Mwanamke Hapati Kuswali Kazini Anaakhirisha Na Kujumuisha Swalaah Kila Siku Nini Hukmu Yake?

 

SWALI

Assaalaam Alaykum Ndungu zangu

Ndugu yetu anauliza kazini kwake hapana pahala paku Sali, upo  msikiti wa wanaume na wenyewe hawasali wote pamoja ili wakimaliza wanawake wapate fursa ya kusali. Na hapo officeni kwake hawazi kusali kumejaa wanaume hapati pahala pakujikinga ili aweze kusali.  Akirudu nyumbani kwake anasali nakimaliza kusali tu ina adhiniwa Sala ya Asri. Kuanzia Jumamosi mpaka Jumatano mambo ndio hayo.  Sasa inamjuzia kuchelewesha sala yake kila siku au anaweza kusali Adhuhuri na asri pamoja

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukran kwa swali lako ambalo ni zuri kuhusu Swalah ambayo ni nguzo kubwa ya Uislamu. bila ya Swalah basi amali zote zitakuwa hazina maana yoyote. Swalah ni ‘Ibadah moja kama ‘Ibadah nyenginezo zilizowekewa wakati mahsusi. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anatuelezea Anaposema:

 

فَإِذَا قَضَيْتُمُ الصَّلاَةَ فَاذْكُرُواْ اللّهَ قِيَامًا وَقُعُودًا وَعَلَى جُنُوبِكُمْ فَإِذَا اطْمَأْنَنتُمْ فَأَقِيمُواْ الصَّلاَةَ إِنَّ الصَّلاَةَ كَانَتْ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ كِتَابًا مَّوْقُوتًا

Mwishapo kuswali mdhukuruni Allaah, msimamapo na mkaapo na mlalapo ubavu. Na mtakapopata amani (mkawa katika salama, hapan vita), basi simamisheni Swalah (kama kawaida). Kwa hakika Swalah kwa Waumini ni faradhi iliyowekewa nyakati makhsusi. [An-Nisaa 4: 103]  

 

Wenye tafsiri ya Jalalayn wamesema: “Yaani imewekewa wakati wake, hivyo haiakhirishwi kwa wakati huo maalumu” (Jalalud Din Suyuti na Jalalud Din Mahally, Muhadhdhab Tafsiir ul Jalalayn iliyohakikiwa na Sh. ‘Ali bin Mustafa Khaluuf, uk. 96).

 

Sheikh Al-Amiyn bin Aliy Mazrui anasema: “Hapo waamrishwa Islamu watekeleze Swalah kwa ukamilifu wake pamoja na kutunga nyakati zake” (Tafsiri ya Qurani Tukufu, Mjalada wa 2, uk. 142).

 

Sheikh Muhammad ‘Ali as-Swaabuny anasema yafuatayo kuhusu aya hii: “Swalah ni faradhi kwa wakati wake maalumu, haifai kabisa kuichelewesha kabisa” (Swaf-watut Tafaasiir, Mj. 1, uk. 302). Na Dkt. Muhammad Sulaymaan ‘Abdallah al-Ashqaar katika mukhtasari wa Tafsiri ya Fat-hul Qadiir ameeleza yafuatayo: “Yaani mutakapokuwa katika hali ya amani na hakuna adui yeyote ambaye munamuogopa. Basi simamisheni Swalah kwa kuijia ile inapoingia wakati wake kwa njia ya kisheria kwa kumtaja Allaah سبحانه وتعالى  na kutekeleza nguzo zake na kuwa na utulivu . Kwa hakika Swalah kwa Waumini ni faradhi iliyowekewa nyakati makhsusi yaani wakati maalumu unaojulikana kwa kila moja wapo ina mwanzo na wakati wake wa mwisho. Haifai kuikadimisha (kuileta mbele) au kuiakhirisha. Hakika Allaah سبحانه وتعالى      Ameifanya ni faradhi kwa waja wake na kuwawekea wakati makhsusi. Haifai kwa yeyote kuitekeleza kwa nyakati nyengine zisizokuwa hizo isipokuwa kwa udhuru wa kisheria kama kwa kulala au kusahau au mfano wake. Na kwa hilo Akatuamuru kuswali hata katika hali ya hofu pamoja na kubeba silaha na kwa njia iliyobainishwa na wala hakuwapatia idhini kuichelewesha kwa wakati uliowekwa” (Zubdatut Tafsiir Min Fathil Qadiir, uk. 120).

 

Kwa tafsiri zote ambazo tumetoa ni wazi kabisa kuwa bila ya udhuru wa kisheria haifai kuiakhirisha Swalah. Hivyo, inatakiwa kila Muislamu aswali Swalah kwa wakati wake makhsusi uliowekwa. Na kwa dada yetu njia ya kufanya ni kutafuta nafasi sehemu yoyote awe ni mwenye kuswali kwani ardhi imefanywa ni Msikiti kwa Ummah huu. Mwenye kuemewa (kushindwa) kusimama katika Swalah ya faradhi kwa ajili ya ugonjwa au jambo jengine (kama kuwa katika mahali ambapo hapana nafasi ya kusimama au akawa katika chombo ambacho akisimama ataanguka na kadhalika) ataswali kwa kukaa kitako cha “Iftiraashi”. Ikiwa hawezi kukaa kitako hicho basi atakaa kitako awezacho. Akishindwa kukaa ataswali kwa kulala ubavu (aelekee Qiblah kwa mwili wake na uso wake). Akiemewa na kulala ubavu, ataswali kwa kulala chali (tani) kwa maungo yake na aelekee Qiblah kwa uso wake. Akiemewa kulala kwa chali ataashiria kwa kichwa; asipoweza ataashiria kwa macho; na ikiwa pia hawezi basi ataipitisha Swalah katika moyo wake. Allah haikalishi nafsi ila uweza wake (Sauti ya Haki, Toleo nambari 3/ 76, uk. 3, September 1976/ Ramadhan 1396, Muhariri ni Sheikh Mohamed Kasim Mazrui).

Kwa kauli hiyo hapo juu udhuru wa kuitoa Swalah katika wakati wake inaondoka kabisa na hivyo mtu ikiwa nafasi katika ofisi ni ndogo ya kusimama anaweza kuswali kwa kukaa.

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share