Haki Za Mke Mkubwa Na Mke Mdogo

 SWALI: 

Assalam  alikum wa rahmatulah wa barakatuh 

Nina rafiki yangu mtu wa Kenya ameolewa na mume mwenye mke, mke mkubwa mume hajamuingilia miaka mitatu sasa alimuoa kijamaa bint Ami na ameshindwa kumleta hapa yuko Tanzania na yule mke amejua kama mumewe ameoa lakini mume amemwambia kua ameoa kimaslaha na haishi na huyu mke mpya lakini si kweli anaishi nae, na pia mume anamjali sana bint Ami kushinda huyu na huyu hajatulia kinafsi anahisi huzuni, naomba utujulishe haki ya mke mkubwa na mke mdogo kutoka kwa mume ni nini? Na huyu mke mdogo unamshauri nini, na kuhusu huyu mume mafrudh awe vipi kuwa adel wake zake?

JAZAKA ALLAH KHAYRA

  


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ahli zake, Sahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum jamiy'an) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Swali hili ni muhimu sana kama yalivyo maswali mengine yanayohusiana na ndoa. Na haya matatizo ya ndoa na talaka ni miongoni mwa mas-ala ya kijamii yanayozoretesha jamii yetu. Na mara nyingi matatizo yanatukumba kwa kutotaka kufuata kanuni na sheria zilizowekwa na Uislamu. Mojawapo ya hilo ni hili la uke wenza na ndio Allah Akatueleza yafuatayo:

 

“Basi oeni mnaowapenda katika wanawake, wawili au watatu au wane. na mkiogopa kuwa hamwezi kufanya uadilifu, basi mmoja tu” (4: 3).

 

Katika aayah ya hapo juu imeweka baadhi ya vikwazo na masharti ya uke wenza na hivyo haifai kwa mtu kukiuka.

 

Ya kwanza: Mwanamme hawezi kuoa wake zaidi ya wanne.

 

Ya pili: Mwanamme anatakiwa atekeleze uadilfu baina ya wake zake. Na jambo hili ni wajibu kwake. Uadilifu unajumlisha makazi, chakula, mavazi, kuwatendea wema, kuwagawia muda sawa, na kadhalika. Na katika haya mume anabeba majukumu yote na ataulizwa Siku ya Kiyama kwa kutotekeleza kw amoja wapo ya tuliyo yataja. Kwa yule ambaye hana hakika ya kufanya uadilifu baina yao, Qur-aan inamwelekeza: “Hivyo oa mmoja tu”.

 

Haya yanatuelekeza kuwa wake wote wana haki sawa kabisa na hadhi kwa mume wao. Haifai kumpendelea mmoja juu ya mwengine. Na hii inamaanisha katika sheria ya Kiislamu, lau mume hatoweza kutoa msaada wa kutosha kwa yeyote miongoni mwa wake zake, huyo mke anaweza kwenda kwa Qadhi (au mahakama ya Kiislam) kushitaki na kudai talaka.

 

Na Allah Anajua zaidi.

 

 

Share