Ndoa Mara Mbili Na Mtu Mmoja Nini Hukmu Yake?

Ndoa Mara Mbili Na Mtu Mmoja Nini Hukmu Yake?

 

Alhidaaya.com

 

 

 

SWALI:

 

 

asalam aleykum,

 

sheikkh wangu nimeshindwa kuelewa. au kufahamu iweje ndoa ikafungwa mara mbili na wahusika ni wale wale, sasa naomba unieleweshe kwa ufasaha. Na sababu iliyo fanya ndoa ifungwe mara mbili ni upande mmoja wa bwana harusi, ilifungwa ndoa ya kisiri pasi na kuwatambulisha wenzi wao

 

Sasa upande wa bibi harusi bila kujua na wazazi wake wakawa wamepanga tarehe ndipo hapo ikafungwa kwa mara ya pili.

Wahaza asalam aleykum

   

 

JIBU:

 

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Swali kama hilo  limekuwa ni tatizo sugu katika maeneno yetu na nchi nyengine za Kiislamu. Inatakiwa ifahamike kuwa katika Uislamu hakuna kabisa ndoa ya siri, bali ndoa inapaswa kutangazwa kama ilivyothibiti katika Hadiyth:

 

 

عَنْ عَامِرِ بْنِ عَبْدِ اَللَّهِ بْنِ اَلزُّبَيْرِ، عَنْ أَبِيهِ، أَنَّ رَسُولَ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ  قَالَ:{أَعْلِنُوا اَلنِّكَاحَ} رَوَاهُ أَحْمَدُ، وَصَحَّحَهُ اَلْحَاكِمُ

Kutoka kwa ‘Aamir bin ‘Abdillaah bin Az-Zubayr kutoka kwa baba yake amesema kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  amesema: “Tangazeni ndoa.” [Ahmad na akaisahihisha Al-Haakim]

 

Na hivyo basi ndoa ina masharti yake ili ipate kusihi. Miongoni mwayo ni:

 

 

1. Kupatikana kwa mashahidi wawili waadilifu kama alivyosema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

لا نكاح إلا بوليّ وشاهدين

 

“Hakuna Nikaah (Ndoa) pasi na walii na mashahidi wawili.” [Al-Bayhaqiy na ad-Daaraqutwniy, At-Twabaraaniy na Swahiyh Al-Jaami’ (7558)]

 

 

 

2.  Baba au walii wa mke ni lazima aweko na kutoa idhini kutokana na Hadiyth:  

 

عَنْ عَائِشَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا قَالَتْ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ {أَيُّمَا اِمْرَأَةٍ نَكَحَتْ بِغَيْرِ إِذْنِ وَلِيِّهَا، فَنِكَاحُهَا بَاطِلٌ، فَإِنْ دَخَلَ بِهَا فَلَهَا اَلْمَهْرُ بِمَا اِسْتَحَلَّ مِنْ فَرْجِهَا، فَإِنِ اشْتَجَرُوا فَالسُّلْطَانُ وَلِيُّ مَنْ لَا وَلِيَّ لَهُ}

Kutoka kwa ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) kwamba: amesema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)    amesema: “Mwanamke yeyote anayeolewa bila idhini ya walii wake ndoa yake ni batili. (Mume) akimuingilia mwanamke huyo ana haki ya kupata mahari kwa alichohalalishia tupu yake. Wakishindana  basi sultani (mtawala) ni walii wa asiyekuwa na walii.” [At-Tirmidhiy, Abuu Daawuwd, Ibn Maajah]  

 

 

3.  Kukubali kwa wanandoa miongoni mwa mengine kwa dalili:

 

 عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ أَنَّ رَسُولَ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ قَالَ: {لَا تُنْكَحُ اَلْأَيِّمُ حَتَّى تُسْتَأْمَرَ، وَلَا تُنْكَحُ اَلْبِكْرُ حَتَّى تُسْـتَأْذَنَ" قَالُوا : يَا رَسُولَ اَللَّهِ، وَكَيْفَ إِذْنُهَا ؟ قَالَ: " أَنْ تَسْكُتَ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  amesema: “Asiolewe mke mkuu mpaka atakwe amri, wala asiolewe mwanamwali mpaka atakwe idhini. Maswahaba wakasema: Ee Rasuli wa Allaah! Ni vipi idhini yake (huyo mwali)? Akasema: Ni kunyamaza.” [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

Sharti moja tayari likuwa halipo nalo ni kupatikana idhini ya walii kwani familia ya mke ilikuwa haijui. Na ikiwa mume na mke walichukuana kwa mwenye kuozesha wakawa wao watatu pekee hapo pia mashahidi hawakupatikana. Ikiwa itakuwa hivyo basi huyo mume na mke walikuwa wakizini kabla hiyo ndoa ya pili kufanyika.

 

 

Uislamu ni Dini kamili ambayo inakidhi mahitaji yetu katika hii dunia, tukikengeuka tu na maagizo yake basi huwa na tatizo au matatizo. Na ndio Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

 

وَمَنْ أَعْرَضَ عَن ذِكْرِي فَإِنَّ لَهُ مَعِيشَةً ضَنكًا وَنَحْشُرُهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ أَعْمَىٰ ﴿١٢٤﴾ قَالَ رَبِّ لِمَ حَشَرْتَنِي أَعْمَىٰ وَقَدْ كُنتُ بَصِيرًا ﴿١٢٥﴾ قَالَ كَذَٰلِكَ أَتَتْكَ آيَاتُنَا فَنَسِيتَهَا ۖ وَكَذَٰلِكَ الْيَوْمَ تُنسَىٰ ﴿١٢٦﴾

Na atakayejitenga na ukumbusho Wangu basi hakika atapata maisha ya dhiki, na Tutamfufua Siku ya Qiyaamah hali akiwa kipofu. Atasema: Rabb   wangu! Kwa nini Umenifufua kipofu, na hali nilikuwa naona? (Allaah) Atasema: Hivyo ndivyo, zilikufikia Aayaat Zetu ukazisahau   na kadhaalika leo umesahauliwa. [Twaahaa: 124 – 126]

 

 

Sasa, katika nidhamu ya Kiislamu ndoa hufungwa mara moja peke yake, na hivyo inapofungwa huwa ndio basi haifungwi tena labda tu waachane na eda imalizike baada ya kumalizika eda ndio ndoa mpya inaweza fungwa ikiwa wanaona kuwa wanaweza kuishi pamoja.

 

 

Mara nyingi ndoa hizi huwa zikifungwa namna ulivyotaja kwa sababu za itikadi za kishirikina ambazo Muislamu wa kweli hafai kabisa kuwa na sifa kama hiyo au kwa sababu huyu ni mke wa pili na mume hataki mke wa kwanza ajue.

 

 

Lakini katika njia zote hizo mbili wazazi wa mke huwa wanajuwa.

 

Hivyo, kulingana na swali lako ki Shariy’ah ile ndoa ya kwanza haitakuwa ni ndoa sahihi na ikiwa waliishi pamoja na wakakutana kimwili itabidi waombe maghfirah na watubie sana kwa Rabb wao ili Awaghufurie.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share