023 - Al-Muuminuwn

 

الْمُؤمِنُون

 

023-Al-Muuminuwn

 

 

023-Al-Muuminuwn: Utangulizi Wa Suwrah

 

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

 

قَدْ أَفْلَحَ الْمُؤْمِنُونَ ﴿١﴾

1. Kwa yakini wamefaulu Waumini.[1]

 

 

 

الَّذِينَ هُمْ فِي صَلَاتِهِمْ خَاشِعُونَ ﴿٢﴾

2. Ambao katika Swalaah zao huwa wananyenyekea.

 

 

 

وَالَّذِينَ هُمْ عَنِ اللَّغْوِ مُعْرِضُونَ ﴿٣﴾

3. Na ambao wanajiepusha na mambo ya upuuzi.

 

 

 

وَالَّذِينَ هُمْ لِلزَّكَاةِ فَاعِلُونَ ﴿٤﴾

4. Na ambao wanatoa Zakaah.

 

 

 

وَالَّذِينَ هُمْ لِفُرُوجِهِمْ حَافِظُونَ ﴿٥﴾

5. Na ambao wanazihifadhi tupu zao.

 

 

 

إِلَّا عَلَىٰ أَزْوَاجِهِمْ أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُمْ فَإِنَّهُمْ غَيْرُ مَلُومِينَ ﴿٦﴾

6. Isipokuwa kwa wake zao, au kwa iliyowamiliki mikono yao ya kuume basi hao hawalaumiwi.

 

 

 

فَمَنِ ابْتَغَىٰ وَرَاءَ ذَٰلِكَ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْعَادُونَ ﴿٧﴾

7. Lakini atakayetaka kinyume ya hayo, basi hao ndio wapindukao mipaka.

 

 

 

وَالَّذِينَ هُمْ لِأَمَانَاتِهِمْ وَعَهْدِهِمْ رَاعُونَ ﴿٨﴾

8. Na ambao amana zao na ahadi zao wanazichunga.[2]

 

 

 

وَالَّذِينَ هُمْ عَلَىٰ صَلَوَاتِهِمْ يُحَافِظُونَ ﴿٩﴾

9. Na ambao wanazihifadhi Swalaah zao.

 

 

 

أُولَـٰئِكَ هُمُ الْوَارِثُونَ ﴿١٠﴾

10. Hao ndio warithi.

 

 

 

الَّذِينَ يَرِثُونَ الْفِرْدَوْسَ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ ﴿١١﴾

11. Ambao watarithi (Jannah ya) Al-Firdaws, wao humo ni wenye kudumu.

 

 

 

وَلَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ مِن سُلَالَةٍ مِّن طِينٍ ﴿١٢﴾

12. Kwa yakini Tumemuumba binaadam kutokana na mchujo safi wa udongo.[3]

 

 

 

ثُمَّ جَعَلْنَاهُ نُطْفَةً فِي قَرَارٍ مَّكِينٍ ﴿١٣﴾

13. Kisha Tukamfanya kuwa tone la manii katika kalio makini.

 

 

 

ثُمَّ خَلَقْنَا النُّطْفَةَ عَلَقَةً فَخَلَقْنَا الْعَلَقَةَ مُضْغَةً فَخَلَقْنَا الْمُضْغَةَ عِظَامًا فَكَسَوْنَا الْعِظَامَ لَحْمًا ثُمَّ أَنشَأْنَاهُ خَلْقًا آخَرَ ۚ فَتَبَارَكَ اللَّـهُ أَحْسَنُ الْخَالِقِينَ ﴿١٤﴾

14. Kisha Tukaumba tone la manii kuwa pande la damu linaloning’inia, Tukaumba pande la damu hilo linaloning’inia kuwa kinofu cha nyama, Tukaumba kinofu hicho cha nyama kuwa mifupa, Tukavisha mifupa hiyo nyama, kisha Tukamuanzisha kiumbe kingine. Basi Amebarikika Allaah Mbora wa wenye kuumba.

 

 

 

ثُمَّ إِنَّكُم بَعْدَ ذَٰلِكَ لَمَيِّتُونَ ﴿١٥﴾

15. Kisha hakika nyinyi baada ya hayo, ni wenye kufa.

 

 

 

ثُمَّ إِنَّكُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ تُبْعَثُونَ ﴿١٦﴾

16. Kisha hakika nyinyi Siku ya Qiyaamah mtafufuliwa.

 

 

 

وَلَقَدْ خَلَقْنَا فَوْقَكُمْ سَبْعَ طَرَائِقَ وَمَا كُنَّا عَنِ الْخَلْقِ غَافِلِينَ ﴿١٧﴾

17. Kwa yakini Tumeumba juu yenu tabaka za mbingu saba, na Hatukuwa Wenye Kughafilika kuhusu uumbaji.[4]

 

 

 

وَأَنزَلْنَا مِنَ السَّمَاءِ مَاءً بِقَدَرٍ فَأَسْكَنَّاهُ فِي الْأَرْضِ ۖ وَإِنَّا عَلَىٰ ذَهَابٍ بِهِ لَقَادِرُونَ ﴿١٨﴾

18. Na Tukateremsha kutoka mbinguni maji kwa kiasi, na Tukayawekea maskani ardhini. Nasi kwa kuyaondosha bila shaka Ni Wenye uwezo.

 

 

 

فَأَنشَأْنَا لَكُم بِهِ جَنَّاتٍ مِّن نَّخِيلٍ وَأَعْنَابٍ لَّكُمْ فِيهَا فَوَاكِهُ كَثِيرَةٌ وَمِنْهَا تَأْكُلُونَ ﴿١٩﴾

19. Kisha Tukakuanzishieni kwa maji hayo mabustani ya mitende na mizabibu, mnapata humo matunda mengi, na katika hayo mnakula.

 

 

 

وَشَجَرَةً تَخْرُجُ مِن طُورِ سَيْنَاءَ تَنبُتُ بِالدُّهْنِ وَصِبْغٍ لِّلْآكِلِينَ ﴿٢٠﴾

20. Na mti (wa zaituni pia) unaotoka katika Mlima wa Sinai, unaozalisha mafuta na kuwa kitoweo cha ladha kwa walaji.

 

 

 

وَإِنَّ لَكُمْ فِي الْأَنْعَامِ لَعِبْرَةً ۖ نُّسْقِيكُم مِّمَّا فِي بُطُونِهَا وَلَكُمْ فِيهَا مَنَافِعُ كَثِيرَةٌ وَمِنْهَا تَأْكُلُونَ ﴿٢١﴾

21. Na hakika katika wanyama wa mifugo mnapata zingatio. Tunakunywisheni kile kitokacho matumboni mwao (maziwa), na mnapata humo manufaa mengi, na kati yao mnawala.

 

 

 

وَعَلَيْهَا وَعَلَى الْفُلْكِ تُحْمَلُونَ ﴿٢٢﴾

22. Na juu yao (hao wanyama), na juu ya merikebu mnabebwa.

 

 

 

وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا نُوحًا إِلَىٰ قَوْمِهِ فَقَالَ يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّـهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرُهُ ۖ أَفَلَا تَتَّقُونَ ﴿٢٣﴾

23. Kwa yakini Tulimpeleka Nuwh kwa kaumu yake, akasema: Enyi kaumu yangu! Mwabuduni Allaah, hamna mwabudiwa wa haki ghairi Yake. Je, basi hamtokuwa na taqwa? 

 

 

 

فَقَالَ الْمَلَأُ الَّذِينَ كَفَرُوا مِن قَوْمِهِ مَا هَـٰذَا إِلَّا بَشَرٌ مِّثْلُكُمْ يُرِيدُ أَن يَتَفَضَّلَ عَلَيْكُمْ وَلَوْ شَاءَ اللَّـهُ لَأَنزَلَ مَلَائِكَةً مَّا سَمِعْنَا بِهَـٰذَا فِي آبَائِنَا الْأَوَّلِينَ ﴿٢٤﴾

24. Wakasema wakuu waliokufuru miongoni mwa kaumu yake: Huyu si chochote ila ni binaadam kama nyinyi, anataka ajifadhilishe juu yenu. Na lau Allaah Angelitaka (kutuma Rasuli), bila shaka Angeliteremsha Malaika. Hatukusikia haya kwa baba zetu wa awali.

 

 

 

إِنْ هُوَ إِلَّا رَجُلٌ بِهِ جِنَّةٌ فَتَرَبَّصُوا بِهِ حَتَّىٰ حِينٍ ﴿٢٥﴾

25. Yeye si lolote ila ni mtu ana wazimu, basi mngojeeni na mwangalieni tu kwa muda.

 

 

 

قَالَ رَبِّ انصُرْنِي بِمَا كَذَّبُونِ ﴿٢٦﴾

26. (Nuwh) akasema: Rabb wangu! Ninusuru kwa kuwa wamenikadhibisha.

 

 

 

فَأَوْحَيْنَا إِلَيْهِ أَنِ اصْنَعِ الْفُلْكَ بِأَعْيُنِنَا وَوَحْيِنَا فَإِذَا جَاءَ أَمْرُنَا وَفَارَ التَّنُّورُ ۙ فَاسْلُكْ فِيهَا مِن كُلٍّ زَوْجَيْنِ اثْنَيْنِ وَأَهْلَكَ إِلَّا مَن سَبَقَ عَلَيْهِ الْقَوْلُ مِنْهُمْ ۖ وَلَا تُخَاطِبْنِي فِي الَّذِينَ ظَلَمُوا ۖ إِنَّهُم مُّغْرَقُونَ ﴿٢٧﴾

27. Basi Tukamfunulia Wahy kwamba: Unda jahazi mbele ya Macho Yetu[5] na Wahy Wetu. Itakapokuja Amri Yetu, na tanuri likafoka, basi waingize humo kila namna dume na jike na ahli zako isipokuwa yule miongoni mwao iliyekwishamtangulia kauli, na wala usinisemeshe kuhusu hao waliodhulumu, hakika wao ni wenye kugharikishwa.[6]

 

 

 

فَإِذَا اسْتَوَيْتَ أَنتَ وَمَن مَّعَكَ عَلَى الْفُلْكِ فَقُلِ الْحَمْدُ لِلَّـهِ الَّذِي نَجَّانَا مِنَ الْقَوْمِ الظَّالِمِينَ ﴿٢٨﴾

28. Basi utakapopanda na kutulia wewe na wale walio pamoja nawe jahazini, sema: AlhamduliLLaah (Himidi Anastahiki Allaah) Ambaye Ametuokoa kutokana na watu madhalimu.

 

 

 

وَقُل رَّبِّ أَنزِلْنِي مُنزَلًا مُّبَارَكًا وَأَنتَ خَيْرُ الْمُنزِلِينَ ﴿٢٩﴾

29. Na sema: Rabb wangu! Niteremshe mteremko wa baraka, Nawe ni Mbora wa wenye kuteremsha.

 

 

 

إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ وَإِن كُنَّا لَمُبْتَلِينَ ﴿٣٠﴾

30. Hakika katika hayo bila shaka kuna Aayaat (Ishara, Dalili, Mawaidha, Mazingatio) na hakika Tumekuwa Wenye Kuwafanyia mitihani.

 

 

 

ثُمَّ أَنشَأْنَا مِن بَعْدِهِمْ قَرْنًا آخَرِينَ ﴿٣١﴾

31. Kisha Tukaanzisha baada yao karne nyingine.

 

 

 

فَأَرْسَلْنَا فِيهِمْ رَسُولًا مِّنْهُمْ أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرُهُ ۖ أَفَلَا تَتَّقُونَ ﴿٣٢﴾

32. Tukawapelekea Rasuli miongoni mwao (awalinganie) kwamba: Mwabuduni Allaah, hamna mwabudiwa wa haki ghairi Yake. Je, basi hamtokuwa na taqwa? 

 

 

 

وَقَالَ الْمَلَأُ مِن قَوْمِهِ الَّذِينَ كَفَرُوا وَكَذَّبُوا بِلِقَاءِ الْآخِرَةِ وَأَتْرَفْنَاهُمْ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا مَا هَـٰذَا إِلَّا بَشَرٌ مِّثْلُكُمْ يَأْكُلُ مِمَّا تَأْكُلُونَ مِنْهُ وَيَشْرَبُ مِمَّا تَشْرَبُونَ ﴿٣٣﴾

33. Na wakasema wakuu miongoni mwa kaumu yake waliokufuru na wakakadhibisha mkutano wa Aakhirah, na Tukawaneemesha na kuwastarehesha katika uhai wa dunia: Huyu si lolote ila ni binaadam kama nyinyi, anakula vile vile mlavyo nyinyi, na anakunywa vile vile mnywavyo.[7]

 

 

 

وَلَئِنْ أَطَعْتُم بَشَرًا مِّثْلَكُمْ إِنَّكُمْ إِذًا لَّخَاسِرُونَ ﴿٣٤﴾

34. Na mkimtii binaadam kama nyinyi, basi hapo hakika nyinyi mtakuwa wenye kukhasirika.

 

 

 

أَيَعِدُكُمْ أَنَّكُمْ إِذَا مِتُّمْ وَكُنتُمْ تُرَابًا وَعِظَامًا أَنَّكُم مُّخْرَجُونَ ﴿٣٥﴾

35. Je, anakuahidini kwamba nyinyi mtakapokufa, mkawa mchanga na mifupa kuwa ati mtatolewa (kuwa hai)?[8]

 

 

 

هَيْهَاتَ هَيْهَاتَ لِمَا تُوعَدُونَ ﴿٣٦﴾

36. Mbali kabisa, hayawezekani kabisa! Hayo mnayoahidiwa.

 

 

 

إِنْ هِيَ إِلَّا حَيَاتُنَا الدُّنْيَا نَمُوتُ وَنَحْيَا وَمَا نَحْنُ بِمَبْعُوثِينَ ﴿٣٧﴾

37. Hakuna lolote isipokuwa tu uhai wetu wa duniani, tunakufa na tunaishi, na wala sisi hatutofufuliwa.

 

 

 

إِنْ هُوَ إِلَّا رَجُلٌ افْتَرَىٰ عَلَى اللَّـهِ كَذِبًا وَمَا نَحْنُ لَهُ بِمُؤْمِنِينَ ﴿٣٨﴾

38. Yeye si lolote isipokuwa mtu aliyemtungia Allaah uongo, nasi hatutomwamini. 

 

 

 

قَالَ رَبِّ انصُرْنِي بِمَا كَذَّبُونِ ﴿٣٩﴾

39. (Rasuli huyo) akasema: Rabb wangu! Ninusuru kwa sababu wamenikadhibisha.

 

 

 

قَالَ عَمَّا قَلِيلٍ لَّيُصْبِحُنَّ نَادِمِينَ ﴿٤٠﴾

40. (Allaah) Akasema: Muda mchache tu, bila shaka watapambazukiwa wawe wenye kujuta.

 

 

 

فَأَخَذَتْهُمُ الصَّيْحَةُ بِالْحَقِّ فَجَعَلْنَاهُمْ غُثَاءً ۚ فَبُعْدًا لِّلْقَوْمِ الظَّالِمِينَ ﴿٤١﴾

41. Basi ukawachukua ukelele angamizi kwa haki, Tukawafanya kama takataka za majani zinazoelea juu ya maji. Basi wametokomelea mbali watu madhalimu.

 

 

 

ثُمَّ أَنشَأْنَا مِن بَعْدِهِمْ قُرُونًا آخَرِينَ ﴿٤٢﴾

42. Kisha Tukaanzisha baada yao karne nyingi nyinginezo. 

 

 

 

مَا تَسْبِقُ مِنْ أُمَّةٍ أَجَلَهَا وَمَا يَسْتَأْخِرُونَ ﴿٤٣﴾

43. Hapana ummah uwezao kutanguliza ajali yake, na wala hawawezi kuakhirisha.

 

 

 

 

ثُمَّ أَرْسَلْنَا رُسُلَنَا تَتْرَىٰ ۖ كُلَّ مَا جَاءَ أُمَّةً رَّسُولُهَا كَذَّبُوهُ ۚ فَأَتْبَعْنَا بَعْضَهُم بَعْضًا وَجَعَلْنَاهُمْ أَحَادِيثَ ۚ فَبُعْدًا لِّقَوْمٍ لَّا يُؤْمِنُونَ ﴿٤٤﴾

44. Kisha Tukatuma Rusuli Wetu waliofuatana mfululizo. Kila ummah alipowajia Rasuli wao, walimkadhibisha. Basi Tukawafuatanisha baadhi yao kwa wao (kwa maangamizi). Na Tukawafanya ni hadithi za kusimuliwa. Basi wametokomelea mbali watu wasioamini.

 

 

 

ثُمَّ أَرْسَلْنَا مُوسَىٰ وَأَخَاهُ هَارُونَ بِآيَاتِنَا وَسُلْطَانٍ مُّبِينٍ ﴿٤٥﴾

45. Kisha Tukamtuma Muwsaa na kaka yake Haaruwn kwa Aayaat (Ishara, Dalili) Zetu na mamlaka bayana.

 

 

 

إِلَىٰ فِرْعَوْنَ وَمَلَئِهِ فَاسْتَكْبَرُوا وَكَانُوا قَوْمًا عَالِينَ ﴿٤٦﴾

46. Kwa Firawni, na wakuu wake, lakini walitakabari, na wakawa watu waliojiona.

 

 

 

فَقَالُوا أَنُؤْمِنُ لِبَشَرَيْنِ مِثْلِنَا وَقَوْمُهُمَا لَنَا عَابِدُونَ ﴿٤٧﴾

47. Wakasema: Itawezekanaje tuwaamini binaadam wawili kama sisi, na hali watu wao kwetu ni watumwa?

 

 

 

فَكَذَّبُوهُمَا فَكَانُوا مِنَ الْمُهْلَكِينَ ﴿٤٨﴾

48. Wakawakadhibisha. Basi wakawa miongoni mwa walioangamizwa.

 

 

 

وَلَقَدْ آتَيْنَا مُوسَى الْكِتَابَ لَعَلَّهُمْ يَهْتَدُونَ ﴿٤٩﴾

49. Na kwa yakini Tulimpa Muwsaa Kitabu (Tawraat) ili waongoke.

 

 

 

وَجَعَلْنَا ابْنَ مَرْيَمَ وَأُمَّهُ آيَةً وَآوَيْنَاهُمَا إِلَىٰ رَبْوَةٍ ذَاتِ قَرَارٍ وَمَعِينٍ ﴿٥٠﴾

50. Na Tukamjaalia mwana wa Maryam na mama yake kuwa ni Aayah (Ishara za Muujiza, Hoja, Dalili kubwa ya wazi), na Tukawapa kimbilio katika sehemu iliyoinuka na penye utulivu na chemchemu.

 

 

 

يَا أَيُّهَا الرُّسُلُ كُلُوا مِنَ الطَّيِّبَاتِ وَاعْمَلُوا صَالِحًا ۖ إِنِّي بِمَا تَعْمَلُونَ عَلِيمٌ ﴿٥١﴾

51. Enyi Rusuli! Kuleni katika vizuri na tendeni mema, hakika Mimi kwa yale myatendayo Ni Mjuzi.[9]

 

 

 

وَإِنَّ هَـٰذِهِ أُمَّتُكُمْ أُمَّةً وَاحِدَةً وَأَنَا رَبُّكُمْ فَاتَّقُونِ ﴿٥٢﴾

52. Na kwamba hakika huu ummah wenu, ni ummah mmoja, Nami Ni Rabb   wenu, basi Nicheni.

 

 

 

فَتَقَطَّعُوا أَمْرَهُم بَيْنَهُمْ زُبُرًا ۖ كُلُّ حِزْبٍ بِمَا لَدَيْهِمْ فَرِحُونَ ﴿٥٣﴾

53. Wakafarikiana makundi makundi baina yao kuhusu Dini yao, kila kundi kwa waliyo nayo linafurahia.

 

 

 

 

فَذَرْهُمْ فِي غَمْرَتِهِمْ حَتَّىٰ حِينٍ ﴿٥٤﴾

54. Basi waachilie mbali katika mkanganyiko wao kwa muda.

 

 

 

 

أَيَحْسَبُونَ أَنَّمَا نُمِدُّهُم بِهِ مِن مَّالٍ وَبَنِينَ ﴿٥٥﴾

55. Je, wanadhani kwamba kwa vile Tunavyowakunjulia kwa mali na watoto.

 

 

 

نُسَارِعُ لَهُمْ فِي الْخَيْرَاتِ ۚ بَل لَّا يَشْعُرُونَ ﴿٥٦﴾

56. (Ndio kuwa) Tunawaharakishia katika kheri (Zetu)? Bali hawahisi.

 

 

 

 

إِنَّ الَّذِينَ هُم مِّنْ خَشْيَةِ رَبِّهِم مُّشْفِقُونَ ﴿٥٧﴾

57. Hakika wale ambao pamoja na kumwogopa Rabbi wao, bado ni wenye kuchelea (Adhabu Yake).

 

 

 

وَالَّذِينَ هُم بِآيَاتِ رَبِّهِمْ يُؤْمِنُونَ ﴿٥٨﴾

58. Na wale ambao Aayaat (na Ishara za kiulimwengu) za Rabb wao wanaziamini.

 

 

 

وَالَّذِينَ هُم بِرَبِّهِمْ لَا يُشْرِكُونَ ﴿٥٩﴾

59. Na wale ambao Rabb wao hawamshirikishi.

 

 

 

وَالَّذِينَ يُؤْتُونَ مَا آتَوا وَّقُلُوبُهُمْ وَجِلَةٌ أَنَّهُمْ إِلَىٰ رَبِّهِمْ رَاجِعُونَ ﴿٦٠﴾

60. Na ambao wanatoa vile wavitoavyo na huku nyoyo zao zinakhofu kwamba hakika watarejea kwa Rabb wao.[10]

 

 

 

أُولَـٰئِكَ يُسَارِعُونَ فِي الْخَيْرَاتِ وَهُمْ لَهَا سَابِقُونَ ﴿٦١﴾

61. Hao wanakimbilia katika mambo ya kheri, na wao ndio wenye kuyatanguliza.  

 

 

 

وَلَا نُكَلِّفُ نَفْسًا إِلَّا وُسْعَهَا ۖ وَلَدَيْنَا كِتَابٌ يَنطِقُ بِالْحَقِّ ۚ وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ ﴿٦٢﴾

62. Na wala Hatuikalifishi nafsi yoyote isipokuwa kwa kadiri ya uwezo wake. Na Kwetu kuna Kitabu kisemacho haki, nao hawatodhulumiwa.

 

 

 

بَلْ قُلُوبُهُمْ فِي غَمْرَةٍ مِّنْ هَـٰذَا وَلَهُمْ أَعْمَالٌ مِّن دُونِ ذَٰلِكَ هُمْ لَهَا عَامِلُونَ ﴿٦٣﴾

63. Bali nyoyo zao zimo katika mkanganyiko kutokana na haya. Na wanazo amali (ovu) pasi na hizo, wao wanazitenda.

 

 

 

حَتَّىٰ إِذَا أَخَذْنَا مُتْرَفِيهِم بِالْعَذَابِ إِذَا هُمْ يَجْأَرُونَ ﴿٦٤﴾

64. Mpaka Tutakapowachukua kwa adhabu wastareheshwa wao wa anasa za dunia, basi wao hapo watapiga mayowe.

 

 

 

 

لَا تَجْأَرُوا الْيَوْمَ ۖ إِنَّكُم مِّنَّا لَا تُنصَرُونَ ﴿٦٥﴾

65. Msipige mayowe leo. Hakika nyinyi Kwetu hamtonusuriwa.  

 

 

 

قَدْ كَانَتْ آيَاتِي تُتْلَىٰ عَلَيْكُمْ فَكُنتُمْ عَلَىٰ أَعْقَابِكُمْ تَنكِصُونَ ﴿٦٦﴾

66. Kwa yakini zilikuwa Aayaat Zangu zikisomwa kwenu, lakini mlikuwa mnarudi nyuma juu ya visigino vyenu (kukanusha). 

 

 

 

مُسْتَكْبِرِينَ بِهِ سَامِرًا تَهْجُرُونَ ﴿٦٧﴾

67. Mkitakabari kwayo, mkikaa usiku kuisimulia (Qur-aan) kwa kubwabwaja maovu ya batili.

 

 

 

أَفَلَمْ يَدَّبَّرُوا الْقَوْلَ أَمْ جَاءَهُم مَّا لَمْ يَأْتِ آبَاءَهُمُ الْأَوَّلِينَ ﴿٦٨﴾

68. Je, hawakuzingatia kauli (ya Allaah; Qur-aan) au yamewajia yasiyowafikia baba zao wa awali?

 

 

 

أَمْ لَمْ يَعْرِفُوا رَسُولَهُمْ فَهُمْ لَهُ مُنكِرُونَ ﴿٦٩﴾

69. Au hawajamtambua Rasuli wao (Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم), basi wao ndio wanamkanusha?

 

 

 

أَمْ يَقُولُونَ بِهِ جِنَّةٌ ۚ بَلْ جَاءَهُم بِالْحَقِّ وَأَكْثَرُهُمْ لِلْحَقِّ كَارِهُونَ ﴿٧٠﴾

70. Au wanasema ana wazimu? Bali amewajia kwa haki, na wengi wao hiyo haki wanaichukia.

 

 

 

وَلَوِ اتَّبَعَ الْحَقُّ أَهْوَاءَهُمْ لَفَسَدَتِ السَّمَاوَاتُ وَالْأَرْضُ وَمَن فِيهِنَّ ۚ بَلْ أَتَيْنَاهُم بِذِكْرِهِمْ فَهُمْ عَن ذِكْرِهِم مُّعْرِضُونَ ﴿٧١﴾

71. Na lau kama haki ingelifuata hawaa zao, basi zingelifisidika mbingu na ardhi na waliokuwemo humo. Bali Tumewaletea ukumbusho wao lakini wao ni wenye kupuuza ukumbusho wao.

 

 

 

أَمْ تَسْأَلُهُمْ خَرْجًا فَخَرَاجُ رَبِّكَ خَيْرٌ ۖ وَهُوَ خَيْرُ الرَّازِقِينَ ﴿٧٢﴾

72. Au unawaomba ujira? Basi ujira wa Rabb wako ni bora zaidi. Naye Ni Mbora wa wenye kuruzuku.

 

 

 

وَإِنَّكَ لَتَدْعُوهُمْ إِلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ ﴿٧٣﴾

73. Na bila shaka wewe (Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) unawaita kuelekea njia iliyonyooka.

 

 

 

وَإِنَّ الَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِالْآخِرَةِ عَنِ الصِّرَاطِ لَنَاكِبُونَ ﴿٧٤﴾

74. Na hakika wale wasioiamini Aakhirah wanajitenga na njia hiyo.

 

 

 

 

وَلَوْ رَحِمْنَاهُمْ وَكَشَفْنَا مَا بِهِم مِّن ضُرٍّ لَّلَجُّوا فِي طُغْيَانِهِمْ يَعْمَهُونَ ﴿٧٥﴾

75. Na lau kama Tungeliwarehemu, na Tukawaondoshea dhara waliyokuwa nayo, bila shaka wangeng’ang’ania ukaidi katika upindukaji mipaka wa kuasi kwao, wakitangatanga kwa upofu.

 

 

 

وَلَقَدْ أَخَذْنَاهُم بِالْعَذَابِ فَمَا اسْتَكَانُوا لِرَبِّهِمْ وَمَا يَتَضَرَّعُونَ ﴿٧٦﴾

76. Kwa yakini Tuliwachukua kwa adhabu, basi hawakunyenyekea kujisalimisha kwa Rabb wao, na wala hawakuomba duaa kwa udhalili na unyenyekevu.

 

 

 

حَتَّىٰ إِذَا فَتَحْنَا عَلَيْهِم بَابًا ذَا عَذَابٍ شَدِيدٍ إِذَا هُمْ فِيهِ مُبْلِسُونَ ﴿٧٧﴾

77. Mpaka Tutakapowafungulia mlango wenye adhabu kali, tahamaki watakuwa humo ni wenye kukata tamaa.

 

 

 

وَهُوَ الَّذِي أَنشَأَ لَكُمُ السَّمْعَ وَالْأَبْصَارَ وَالْأَفْئِدَةَ ۚ قَلِيلًا مَّا تَشْكُرُونَ ﴿٧٨﴾

78. Naye (Allaah) Ndiye Ambaye Amekuumbieni kusikia na kuona na nyoyo. Ni kudogo mno kushukuru kwenu.

 

 

 

وَهُوَ الَّذِي ذَرَأَكُمْ فِي الْأَرْضِ وَإِلَيْهِ تُحْشَرُونَ ﴿٧٩﴾

79. Naye Ndiye Ambaye Amekutawanyeni katika ardhi, na Kwake mtakusanywa.

 

 

 

وَهُوَ الَّذِي يُحْيِي وَيُمِيتُ وَلَهُ اخْتِلَافُ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ ۚ أَفَلَا تَعْقِلُونَ ﴿٨٠﴾

80. Naye Ndiye Ambaye Anahuisha na Kufisha, na ni Yake mabadiliko ya mfuatano wa usiku na mchana. Je, basi hamtii akilini?

 

 

 

بَلْ قَالُوا مِثْلَ مَا قَالَ الْأَوَّلُونَ ﴿٨١﴾

81. Bali wamesema kama walivyosema watu wa awali.

 

 

 

قَالُوا أَإِذَا مِتْنَا وَكُنَّا تُرَابًا وَعِظَامًا أَإِنَّا لَمَبْعُوثُونَ ﴿٨٢﴾

82. Wamesema: Je, tutakapokufa na tukawa mchanga na mifupa, je, hivi sisi tutafufuliwa? [11]

 

 

 

لَقَدْ وُعِدْنَا نَحْنُ وَآبَاؤُنَا هَـٰذَا مِن قَبْلُ إِنْ هَـٰذَا إِلَّا أَسَاطِيرُ الْأَوَّلِينَ ﴿٨٣﴾

83. Kwa yakini tumeahidiwa haya sisi na baba zetu kabla. Haya si chochote isipokuwa hekaya za watu wa kale.

 

 

 

قُل لِّمَنِ الْأَرْضُ وَمَن فِيهَا إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ ﴿٨٤﴾

84. Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Ni ya nani ardhi na wale waliomo humo mkiwa mnajua?

 

 

 

سَيَقُولُونَ لِلَّـهِ ۚ قُلْ أَفَلَا تَذَكَّرُونَ ﴿٨٥﴾

85. Watasema: Ni ya Allaah Pekee. Sema: Je, basi hamkumbuki?

 

 

 

قُلْ مَن رَّبُّ السَّمَاوَاتِ السَّبْعِ وَرَبُّ الْعَرْشِ الْعَظِيمِ ﴿٨٦﴾

86. Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Nani Rabb wa mbingu saba, na Rabb wa ‘Arsh ‘Adhimu?

 

 

 

سَيَقُولُونَ لِلَّـهِ ۚ قُلْ أَفَلَا تَتَّقُونَ ﴿٨٧﴾

87. Watasema: Ni ya Allaah Pekee Sema: Je, basi hamtokuwa na taqwa?

 

 

 

قُلْ مَن بِيَدِهِ مَلَكُوتُ كُلِّ شَيْءٍ وَهُوَ يُجِيرُ وَلَا يُجَارُ عَلَيْهِ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ ﴿٨٨﴾

88. Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Nani katika mikono Yake uko ufalme wa kila kitu, Naye Ndiye Alindae, na wala hakilindwi chochote kinyume Naye, ikiwa mnajua?

 

 

 

سَيَقُولُونَ لِلَّـهِ ۚ قُلْ فَأَنَّىٰ تُسْحَرُونَ ﴿٨٩﴾

89. Watasema: Ni Allaah Pekee. Sema: Basi vipi mnazugwa?

 

 

 

بَلْ أَتَيْنَاهُم بِالْحَقِّ وَإِنَّهُمْ لَكَاذِبُونَ ﴿٩٠﴾

90. Bali Tumewajia na haki, na kwa hakika wao ni wenye kukadhibisha.

 

 

 

مَا اتَّخَذَ اللَّـهُ مِن وَلَدٍ وَمَا كَانَ مَعَهُ مِنْ إِلَـٰهٍ ۚ إِذًا لَّذَهَبَ كُلُّ إِلَـٰهٍ بِمَا خَلَقَ وَلَعَلَا بَعْضُهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ ۚ سُبْحَانَ اللَّـهِ عَمَّا يَصِفُونَ ﴿٩١﴾

91. Allaah Hakujifanyia mwana yeyote, na wala hakuna pamoja Naye mwabudiwa yeyote. Ingekuwa hivyo, basi kila mwabudiwa angelichukua vile alivyoviumba, na baadhi yao wangeliwashinda wengineo. Subhaana Allaah (Utakasifu ni wa Allaah) kutokana na ambayo wanayavumisha.[12]

 

 

 

عَالِمِ الْغَيْبِ وَالشَّهَادَةِ فَتَعَالَىٰ عَمَّا يُشْرِكُونَ ﴿٩٢﴾

92. Mjuzi wa ghaibu na dhahiri. Basi Ametukuka kwa ‘Uluwa kutokana na yale wanayomshirikisha.

 

 

 

قُل رَّبِّ إِمَّا تُرِيَنِّي مَا يُوعَدُونَ ﴿٩٣﴾

93. Sema: Rabb wangu! Ukinionyesha yale wanayoahidiwa (ya kuletewa adhabu).

 

 

 

رَبِّ فَلَا تَجْعَلْنِي فِي الْقَوْمِ الظَّالِمِينَ ﴿٩٤﴾

94. Rabb wangu! Basi Usinijaalie kuwemo ndani ya watu hao madhalimu.

 

 

 

وَإِنَّا عَلَىٰ أَن نُّرِيَكَ مَا نَعِدُهُمْ لَقَادِرُونَ ﴿٩٥﴾

95. Na hakika Sisi Kukuonyesha yale Tunayowaahidi (ya adhabu) Tunaweza bila shaka yoyote.  

 

 

 

ادْفَعْ بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ السَّيِّئَةَ ۚ نَحْنُ أَعْلَمُ بِمَا يَصِفُونَ ﴿٩٦﴾

96. Zuia maovu kwa (kuwarudishia) yale ambayo ni mema zaidi. Sisi Tunajua zaidi yale wanayoyavumisha. 

 

 

 

وَقُل رَّبِّ أَعُوذُ بِكَ مِنْ هَمَزَاتِ الشَّيَاطِينِ ﴿٩٧﴾

97. Na sema: Rabb wangu! Najikinga Kwako kutokana na udokezi wa mashaytwaan.[13]

 

 

وَأَعُوذُ بِكَ رَبِّ أَن يَحْضُرُونِ ﴿٩٨﴾

98. Na najikinga Kwako Rabb wasinihudhurie.

 

 

 

حَتَّىٰ إِذَا جَاءَ أَحَدَهُمُ الْمَوْتُ قَالَ رَبِّ ارْجِعُونِ ﴿٩٩﴾

99. Mpaka yatakapomfikia mmoja wao mauti, atasema: Rabb wangu! Nirejesheni (duniani).[14]

 

 

 

لَعَلِّي أَعْمَلُ صَالِحًا فِيمَا تَرَكْتُ ۚ كَلَّا ۚ إِنَّهَا كَلِمَةٌ هُوَ قَائِلُهَا ۖ وَمِن وَرَائِهِم بَرْزَخٌ إِلَىٰ يَوْمِ يُبْعَثُونَ ﴿١٠٠﴾

100. Ili nikatende mema katika yale niliyoyaacha. (Ataambiwa) Laa hasha! Hakika hilo ni neno alisemalo yeye tu.  Na mbele yao kuna Barzakh[15] mpaka Siku watakayofufuliwa.  

 

 

 

فَإِذَا نُفِخَ فِي الصُّورِ فَلَا أَنسَابَ بَيْنَهُمْ يَوْمَئِذٍ وَلَا يَتَسَاءَلُونَ ﴿١٠١﴾

101. Na litakapopulizwa baragumu, basi hakutokuwa na unasaba baina yao Siku hiyo, na wala hawatoulizana.[16]

 

 

 

فَمَن ثَقُلَتْ مَوَازِينُهُ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ ﴿١٠٢﴾

102. Basi yule ambaye mizani yake itakuwa nzito, hao ndio wenye kufaulu.

 

 

 

وَمَنْ خَفَّتْ مَوَازِينُهُ فَأُولَـٰئِكَ الَّذِينَ خَسِرُوا أَنفُسَهُمْ فِي جَهَنَّمَ خَالِدُونَ ﴿١٠٣﴾

103. Na yule ambaye mizani zake zitakuwa khafifu, basi hao ni wale ambao wamekhasirika nafsi zao. Watadumu ndani ya Jahannam.

 

 

 

تَلْفَحُ وُجُوهَهُمُ النَّارُ وَهُمْ فِيهَا كَالِحُونَ ﴿١٠٤﴾

104. Moto utababua nyuso zao. Nao humo watakuwa ni wenye midomo iliyosinyaa na kuvutika mbali na meno.

 

 

 

أَلَمْ تَكُنْ آيَاتِي تُتْلَىٰ عَلَيْكُمْ فَكُنتُم بِهَا تُكَذِّبُونَ ﴿١٠٥﴾

105. (Wataambiwa): Je, hazikuwa Aayaat Zangu zinasomwa kwenu na nyinyi mkawa mnazikadhibisha?

 

 

 

قَالُوا رَبَّنَا غَلَبَتْ عَلَيْنَا شِقْوَتُنَا وَكُنَّا قَوْمًا ضَالِّينَ ﴿١٠٦﴾

106. Watasema: Rabb wetu! Ulitughilibu ufedhuli wetu, na tulikuwa watu waliopotea.

 

 

 

رَبَّنَا أَخْرِجْنَا مِنْهَا فَإِنْ عُدْنَا فَإِنَّا ظَالِمُونَ ﴿١٠٧﴾

107. Rabb wetu! Tutoe humo (motoni), na tukirudia tena, basi hakika sisi ni madhalimu.

 

 

 

قَالَ اخْسَئُوا فِيهَا وَلَا تُكَلِّمُونِ ﴿١٠٨﴾

108. Wataambiwa: Hizikeni humo! Na wala msinisemeshe!

 

 

 

إِنَّهُ كَانَ فَرِيقٌ مِّنْ عِبَادِي يَقُولُونَ رَبَّنَا آمَنَّا فَاغْفِرْ لَنَا وَارْحَمْنَا وَأَنتَ خَيْرُ الرَّاحِمِينَ ﴿١٠٩﴾

109. Hakika lilikuwa kundi miongoni mwa Waja Wangu, wakisema: Rabb wetu! Tumeamini, basi Tughufurie na Uturehemu, Nawe Ni Mbora wa wenye kurehemu.

 

 

 

فَاتَّخَذْتُمُوهُمْ سِخْرِيًّا حَتَّىٰ أَنسَوْكُمْ ذِكْرِي وَكُنتُم مِّنْهُمْ تَضْحَكُونَ ﴿١١٠﴾

110. Mkawafanyia dhihaka, hadi wakakusahaulisheni kunidhukuru na mlikuwa ni wenye kuwacheka.

 

 

 

إِنِّي جَزَيْتُهُمُ الْيَوْمَ بِمَا صَبَرُوا أَنَّهُمْ هُمُ الْفَائِزُونَ ﴿١١١﴾

111. Hakika Mimi Nimewalipa leo (Jannah) kwa vile walivyosubiri, hakika wao ndio wenye kufuzu.

 

 

 

قَالَ كَمْ لَبِثْتُمْ فِي الْأَرْضِ عَدَدَ سِنِينَ ﴿١١٢﴾

112. (Allaah) Atasema: Muda gani mlikaa katika ardhi kwa idadi ya miaka?

 

 

 

قَالُوا لَبِثْنَا يَوْمًا أَوْ بَعْضَ يَوْمٍ فَاسْأَلِ الْعَادِّينَ ﴿١١٣﴾

113. Watasema: Tumekaa siku au sehemu tu ya siku. Basi waulize wanaohesabu.

 

 

 

قَالَ إِن لَّبِثْتُمْ إِلَّا قَلِيلًا ۖ لَّوْ أَنَّكُمْ كُنتُمْ تَعْلَمُونَ ﴿١١٤﴾

114. (Allaah) Atasema: Hamkukaa (huko duniani) isipokuwa kidogo tu, lau mngelikuwa mnajua.

 

 

 

أَفَحَسِبْتُمْ أَنَّمَا خَلَقْنَاكُمْ عَبَثًا وَأَنَّكُمْ إِلَيْنَا لَا تُرْجَعُونَ ﴿١١٥﴾

115. Je, mlidhania kwamba Sisi Tulikuumbeni bila kusudio mcheze tu, na kwamba nyinyi Kwetu hamtorejeshwa?

 

 

 

فَتَعَالَى اللَّـهُ الْمَلِكُ الْحَقُّ ۖ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ رَبُّ الْعَرْشِ الْكَرِيمِ ﴿١١٦﴾

116. Basi Ametukuka Allaah kwa ‘Uluwa, Mfalme wa haki. Hapana mwabudiwa wa haki ila Yeye, Rabb wa ‘Arsh Kariym.[17]

 

 

 

 

وَمَن يَدْعُ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ لَا بُرْهَانَ لَهُ بِهِ فَإِنَّمَا حِسَابُهُ عِندَ رَبِّهِ ۚ إِنَّهُ لَا يُفْلِحُ الْكَافِرُونَ ﴿١١٧﴾

117. Na yeyote yule anayeomba duaa (au kuabudu) pamoja na Allaah mwabudiwa mwengine ambapo hana ushahidi wa hilo, basi hakika hesabu yake iko kwa Rabb wake. Hakika hawafaulu makafiri.

 

 

 

وَقُل رَّبِّ اغْفِرْ وَارْحَمْ وَأَنتَ خَيْرُ الرَّاحِمِينَ ﴿١١٨﴾

118. Na sema: Rabb wangu! Ghufuria na Rehemu, Nawe Ni Mbora wa wenye kurehemu.

 

 

 

 

 

[1] Sifa Za Watakaofaulu Na Kujaaliwa Kupata Jannatul-Firdaws:

 

Sifa za watakaofaulu na kujaaliwa kupata Jannatul- Firdaws zimetajwa katika Suwrah hii kuanzia Aayah namba (2) hadi namba (9). Na sifa hizo zimeanza kutaja khushuw’ (unyenyekevu) katika Swalaah na kumalizikia kwa kuhifadhi Swalaah. Hali kadhaalika, sifa kama hizi taqriban, zimetajwa katika Suwrah Al-Ma’aarij (70:23-34) ila katika Suwrah hiyo Swalaah imeanza kutajwa kwa kuidumisha na imemalizwa kutajwa kwa kuihifadhi kama ilivyotajwa katika Suwrah hii ya Al-Muuminuwn. Kisha katika Suwrah Al-Ma’aarij Allaah (سبحانه وتعالى) Anaahidi Jannah baada ya hapo Aayah namba (35).  Basi hii inadhihirisha umuhimu wa kudumisha na kuhifadhi Swalaah na kuiswali kwa khushuw’. Rejea pia Al-Baqarah (2:3), na An-Nisaa (4:108).

 

[2] Amrisho La Kutimiza Ahadi: Rejea An-Nahl (16:90-92, 94), Al-Ma’aarij (70:32), Al-Ahzaab (33:72).

 

[3] Uumbaji Wa Mwanaadam:

 

Aayah hii hadi namba (16) zinataja daraja za kuumbwa binaadam hadi kufufuliwa. Rejea Al-Hajj (22:5), Ghaafir (40:67).

 

[4] Baadhi Ya Neema Za Allaah (سبحانه وتعالى) Kwa Wanaadam:

Kuanzia Aayah hii hadi namba (22), Allaah (سبحانه وتعالى) Anataja baadhi ya Neema Zake. Na neema kama hizi na zaidi Anazitaja katika An-Nahl kwenye Aayah mbali mbali. Rejea An-Nahl (16:5-16), (65-69), (72), (80-81). Rejea pia Ibraahiym (14:34) kwenye maelezo bayana.

 

[5] Kuthibitisha Sifa Za Allaah (سبحانه وتعالى): Rejea Huwd (11:37).

 

[6] Nuwh (عليه السّلام) Na Kizazi Kilobakia: 

Aayah hii hadi namba (31), zinathibitisha kuwa Nuwh (عليه السّلام) na kizazi kilichopanda katika safina (jahazi), ndio kizazi kilichobakia na kuendelea kuzaliana karne kwa karne. Na ndio maana Nuwh (عليه السّلام) akawa baba wa wanaadam baada ya Aadam (عليه السّلام) na pia yeye ni Rasuli wa kwanza ardhini.

Rejea Asw-Swaffaat (37:77).

 

[7] Ada Ya Washirikina Kutaka Kutumiwa Rasuli Asiye Binaadam:

 

Washirikina wa kaumu za kale kama kaumu ya Nuwh (عليه السّلام)  hawakumwamini Rasuli wao kwa kutoa sababu mojawapo ya kuwa wanakula na kunywa. Hivo walitaka kutumiwa asiyekuwa binaadam kama Malaika. Na hii ni sawa na ada ya washirikina wa zama za Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) . Rejea Al-Furqaan (25:7) na Al-Israa (17:90-95) ambako walidai mengineyo. Na kuna rejea humo nyenginezo.

 

[8] Makafiri Hawakuamini Kuwa Watafufuliwa:

 

Rejea Al-Israa (17:49) kwenye maelezo bayana na rejea mbali mbali.

 

[9] Kula Vizuri Na Vya Halali Ni Sababu Mojawapo Ya Kutaqabaliwa Duaa:

 

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:  “Enyi watu, hakika Allaah ni Mzuri na Hapokei ila kilicho kizuri. Na Allaah Amewaamrisha Waumini yale yale Aliyowaamrisha Rusuli (Mitume) Akasema:  

 

يَا أَيُّهَا الرُّسُلُ كُلُوا مِنَ الطَّيِّبَاتِ وَاعْمَلُوا صَالِحًا ۖ إِنِّي بِمَا تَعْمَلُونَ عَلِيمٌ ﴿٥١﴾

“Enyi Rusuli! Kuleni katika vizuri na tendeni mema, hakika Mimi kwa yale myatendayo Ni Mjuzi.”  [Al-Muuminuwn (23:51)] 

 

Na Anasema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُلُوا مِن طَيِّبَاتِ مَا رَزَقْنَاكُمْ  

“Enyi walioamini! Kuleni vizuri Tulivyokuruzukuni.” [Al-Baqarah (2:172)]. 

 

Kisha akamtaja mtu aliyekuwa safarini, nywele zimemsimama timtim na mwili umejaa vumbi, anainua mikono yake mbinguni akiomba: Ee Rabb! Ee Rabb! Na hali chakula chake ni haramu, kinywaji chake ni haramu na mavazi yake ni haramu, na amelishwa vya haramu, basi vipi ataitikiwa duaa yake?!” [Muslim]

 

[10] Sifa Ya Waumini Wanapotenda Mema Huwa Baina Ya Khofu Na Matarajio:

 

Amesimulia ‘Abdur-Rahmaan bin Sa’iyd bin Wahab Al-Hamdaaniyy kwamba ‘Aaishah (رضي الله عنها)  mke wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: Nilimuuliza Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) kuhusu Aayah hii:

وَالَّذِينَ يُؤْتُونَ مَا آتَوا وَّقُلُوبُهُمْ وَجِلَةٌ  

“Na ambao wanatoa vile wavitoavyo na huku nyoyo zao zinakhofu.”

 

‘Aaishah akasema: Je, hao ni wale wanaokunywa pombe na wanaoiba?  Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Hapana ee bint wa Asw-Swiddiyq! Lakini hao ni wale wanaofunga (Swiyaam), na wanaswali, na wanatoa swadaqa, na huku (pamoja na hayo yote) wanakhofu wasitaqabaliwe.” Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akaendelea kusema kwa kutaja Kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى):  

أُولَـٰئِكَ يُسَارِعُونَ فِي الْخَيْرَاتِ وَهُمْ لَهَا سَابِقُونَ ﴿٦١﴾

“Hao wanakimbilia katika mambo ya kheri, na wao ndio wenye kuyatanguliza.”  

 

[11] Makafiri Hawaamini Kufufuliwa:  

 

Rejea Al-Israa (17:49) kwenye maelezo bayana na rejea mbali mbali.

 

 

[12] Haiwezekani Kuweko Waabudiwa Na Waumbaji Zaidi Ya Mmoja:

 

Rejea pia Al-Anbiyaa (21:22).  

 

Imaam As-Sa’diy (رحمه الله)  ameifafanua akisema

 

Uongo unaojulikana kutokana na Maelezo haya ya Allaah, na Maelezo ya Rusuli Wake, na unajulikana pia kwa akili sahihi (ya kawaida). Kwa sababu hiyo, ndio Allaah (سبحانه وتعالى) Akatanabahisha kwa dalili za kiakili juu ya kutowezekana kuwa na waabudiwa wawili, ndio Anasema:

إِذًا

“Ingekuwa hivyo”

 

Anakusudia: Kama kungekuwa na mwabudiwa mwingine kinyume na Allaah kama wanavyosema (makafiri), 

 

لَّذَهَبَ كُلُّ إِلَـٰهٍ بِمَا خَلَقَ  

“Basi kila mwabudiwa angelichukua vile alivyoviumba.”

 

Anakusudia: Angejitenga kila mmoja wa waabudiwa wawili kwa viumbe aliowaumba, na akawa nao hao tu, na angepupia kumzuia mwenzie na kumshinda kabisa:

وَلَعَلَا بَعْضُهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ ۚ  

“Na baadhi yao wangeliwashinda wengineo.” 

 

Atakaeshinda ndiye atakuwa mwabudiwa. Na si hivyo ikiwa kila mmoja anamzuia mwenzie tu, hapa haiwezekani ulimwengu kuwa hivyo, na wala haikubaliki kiakili mpangilio huu wa kushangaza.  Chukua mazingatio ya hilo kwa jua na mwezi, nyota zinazotembea na zisizotembea. Hivyo vyote tangu vimeumbwa vipo katika nidhamu moja na mpangilio mmoja, hivyo vyote vimedhalilishwa (vinanyenyekea na kufuata) kwa Uwezo wa Allaah, uliopangiliwa kwa hikmah ikiwa ni mambo yenye maslahi kwa viumbe wote, na wala si maslahi ya mmoja kinyume na mwingine. Na hautaona mapungufu yeyote yale, na wala hakuna tofauti japo ndogo kwenye jambo lolote lile. Sasa je, inakubalika kiakili jambo kama hili kuwa la waabudiwa wawili ambao wote ni waumbaji?! 

 

 سُبْحَانَ اللَّـهِ عَمَّا يَصِفُونَ ﴿٩١﴾

“Subhaana Allaah (Utakasifu ni wa Allaah) kutokana na ambayo wanayavumisha.”

 

Hakika uhalisia na muonekano mzuri na mpangilio wa ulimwengu na vilivyopo, vyote vinatufahamisha kuwa Mwendeshaji wa haya ni Mwabudiwa Mmoja tu, Mkamilifu wa Majina na Sifa. Viumbe wote wanamuhitajia Yeye, katika Rubuwbiyyah Yake (Uola, umiliki, uendeshaji wa ulimwengu, uumbaji, utoaji rizki, uhuishaji na ufishaji, nk), na katika Uluwhiyyah Yake (kutekelezwa ibaada kwa ajili Yake), kama ilivyo visinge kuwepo viumbe wala kudumu isipokuwa baada ya kuviumba Allaah, ndio kama hivyo, viumbe hawatokuwa na maisha mazuri na hali nzuri isipokuwa kwa kumwabudu Yeye, na kufanya utiifu kwa ajili ya Allaah Pekee. [Tafsiyr Imaam As-Sa’diy]

 

[13] Kinga Dhidi Ya Udokezi Wa Mashaytwaan Na Kufazaika Usingizini:

 

Hii ni miongoni mwa Adhkaar Za Asubuhi Na Jioni. Rejea Hiswnul-Muslim Duaa Namba (30). Na Hadiyth yake ni hii ifuatayo:  

   

 حَدَّثَنَا عَلِيُّ بْنُ حُجْرٍ، حَدَّثَنَا إِسْمَاعِيلُ بْنُ عَيَّاشٍ، عَنْ مُحَمَّدِ بْنِ إِسْحَاقَ، عَنْ عَمْرِو بْنِ شُعَيْبٍ، عَنْ أَبِيهِ، عَنْ جَدِّهِ، أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم قَالَ ‏ "‏ إِذَا فَزِعَ أَحَدُكُمْ فِي النَّوْمِ فَلْيَقُلْ أَعُوذُ بِكَلِمَاتِ اللَّهِ التَّامَّةِ مِنْ غَضَبِهِ وَعِقَابِهِ وَشَرِّ عِبَادِهِ وَمِنْ هَمَزَاتِ الشَّيَاطِينِ وَأَنْ يَحْضُرُونِ ‏.‏ فَإِنَّهَا لَنْ تَضُرَّهُ ‏"‏ ‏.‏ قَالَ وَكَانَ عَبْدُ اللَّهِ بْنُ عَمْرٍو يُلَقِّنُهَا مَنْ بَلَغَ مِنْ وَلَدِهِ وَمَنْ لَمْ يَبْلُغْ مِنْهُمْ كَتَبَهَا فِي صَكٍّ ثُمَّ عَلَّقَهَا فِي عُنُقِهِ ‏.‏ قَالَ أَبُو عِيسَى هَذَا حَدِيثٌ حَسَنٌ غَرِيبٌ

Amesimulia ‘Amr Bin Shu’ayb kutoka kwa baba yake kutoka kwa babu yake (رضي الله عنهم) : Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Pindi mmoja wenu akifazaika usingizini basi aseme:

أَعُوذُ بِكَلِمَاتِ اللَّهِ التَّامَّاتِ مِنْ غَضَبِهِ وَعِقَابِهِ وَشَرِّ عِبَادِهِ وَمِنْ هَمَزَاتِ الشَّيَاطِينِ وَأَنْ يَحْضُرُونِ

Najikinga na maneno ya Allaah  yaliotimia kutokana na ghadhabu Zake, na adhabu Yake, na shari ya waja Wake, na kutokana na vioja vya mashaytwaan na kunijia kwao, basi  hawatomdhuru.  [At-Tirmidhiy na pia Abu Daawuwd, Ahmad, ameisahihisha Al-Albaaniy - Swahiyh Abi Daawuwd (3893), Swahiyh At-Tirmidhiy (3/171), Adhkaar za kuondosha wasiwasi usingizini au kusikia uoga na mfadhaiko]

 

Rejea Alhidaaya.com Makala Kutoka Duaa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu Na Sharh Yake Duaa Namba (23).  

 

[14] Binaadam Hujuta Anapotolewa Roho Akiwa Ni Kafiri Au Muasi Au Asipotenda Mema:

 

Aayah hii na ifuatayo inataja jinsi mtu anavyojuta pindi akiwa ni kafiri, au ni muasi au asiyetenda mema alipokuwa hai duniani. Rejea Al-Munaafiquwn (63:10-11).

 

[15] Barzakh:

 

Maana yake katika lugha ni: kizuizi. Rejea Ar-Rahmaan (55:20).

 

Kiistilahi, ni kipindi ambacho kinatenganisha dunia na Aakhirah. Ni kipindi baina ya kifo cha mtu hadi atakapofufuliwa siku ya Qiyaamah, nayo ni maisha ya mtu kuanzia anapofariki akazikwa kwa kuingizwa kaburini akabakia humo hadi Siku ya Qiyaamah. Na maisha hayo humo ni kulingana na aina ya mtu. Akiwa ni Muumini, basi maisha yake yatakuwa ni ya raha. Ama akiwa ni kafiri au muasi, basi maisha yake yatakuwa ni adhabu kutokana na dalili kutoka kwenye Qur-aan. Rejea Ghaafir (40:45-46).

 

Na Barzakh ni katika mambo ya ghaibu ambayo Muumini anapaswa kuamini kama ilivyothibiti katika Qur-aan na Sunnah. Imaam Ibn Baaz (رحمه الله)  ameelezea katika Fatwa ifuatayo alipoulizwa:

 

“Maisha ya mwanaadamu yamegawanyika katika sehemu tatu: Maisha ya dunia ambayo ndiyo tunayoishi, maisha ya Aakhirah ambayo yanajulikana, kati ya maisha ya dunia na Aakhirah ni maisha ya barzakh, basi ni yapi maisha ya barzakh?  Je, mtu huwa kwa mwili wake na roho yake?”  

 

Akajibu: “Maisha ya barzakh ni kulingana na maisha yake hapa duniani. Muumini hustareheshwa katika barzakh huku roho yake ikiwa iko Jannah, na mwili wake utapata baadhi ya starehe. Na kafiri roho yake itaonyeshwa moto, yeye atapata sehemu ya adhabu yake, na mwili wake utapata sehemu ya adhabu yake. Haya ndio maisha ya barzakh. Muumini atakuwa yuko katika furaha na raha. Na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema kuwa roho za Waumini zinazunguka Peponi popote zinapotaka. Ama makafiri, hao ni kama Alivyoeleza Allaah kuhusu watu wa Firawni: (Rejea Ghaafir (40:45-46). Hivyo basi, roho za makafiri zinaadhibiwa na miili yao itapata sehemu ya adhabu zake mpaka Allaah Awafufue wote, kisha roho za Waumini zitabaki Peponi, na roho za makafiri zitaingia motoni - tunamuomba Allaah Atusalimishe nao - zidumu humo milele; hawa watadumu milele Peponi, na hawa watadumu milele Motoni. Tunamuomba Allaah Atusalimishe.”  [Al-Mawqi' Ar-Rasmiy li-Samaahat Ash-Shaykh Al-Imaam Ibn Baaz]

 

Na Hadiyth nyenginezo zimethibiti:

 

عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ، قَالَ مَرَّ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم عَلَى قَبْرَيْنِ فَقَالَ: ((أَمَا إِنَّهُمَا لَيُعَذَّبَانِ وَمَا يُعَذَّبَانِ فِي كَبِيرٍ أَمَّا أَحَدُهُمَا فَكَانَ يَمْشِي بِالنَّمِيمَةِ وَأَمَّا الآخَرُ فَكَانَ لاَ يَسْتَتِرُ مِنْ بَوْلِهِ‏)) متفق عليه

Amesimulia Ibn 'Abbaas  (رضي الله عنهما): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) aliyapitia makaburi mawili na akasema: “Hakika hawa wawili wanaadhibiwa, na wala hawaadhibiwi kwa sababu ya jambo kubwa (la kuwashinda kulitekeleza au kujiepusha nalo).” Kisha hapo hapo Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: ”Hapana! Bali ni kubwa (dhambi kubwa na adhabu zake)!  Ama mmoja wao, huyu alikuwa akipita kufitinisha watu, na ama mwingine, huyu alikuwa hajikingi na mkojo wake [anapokojoa].” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

عَنْ أَبِي سَعِيدٍ الْخُدْرِيَّ (رضي الله عنه) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((إِذَا وُضِعَتْ الْجِنَازَةُ وَاحْتَمَلَهَا النَّاسُ – أوِ الرِّجَالُ عَلَى أَعْنَاقِهِمْ، فَإِنْ كَانَتْ صَالِحَةً قَالَتْ: قَدِّمُونِي. وَإِنْ كَانَتْ غَيْرَ صَالِحَةٍ قَالَتْ: يَا وَيْلَهَا! أَيْنَ يَذْهَبُونَ بِهَا؟ يَسْمَعُ صَوْتَهَا كُلُّ شَيْءٍ إلاَّ الإِنْسَانَ وَلَوْ سَمِعَهُ صَعِقَ)) البخاري

Amesimulia Abuu Sa’iyd Al-Khudriyy (رضي الله عنه):   Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Linapowekwa jeneza na likabebwa na watu - au wanaume shingoni mwao -, basi ikiwa ni la mtu mwema husema: Niwahisheni [nitangulizeni]. Lakini ikiwa si la mtu mwema husema: Ole wake! Wanalipeleka wapi? Sauti yake inasikika na kila kitu isipokuwa binaadamu. Na lau angeisikia angelizimia.” [Al-Bukhaariy].

 

[16] Siku Ya  Qiyaamah Hakuna Ndugu Wala Jamaa Atakayetaka Kumsaidia Ndugu Ya Jamaa Yake: Rejea ‘Abasa (80:33-42).

 

[17] ‘Arsh Kariym:

 

Maana yake ni ‘Arsh yenye mwonekano mzuri na umbo la kuvutia. [Tafsiyr Ibn Kathiyr]

 

Tofauti Kati Ya ‘Arsh Ya Ar-Rahmaan Na ’Arsh Ya Wanaadamu: Rejea Al-Haaqqah (69:17).

 

Share