, kama vile Uyahudi na Unaswara, hao wamekwenda kombo na wala hawaelewi misingi ya Uislamu. Kwani hata huo Uyahudi na Unaswara unaofuatwa leo, hauna uhusiano sahihi na hivyo Vitabu Alivyovishusha Mola wetu (Subhaanahu wa Ta’ala). Sasa ni wapi tena tunataka kuwabebesha watoto wetu elimu ya Yesu aliyevumbuliwa na Ukiristo hali ya kuwa Uislamu unayo mafundisho yake sahihi ya Nabii ‘Iysa bin Maryam (‘Alayhis Salaam)?

 

Mola wetu Amesema:

 

{{Bila shaka Diyn (ya haki) mbele ya Allaah ni Uislamu. Na waliopewa Kitabu (Mayahudi na Manaswara) hawakukhitalifiana ila baada ya kuwajia ilimu.}} [Al-‘Imraan: 19]

 

Na Akasema pia:

 

{{Na anayetaka dini isiyokuwa ya Kiislamu basi haitakubaliwa kwake. Naye Akhera atakuwa katika wenye khasara (kubwa kabisa).}} [Al-‘Imraan: 85]

 

Kwa hivyo, tuelewe Waislamu kwamba, iwapo tumeukubali Uislamu kuwa ni Diyn yetu, basi hayo hapo juu ndio mafunzo sahihi, wala Mola wetu hajatutaka tuchanganye imani zetu zilizo safi dhidi ya imani za kikafiri. Na kwa hakika Uislamu wetu unatufunza kutochanganya ukafiri na Uislamu:

 

{{Sema: “Enyi makafiri. Siabudu munachoabudu. Wala nyinyi hamuabudu ninayemuabudu. Wala sitaabudu munachoabudu. Wala nyinyi hamutaabudu ninayemuabudu. Nyinyi muna dini yenu nami nina Diyn yangu.”}} [Al-Kaafiruun: 1-6]

 

Yapo mambo ambayo kweli tunaweza kushirikiana na makafiri, kama vile elimu sahihi za dunia kwa mfano utabibu na ufundi; lakini abadan sio ndani ya misingi ya Kiislamu hadi kufikia binti wa Kiislamu kutoona tofauti baina ya kuvaa ama kutovaa hijaab.

 

Tumche Mola wetu (Subhaanahu wa Ta’ala), na tumuabudu Yeye kama Alivyotuamuru bila ya kumshirikisha. Tunamuomba Mola wetu Atuongoze katika njia sahihi na Atukhitimishe kwa qawli ya haki iliyothibiti.

 

Share