Kutokumtimizia Mume Haja Ya Kitendo Cha Ndoa

 

SWALI

Kwa jina la M/Mungu mwenye kuneemesha neema kubwa kubwa na mwenye kuneeesha neema ndogo ndogo.

Mimi nina suala langu nataka nielimishwe zaidi.

Ninajua kama mume anapokutaka kwa tendo la ndoa ni vibaya kumkatalia,lakini je hata kama una dharura mfano una maumivu mwilini (yaani yale maumivu yamekufanya huna furaha na tendo lile kwa pale) au umechoka na kuchoka wenyewe sio kama nadanganya nimechoka kabisa jee sababu hizi nikisema nitakuwa nimo makosani? Na pia wakati mwengine na mume hua unapotaka tendo wewe hua ana machofu makubwa naye na humridhia sasa hapa nataka maelezo.

 Naomba majibu kwa ufasaha


JIBU:

AlhamduliLLaah - Sifa njema zote Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amewaamrisha wanaume wa Kiislamu waishi na wake zao kwa wema. Kama Alivyosema:

"……… na kaeni nao kwa wema..[]

Miongoni mwa kuishi kwa wema ni kusubiriana kwa wote wawili, pale tatizo la kweli na la msingi linapomtokea mmoja wao akashindwa kumtekeleza mwenzake haki yake, kwani tendo la ndoa ni haki ya wote wawili japokuwa mke kumtekelezea mume kumesisitizwa zaidi kama kama ulivyofahamu wewe mwenyewe. Sasa itakapotokea kuwa umechoka kweli na ukasema hata kama mume hakuridhika, hutakuwa umekosea na hata mumeo nae akisema amechoka ukamridhia au hukumridhia hatakuwa amekosea, kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amekwishatuelezea katika Aayah iliyotangulia na yamebainishwa zaidi katika Suwrah 2 Aayah ya 228  

  "…. Nao [wanawake] wanayo haki kwa sharia [kufanyiwa na waume zao] kama ile haki iliyo juu yao kuwafanyia waume zao. na wanaume wana daraja zaidi kuliko wao, na Allaah ni Mwenye Nguvu, Mwenye Hikma"

Kuridhiana mume na mke ni jambo linalozidisha mapenzi katika ndoa na inampasa kila mmoja awe ana subira kwa mwenziwe anapokuwa hayuko katika hali ya kawaida.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share