Akishatoa Mahari Anayo Haki Kumuamrisha Au Kumkataza Jambo Kwa Aliyemchumbia?

SWALI:

 

Wakati mwanamke nishamposa na nimeshamtolea mahari nina haki yoyote ile ya kumwambia kitu mfano asitoke kila wakati na je yeye ana haki yoyote ile kwa kumwambia mchumba wake kitu chochote kile?  - Ni haki kumchezea mkeo mwili wake wote? Natumai nitapata jibu zuri


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kumdhibiti mke baada ya kumtolea mahari. Mambo ya kijamii na hasa ya ndoa ni nyeti sana kwa kiasi ambacho Uislamu umeyapatia kipaumbele kusije kukatokea mushkeli ambao hautarajiwi. Unapomposa msichana na pengine kutoa mahari kwa sababu ya kukubaliwa posa yako bado huwa kisheria hajawa mke wako hivyo huna udhibiti. Bado mwanamke huyo yuko katika udhibiti na amri ya wazazi wake.

 

Jambo ambalo unaweza kufanya ni kuweza kukubaliana wakati wa posa pamoja na wazazi wake kuhusu hilo na yeye mwenyewe kuridhia. Ile haki ambayo umepatiwa ni kuweza kumtembelea na kukutana na mkeo mtarajiwa nyumbani kwao sio katika faragha bali akiwa na aliye maharimu wake. Yote haya ni kuweza kudhibiti watu hao wawili wasiwe ni wenye kuingia katika maasiya. Kutoa mahari si dhamana kuwa utamuoa bali zipo ndoa nyingi zilizovunjika kwa sababu moja au nyingine. Katika muda huo, ima mwanamke au mwanamme anaweza kuivunja hiyo ndoa kisheria bila ya wasiwasi wowote.

 

Ama kuhusu mkeo ni ruhusa kabisa kuchezea naye mwili wake wote kama alivyo yeye mwenye ruhusa kuuchezea mwili wako wako. Kitu kinacho katazwa ni kufanya mapenzi kupitia sehemu ya nyuma (liwati).

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share