Dalili Za Watu Wa Matamanio Ni Moja Kati Ya Aina Tatu

 

 

Dalili Za Watu Wa Matamamio Ni Moja Kati Ya Aina Tatu

 

Imetarjumiwa Na: Naaswir Haamid

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Shukrani zote ni za Rabb wa ulimwengu. Kwa hakika, mwisho mwema ni wa wenye taqwa, hakuna uadui isipokuwa kwa madhalimu. Rahmah na amani ziwe juu ya yule aliyetumwa kama ni Rahmah kwa ulimwengu, watu wake wa nyumbani na Swahaba zake.

 

 

Kwa kuendelea,

 

Kuna nukta tatu ambazo ni hoja kuu za kupotoka na kutoongoka kwa watu wa matamanio ambao wanaegemea matamanio yao na bila ya kuwa na ‘ilmu kuzua mambo ndani ya Dini ambayo hayamo.

 

 

Sababu Hizi Ni:

 

 

1-Kutokuwa na dalili kwa yale wanayoyazungumza.

 

 

 2- Dalili zao hazina usahihi.

 

 

3- Dalili zao ni sahihi lakini hazinasibiani na hoja husika.

 

 

Kwa kuomba msaada wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na kumtegemea Yeye; nitachambua kwa kina hayo hapo juu:

 

 

Awali Ya Yote, Maana ya Uzushi

 

 

Uzushi ni kuanzisha kitu kipya ndani ya Dini ambacho mzushi anazua kwa utashi wake binafsi na bila ya kuwa na msingi kutoka katika Qur-aan au Sunnah kwa minajili ya kuwa karibu na Allaah. Kuanzisha mambo mapya ndani ya Dini ni dhambi kubwa. Ukweli ni kwamba, ni miongoni mwa madhambi (makubwa ni) kumfanya Allaah kuwa na mshirika kama ambavyo Allaah (‘Azza wa Jalla) Anasema:

 

أَمْ لَهُمْ شُرَكَاءُ شَرَعُوا لَهُم مِّنَ الدِّينِ مَا لَمْ يَأْذَن بِهِ اللَّـهُ ۚ  ﴿٢١﴾ 

Je, wanao washirika waliowaamuru Dini yale ambayo Allaah Hakuyatolea idhini?  [Ash-Shuwraa: 21].

 

 

Na kwa sababu ya hili, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amefafanua uzushi kuwa “jambo ovu kabisa” kama alivyosema ndani ya Hadiyth ambayo imesimuliwa na Jaabir (Radhwiya Allaahu ‘anhu):

 

إنُّ َشَرُّ الْأُمُورِ مُحْدَثَاتُهَا

 “Kwa hakika, mambo yaliyo maovu kabisa ni yale mambo yanayozushwa.” [Muslim na pia katika Swahiyhul-Jaami’, 1353].

 

 

Na uzushi ni sehemu ya ushirikina (shirk). Hutamuona mzushi aliyebobea katika uzushi, isipokuwa yumo katika shirki aidha katika mambo (madhambi) makubwa au madogo. Au utamuona kutokuwa tofauti dhidi ya ushirikina na kutafuta hoja kwa watu wa shirk.

 

Sufyaan Ath-Thawriy amesema:

 “Uzushi unapendwa zaidi na Ibliys kuliko upotofu. Mtu anaweza kuomba msamaha kwa kupotoka, lakini hawezi kuomba msamaha kwa uzushi.” [Chanzo; ‘Aqiydah Ya Ahlus-Sunnah cha Al-Lalakaa’iy 1/132].

 

 

Ndugu Yangu Mpenzi Ambaye Unasoma Makala Hii,

 

Elewa, tambua vyema na hifadhi yafuatayo na yachukue kama ni silaha yako dhidi ya wazushi:

 

Yeyote anayedai tendo la ‘ibaadah kuwa ni sahihi basi analazimika kuleta mbele dalili na kuthibitisha kwamba imethibiti katika Shari’ah. Jukumu la kuthibitisha litakuwa ni juu yake na si juu yako. Usihadaiwe kwa maneno ya mzushi “ushahidi gani kwamba lile na lile ni uzushi?”  Mjibu: Ushahidi wako upi kwamba tendo hili ni la ki-Shari’ah”.

 

Na inatosha kwa watu wa Sunnah kudai ushahidi kwamba uzushi si sahihi, na kumwabudu Allaah katika hilo haliruhusiki, kwa sababu hakuna ushahidi katika hilo. Haiwezekani kupatikana dalili ya kila uzushi ili tupingane nayo, isipokuwa, kuna ushahidi wa jumla unaokataza uzushi wote kama ilivyo ndani ya Hadiyth iliyosimuliwa na Jaabir (Radhwiya Allaahu ‘anhu):

 

كل بدعة ضلالة

 “Kila uzushi ni upotofu.” [Muslim na pia katika Swahiyhul-Jaami’, 1353].

 

Na Hadiyth katika [Al-Bukhaariy na Muslim]:

 

مَنْ أَحْدَثَ فِي أَمْرِنَا هَذَا مَا لَيْسَ مِنْهُ فَهُوَ رَدٌّ

”Yeyote anayezua jambo katika jambo letu (Dini) ambalo halimo litakataliwa.”

 

Hivyo, kama mzushi akisema kwa uongo na usingiziaji: “Haikatazwi watu kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) katika mtindo ambao wameuanzisha wenyewe alimuradi tu haupingani na Shari’ah ya Kiislamu.”  Basi mwambie: Umesema uongo bali imekatazwa hilo.” Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema:

 

إِيَّاكُمْ وَمُحْدَثَاتِ الأُمُورِ

“Tahadharini na mambo ya uzushi”

 

Na Allaah (‘Azza wa Jalla) Amekamilisha Dini na Akatimiza Neema kwa hivyo hairuhusiki kuzua dhikri wala Swalah wala kitu chengine chochote. Na mwambie (huyo mzushi): Kwa nini useme alimuradi tu haipingani na Shari’ah hali ya kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza uzushi ambao ni kwenda kinyume na Shari’ah na misingi yake. Ungelitia akilini, hayo unayosema, basi usingelitamka tamko kama hilo lenye utata

 

 

 

Ndugu Yangu Ambaye Unasoma Hii,

 

Namna gani wazushi wanajiamini kuchupa mpaka pale linapokuja suala la Allaah, Rasuli Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Dini ya Uislamu. Sikiliza yale anayosema mzushi:

 

“Kuonesha furaha kwa kuzaliwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni tendo la ki Shari’ah na kuna dalili nyingi kuhusu hilo”

 

Subhaana Allaah! (Ametakasika Allaah!) Je ziko wapi hizo dalili nyingi?  Hawezi kutaja hata dalili moja juu ya madai yake kuwa ziko dalili nyingi.   Lakini lile alilonalo na matamanio yake ndivyo yanavyotumika, kutetea kwa uzushi katika madai mepesi bila ya kuweka wazi ushahidi. Lakini sisi tunaona kwamba Allaah Mtukufu Ameweka bayana dalili nyingi za Tawhiyd [Kumpwekesha Yeye], kwa Aayah za kawniyyah [kiulimwengu] na Shari’ah.  Ameweka pia dalili nyingi kusadikisha Wajumbe Wake na kuwaunga mkono kwa Aayah nyingi. Hali ya kuwa tunaona wazushi wakizua uzushi ambao hauna ushahidi na kubadili ukweli kwa uongo. Lile tu analoweza kusema ni “Kuna dalili nyingi.”

 

 

 

Msomaji Wangu Mwema,

 

Tambua, Allaah Anilinde mimi na wewe kutokana na uzushi na watu wake, kwamba watu wa uzushi na matamanio yake hawana ushahidi kwa uzushi wao na hii ndio njia yao ya jumla jamala pale wanapoliendea jambo lao la uzushi na upotofu.

 

 

Na iwapo watu watawakana na kuwataka wathibitishe ushahidi wao, basi watataja simulizi ambazo hazina usahihi kutoka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Simulizi hizo ima za uongo au ambazo isnadi yake imekatika, au hawana ushahidi au wana ushahidi ambao si sahihi.

 

 

Hii ndio maana tunaona kwamba Wenye kuihami Dini na ‘Aqiydah sahihi wa zama zilizopita na sasa wamesimama kidete dhidi ya simulizi zisizo sahihi na zile zenye wasimulizi wepesi, wakathibitisha yale yaliyo sahihi na yale yasiyo sahihi. Na hii ni sifa nzuri ambayo watu wa Hadiyth wamekuwa nayo peke yao, si kama walivyo watu wa uzushi na wa matamanio ambao hawajui lipi ni sahihi na lipi lisilo sahihi. Wakathibitisha ‘Aqiydah na ‘ibaadah zao kwa masimulizi ya uongo na ubatilifu. Hivyo wamepotoka na wamepotoa wengine. Hizo ndizo sababu mbili za upotofu wa watu wa uzushi, kutokuwa na ushahidi na kuwa na thibati zisizokuwa sahihi.

 

 

Ama sababu ya tatu na hii ndio iliyokuwa ni hoja ya hatari zaidi kwa wapotofu wa watu wa upotofu na uzushi, matumizi yao ya dalili sahihi ambazo hazihusiani katika hoja zao au wanazo dalili lakini zipo nje ya mada.

 

 

Kwa Ndugu Yangu Ambaye Anasoma Hii,

 

Tambua, Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Awe na Rahmah juu yangu na yako; wengi katika viumbe vya Allaah miongoni mwa wanaadamu na majini wamezifasiri sivyo Aayah kisha baadaye wakaja na uzushi wao na upotofu. Pamoja na hayo, hoja ya kuwa na mapenzi kwa mawalii na waja wema wao wakaanza kuwaabudu ghairi ya Allaah. Na hoja ya kuwatukuza Ahlul-Bayt na kuwaitakidi yasiyostahiki isipokuwa kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Na hoja ya kumdhukuru Allaah na kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakazusha Mawlid, kuimba mashairi, kucheza na nyimbo za jazba; kupandisha hamasa wakidai kwamba ni katika ‘ibaadah kwa Allaah.  

 

 

Na hoja ya Jihaad wakamwaga damu ya wasio na hatia. Na hoja ya kumtukuza Rabb kwa kumfananisha Naye kwa viumbe Vyake, wakaanza kuzikanusha Sifa Zake kwa hoja ya kuwa na wivu wa Dini, wakawakufurisha Waislamu kuwatoa nje ya Dini, na kwenda kinyume na mikataba na makubaliano. Na hoja ya kujifanya wachaji na kujiweka mbali na machafu, wakaharamisha mazuri Aliyoyahalisha Allaah kwa waja Wake. Na hoja ya kutafuta mibadala, wakazua ndani ya Dini yale ambayo Allaah Hajaruhusu.

 

 Wanatumia dalili zisizokatazwa bila ya vikwazo, dalili zisizojieleza bila ya kuwa na maelezo, na wanatumia dalili za jumla bila ya kuzihusisha. Wametumia Shari’ah za wale ambao walikuwa kabla yetu badala ya Shari’ah zetu. Na hili ndilo ambalo Ibliys amefanya kabla yao pale aliposema:

 

 

   أَنَا خَيْرٌ مِّنْهُ خَلَقْتَنِي مِن نَّارٍ وَخَلَقْتَهُ مِن طِينٍ ﴿١٢﴾ 

Mimi ni bora kuliko yeye. Umeniumba kwa moto, na yeye Umemuumba kwa udongo. [Al-A’raaf: 12].

 

 

Kisha baada yake walikuwa ni makafiri wa awali na kusema:

 

.. لَوْ شَاءَ اللَّـهُ مَا أَشْرَكْنَا وَلَا آبَاؤُنَا ..﴿١٤٨﴾

 

Lau Allaah Angetaka, tusingelifanya shirki, wala baba zetu.. [Al-An’aam: 148].

 

 

Hivyo kuwa muangalifu, Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akulinde, ni namna gani maneno ya wale wanaokusanya pamoja ukweli na uongo. Ni kweli kwamba Ibliys aliumbwa kutokana na moto, na Aadam ('Alayhis-salaam) aliumbwa kutokana na udongo, lakini haikubaliki kutumia kwake Ibliys kwa Aayah hizi kama ni ushahidi kwamba yeye ni bora kuliko Aadam.

 

 

Na makafiri walisema: “Angalipenda Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) tusingalimshirikisha” na hili ni kweli. Kwa sababu Atakalo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) huwa, na Asilolitaka haliwezekani. Na hakuna yeyote atakayeweza kumshirikisha bila ya uwezo wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), lakini hii ni kuruhusu Kwake [iwezekane] kwa Qadar [makadirio] Yake ya kawniyyah na si kwamba Ameiwekea ruhusa katika Shari’ah.  Kwa hilo, ingawa Allaah Amemwezesha kafiri kutokuamini, lakini Hakuruhusu hivyo wala Haridhii kwalo kama Anavyosema:  

 

إِن تَكْفُرُوا فَإِنَّ اللَّـهَ غَنِيٌّ عَنكُمْ ۖ وَلَا يَرْضَىٰ لِعِبَادِهِ الْكُفْرَ ۖ ..﴿٧﴾ 

Mkikufuru, basi hakika Allaah ni Mkwasi kwenu, na wala Haridhii kufuru kwa waja Wake. [Az-Zumar: 7].

 

 

Na ndivyo ilivyo kwa wazushi, anachanganya haki pamoja na batili. Lau ingelikuwa uzushi wake ni ubatili mtupu asingeliweza kuusambaza. Anafanya tendo la Ahlul-Kitaab (Mayahudi na Manaswara) ambao wamechanganya haki na batili, au tendo la mfanya biashara anayeghushi kwa kuchanganya bidhaa mbaya pamoja na bidhaa nzuri. Na laiti angeliweka wazi bidhaa zake mbovu, asingeliweza kuiuza na kupata pesa mara moja.

 

 

Basi tahadharini enyi watu wa Tawhiyd na Sunnah, tahadharini na njia za watu wa uzushi na matamanio. Na ni lazima mpigane nao kwa silaha ya ‘ilmu yenye kunufaisha. Ni uzuri ulioje maneno ya Shaykhul-Islaam al-Mujaddid Muhammad bin ‘Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) katika katika Kashf Shubuhaat uk. 11:

 

 

“Mjinga miongoni mwa watu wa Tawhiyd anaweza kuwashinda maelfu ya wasomi wa kikafiri kama Allaah Mtukufu alivyosema:

 

وَإِنَّ جُندَنَا لَهُمُ الْغَالِبُونَ ﴿١٧٣﴾

Na kwamba hakika jeshi Letu ndilo litakaloshinda. [As-Swaafaat: 173,

 

 

Amesema kweli (Rahimahu Allaah), kwani mzushi hatoweza kumkabili mtu wa Sunnah. Atahiyari kumkwepa kama anavyomkwepa mbwa mwitu. Mzushi ataitema sumu yake maeneo mengi na hata nyuma za kuta. Utawadhania wako pamoja lakini nyoyo zao zimegawanyika; makundi, madhehebu na ‘Aqiydah mbali mbali. Hawawatendi ila kizani, na mwishowe hudhihirika mambo yao. Huenda watu walikuwa hawatambui uhakika wao hapo zamani, lakini watu wa leo wameziona kanda na picha zao walizopiga wenyewe wakifanya ‘matambiko’ au wanazoona ni ‘ibaadah kwao. Tunamuomba Allaah kutughufuria na kutuokoa.

 

 

Mukhtasari

 

 

Sababu za kupotoka kwa watu wa uzushi ni aidha; kutokuwa na dalili, au kuwa na dalili ambayo si sahihi au kuwa na dalili sahihi ambayo haiendani pamoja na hoja zao.

 

 

Ninamuomba Allaah (‘Azza wa Jalla) Anithibitishe katika haki bayana pamoja na kila Sunni (Ahlus Sunnah wal Jama’aah) na Atuepushe na fitnah za dhahiri na zilofichika. Na Sifa Njema ni za Allaah mwanzo na mwisho wake. Na Swalah na amani ziwe juu ya Rasuli Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), nyumba yake na Swahaba zake.

 

 

 

 

Share