Vipi Naweza Kuimarisha Ndoa Yangu?

 

SWALI:

Mimi ni mwanamke mwenye umri wa miaka… ninaeishi …. mjini Zanzibar, bado sijaolewa kwa muda huu, Allah

akipenda natarajia kufunga ndoa mfunguo sita mwaka  (2006) sasa ninachokiomba unipe elimu kupitia kwenye Qur-aan na Hadiyth za mtume ili niweze kuinusuru ndoa yangu na nia yangu nataka kufanya yote kwa mume kwa ajili ya Allah.


 

JIBU  

Sifa zote njema Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allahu 'anhum jamiy'an) na watangu wema mpaka Siku ya Qiyaamah.

Kwanza kabisa tunaoma radhi sana kwa kuchelewa kukujibu Swali lako, jambo ambalo limetushinda nguvu. Tunatumai utafahamu hali  ngumu zetu tulizonazo za kazi hizi wa wingi wa maswali na upungufu wa wanaojibu maswali haya.

Ukitaka nyumba yako iimarike, inakulazimu uzifahamu haki zako kwa mume wako, na mume wako nae analazimika kuzifahamu haki zake kwako.

Baadhi ya haki za Mume kwa Mke:

1. Unatakiwa mwanamke wa Kiislamu umtii mume wako kwa kila anachokuamrisha,

Uzindushi: huo utiifu unatakiwa usiambatane na aina yoyote ya kumuasi Mwenyezi Mungu ndani yake, kama vile Mume kumuamuru mke wake avue hijabu, au aache kuswali, au kutaka kumjamii akiwa ndani ya siku zake, au akataka kumlawiti, n.k.

Amesema Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) "Si ruhusa kufanya utiifu katika jambo la kumuasi Mwenyezi Mungu, Hakika ya utiifu unatakiwa ufanyike katika mambo yaliyo mema pekee" Al-Bukhaariy Hadiyth Namba 7257, na Muslim Hadiyth Namba 1840;

2. Mwanamke wa Kiislamu unatakiwa ukae nyumbani, na usitoke ila kwa ruhusa ya Mume,

Mwenyezi Mungu anasema: "Na kaeni majumbani mwenu, wala msioneshe mapambo yenu kama walivyokuwa wakionesha mapambo yao wanawake wa zama za Ujima" (Al-Ahzaab:33)

3. Mwanamke wa Kiislamu unatakiwa umtii mumeo pindi anapokuita kitandani;

4. Usimruhusu yeyote kuingia ndani ya nyumba ya mumeo ila kwa ruhusa yake;

5. Usifunge funga ya Sunnah wakati mumeo yupo mjini ila kwa ruhusa yake.

Anasema Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), "Si halali kwa mwanamke kufunga (funga ya sunnah) na mumewe akiwa yupo mjini ila kwa ruhusa yake, na wala asiruhusu (mtu) kuingia ndani ya nyumba ya mume wake ila kwa ruhusa yake.";

6. Usitoe chochote katika miliki ya mumeo ila kwa ruhusa yake:

Anasema Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), "Hana ruhusa mwanamke yeyote kutoa kitu chochote kutoka kwenye nyumba ya mume wake ila kwa idhini yake" (Abu Dawuud Namba 3565 na At-Tirmidhiy 670);

7. Unatakiwa umuhudumie mumeo pamoja na watoto wake kwa kutoa huduma za nyumbani;

8. Unatakiwa umuhifadhi mumeo kwa kumlindia heshima yake, mali yake na watoto wake;

9. Unatakiwa umshukuru mumeo na wala usiukanushe wema wake, na utangamane nae kwa wema.

Anasema Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) " Mwenyezi Mungu Hatomuangalia mwanamke asiyemshukuru mumewe na kutoridhika nae" Sunan An-Nasaaiy Namba 249;

10. Ujipodoe na ujirembe kwa ajili ya mumeo;

11. Usijikweze endapo utamsaidia yeye na watoto wake kutoka katika mali yako;

12. Unatakiwa uridhike na kidogo, na utosheke nacho, na wala usimlazimishe zaidi ya uwezo wake.

Anasema Mwenyezi Mungu "Na atoe mwenye wasaa kwa kadiri ya wasaa wake; na yule ambae amepungikiwa riziki yake, atoe katika kile alichopewa na Mwenyezi Mungu; Mwenyezi Mungu hamkalifishi mtu yoyote ila kwa kadiri ya Alichompa Atajaalia Mwenyezi Mungu baada ya dhiki faraja." (At-Twalaaq: 7);

13. Usifanye jambo litakalomuudhi na kumkasirisha;

14. Unatakiwa uishi na Wazazi na ndugu wa mume kwa wema;

15. Ujitahidi udumu na mumeo, wala usiombe talaka pasi na sababu za kisheria;

16. Unatakiwa ujiepushe na mapambo pindi utakapofiwa na mumeo kwa muda wa miezi minne na siku kumi;

 

Baadhi ya haki za mke kwa mume:

 

1. Kuishi na mke kwa wema;

Anasema Mwenyezi Mungu, "Na ishini nao kwa wema…" (An-Nisaa :19)

Na Anasema tena Mwenyezi Mungu: "Na Wanawake nao wanayo haki ya kufanyiwa wema na waume zao"  (Al-Baqarah: 228);

 

2, 3, 4, Kumlisha, kumvisha, na kumpa makazi mnasaba (yanayowafiki);

 

5. Kuwa mpole kwa mke, kucheza nae na kuutilia maanani udogo wa umri wake;

6. Akeshe baadhi ya nyakati pamoja na mke wake wakisimuliana khabari mbalimbali;

7. Amuelimishe mambo yanayoihusu dini yake na amuhimize katika utiifu

8. Ayafumbie macho baadhi ya makosa ya mke iwapo hayaikiuki sheria ya Mwenyezi Mungu;

9. Wala asimkere kwa kumpiga usoni au kumkashifu;

10. Asimuhame pindi anapomuhama - ila iwe ndani ya nyumba yake;

11. Amuhifadhi kwa maneno na vitendo;

12. Endapo ataombwa ruhusa kwenda kuwatembelea ndugu na jamaa na akawa na uhakika wa usalama wa huko aendako, anatakiwa amruhusu;

13. Hatakiwi kutaja siri za mkewe na kueneza dosari zake;

14. Mume nae anatakiwa ajipambe kwa ajili ya mke wake, kama ambavyo mke hutakiwa kujipamba kwa ajili mume wake;

15. Anatakiwa awe na dhana njema juu ya mke wake;

16. Endapo mume ana mke zaidi ya mmoja, anatakiwa awe muadilifu katika kugawanya chakula, mavazi, makazi, malazi, n.k.

Haya na mengineyo mkiyatimiza nyumba yenu insha Allah itaimarika.

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share