035 - Faatwir

 

    فَاطِر

 

035-Faatwir

 

035-Faatwir: Utangulizi Wa Suwrah

 

 

Alhidaaya.com

 

 

 

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

 

 

الْحَمْدُ لِلَّـهِ فَاطِرِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ جَاعِلِ الْمَلَائِكَةِ رُسُلًا أُولِي أَجْنِحَةٍ مَّثْنَىٰ وَثُلَاثَ وَرُبَاعَ ۚ يَزِيدُ فِي الْخَلْقِ مَا يَشَاءُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ ﴿١﴾

1. AlhamduliLLahi (Himdi Anastahiki Allaah), Muanzilishi wa mbingu na ardhi, Mwenye Kuwafanya Malaika kuwa wajumbe wenye mbawa mbili-mbili, na tatu-tatu na nne-nne. Huzidisha katika uumbaji Atakavyo. Hakika Allaah Ni Muweza juu ya kila kitu.

 

 

 

مَّا يَفْتَحِ اللَّـهُ لِلنَّاسِ مِن رَّحْمَةٍ فَلَا مُمْسِكَ لَهَا ۖ وَمَا يُمْسِكْ فَلَا مُرْسِلَ لَهُ مِن بَعْدِهِ ۚ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ ﴿٢﴾

2. Rehma yoyote Anayoifungua Allaah kwa watu, basi hakuna wa kuizuia, na Anayoizuia, basi hakuna wa kuipeleka baada Yake,[1] Naye Ni Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Hikmah wa yote.

 

 

 

يَا أَيُّهَا النَّاسُ اذْكُرُوا نِعْمَتَ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ ۚ هَلْ مِنْ خَالِقٍ غَيْرُ اللَّـهِ يَرْزُقُكُم مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ ۚ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۖ فَأَنَّىٰ تُؤْفَكُونَ ﴿٣﴾

3. Enyi watu! Kumbukeni Neema za Allaah kwenu. Je, kuna muumbaji yeyote badala ya Allaah Anayekuruzukuni kutoka mbinguni na ardhini? Hapana Muabudiwa wa haki ila Yeye. Basi vipi mnaghilibiwa?

 

 

وَإِن يُكَذِّبُوكَ فَقَدْ كُذِّبَتْ رُسُلٌ مِّن قَبْلِكَ ۚ وَإِلَى اللَّـهِ تُرْجَعُ الْأُمُورُ ﴿٤﴾

4. Na wakikukadhibisha (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم), basi   wamekwisha kadhibishwa Rusuli kabla yako. Na kwa Allaah yanarejeshwa mambo yote.

 

 

 

يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنَّ وَعْدَ اللَّـهِ حَقٌّ ۖ فَلَا تَغُرَّنَّكُمُ الْحَيَاةُ الدُّنْيَا ۖ وَلَا يَغُرَّنَّكُم بِاللَّـهِ الْغَرُورُ ﴿٥﴾

5. Enyi watu!  Hakika Ahadi ya Allaah ni haki. Basi usikughururini kabisa uhai wa dunia, na wala (shaytwaan) mwenye kughuri asikughururini kabisa kuhusu Allaah.

 

 

 

إِنَّ الشَّيْطَانَ لَكُمْ عَدُوٌّ فَاتَّخِذُوهُ عَدُوًّا ۚ إِنَّمَا يَدْعُو حِزْبَهُ لِيَكُونُوا مِنْ أَصْحَابِ السَّعِيرِ ﴿٦﴾

6. Hakika shaytwaan kwenu ni adui, basi mfanyeni kuwa ni adui. Hakika anaitia kikosi chake ili wawe miongoni mwa watu wa moto uliowashwa vikali mno. 

 

 

الَّذِينَ كَفَرُوا لَهُمْ عَذَابٌ شَدِيدٌ ۖ وَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَهُم مَّغْفِرَةٌ وَأَجْرٌ كَبِيرٌ ﴿٧﴾

7. Wale waliokufuru watapata adhabu kali, na wale walioamini na wakatenda mema watapata maghfirah na ujira mkubwa.

 

 

 

أَفَمَن زُيِّنَ لَهُ سُوءُ عَمَلِهِ فَرَآهُ حَسَنًا ۖ فَإِنَّ اللَّـهَ يُضِلُّ مَن يَشَاءُ وَيَهْدِي مَن يَشَاءُ ۖ فَلَا تَذْهَبْ نَفْسُكَ عَلَيْهِمْ حَسَرَاتٍ ۚ إِنَّ اللَّـهَ عَلِيمٌ بِمَا يَصْنَعُونَ ﴿٨﴾

8. Je, yule aliyepambiwa uovu wa amali yake akaiona ni nzuri (je, ni sawa na aliyehidika?). Basi hakika Allaah Anampotoa Amtakaye na Anamhidi Amtakaye. Hivyo basi isihiliki nafsi yako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kwa ajili ya kuwajutia. Hakika Allaah Ni Mjuzi kwa yale wayatendayo.

 

 

 

وَاللَّـهُ الَّذِي أَرْسَلَ الرِّيَاحَ فَتُثِيرُ سَحَابًا فَسُقْنَاهُ إِلَىٰ بَلَدٍ مَّيِّتٍ فَأَحْيَيْنَا بِهِ الْأَرْضَ بَعْدَ مَوْتِهَا ۚ كَذَٰلِكَ النُّشُورُ ﴿٩﴾

9. Na Allaah Ambaye Ametuma pepo za Rehma kisha zikatimua mawingu, Tukayaendesha katika nchi iliyokufa, Tukahuisha kwayo ardhi baada ya kufa kwake. Hivyo ndivyo kufufuliwa.[2]

 

 

 

مَن كَانَ يُرِيدُ الْعِزَّةَ فَلِلَّـهِ الْعِزَّةُ جَمِيعًا ۚ إِلَيْهِ يَصْعَدُ الْكَلِمُ الطَّيِّبُ وَالْعَمَلُ الصَّالِحُ يَرْفَعُهُ ۚ وَالَّذِينَ يَمْكُرُونَ السَّيِّئَاتِ لَهُمْ عَذَابٌ شَدِيدٌ ۖ وَمَكْرُ أُولَـٰئِكَ هُوَ يَبُورُ ﴿١٠﴾

10. Yeyote Anayetaka utukufu, basi utukufu wote uko kwa Allaah. Kwake Pekee linapanda Neno zuri[3] na amali njema Huitukuza. Na wale wanaopanga njama za maovu watapata adhabu shadidi. Na njama za hao ni zenye kuangamia.

 

 

 

وَاللَّـهُ خَلَقَكُم مِّن تُرَابٍ ثُمَّ مِن نُّطْفَةٍ ثُمَّ جَعَلَكُمْ أَزْوَاجًا ۚ وَمَا تَحْمِلُ مِنْ أُنثَىٰ وَلَا تَضَعُ إِلَّا بِعِلْمِهِ ۚ وَمَا يُعَمَّرُ مِن مُّعَمَّرٍ وَلَا يُنقَصُ مِنْ عُمُرِهِ إِلَّا فِي كِتَابٍ ۚ إِنَّ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ ﴿١١﴾

11. Na Allaah Amekuumbeni kutokana na udongo, kisha kutokana na tone la manii, kisha Akakufanyeni jozi; mwanamume na mwanamke. Na mwanamke yeyote habebi mimba na wala hazai isipokuwa kwa Ujuzi Wake. Na hapewi umri mrefu yeyote yule mwenye umri mrefu na wala hapunguziwi katika umri wake isipokuwa imo Kitabuni. Hakika hayo kwa Allaah ni mepesi.

 

 

 

وَمَا يَسْتَوِي الْبَحْرَانِ هَـٰذَا عَذْبٌ فُرَاتٌ سَائِغٌ شَرَابُهُ وَهَـٰذَا مِلْحٌ أُجَاجٌ ۖ وَمِن كُلٍّ تَأْكُلُونَ لَحْمًا طَرِيًّا وَتَسْتَخْرِجُونَ حِلْيَةً تَلْبَسُونَهَا ۖ وَتَرَى الْفُلْكَ فِيهِ مَوَاخِرَ لِتَبْتَغُوا مِن فَضْلِهِ وَلَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ ﴿١٢﴾

12. Na bahari mbili hazilingani sawa; haya ni (maji) matamu ladha yake, yenye kukata kiu, kinywaji chake cha kuburudisha, na haya ni ya chumvi kali. Na katika kila moja mnakula nyama laini safi na mnatoa mapambo mnayoyavaa. Na utaona merikebu humo zikipasua maji ili mtafute Fadhila Zake, na ili mpate kushukuru.

 

 

 

يُولِجُ اللَّيْلَ فِي النَّهَارِ وَيُولِجُ النَّهَارَ فِي اللَّيْلِ وَسَخَّرَ الشَّمْسَ وَالْقَمَرَ كُلٌّ يَجْرِي لِأَجَلٍ مُّسَمًّى ۚ ذَٰلِكُمُ اللَّـهُ رَبُّكُمْ لَهُ الْمُلْكُ ۚ وَالَّذِينَ تَدْعُونَ مِن دُونِهِ مَا يَمْلِكُونَ مِن قِطْمِيرٍ ﴿١٣﴾

13. Anauingiza usiku katika mchana, na Anauingiza mchana katika usiku, na Ametiisha jua na mwezi; kila kimoja kinakwenda mpaka muda maalumu uliokadiriwa. Huyo Ndiye Allaah Rabb wenu, Ufalme ni Wake Pekee.  Na wale mnaowaomba badala Yake hawamiliki hata kijiwavu cha kokwa ya tende.[4]

 

 

 

إِن تَدْعُوهُمْ لَا يَسْمَعُوا دُعَاءَكُمْ وَلَوْ سَمِعُوا مَا اسْتَجَابُوا لَكُمْ ۖ وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ يَكْفُرُونَ بِشِرْكِكُمْ ۚ وَلَا يُنَبِّئُكَ مِثْلُ خَبِيرٍ ﴿١٤﴾

14.  Mkiwaomba, hawasikii maombi yenu, na hata wakisikia, hawatakuitikieni.  Na Siku ya Qiyaamah watakanusha ushirikina wenu, na wala hakuna atakayekujulisha vilivyo, kama Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri.

 

 

يَا أَيُّهَا النَّاسُ أَنتُمُ الْفُقَرَاءُ إِلَى اللَّـهِ ۖ وَاللَّـهُ هُوَ الْغَنِيُّ الْحَمِيدُ ﴿١٥﴾

15. Enyi watu!  Nyinyi ni mafakiri kwa Allaah! Na Allaah Ndiye Mkwasi, Mwenye Kustahiki Kuhimidiwa kwa yote.

 

 

 

 

إِن يَشَأْ يُذْهِبْكُمْ وَيَأْتِ بِخَلْقٍ جَدِيدٍ ﴿١٦﴾

16. Akitaka Atakuondosheni mbali na Alete viumbe vipya.

 

 

 

وَمَا ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ بِعَزِيزٍ ﴿١٧﴾

17. Na hilo halina uzito wowote kwa Allaah.

 

 

 

وَلَا تَزِرُ وَازِرَةٌ وِزْرَ أُخْرَىٰ ۚ وَإِن تَدْعُ مُثْقَلَةٌ إِلَىٰ حِمْلِهَا لَا يُحْمَلْ مِنْهُ شَيْءٌ وَلَوْ كَانَ ذَا قُرْبَىٰ ۗ إِنَّمَا تُنذِرُ الَّذِينَ يَخْشَوْنَ رَبَّهُم بِالْغَيْبِ وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ ۚ وَمَن تَزَكَّىٰ فَإِنَّمَا يَتَزَكَّىٰ لِنَفْسِهِ ۚ وَإِلَى اللَّـهِ الْمَصِيرُ ﴿١٨﴾

18. Na mbebaji hatobeba mzigo (wa dhambi) wa mwengine. Na aliyeelemeshwa mzigo akiita ili kusaidiwa kubebewa mzigo wake, hatobebewa chochote, japokuwa ni jamaa wa karibu.[5] Hakika wewe unaonya wale wanaomkhofu Rabb wao bila kuyaona unayowalingania, na wakasimamisha Swalaah. Na yeyote anayejitakasa, basi hakika anajitakasa kwa ajili ya nafsi yake. Na kwa Allaah ndio mahali pa kuishia.

 

 

 

وَمَا يَسْتَوِي الْأَعْمَىٰ وَالْبَصِيرُ ﴿١٩﴾

19. Na halingani sawa kipofu na mwenye kuona.[6]

 

 

وَلَا الظُّلُمَاتُ وَلَا النُّورُ ﴿٢٠﴾

20. Wala viza na nuru.

 

 

وَلَا الظِّلُّ وَلَا الْحَرُورُ ﴿٢١﴾

21. Wala kivuli na joto.

 

 

 

وَمَا يَسْتَوِي الْأَحْيَاءُ وَلَا الْأَمْوَاتُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يُسْمِعُ مَن يَشَاءُ ۖ وَمَا أَنتَ بِمُسْمِعٍ مَّن فِي الْقُبُورِ ﴿٢٢﴾

22. Na hawalingani sawa walio hai na wafu. Hakika Allaah Anamsikilizisha Amtakaye, nawe huwezi kuwasikilizisha walioko makaburini.

 

إِنْ أَنتَ إِلَّا نَذِيرٌ ﴿٢٣﴾

 

23. Wewe (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) si chochote isipokuwa mwonyaji tu.

 

 

إِنَّا أَرْسَلْنَاكَ بِالْحَقِّ بَشِيرًا وَنَذِيرًا ۚ وَإِن مِّنْ أُمَّةٍ إِلَّا خَلَا فِيهَا نَذِيرٌ ﴿٢٤﴾

24. Hakika Sisi Tumekupeleka kwa haki ili ubashiri na uonye. Na hakuna ummah wowote isipokuwa amepita humo mwonyaji.

 

 

 

وَإِن يُكَذِّبُوكَ فَقَدْ كَذَّبَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ جَاءَتْهُمْ رُسُلُهُم بِالْبَيِّنَاتِ وَبِالزُّبُرِ وَبِالْكِتَابِ الْمُنِيرِ ﴿٢٥﴾

25. Na wakikukadhibisha (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم), basi wamekwishakadhibisha wale wa nyuma yao. Waliwajia Rusuli wao kwa hoja bayana, na Vitabu vya Hukumu, na Kitabu chenye Nuru.

 

 

ثُمَّ أَخَذْتُ الَّذِينَ كَفَرُوا ۖ فَكَيْفَ كَانَ نَكِيرِ ﴿٢٦﴾

26. Kisha Nikawashika (kuwaadhibu) wale waliokufuru, basi kulikuwa vipi Kukana Kwangu!  

 

 

 

أَلَمْ تَرَ أَنَّ اللَّـهَ أَنزَلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَأَخْرَجْنَا بِهِ ثَمَرَاتٍ مُّخْتَلِفًا أَلْوَانُهَا ۚ وَمِنَ الْجِبَالِ جُدَدٌ بِيضٌ وَحُمْرٌ مُّخْتَلِفٌ أَلْوَانُهَا وَغَرَابِيبُ سُودٌ ﴿٢٧﴾

27. Je, huoni kwamba Allaah Ameteremsha maji kutoka mbinguni, Tukatoa kwayo matunda ya rangi mbalimbali? Na miongoni mwa milima iko michirizi myeupe na myekundu yenye kutofautiana rangi zake, na myeusi iliyokoza sana.

 

 

 

وَمِنَ النَّاسِ وَالدَّوَابِّ وَالْأَنْعَامِ مُخْتَلِفٌ أَلْوَانُهُ كَذَٰلِكَ ۗ إِنَّمَا يَخْشَى اللَّـهَ مِنْ عِبَادِهِ الْعُلَمَاءُ ۗ إِنَّ اللَّـهَ عَزِيزٌ غَفُورٌ ﴿٢٨﴾

28. Na katika watu, na viumbe wanaotembea, na wanyama wa mifugo, rangi zao vile vile zinatofautiana Hakika wanaomkhofu Allaah katika Waja Wake ni ‘Ulamaa.[7] Hakika Allaah Ni Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwingi wa Kughufuria.

 

 

 

إِنَّ الَّذِينَ يَتْلُونَ كِتَابَ اللَّـهِ وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ وَأَنفَقُوا مِمَّا رَزَقْنَاهُمْ سِرًّا وَعَلَانِيَةً يَرْجُونَ تِجَارَةً لَّن تَبُورَ ﴿٢٩﴾

29. Hakika wale wanaosoma Kitabu cha Allaah, na wakasimamisha Swalaah, na wakatoa kutokana na yale Tuliyowaruzuku kwa siri na dhahiri, wanataraji tijara ambayo haitoteketea.

 

 

 

لِيُوَفِّيَهُمْ أُجُورَهُمْ وَيَزِيدَهُم مِّن فَضْلِهِ ۚ إِنَّهُ غَفُورٌ شَكُورٌ ﴿٣٠﴾

30. Ili (Allaah) Awalipe ujira wao timilifu, na Awazidishie kutokana na Fadhila Zake. Hakika Yeye Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwingi wa Kupokea Shukurani.

 

 

 

وَالَّذِي أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ مِنَ الْكِتَابِ هُوَ الْحَقُّ مُصَدِّقًا لِّمَا بَيْنَ يَدَيْهِ ۗ إِنَّ اللَّـهَ بِعِبَادِهِ لَخَبِيرٌ بَصِيرٌ ﴿٣١﴾

31. Na yale ambayo Tumekufunulia Wahy (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) ya Kitabu, ndio haki yenye kusadikisha yale yaliyoko kabla yake. Hakika Allaah kwa Waja Wake bila shaka Ni Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri, Mwenye Kuona yote.

 

 

 

ثُمَّ أَوْرَثْنَا الْكِتَابَ الَّذِينَ اصْطَفَيْنَا مِنْ عِبَادِنَا ۖ فَمِنْهُمْ ظَالِمٌ لِّنَفْسِهِ وَمِنْهُم مُّقْتَصِدٌ وَمِنْهُمْ سَابِقٌ بِالْخَيْرَاتِ بِإِذْنِ اللَّـهِ ۚ ذَٰلِكَ هُوَ الْفَضْلُ الْكَبِيرُ ﴿٣٢﴾

32. Kisha Tukawarithisha Kitabu wale Tuliowakhitari miongoni mwa Waja Wetu. Basi miongoni mwao yupo mwenye kudhulumu nafsi yake, na miongoni mwao yupo aliye wastani, na miongoni mwao yupo aliyesabiki kwa mambo mengi ya kheri kwa Idhini ya Allaah. Hiyo ndio fadhila kubwa.[8]

 

 

 

جَنَّاتُ عَدْنٍ يَدْخُلُونَهَا يُحَلَّوْنَ فِيهَا مِنْ أَسَاوِرَ مِن ذَهَبٍ وَلُؤْلُؤًا ۖ وَلِبَاسُهُمْ فِيهَا حَرِيرٌ ﴿٣٣﴾

33. Jannaat za kudumu milele wataziingia. Watapambwa humo kwa vikuku vya dhahabu na lulu, na mavazi yao humo ni hariri.[9]

 

 

 

وَقَالُوا الْحَمْدُ لِلَّـهِ الَّذِي أَذْهَبَ عَنَّا الْحَزَنَ ۖ إِنَّ رَبَّنَا لَغَفُورٌ شَكُورٌ ﴿٣٤﴾

34. Na watasema: AlhamduliLLaah (Himidi Anastahiki Allaah) Ambaye Ametuondoshea huzuni. Hakika Rabb wetu bila shaka Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwingi wa Kupokea Shukurani.

 

 

 

الَّذِي أَحَلَّنَا دَارَ الْمُقَامَةِ مِن فَضْلِهِ لَا يَمَسُّنَا فِيهَا نَصَبٌ وَلَا يَمَسُّنَا فِيهَا لُغُوبٌ ﴿٣٥﴾

35. Ambaye Ametuweka nyumba yenye kudumu kwa Fadhila Zake, haitugusi humo taabu na mashaka, na wala hayatugusi humo machovu.

 

 

 

وَالَّذِينَ كَفَرُوا لَهُمْ نَارُ جَهَنَّمَ لَا يُقْضَىٰ عَلَيْهِمْ فَيَمُوتُوا وَلَا يُخَفَّفُ عَنْهُم مِّنْ عَذَابِهَا ۚ كَذَٰلِكَ نَجْزِي كُلَّ كَفُورٍ ﴿٣٦﴾

36. Na wale waliokufuru watapata moto wa Jahannam.  Hawatahukumiwa (kifo) wakafa, na wala hawatakhafifishiwa adhabu yake. Hivyo ndivyo Tunavyomlipa kila mwingi wa kukufuru.[10]

 

 

 

وَهُمْ يَصْطَرِخُونَ فِيهَا رَبَّنَا أَخْرِجْنَا نَعْمَلْ صَالِحًا غَيْرَ الَّذِي كُنَّا نَعْمَلُ ۚ أَوَلَمْ نُعَمِّرْكُم مَّا يَتَذَكَّرُ فِيهِ مَن تَذَكَّرَ وَجَاءَكُمُ النَّذِيرُ ۖ فَذُوقُوا فَمَا لِلظَّالِمِينَ مِن نَّصِيرٍ ﴿٣٧﴾

37.  Nao watapiga mayowe humo: Rabb wetu! Tutoe tutende mema ghairi ya yale tulokuwa tukitenda. (Wataambiwa): Je, kwani Hatukukupeni umri wa kukumbuka mwenye kukumbuka humo? Na alikujieni mwonyaji. Basi onjeni! Kwani madhalimu hawana yeyote yule wa kuwanusuru.

 

 

 

إِنَّ اللَّـهَ عَالِمُ غَيْبِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ إِنَّهُ عَلِيمٌ بِذَاتِ الصُّدُورِ ﴿٣٨﴾

38. Hakika Allaah Ni Mjuzi wa ghaibu za mbinguni na ardhini. Hakika Yeye Ni Mjuzi wa yaliyomo vifuani.

 

 

 

هُوَ الَّذِي جَعَلَكُمْ خَلَائِفَ فِي الْأَرْضِ ۚ فَمَن كَفَرَ فَعَلَيْهِ كُفْرُهُ ۖ وَلَا يَزِيدُ الْكَافِرِينَ كُفْرُهُمْ عِندَ رَبِّهِمْ إِلَّا مَقْتًا ۖ وَلَا يَزِيدُ الْكَافِرِينَ كُفْرُهُمْ إِلَّا خَسَارًا ﴿٣٩﴾

39. Yeye Ndiye Ambaye Amekufanyeni warithi kwenye ardhi. Basi yeyote aliyekufuru, kufuru yake itamrudia mwenyewe.  Na kufuru za makafiri haziwazidishii mbele ya Rabb wao isipokuwa kuchukiwa, na wala kufuru za makafiri haziwazidishii isipokuwa khasara.

 

 

 

قُلْ أَرَأَيْتُمْ شُرَكَاءَكُمُ الَّذِينَ تَدْعُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ أَرُونِي مَاذَا خَلَقُوا مِنَ الْأَرْضِ أَمْ لَهُمْ شِرْكٌ فِي السَّمَاوَاتِ أَمْ آتَيْنَاهُمْ كِتَابًا فَهُمْ عَلَىٰ بَيِّنَتٍ مِّنْهُ ۚ بَلْ إِن يَعِدُ الظَّالِمُونَ بَعْضُهُم بَعْضًا إِلَّا غُرُورًا ﴿٤٠﴾

40. Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Je, mnawaona washirika wenu ambao mnawaomba badala ya Allaah? Nionyesheni ni nini walichoumba katika ardhi? Au wana ushirika wowote ule mbinguni?[11] Au Tumewapa kitabu chochote kile, kisha wao kwa hicho wakawa na hoja bayana? Hapana! Bali madhalimu hawaahidiani wao kwa wao isipokuwa ghururi.

 

 

 

إِنَّ اللَّـهَ يُمْسِكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ أَن تَزُولَا ۚ وَلَئِن زَالَتَا إِنْ أَمْسَكَهُمَا مِنْ أَحَدٍ مِّن بَعْدِهِ ۚ إِنَّهُ كَانَ حَلِيمًا غَفُورًا ﴿٤١﴾

41. Hakika Allaah Anazuia mbingu na ardhi zisitoweke. Na zikitoweka, hakuna yeyote wa kuzishikilia baada Yake. Hakika Yeye daima Ni Mvumilivu, Mwingi wa Kughufuria.

 

 

 

 

وَأَقْسَمُوا بِاللَّـهِ جَهْدَ أَيْمَانِهِمْ لَئِن جَاءَهُمْ نَذِيرٌ لَّيَكُونُنَّ أَهْدَىٰ مِنْ إِحْدَى الْأُمَمِ ۖ فَلَمَّا جَاءَهُمْ نَذِيرٌ مَّا زَادَهُمْ إِلَّا نُفُورًا ﴿٤٢﴾

42. Na wakaapa kwa Allaah, viapo vyao thabiti vya nguvu, kwamba akiwajia mwonyaji, bila shaka watakuwa waliohidika zaidi kuliko nyumati nyenginezo (zilotangulia). Lakini alipowajia mwonyaji haikuwazidishia isipokuwa kukimbia kwa chuki.

 

 

 

 

اسْتِكْبَارًا فِي الْأَرْضِ وَمَكْرَ السَّيِّئِ ۚ وَلَا يَحِيقُ الْمَكْرُ السَّيِّئُ إِلَّا بِأَهْلِهِ ۚ فَهَلْ يَنظُرُونَ إِلَّا سُنَّتَ الْأَوَّلِينَ ۚ فَلَن تَجِدَ لِسُنَّتِ اللَّـهِ تَبْدِيلًا ۖ وَلَن تَجِدَ لِسُنَّتِ اللَّـهِ تَحْوِيلًا ﴿٤٣﴾

43. Kwa kutakabari katika ardhi na kupanga njama ovu. Lakini njama ovu hazimzunguki isipokuwa mwenyewe. Je, basi wanangojea nini isipokuwa desturi ya watu wa awali. Basi hutapata katika Desturi ya Allaah mabadiliko, na wala hutapata katika Desturi ya Allaah mageuko.[12]

 

 

 

أَوَلَمْ يَسِيرُوا فِي الْأَرْضِ فَيَنظُرُوا كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ وَكَانُوا أَشَدَّ مِنْهُمْ قُوَّةً ۚ وَمَا كَانَ اللَّـهُ لِيُعْجِزَهُ مِن شَيْءٍ فِي السَّمَاوَاتِ وَلَا فِي الْأَرْضِ ۚ إِنَّهُ كَانَ عَلِيمًا قَدِيرًا ﴿٤٤﴾

44. Je, hawakutembea katika ardhi, wakatazama vipi ilikuwa hatima ya wale walio kabla yao[13], nao walikuwa wenye nguvu zaidi kuliko wao? Na hakuna lolote limshindalo Allaah mbinguni wala ardhini. Hakika Yeye daima Ni Mjuzi wa yote, Mweza wa yote.

 

 

 

وَلَوْ يُؤَاخِذُ اللَّـهُ النَّاسَ بِمَا كَسَبُوا مَا تَرَكَ عَلَىٰ ظَهْرِهَا مِن دَابَّةٍ وَلَـٰكِن يُؤَخِّرُهُمْ إِلَىٰ أَجَلٍ مُّسَمًّى ۖ فَإِذَا جَاءَ أَجَلُهُمْ فَإِنَّ اللَّـهَ كَانَ بِعِبَادِهِ بَصِيرًا ﴿٤٥﴾

45. Na lau Allaah Angeliwaadhibu watu kwa sababu ya waliyoyachuma, Asingeliacha juu ya ardhi kiumbe chochote kitembeacho, lakini Anawaakhirisha mpaka muda maalumu uliokadiriwa. Na utakapofika muda wao, basi hakika Allaah daima Ni Mwenye Kuona Waja Wake.

 

 

 

[1] Hakuna Awezaye Kuzuia Rehma Ya Allaah Wala Kuitoa Anayoizuia Allaah:

 

Hivyo ni sawa na duaa ifuatayo inayosomwa katika kismamo cha baada ya kurukuu na baada ya kumaliza Swalaah:

اللّهُـمَّ لا مانِعَ لِما أَعْطَـيْت، وَلا مُعْطِـيَ لِما مَنَـعْت، وَلا يَنْفَـعُ ذا الجَـدِّ مِنْـكَ الجَـد

“Ee Allaah, hakuna mwenye kukizuia Ulichokitoa, wala Mwenye kutoa Ulichokizuia, na wala utajiri wa mtu haumnufaishi mwenye utajiri mbele Yako.”

 

[2] Mfano Wa Ardhi Iliyokufa (Kame), Kisha Allaah (سبحانه وتعالى) Akaihuisha Kwa Mvua, Ni Mfano Wa Kuwahuisha Watu Kutoka Makaburini Mwao Siku Ya Qiyaamah:

 

Rejea Ar-Ruwm (30:50).

 

[3] Neno Zuri Ni Aina Zote Za Dhikru-Allaah (Kumdhukuru Allaah):

Neno zuri ambalo hupanda juu kwa Allaah (سبحانه وتعالى), ni aina zote za kumdhukuru Allaah (سبحانه وتعالى). Miongoni mwazo ni kusoma Qur-aan, kuleta Tasbiyh (Kumtakasa Allaah), Tahmiyd (Kumhimidi Allaah), Tahliyl (Kumpwekesha Allaah), Takbiyr (Kumtukuza Allaah), Istighfaar (kuomba maghfirah), Duaa na Adhkaar nyenginezo.  Na Hadiyth ifuatayo imethibitisha:

 

حَدَّثَنَا أَبُو بِشْرٍ، بَكْرُ بْنُ خَلَفٍ حَدَّثَنِي يَحْيَى بْنُ سَعِيدٍ، عَنْ مُوسَى بْنِ أَبِي عِيسَى الطَّحَّانِ، عَنْ عَوْنِ بْنِ عَبْدِ اللَّهِ، عَنْ أَبِيهِ، أَوْ عَنْ أَخِيهِ، عَنِ النُّعْمَانِ بْنِ بَشِيرٍ، قَالَ قَالَ رَسُولُ اللَّهِ ـ صلى الله عليه وسلم ـ ‏ "‏ إِنَّ مِمَّا تَذْكُرُونَ مِنْ جَلاَلِ اللَّهِ التَّسْبِيحَ وَالتَّهْلِيلَ وَالتَّحْمِيدَ يَنْعَطِفْنَ حَوْلَ الْعَرْشِ لَهُنَّ دَوِيٌّ كَدَوِيِّ النَّحْلِ تُذَكِّرُ بِصَاحِبِهَا أَمَا يُحِبُّ أَحَدُكُمْ أَنْ يَكُونَ لَهُ - أَوْ لاَ يَزَالَ لَهُ - مَنْ يُذَكِّرُ بِهِ

Amesimulia Nu’maan bin Bashiyr (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakika Tasbiyh (Kumtakasa), Tahliyl (Kumpwekesha), na Tahmiyd (Kumhimidi) ambayo ni maneno mnayomtukuza kwayo Allaah, yanazunguka kwenye ‘Arsh, yanavuma kama nyuki na yanamtaja aliyeyatamka. Je, hakuna yeyote kati yenu ambaye angependa kuwa na -au kuendelea kuwa- na kitu ambacho kitamtaja (mbele ya Allaah?)”  [Sunan Ibn Maajah na ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh Ibn Maajah (3086), na As-Silsilah Asw-Swahiyhah (3358)]

 

[4] Aina Tatu Za Mfano Wa Udogo Katika Tende:

 

Allaah (سبحانه وتعالى) Anapiga mifano ya udogo katika tende kwa kutaja aina tatu za viliomo ndani yake. (i) Fatiylun: Uzi katika kokwa ya tende. Rejea An-Nisaa (4:49, 77), Al-Israa (17:71). (ii) Naqiyrun: Kitone cha kokwa ya tende. Rejea An-Nisaa (4:53), (4:124). (iii) Qitwmiyrun: Kijiwavu cha kokwa ya tende kwenye Aayah hii ya Suwrah Faatwir (35:13). 

 

[5] Hakuna Mwenye Uhusiano Wa Damu Atakayemsaidia Jamaa Yake Siku Ya Qiyaamah:

 

Siku ya Qiyaamah, kila mtu atabeba dhambi zake, na hakuna atakayemsaidia jamaa, wala ndugu, wala wazazi, bali kila mmoja atajali nafsi yake! Rejea ‘Abasa (80:33-37), Al-Muuminuwn (23:101). 

 

[6] Mifano Ya Tofauti Ya Kafiri Na Muumini:

 

Kuanzia Aayah hii Faatwir (35:19) hadi namba (22), Allaah (سبحانه وتعالى) Anapiga mfano wa tofauti ya kafiri na Muumini ya kwamba hawalingani sawa; kipofu na mwenye kuona, viza na nuru, vivuli na joto na waliohai na wafu:

 

(i) Kipofu Na Mwenye Kuona:

 

Na kipofu asiyeiona Dini ya Allaah, halingani na yule mwenye kuona ambaye anaiona njia ya haki na anaifuata. [Tafsiyr Al-Muyassar]

 

Na Allaah (سبحانه وتعالى) Anataja hivyo katika Suwrah Ar-Ra’d (13:19) kwamba anayejua Aliyoteremshiwa Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) ni haki, hawi sawa na kipofu asiyetambua hilo.

 

Rejea pia Al-An’aam (6:50), Ar-Ra’d (13:16), Ghaafir (40:58), Huwd (11:24), Az-Zukhruf (43:40). 

 

(ii) Viza Na Nuru (Mwanga):

 

Rejea Suwrah Ibraahiym (14:1) kwenye maelezo bayana na rejea mbalimbali.

 

(iii) Vivuli Na Joto:

 

Imaam Ibn Kathiyr amejumuisha maana ya yote yaliyotajwa katika Aayah hizo za kuanzia namba (19) hadi namba (22).

 

Muumini ni mwenye kusikia na mwenye kuona, anatembea katika Nuru juu ya Swiraatw Al-Mustaqiym (Njia Iliyonyooka) duniani na Aakhirah hadi afikie kustakiri mahali pake katika Jannah (Pepo au mabustani) yenye vivuli na chemchemu. Na kafiri ni kipofu na kiziwi, anatembea katika viza na hatoki humo, bali anatangatanga ndani ya upotofu wake duniani na Aakhirah hadi afikie katika joto na moto uwakao vikali kama Anavyosema Allaah katika Suwrah Al-Waaqi’ah (56:43-44).  [Tafsiyr Ibn Kathiyr]

 

(iv) Waliohai (Waumini) Na Wafu (Makafiri)

 

Ni sawa na nyoyo zilizohai na nyoyo zilizokufa.

 

Wafu ni kama makafiri, hawawi sawa na waliohai ambao ni Waumini. Rejea Al-An’aam (6:122) kwenye ufafanuzi. Na pia rejea pia Huwd (11:24).

 

[7] Wanaomkhofu Allaah Ni ‘Ulamaa:

 

Yaani: Bali wale walio na ilimu hakika wanamcha Allaah (سبحانه وتعالى) kama Anavyopaswa kuogopwa, kwa sababu kadiri maarifa ya kumjua Allaah (سبحانه وتعالى)  Mwenye Uwezo, Mjuzi wa yote, Ambaye  Ana Sifa Kamilifu  na Ameelezewa kwa Majina Mazuri kabisa,  ndivyo watakavyozidi kumcha. [Tafsiyr Ibn Kathiyr]

 

[8] Aina Za Watu Na Amali Zao:

 

Kisha Tukawapa Qur-aan, baada ya kuangamia nyumati zilizopita, wale Tuliowachagua miongoni mwa ummah wa Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم). Basi kati yao kuna: (i) Aliyeidhulumu nafsi yake kwa kufanya baadhi ya maasia. (ii) Aliyekuwa wastani, naye ni yule mwenye kutekeleza yaliyo wajibu na kuepuka yaliyoharamishwa. (iii) Mwenye kutangulia kufanya mambo ya kheri kwa Idhini ya Allaah, naye ni yule mwenye kukimbilia na kujitahidi kufanya amali njema za faradhi na za ziada. Na kupewa Kitabu huko na kuchaguliwa ummah huu ndio fadhila kubwa. [Tafsiyr Al-Muyassar]

 

[9] Neema Za Watu Wa Jannah, Watamhimidi Allaah Na Watadumu Katika Raha Za Milele:

 

Kuanzia Aayah hii hadi namba (35) zinataja neema watakazozipata watu wa Jannah watakapoingizwa humo. Na neema na raha za watu wa Jannah, zimetajwa kwa wingi katika Qur-aan na Sunnah. Allaah (سبحانه وتعالى)  Ameisifu Jannah kuwa haikupatapo kusikika wala kuonekana wala kuwaziwa. Rejea As-Sajdah (32:17). Na pia  rejea Aayah namba (33-34) pamoja na Aayah hii namba (35). Rejea pia At-Tawbah (9:72), Asw-Swaaffaat (37:41-49), Az-Zukhruf (43:68-73), Muhammad (47:15), Ar-Rahmaan (55:46-76), Al-Waaqi’ah (56:15-40), Atw-Twuwr (52:17-24), Al-Insaan (76:12-22), An-Nabaa (78:31-36), Al-Mutwaffifiyn (83:22-28), Al-Ghaashiyah (88:8-16) na kwengineko kwingi.

 

Na miongoni mwa Hadiyth zinazotaja kuwa watu wa Jannah watakuwa hai na watadumu milele katika neema na raha za Jannah ni hii ifuatayo:

 

وعن أبي سعيد وأبي هريرة رضي الله عنهما : أنَّ رسولَ اللهِ صلى الله عليه وسلم قال : (( إذَا دَخَلَ أهْلُ الجَنَّةِ الجَنَّةَ يُنَادِي مُنَادٍ : إنَّ لَكُمْ أنْ تَحْيَوْا ، فَلاَ تَمُوتُوا أَبَداً ، وإنَّ لَكُمْ أنْ تَصِحُّوا ، فلا تَسْقَمُوا أبداً ، وإنَّ لَكمْ أنْ تَشِبُّوا فلا تَهْرَمُوا أبداً ، وإنَّ لَكُمْ أَنْ تَنْعَمُوا ، فَلاَ تَبْأسُوا أَبَداً )) .   رواه مسلم .

Amesimulia Abuu Sa’iyd na Abuu Hurayrah (رضي الله عنهما): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Watu wa Jannah watakapoingia Jannah, atanadi mwenye kunadi: “Hakika nyinyi mtaishi milele wala hamtakuwa wagonjwa, nanyi mtakuwa barobaro milele wala hamtazeeka, nanyi mtaneemeka milele wala hamtapata shida.” [Muslim] 

 

[10] Watu Wa Motoni Hawatakufa Wala Hawatapunguziwa Adhabu Bali Watadumu Katika Adhabu:

 

Rejea Az-Zukhruf (43:74-77), Twaahaa (20:74), Al-A’laa (87:12-13), Al-Israa (17/l97), An-Nisaa (4:56), Yuwnus (10:52), As-Sajdah (32:21), An-Nabaa (78:30).

 

Na miongoni mwa Hadiyth zinazotaja kuwa watu wa motoni hawatakufa wala kuishi uhai wa raha humo bali wataendelea kuadhibiwa ni zifuatazo:

 

وَحَدَّثَنِي نَصْرُ بْنُ عَلِيٍّ الْجَهْضَمِيُّ، حَدَّثَنَا بِشْرٌ، - يَعْنِي ابْنَ الْمُفَضَّلِ - عَنْ أَبِي مَسْلَمَةَ، عَنْ أَبِي نَضْرَةَ، عَنْ أَبِي سَعِيدٍ، قَالَ قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم ‏ "‏ أَمَّا أَهْلُ النَّارِ الَّذِينَ هُمْ أَهْلُهَا فَإِنَّهُمْ لاَ يَمُوتُونَ فِيهَا وَلاَ يَحْيَوْنَ وَلَكِنْ نَاسٌ أَصَابَتْهُمُ النَّارُ بِذُنُوبِهِمْ - أَوْ قَالَ بِخَطَايَاهُمْ - فَأَمَاتَهُمْ إِمَاتَةً حَتَّى إِذَا كَانُوا فَحْمًا أُذِنَ بِالشَّفَاعَةِ فَجِيءَ بِهِمْ ضَبَائِرَ ضَبَائِرَ فَبُثُّوا عَلَى أَنْهَارِ الْجَنَّةِ ثُمَّ قِيلَ يَا أَهْلَ الْجَنَّةِ أَفِيضُوا عَلَيْهِمْ ‏.‏ فَيَنْبُتُونَ نَبَاتَ الْحِبَّةِ تَكُونُ فِي حَمِيلِ السَّيْلِ ‏"‏ ‏.‏ فَقَالَ رَجُلٌ مِنَ الْقَوْمِ كَأَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم قَدْ كَانَ بِالْبَادِيَةِ ‏.‏

Amesimulia Abuu Sa’iyd (رضي الله عنه):  Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Watu wa motoni ni wale ambao watasalia humo milele, na hakika hawatakufa wala hawataishi humo maisha ya raha.  Lakini watu ambao moto utawasibu kwa ajili ya dhambi zao, au akasema (msimuliaji) kwa ajili ya maovu yao, hawa (Allaah) Atawafisha mpaka wageuke makaa. Kisha watapewa uombezi na kuletwa makundi kwa makundi na kutawanywa kwenye mito ya Jannah (Peponi) kisha itasemwa: Enyi watu wa Jannah! Wamwagieni maji. Kisha watamea kama inavyochipuka mbegu kwenye udongo unaobebwa na mafuriko.” Mtu mmoja miongoni mwa watu akasema: (Inaonekana) kana kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) ameishi jangwani (akaona hali hiyo). [Muslim]

 

Na pia:

 

حَدَّثَنَا عُمَرُ بْنُ حَفْصِ بْنِ غِيَاثٍ، حَدَّثَنَا أَبِي، حَدَّثَنَا الأَعْمَشُ، حَدَّثَنَا أَبُو صَالِحٍ، عَنْ أَبِي سَعِيدٍ الْخُدْرِيِّ ـ رضى الله عنه ـ قَالَ قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم ‏"‏ يُؤْتَى بِالْمَوْتِ كَهَيْئَةِ كَبْشٍ أَمْلَحَ فَيُنَادِي مُنَادٍ يَا أَهْلَ الْجَنَّةِ، فَيَشْرَئِبُّونَ وَيَنْظُرُونَ فَيَقُولُ هَلْ تَعْرِفُونَ هَذَا فَيَقُولُونَ نَعَمْ هَذَا الْمَوْتُ، وَكُلُّهُمْ قَدْ رَآهُ، ثُمَّ يُنَادِي يَا أَهْلَ النَّارِ، فَيَشْرَئِبُّونَ وَيَنْظُرُونَ، فَيَقُولُ هَلْ تَعْرِفُونَ هَذَا فَيَقُولُونَ نَعَمْ هَذَا الْمَوْتُ، وَكُلُّهُمْ قَدْ رَآهُ، فَيُذْبَحُ ثُمَّ يَقُولُ يَا أَهْلَ الْجَنَّةِ، خُلُودٌ فَلاَ مَوْتَ، وَيَا أَهْلَ النَّارِ، خُلُودٌ فَلاَ مَوْتَ ثُمَّ قَرَأَ ‏وَأَنْذِرْهُمْ يَوْمَ الْحَسْرَةِ إِذْ قُضِيَ الأَمْرُ وَهُمْ فِي غَفْلَةٍ ‏ وَهَؤُلاَءِ فِي غَفْلَةٍ أَهْلُ الدُّنْيَا ‏وَهُمْ لاَ يُؤْمِنُونَ‏

Amesimulia Abuu Sa‘iyd Al-Khudriyy (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Kifo kitaletwa katika umbo la kondoo mweupe, na hapo ataita muitaji: Enyi watu wa Jannah! Watu hao watachuchumia ili kuangalia. Muitaji atauliza kwa kusema: Je huyu mnamjua? Watasema ndio, huyu ni umauti. Na wote walikwishauona (wakati wa kutolewa roho duniani). Kisha atanadi tena: Enyi watu wa motoni! Watu hao watachuchumia ili kuangalia. Atauliza: Je, huyu mnamjua? Watajibu: Ndio, huyu ni umauti. Na wote walikwishauona (umauti). Hapo atachinjwa, kisha mwenye kunadi atasema: Enyi watu wa Peponi! Mtadumu milele hapana kifo. Na enyi watu wa motoni! Mtadumu milele hapana kifo. Kisha atasoma:

 

وَأَنذِرْهُمْ يَوْمَ الْحَسْرَةِ إِذْ قُضِيَ الْأَمْرُ وَهُمْ فِي غَفْلَةٍ وَهُمْ لَا يُؤْمِنُونَ ﴿٣٩﴾

“Na waonye Siku ya majuto itakapohukumiwa amri, na hali wao wamo katika mghafala, wala hawaamini.” [Maryam (10:39) – Al-Bukhaariy]

 

Mateso na adhabu za watu wa motoni zimetajwa katika Qur-aan sehemu nyingi. Na mateso hayo yanawaanzia tokea wanapotolewa roho za, rejea Al-An’aam (6:93),  Al-Anfaal (8:50). Na adhabu zao wanapofika motoni, rejea An-Nabaa (78:21) kwenye maelezo bayana kuhusu aina za mateso na adhabu za watu wa motoni. Na kuhusu aina za moto na majina yake, rejea Al-Muddath-thir (74:26).

 

[11] Wanaoabudiwa Pasi Na Allaah Hawawezi Kuumba Chochote:

 

Rejea Luqmaan (31:11) na rejea Al-Ahqaaf (46:4) kwenye maelezo na rejea mbalimbali.

 

[12] Desturi Ya Allaah Ya Kuwaadhibu Makafiri:

 

Aayah hii ya Suwrah Faatwir (35:43), inataja Desturi ya Allaah ya Kuwaadhibu washirikina, makafiri na madhalimu. Na katika Suwrah Aal-‘Imraan (3:137), Allaah (سبحانه وتعالى) Anataja pia Desturi Yake kuhusiana na makafiri na Waumini.  Kisha Aayah (35:44) inayofuatia, Allaah (سبحانه وتعالى) Anawataka watembee katika ardhi wajionee adhabu zilowafikia waliokadhibisha na hatima zao. Rejea Al-An’aam (6:11), Yuwsuf (12:109), Al-Kahf (18:55), Al-Hajj (22:46).

 

[13] Makafiri Watembee Katika Ardhi Wajionee Adhabu Zilizowasibu Waliokadhibisha Risala, Na Wajionee Hatima Zao:

 

Rejea Al-An’aam (6:11), Yuwsuf (12:109), Al-Kahf (18:55), Al-Hajj (22:46).

 

 

 

Share