Ibaadah Tatu Usiache Maishani Mwako: 1-Wasiya Wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Swiyaam Siku Tatu Kila Mwezi

 

'Ibaadah Tatu Usiache Kutenda Maishani Mwako

 

Wasiya Wa Kwanza Wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)

Swiyaam Siku Tatu Kila Mwezi

 

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Mambo matatu kutendwa kila mwezi ambayo Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameyausia kwa Waumini ni kama yalivyotajwa katika Hadiyth ifuatayo:  

 

 

عن أبي هريرة رضي الله عنه قال: أَوْصَانِي خَلِيلِي صَلَّى اللهُ عَلَيهِ وَسَلَّمَ بِثَلاثٍ: صِيَامِ ثَلاثَةِ أَيَّامٍ مِنْ كُلِّ شَهْرٍ، وَرَكْعَتَيْ الضُّحَى، وَأَنْ أُوتِرَ قَبْلَ أَنْ أَنَامَ.  رواه البخاري ومسلم

Imepokelewa kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: “Ameniusia khalili wangu (rafiki mwandani) (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) swiyaam (kufunga) siku tatu kila mwezi na (kuswali) Rakaa mbili za Adhw-Dhwuhaa na niswali Witr kabla ya kulala”. [Al-Bukhaariy na Muslim]

  

 

 

Wasiya wa Kwanza:

 

Swiyaam (kufunga) Siku Tatu ambazo thawabu zake ni kama thawabu za Swiyaam mwaka mzima kama ilivyothibiti katika Hadiyth ifuatayo:

 

عَنْ أَبي ذَرٍّ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللهِ صَلَّى اللهُ عَلَيهِ وَسَلَّمَ:((مَنْ صَامَ مِنْ كُلِّ شَهْرٍ ثَلاثَةَ أَيَّامٍ فَذَلِكَ صِيَامُ الدَّهْرِ)) فَأَنْزَلَ اللهُ تُصْدِيقَ ذَلِكَ في كِتَابِهِ الْكَرِيمِمَن جَاءَ بِالْحَسَنَةِ فَلَهُ عَشْرُ أَمْثَالِهَا ۖ ﴿١٦٠﴾، الْيَوْمُ بِعَشَرَةِ أَيّامٍ . أخرجه أحمد والترمذي وقال حديث حسن ، والنسائي وابن ماجه وابن خزيمة

Imepokelewa kutoka kwa Abu Dharr (Radhwiya Allaahu ‘anhu). Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam0 amesema: ((Yeyote atakayefunga (Swiyaam) kila mwezi siku tatu, ni sawa na swiyaam ya mwaka mzima, kisha Allaah Akateremsha Aayah ithibitishayo hayo:

 

مَن جَاءَ بِالْحَسَنَةِ فَلَهُ عَشْرُ أَمْثَالِهَا ۖ

 

 Atakayekuja kwa ‘amali njema basi atapata (thawabu) kumi mfano wa hiyo. [Imepokewa na At-Tirmidhiy na amesema Hadiyth Hasan, An Nasaaiy na Ibn Maajah, Ibn Khuzaymah na ameisahihisha Shaykh Al-Albaaniy katika Al-Irwaa (4/102)]. Aayah: Surah Al-An’aam (160)]

 

 

Fadhila za Swawm ni nyingi mno. Na siku za kufunga (swiyaam) za Sunnah kila mwezi zinajulikana kuwa ni Jumatatu na Alkhamiys kwa mwenye uwezo wa kufunga siku hizo. Ama ikiwa una udhaifu fulani wa swawm basi ndugu Muislamu, usiache swiyaam (kufunga) angalau siku tatu kwa mwezi upate thawabu za swiyaam mwaka mzima. Na kufanya hivyo utakuwa unatimiza wasia mmojawapo wa Rasuli (Swalla Allaahu’ alayhi wa aalihi wa sallam) aliowanasihi Swahaba zake; Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) na katika Hadiyth nyengine Abu Ad-Dardaai (Radhwiya Allaahu 'anhu).

  

Basi ikiwa kusudiko lako ni kufunga (swiyaam) siku tatu pekee, funga Ayyaamul Biydhw (Masiku Meupe) ambayo maelezo na fadhila zake ni kama ifuatavyo:   

 

Maana Ya Biydhw:  Yameitwa ‘Biydhw’ (meupe) sababu usiku wa siku hizo hung'aa kutokana na mwanga wa mwezi. Ayyaam Al-Biydhw (Masiku Meupe) tarehe zake ni 13, 14 na 15 katika kila mwezi wa kalenda ya Kiislamu.

 

Fadhila za kufunga Swiyaam masiku hayo ni zifuatazo:

 

 عَنْ جريرٍ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ عَن النَّبِيِّ صَلَّى اللهُ عَلَيهِ وَسَلَّمَ قَالَ  : ((صِيَامُ ثَلاثَةِ أَيَّامٍ مِنْ كُلِّ شَهْرٍ صِيَامُ الدَّهْرِ ، أَيَّامُ الْبِيضِ صَبِيحَةَ ثَلاثَ عَشَرَةَ وَأَرْبَعَ عَشَرَةَ وَخَمْسَ عشَرَةَ))    

 Imepokelewa kutoka kwa Jariyr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Swiyaam (kufunga) siku tatu kila mwezi ni sawa na swiyaam ya mwaka; na masiku meupe ni tarehe kumi na tatu, kumi na nne na kumi na tano [13, 14, 15]))  [An-Nasaaiy (2420)  na ameisahihisha Al-Abaaniy katika Swahiyh At-Targhiyb (1040)]

 

Na pia,

 

 عن أبي ذر رضي الله عنه: قال لي رسول الله صلى الله عليه وسلم : ((يَا أَبَا ذَرٍّ ، إِذَا صُمْتَ مِنَ الشَّهْرِ ثَلاثَةَ أَيَّامٍ فَصُمْ ثَلاثَةَ عَشَرَ وَأَرْبَعَةَ عَشَرَ وَخَمْسَةَ))

Imepokelewa kutoka kwa Abu Dharr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliniambia: ((Ee Abu Dharr! Endapo utafunga (swiyaam) siku tatu za kila mwezi, basi funga siku ya 13, ya 14, na ya 15)) [Imepokewa na At-Tirmidhiy na kasema Shaykh Al-Albaaniy kuwa ni Swahiyh]

 

Na pia,

 

 قال صلى الله عليه وسلم: ((أَلا أُخْبِرُكُمْ بِمَا يُذْهِبُ وَحَرَ الصَّدْرِ صَوْمُ ثَلاثَةِ أَيَّامٍ مِنْ كُلِّ شَهْر))

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Je, nikujulisheni jambo litakaloondosha uovu wa moyo? Ni swiyaam (kufunga) siku tatu kila mwezi)) [An-Nasaaiy 2/2386 na ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh An-Nasaaiy (2249)]

 

Asw-Swuyuutwiy (Rahimahu Allaah) amesema katika An-Nihaayah: “Uovu wa moyo ni; udanganyifu, wasiwasi, na imesewma pia ni uhasidi, chuki, na imesemwa pia uadui na imesemwa ghadhabu”

 

Alhidaaya inajaribu kuwakumbusha kwa kuweka tangazo   kila mwezi kabla ya kufika tarehe hizo za   Ayyaamul-Biydhw. 

 

 

Share