Ramadhaan Humalizikia/Huishia na 'Iyd?
Imefasiriwa na : Ummu Ahmad
Ukimuuliza Muislamu yeyote suala hili bila shaka utapata jawabu la “ndio”, Ramadhaan huisha ile siku tunayojumuika pamoja kwa furaha kusheherekea ‘Eid-el-Fitri. Maamrisho ya kujizuwia kula, kunywa na mashirikiano ya kimwili kati ya mke na mume wakati wa mchana wa Mwezi wa Ramadhaan tunayapata moja kwa moja kutoka kwenye Kurani Tukufu na Hadithi za Bwana Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam). Lakini kwa kweli kama tutachunguza kwa undani baraka za Mwezi huu Mtukufu wa Ramadhaan, tutaona kwamba mafunzo yake yanakusudiwa kubakia na kutekelezwa na kila mmoja wetu baada ya kumalizika kwa chuo hichi adhimu kwa muda wote utakaofuatia baada ya Ramadhaan.
Kwanza kabisa, suala zima la kujizuwia na kula, kunywa na matamanio ya kiwiliwili kutoka alfajiri hadi magharibi tunapata mafundisho maalumu. Katika mafunzo hayo ni pamoja na:
1) Utulivu na Upole
2) Kuwa na tafakur
3) Kuishi ndani ya Qur-aan
4) Kuwafikiri waja wenzetu na hali ya Umma wa Kiislam kwa ujumla
5) Kujiweka mbali na mapambo na matamanio ya vitu vya kidunia
Mafunzo haya na neema nyingi nyingi yatatuwezesha, kwa uwezo wa Allaah, kutupa faida ya hali ya juu ya uvumilivu na ustahamilivu katika nafsi zetu. Mwenye Enzi Mungu Anasema katika Qur-aan tukufu:
((Enyi mlioamini! Takeni msaada kwa subira na Sala. Hakika Mwenyezi Mungu Yu pamoja na wanaosubiri)) [Sura Al-Baqarah 153]
Kumpenda Allaah (Subhaanahu Wa Ta'ala) na kumtii kwa maamrisho Yake ndio msingi wa ibada na ndio lengo hasa la sisi wanaadamu kuwepo hapa ulimwenguni. Kwa ajili hiyo basi tunapojiuliza na kutafakari mafunzo tunayopata ndani ya Ramadhaan na umuhimu wake kwa maisha yetu ya kila siku, inatubainikia kuwa lengo hasa la kuingia kwenye chuo hichi adhimu ni kuziweka nyoyo zetu ndani ya taqwa ya kumtii Allaah (Subhaanahu Wa Ta'ala) kwa muda wote unaofuatia baada ya Ramadhaan karimu.
Mwenyezi Mungu Anasema ndani ya Qur-aan tukufu:
((Enyi watu! Yamekujieni mawaidha kutoka kwa Mola wenu Mlezi, na poza kuponyesha yaliyomo vifuani, na uwongofu, na rehema kwa Waumini))
((Sema: Kwa fadhila ya Mwenyezi Mungu na rehema Yake! Basi nawafurahi kwa hayo. Haya ni bora kuliko hayo wanayo yakusanya))
[Sura Yunus 57 – 58]
Hivyo basi ni wazi kabisa kuwa ibada ya funga ya Ramadhaan ni katika nguzo kubwa iliyo muhimu ya dini ya Kiislam iliyokusudiwa kutusaidia kama wanaadamu katika kufanikisha lengo la kuwepo kwetu duniani kama makhalifa wa Allaah (Subhaanahu Wa Ta'ala) .
Kwa kuwa Ramadhaan ni chuo adhimu cha kutuleta ndani yake taqwa pale tunapokuwa wastahamilivu na wanyenyekevu katika kufuata maamrisho ya Allaah ndani ya nafsi zetu tunapata faida ya kuwa waadilifu na kuipigania njia ya Mwenyezi Mungu ndani ya nafsi zetu kwanza. Vita hivi vya kuzilea nafsi kwa ajili ya Allaah(Subhaanahu Wa Ta'ala), huitwa Jihaad.
Jihad inakusanya yale yote, kuanzia vita dhidi ya makafiri na ushirikina na yale yote yaliyokatazwa na Allaah (Subhaanahu Wa Ta'ala) ili kupata daraja ya juu kabisa ya mafanikio katika maisha ya Muislamu mbele ya Allaah (Subhaanahu Wa Ta'ala) Mwenyeezi Mungu Anasema katika Qur-aan tukufu:
((Wale walioamini, na wakahama, na wakapigana Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali yao na nafsi zao, hao wanacheo kikubwa zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu. Na hao ndio wenye kufuzu. [Suratu Tawbah 9:20]
Wengi wetu huelewa neno Jihaad kwa maana finyu kabisa, ya kuchukua silaha na kwenda vitani. Kwa mafundisho ya Bwana Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) kwenda vitani ni katika jihadi ndogo. Jihad kubwa haswa ni kupigana na nafsi zetu kwa kuwacha yale yote tuliyokatazwa na Allaah (Subhaanahu Wa Ta'ala) na Mtume wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) na kufanya yale tuliyoamrishwa ndani ya Uislamu.
Kwa kufanya hivyo tu ndio tutafuzu mbele ya Allaah (Subhaanahu Wa Ta'ala) kwa kuishi maisha bora hapa duniani na kutarajia mema kesho akhera.
Hivyo basi kwisha kwa Ramadhaan isiwe ndiyo mwisho wa sisi kufanya mema na kuishi nje ya mipaka ya Allaah (Subhaanahu Wa Ta'ala), bali tubebe tabia zote njema tulizojifunza ndani ya mwezi huu mtukufu na kwa kufanya hivyo tu , ndio tutakuwa Waislamu wa kweli.
- Login or register to post comments
- Email this page
- Chapisha
