Mume Kasema Nikifanya Jambo Nimetalikika Nami Nimefanya Na Kumdanganya Nini Hukmu Yake?


SWALI:

Asalaam Alaikuum

Kwanza napenda kutoa shukran za dhati kuwa ipo website hii inaweza kutusaidia na sisi na vilevile nawapa shukran wanaotusaidia majibu m/mungu ishaallah atawazidishia ujuzi wao amen.

suali langu mimi  ni kuwa nina mume wangu tunakua tunagombana na pia keshawahi kuniwacha talaak mbili aina kama hii yaani nikifanya nini nimeachika sasa hii ya mara hii nilimuambia kitu katika hivyo kugombana kua ni nimefanya kitu fulani lakini pia nilikua namdanganya tu sijawahi kukifanya hicho kitu sasa  na ni katika vitu alivyo kua akiniambia nikifanya nishaachika sasa ndio kaniambia kama umekifanya hicho kitu basi mimi sio mke wangu tena lakini pia mpaka uniapie na kama hujaniapia basi sio mke wangu sasa kakaa halafu kabadilisha kauli kasema ameshaiondoa hio kauli kua lazima nimuapie basi nisiape tena  kaondoa kauli hiyo kwani mimi sijamuapia nimemuambia tuu sijakifanya hicho kitu naomba munisamehe kama hamunifahamu kwani najitahid kuandika ili munielewe inshaallah mutanielewa na namuomba M\Mungu pia anisamehe na mimi kusema uongo  lakini pia kama itakua mpaka mimi niape basi mimi sitaki muapia kwani ndio tabia yake kila siku nikifanya nini nimeachika  basi nawatakia kila la heri na naomba munijibu upesi ikiwezekana. Ameen


 

 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), ahli zake, Swahaba zake (Radhiya Allahu 'anhum) na walio wafuata kwa wema mpaka siku ya Qiyaamah.

Shukran dada yetu kwa swali lako hilo na kwa hakika haya maswali ya talaka ni mengi na ni nyeti. Kama tulivyokariri mara kadhaa ya kwamba katika halali inayochukiza sana mbele ya Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) ni talaka. Hivyo, tunawanasihi wanaume wasiwe ni wenye kufanya haraka au mzaha katika mas-ala hayo ya talaka. Kwani Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anatuelezea umuhimu wa kukaa na wake zetu vizuri kama Alivyosema:

“Na kaeni nao kwa wema, na ikiwa mmewachukia, basi huenda mkakichukia kitu, na Mwenyezi Mungu Ametia kheri nyingi ndani yake” ().

Talaka amepatiwa mume kwa ajili ya utulivu wake na kuweza kusubiri na kuzingatia kabla ya kuchukua hatua yoyote kama hiyo ambayo inaathiri familia na kizazi kijacho. Inabidi mume apatiwe ushauri nasaha katika jambo la kuishi kwa wema na mkewe la sivyo basi matatizo haya yataendelea kuwepo na nyumba kama hiyo itavunjika hivyo kuwaletea matatizo watoto walioruzukiwa.

Inatakiwa kwamba mume na mke wanapokosana kabla ya kuchukuliana hatua yoyote wakae chini na kutatua tatizo hilo kwa hali ya utulivu na amani. Haina haja kuropokwa maneno kisha kuja kujuta baadae. Na kama tulivyosema kuwa katika mas-ala ya talaka haina mzaha kama alivyotuambia hivyo Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

Uongo katika Uislamu ni mbaya na ni miongoni mwa sifa za unafiki kwa mwenye kulifanya hilo. Na ni kosa ambalo Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema kuwa Muumini hawezi kuwa ana sifa hiyo japokuwa anaweza kuwa muoga au akafanya kosa jengine. Kwa kosa hilo unatakiwa uombe msamaha kutoka kwa Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) na utubie Kwake na usirudie tena kosa hilo na Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasamehe madhambi yote. Lakini mbali na kusema hayo swali la talaka katika hii mas-ala yako bado limebakia pale pale na hili haliwezi kuondolewa kwako wewe kutubia wala mume kusema basi nimeondoa maneno fulani niliyoyasema.  

Kama ulivyoashiria katika swali lako kuwa tayari mume wako amekupatia talaka na hivyo imebaki talaka moja tu ili muachane kabisa kabisa na ikitokea hiyo huwa hamuwezi kurudiana mpaka mke aolewe na mume mwengine kisha aachwe ndipo wakati huo wataweza kurudiana ikiwa kweli wanataka kuendelea kuishi pamoja.

 

Katika talaka hii ambayo imetolewa na mumeo ya mwisho ni kuwa imeekewa masharti – “ikiwa umekifanya hicho kitu basi mimi sio mke wangu tena lakini pia mpaka uniapie na kama hujaniapia basi sio mke wangu sasa”. Hapa tunapata masharti mawili:

1. Ikiwa umefanya hicho kitu si mke wangu, lakini wewe hujafanya, hivyo

    sharti hii limeondoka, na

2.  Kuapa, ambayo pia ameiondoa baadae.

Hivyo, sharti hizo mbili zote zimeondoka na talaka kuwa haipo tena. Lakini kwa sababu ya kuondoa kiapo chake inabidi mume atoe kafara kwa hilo na asipofanya atakuwa ni mwenye kupata dhambi. Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema:

“Allah Hatakushikeni kwa viapo vyenu vya upuuzi, lakini Atakushikeni kwa mnavyoapa kweli kweli kwa makusudio. Basi kafara yake ni kuwalisha masikini kumi kwa chakula cha wastani mnachowalisha ahali zenu, au kuwavisha, au kumkomboa mtumwa. Asiye pata hayo, basi afunge siku tatu. Hii ndiyo kafara ya viapo vyenu mnapoapa. Na hifadhini yamini zenu. Namna hivyo Allah Anakubainishieni Aya Zake ili mpate kushukuru” (5: 89).

Hivyo, kwa sababu ya kuvunja yamini anatakiwa:

1- Kuwalisha masikini kumi wajiba wa siku moja, ikiwa hawezi basi,

2-   Kuwavisha masikini kumi kwa kivazi kilichozowewa, ikiwa hawezi basi,

3- kumuacha mtumwa huru, na ikiwa hawezi basi,

      4-  kufunga siku tatu, nazo ziwe mfululizo kama alivyofasiri Ibn Mas‘uud (Radhiya Allahu 'anhu)

Lakini nasaha yetu ni kuwa mumeo wako anataka azungumziwe kuhusu hasa mas-ala ya kuapa kila wakati na kuweka masharti pamoja na talaka hayai. Na mufahamu kuwa akitoa talaka ingine ndio mumeachana kabisa kabisa mpaka wewe uolewe na mume mwengine, baadae uachwe ndio muweze kurudiana kwa kauli ya Allah (Subhaanahu wa Ta'ala):

“Talaka ni mara mbili. Kisha ni kukaa kwa wema au kuachana kwa vizuri. Wala si halali kwenu kuchukua chochote mlichowapa wake zenu, ila ikiwa wote wawili wakiogopa ya kwamba hawataweza kushikamana na mipaka ya Allaah. Basi mkiogopa kuwa hawataweza kushikamana na mipaka ya Allaah  hapo itakuwa hapana lawama ikiwa mwanamke atajikomboa. Hii ndiyo mipaka ya Allaah; basi msiikiuke. Na watakaoikiuka mipaka ya Allaah, hao ndio madhaalimu. Na kama amempa talaka (ya tatu) basi si halali kwake baada ya hayo mpaka aolewe na mume mwengine. Na akiachwa basi hapana ubaya kwao kurejeana wakiona kuwa watashikamana na mipaka ya Allaah” (2: 229 – 230).

Na Allah Anajua zaidi.

 

Share