Anafaa Kuachika Ikiwa Mume Hawezi Tendo La Ndoa?

 

SWALI:

Mimi nina ndugu yangu ameolewa akiwa msichana wa mika 18, na amebahatika kuzaa mtoto mmoja, na baada ya hapo mume wake hakuwa na uwezo tena wa kumuingilia kutokana na matatizo yaliyompata katika uume wake, na sasa yafikia miaka sita, na ndugu yangu amechoka kusubiri, je, ni haki kwa ndugu yangu kudai kuachika?

 


 

 

JIBU:

 

 

Sifa zote njema anastahiki Allah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Kwanza:  Awali ya yote tunakupa pole kutokana na mtihani uliyokupata, na tunakunasihi uishi na mumeo kwa wema na ikiwa hamna budi ila kuachana basi muachane kwa wema.

Pili:   Ufumbuzi wa tatizo lako kisheria unaweza ukaupata kupitia katika mahakama ya Qadhi kwa hapo ulipo, ama sisi tutakudokeza japo kidogo juu ya mambo yanayopelekea mwanamke husika kudai talaka nayo ni ama ifuatavyo:

1. Kukatika kwa dhakari ya mwanamume pamoja na kende zake, au kukatika kwa dhakari pekee, au kukatika kwa kende pekee pasi na dhakari, (kwa hali hii mwanamke anaweza kudai kuachika endapo kama ataolewa bila ya kuwa na taarifa ya hali hiyo);      

2. Mwanamume kuwa na uume usiofanya kazi (khanithi) na mwanamke akashindwa kusubiri, katika hali hii wanachuoni wanasema mume atapewa muda wa mwaka mmoja kwa kujitibu, na endapo hatomudu kumjamii mke wake ndani ya kipindi cha mwaka mmoja, mwanamke atakuwa na haki ya kudai kuachika, kinyume chake hatoruhusiwa kudai talaka;

3. Kuhasiwa, endapo mwanamke ameolewa na mtu aliyehasiwa, hali kadhalika anaweza kudai kuachika, kwani kitendo hicho nacho humnyima mwanamke haki yake ya kustarehe.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share