Sifa Gani Za Kutafuta Mke?

SWALI:

asalaam aleykum

mimi naomba kuuliza lifuatalo

.naimba mnisaidie kunitajia sifa au jinsi ya kuchagua mchumba kama muonogozo wetu(qur-an) unavyosema kwa lengo la koua au koulewa 

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum)  na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukran kwa swali lako hilo zuri. Uteuzi wa mwenza katika ndoa ni jambo muhimu sana ambalo linatakiwa lizingatiwe au sivyo tutaingia katika balaa kubwa katika maisha yetu ya hapa duniani.

Ndoa ni jambo ambalo limepatiwa kipaumbele na Uislamu kwa kuwa ni Sunnah ya Manabii na Mitume na watu wema. Ndoa ni maumbile ambayo mwanadamu amepatiwa na Allah Aliyetukuka. Katika Uislamu hakuna utawa na kujitenga na majukumu ya kimaisha na kujenga jamii. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hakika Allah ametubadilishia utawa kwa Uislamu ulionyooka” (al-Bayhaqiy). Pia amesema: “Nami naoa wake, mwenye kukengeuka na Sunnah yangu basi si katika mimi” (al-Bukhaariy na Muslim).

Ndoa ni maslahi ya kijamii, hivyo ina faida nyingi. Miongoni mwayo ni:

1.                Kuhifadhi jinsi ya mwanadamu:

Kwa ndoa wanadamu wanaendelea kubakia katika mgongo wa ardhi. Allah Aliyetukuka Anasema: “Na Allah Amekuumbieni wake katika jinsi yenu, na Akakujaalieni kutoka kwa wake zenu watoto na wajukuu” (16: 72).

 2.   Kuhifadhi nasaba za watu.

 

3.                Kusalimika jamii kutoka kupotoka kimaadili: Kwa ajili hiyo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwahimiza sana vijana kuoa pale aliposema: “Enyi kongamano la vijana! Mwenye uwezo wa kuoa basi aoe, kwani hilo linamsaidia kuinamisha macho na kulinda uchi wake. Kwa yule asiyeweza basi afunge kwani kufanya hivyo kunampunguzia matamanio” (al-Jamaa‘ah).

 

4.                Jamii kusalimika na magonjwa:

Magonjwa ya zinaa ni natija ya kuliendea jambo hili la kushibisha matamanio kwa njia ya haramu. Magonjwa haya ni hatari na ukimwi haujapatikana tiba hadi sasa, tahadhari usije ukapata adhabu mara mbili. AIDS ni gonjwa hatari mno.

5.                Utulivu wa kiroho na kinafsi:

 

Ndoa inaleta mapenzi, upole, ulaini na rehema. Allah Aliyetukuka Anasema: “Na katika Ishara Zake ni kuwa Amekuumbieni wake zenu katika jinsi yenu ili mupate utulivu kwao, Naye Amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Bila shaka katika hayo zimo Ishara kwa watu wanaofikiri” (30: 21).

 

6.                Kushirikiana baina wanandoa katika kujenga familia na kuwalea watoto:

Kwa ndoa wanashirikiana wanandoa katika kujenga familia ya Kiislamu na kubeba majukumu hayo.

 

Ama kuhusu sifa njema na nzuri ambazo kwayo mwanamme anafaa achague mkewe na mwanamke naye achague mumewe ni kama zifuatazo kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu:

Kuchagua kwa msingi wa Dini:

 

Huu ni msingi wa kwanza na muhimu sana. Ukweli ni kuwa kila mmoja ana sifa ambayo anaona lau atapata mwendani wake basi ashafika kwenye kilele katika maisha yake. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) naye ametuelezea pale aliposema: “Mwanamke huolewa kwa sababu NNE: Kwa mali yake, nasaba yake, uzuri wake na Dini yake, Tafuta mwenye dini uwe salama (yaani usiharibikiwe katika maisha yako)” (al-Bukhaariy na Muslim).

 

Amesema tena: “Akikujieni ambaye mumeridhika na dini na maadili yake, muozesheni. Msipofanya hivyo kutakuwa na fitna katika ardhi na ufisadi mkubwa” (at-Tirmidhiy).

 

Amesema tena (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Mwenye kumuoa mwanamke kwa sababu ya mali yake Allah hamzidishii ila ufukara; mwenye kumuoa kwa sababu ya nasaba yake, Allah Atamtweza; mwenye kuoa kwa ajili ya kuinamisha macho yake, kulinda uchi wake au kuunganisha kizazi, Allah atambarikia kwayo na atabarikiwa kwake” (atw-Twabraaniy).

 

 Kufadhilisha mwanamke mwenye kuzaa:

 

Alikuja mtu kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuuliza: “Ewe Mtume wa Allah mimi nampenda mwanamke mwenye nasaba nzuri, cheo na mali isipokuwa hazai, je nimuoe?” Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamkataza. Akarudi tena mara ya pili na ya tatu akajibiwa: “Oeni wanawake wenye mapenzi na wazazi, ili nipate kujifakhiri kwa Umma zingine siku ya Qiyaamah” (Abu Daawuud, an-Nasaa’iy na al-Haakim).

 

Na Allah Anajua zaidi

 

Share