034 - Saba-a

 

سَبَاء

 

034-Saba-a

 

034-Saba-a: Utangulizi Wa Suwrah

 

 Alhidaaya.com

  

 

 

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

 

الْحَمْدُ لِلَّـهِ الَّذِي لَهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ وَلَهُ الْحَمْدُ فِي الْآخِرَةِ ۚ وَهُوَ الْحَكِيمُ الْخَبِيرُ ﴿١﴾

1.  AlhamduliLLaah (Himdi Anastahiki Allaah), Ambaye Ni Vyake vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini, na Himidi ni Zake katika Aakhirah, Naye Ni Mwenye Hikmah wa yote, Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri.

 

 

 

 

يَعْلَمُ مَا يَلِجُ فِي الْأَرْضِ وَمَا يَخْرُجُ مِنْهَا وَمَا يَنزِلُ مِنَ السَّمَاءِ وَمَا يَعْرُجُ فِيهَا ۚ وَهُوَ الرَّحِيمُ الْغَفُورُ ﴿٢﴾

2. Anajua yanayoingia ardhini, na yanayotoka humo, na yanayoteremka kutoka mbinguni, na yanayopanda huko, Naye Ndiye Mwenye Kurehemu, Mwingi wa Kughufuria.

 

 

 

 

وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا لَا تَأْتِينَا السَّاعَةُ ۖ قُلْ بَلَىٰ وَرَبِّي لَتَأْتِيَنَّكُمْ عَالِمِ الْغَيْبِ ۖ لَا يَعْزُبُ عَنْهُ مِثْقَالُ ذَرَّةٍ فِي السَّمَاوَاتِ وَلَا فِي الْأَرْضِ وَلَا أَصْغَرُ مِن ذَٰلِكَ وَلَا أَكْبَرُ إِلَّا فِي كِتَابٍ مُّبِينٍ ﴿٣﴾

3. Na wale waliokufuru wakasema: Saa haitotufikia! Sema: Sivyo hivyo! Naapa kwa Rabb wangu! Bila shaka itakufikieni, Mjuzi wa ghaibu. Hakuna kinachofichika Kwake hata chenye uzito wa chembe (kama atomu) mbinguni wala ardhini, wala kidogo zaidi kuliko hicho, wala kikubwa zaidi isipokuwa kimo katika Kitabu kinachobainisha.[1]

 

 

 

 

لِّيَجْزِيَ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ ۚ أُولَـٰئِكَ لَهُم مَّغْفِرَةٌ وَرِزْقٌ كَرِيمٌ ﴿٤﴾

4. Ili Awalipe wale walioamini na wakatenda mema. Hao watapata maghfirah na riziki tukufu.

 

 

 

 

وَالَّذِينَ سَعَوْا فِي آيَاتِنَا مُعَاجِزِينَ أُولَـٰئِكَ لَهُمْ عَذَابٌ مِّن رِّجْزٍ أَلِيمٌ ﴿٥﴾

5. Na wale waliofanya bidii katika Aayaat (na Ishara) Zetu watake kuzibatilisha, hao watapata adhabu mbaya ya kufadhaika, iumizayo.

 

 

 

 

وَيَرَى الَّذِينَ أُوتُوا الْعِلْمَ الَّذِي أُنزِلَ إِلَيْكَ مِن رَّبِّكَ هُوَ الْحَقَّ وَيَهْدِي إِلَىٰ صِرَاطِ الْعَزِيزِ الْحَمِيدِ ﴿٦﴾

6. Na wale waliopewa ilimu wanaona kuwa yale yaliyoteremshwa kwako kutoka kwa Rabb wako ndio haki, na yanaongoza kwenye Njia ya Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Kustahiki Kuhimidiwa kwa yote.

 

 

 

 

وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا هَلْ نَدُلُّكُمْ عَلَىٰ رَجُلٍ يُنَبِّئُكُمْ إِذَا مُزِّقْتُمْ كُلَّ مُمَزَّقٍ إِنَّكُمْ لَفِي خَلْقٍ جَدِيدٍ ﴿٧﴾

7. Na wale waliokufuru wakasema: Je, tukuelekezeni kwa mtu anayekujulisheni kwamba mtakapomomonyolewa mkawa vumbi lililotawanyika mbali, mtakuwa katika umbo jipya?[2]

 

 

 

 

أَفْتَرَىٰ عَلَى اللَّـهِ كَذِبًا أَم بِهِ جِنَّةٌ ۗ بَلِ الَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِالْآخِرَةِ فِي الْعَذَابِ وَالضَّلَالِ الْبَعِيدِ ﴿٨﴾

8. Je, amemtungia Allaah uongo, au ana wazimu?[3]  Bali wale wasioamini Aakhirah watakuwa katika adhabu na upotofu wa mbali.

 

 

 

 

أَفَلَمْ يَرَوْا إِلَىٰ مَا بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُم مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ ۚ إِن نَّشَأْ نَخْسِفْ بِهِمُ الْأَرْضَ أَوْ نُسْقِطْ عَلَيْهِمْ كِسَفًا مِّنَ السَّمَاءِ ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً لِّكُلِّ عَبْدٍ مُّنِيبٍ ﴿٩﴾

9. Je, kwani hawaoni yale yaliyoko mbele yao na yale yaliyo nyuma yao ya mbingu na ardhi? Tungelitaka, Tungeliwadidimiza ardhini, au Tungeliwaangushia juu yao vipande vya mbingu. Hakika katika hayo kuna Aayah (Ishara, Mazingatio) kwa kila mja anayetubia mara kwa mara (kwa Allaah).

 

 

 

 

وَلَقَدْ آتَيْنَا دَاوُودَ مِنَّا فَضْلًا ۖ يَا جِبَالُ أَوِّبِي مَعَهُ وَالطَّيْرَ ۖ وَأَلَنَّا لَهُ الْحَدِيدَ ﴿١٠﴾

10. Na kwa yakini Tulimpa Daawuwd Fadhila kutoka Kwetu, (Tukasema): Ee majabali! Rejesheni kumsabbih (Allaah) pamoja naye na ndege pia. Na Tukamlainishia chuma.[4]

 

 

 

أَنِ اعْمَلْ سَابِغَاتٍ وَقَدِّرْ فِي السَّرْدِ ۖ وَاعْمَلُوا صَالِحًا ۖ إِنِّي بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ ﴿١١﴾

11. Na kwamba: Tengeneza mavazi ya chuma mapana, na kadiria sawasawa katika kuunganisha daraya, na tendeni mema. Hakika Mimi Ni Mwenye Kuona myatendayo.

 

 

 

 

وَلِسُلَيْمَانَ الرِّيحَ غُدُوُّهَا شَهْرٌ وَرَوَاحُهَا شَهْرٌ ۖ وَأَسَلْنَا لَهُ عَيْنَ الْقِطْرِ ۖ وَمِنَ الْجِنِّ مَن يَعْمَلُ بَيْنَ يَدَيْهِ بِإِذْنِ رَبِّهِ ۖ وَمَن يَزِغْ مِنْهُمْ عَنْ أَمْرِنَا نُذِقْهُ مِنْ عَذَابِ السَّعِيرِ ﴿١٢﴾

12. Na Sulaymaan (Tulimtiishia) upepo. Safari yake ya asubuhi ni (mwendo wa) mwezi, na safari yake ya jioni ni (mwendo wa) mwezi, na Tukamtiririzia chemchemu ya shaba. Na (Tulimtiishia pia) kati ya majini wanaofanya kazi mbele yake kwa Idhini ya Rabb wake. Na yeyote atakayezikengeuka Amri Zetu, Tunamuonjesha adhabu ya moto uliowashwa vikali mno. 

 

 

 

يَعْمَلُونَ لَهُ مَا يَشَاءُ مِن مَّحَارِيبَ وَتَمَاثِيلَ وَجِفَانٍ كَالْجَوَابِ وَقُدُورٍ رَّاسِيَاتٍ ۚ اعْمَلُوا آلَ دَاوُودَ شُكْرًا ۚ وَقَلِيلٌ مِّنْ عِبَادِيَ الشَّكُورُ ﴿١٣﴾

13. Wanamfanyia kazi atakayo; (kujenga) ngome ndefu za fakhari na tasawiri, na madeste makubwa kama mahodhi na masufuria makubwa yaliyothibiti imara. (Tukasema): Tendeni enyi familia ya Daawuwd kwa shukurani! Na wachache miongoni mwa Waja Wangu ni wenye kushukuru.[5]

 

 

 

فَلَمَّا قَضَيْنَا عَلَيْهِ الْمَوْتَ مَا دَلَّهُمْ عَلَىٰ مَوْتِهِ إِلَّا دَابَّةُ الْأَرْضِ تَأْكُلُ مِنسَأَتَهُ ۖ فَلَمَّا خَرَّ تَبَيَّنَتِ الْجِنُّ أَن لَّوْ كَانُوا يَعْلَمُونَ الْغَيْبَ مَا لَبِثُوا فِي الْعَذَابِ الْمُهِينِ ﴿١٤﴾

14. Na Tulipomkidhia mauti, hakuna kilichowajulisha kifo chake isipokuwa mdudu wa ardhi akila fimbo yake. Kisha alipoanguka, ikawabainikia majini kwamba lau wangelikuwa wanajua ya ghaibu, basi wasingebakia katika adhabu ya kudhalilisha.

 

 

 

 

لَقَدْ كَانَ لِسَبَإٍ فِي مَسْكَنِهِمْ آيَةٌ ۖ جَنَّتَانِ عَن يَمِينٍ وَشِمَالٍ ۖ كُلُوا مِن رِّزْقِ رَبِّكُمْ وَاشْكُرُوا لَهُ ۚ بَلْدَةٌ طَيِّبَةٌ وَرَبٌّ غَفُورٌ ﴿١٥﴾

15. Kwa yakini ilikuwa ni Aayah (Ishara) kwa (watu wa) Saba-a katika masikani zao. Bustani mbili; kulia na kushoto. (Wakaambiwa): Kuleni katika riziki ya Rabb wenu na mshukuruni. Mji mzuri na Rabb Ambaye Ni Mwingi wa Kughufuria.[6]

 

 

 

فَأَعْرَضُوا فَأَرْسَلْنَا عَلَيْهِمْ سَيْلَ الْعَرِمِ وَبَدَّلْنَاهُم بِجَنَّتَيْهِمْ جَنَّتَيْنِ ذَوَاتَيْ أُكُلٍ خَمْطٍ وَأَثْلٍ وَشَيْءٍ مِّن سِدْرٍ قَلِيلٍ ﴿١٦﴾

16. Lakini wakakengeuka. Basi Tukawapelekea mafuriko ya mabwawa, na Tukawabadilishia badala ya bustani zao mbili, kwa bustani mbili nyinginezo zenye matunda machungu mno, na mivinje, na baadhi ya mikunazi kidogo. 

 

 

 

ذَٰلِكَ جَزَيْنَاهُم بِمَا كَفَرُوا ۖ وَهَلْ نُجَازِي إِلَّا الْكَفُورَ ﴿١٧﴾

17. Hayo Tuliwalipa kwa vile walivyokufuru. Na Hatuadhibu isipokuwa anayekufuru.

 

 

 

وَجَعَلْنَا بَيْنَهُمْ وَبَيْنَ الْقُرَى الَّتِي بَارَكْنَا فِيهَا قُرًى ظَاهِرَةً وَقَدَّرْنَا فِيهَا السَّيْرَ ۖ سِيرُوا فِيهَا لَيَالِيَ وَأَيَّامًا آمِنِينَ ﴿١٨﴾

18. Na Tukaweka baina yao na baina ya miji Tuliyoibariki, miji mingine iliyo karibu karibu, na Tukakadiria humo vituo vya safari. (Tukasema): Safirini humo usiku na mchana kwa amani.

 

 

 

فَقَالُوا رَبَّنَا بَاعِدْ بَيْنَ أَسْفَارِنَا وَظَلَمُوا أَنفُسَهُمْ فَجَعَلْنَاهُمْ أَحَادِيثَ وَمَزَّقْنَاهُمْ كُلَّ مُمَزَّقٍ ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّكُلِّ صَبَّارٍ شَكُورٍ ﴿١٩﴾

19. Wakasema: Rabb wetu! Baidisha baina ya safari zetu. Na wakazidhulumu nafsi zao. Basi Tukawafanya kuwa ni simulizi, na Tukawafarikisha na kuwatawanyatawanya kabisa. Hakika katika hayo bila shaka kuna Aayaat (Ishara, Mazingatio) kwa kila mwingi wa kusubiri na mwingi wa kushukuru.

 

 

وَلَقَدْ صَدَّقَ عَلَيْهِمْ إِبْلِيسُ ظَنَّهُ فَاتَّبَعُوهُ إِلَّا فَرِيقًا مِّنَ الْمُؤْمِنِينَ ﴿٢٠﴾

20. Na kwa yakini Ibliys alisadikisha dhana yake juu yao, basi walimfuata isipokuwa kundi miongoni mwa Waumini.

 

 

 

وَمَا كَانَ لَهُ عَلَيْهِم مِّن سُلْطَانٍ إِلَّا لِنَعْلَمَ مَن يُؤْمِنُ بِالْآخِرَةِ مِمَّنْ هُوَ مِنْهَا فِي شَكٍّ ۗ وَرَبُّكَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ حَفِيظٌ ﴿٢١﴾

21. Na yeye (Ibliys) hakuwa ana madaraka yoyote juu yao isipokuwa ili Tujue ni nani yule anayeamini Aakhirah na nani yule anayeitilia shaka. Na Rabb wako Ni Mwenye Kuhifadhi kila kitu.

 

 

 

قُلِ ادْعُوا الَّذِينَ زَعَمْتُم مِّن دُونِ اللَّـهِ ۖ لَا يَمْلِكُونَ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ فِي السَّمَاوَاتِ وَلَا فِي الْأَرْضِ وَمَا لَهُمْ فِيهِمَا مِن شِرْكٍ وَمَا لَهُ مِنْهُم مِّن ظَهِيرٍ ﴿٢٢﴾

22. Sema: Ombeni wale mnaodai kwa dhana (ni waabudiwa) badala ya Allaah, hawamiliki hata uzito wa chembe (kama atomu) mbinguni wala ardhini, na wala hawana humo ushirika Naye, na wala Yeye (Allaah) Hana msaidizi miongoni mwao.

 

 

 

وَلَا تَنفَعُ الشَّفَاعَةُ عِندَهُ إِلَّا لِمَنْ أَذِنَ لَهُ ۚ حَتَّىٰ إِذَا فُزِّعَ عَن قُلُوبِهِمْ قَالُوا مَاذَا قَالَ رَبُّكُمْ ۖ قَالُوا الْحَقَّ ۖ وَهُوَ الْعَلِيُّ الْكَبِيرُ ﴿٢٣﴾

23. Na wala haitofaa shafaa’ah (uombezi) mbele Yake isipokuwa kwa yule Aliyempa idhini. Mpaka litakapoondolewa fazaiko nyoyoni mwao watasema: Amesema nini Rabb wenu? Watasema: Ya haki, Naye Ni Mwenye ‘Uluwa Uliotukuka, Mkubwa Kabisa.

 

 

 

 

قُلْ مَن يَرْزُقُكُم مِّنَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۖ قُلِ اللَّـهُ ۖ وَإِنَّا أَوْ إِيَّاكُمْ لَعَلَىٰ هُدًى أَوْ فِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ ﴿٢٤﴾

24. Sema: Nani yule anayekuruzukuni kutoka mbinguni na ardhini?  Sema: Ni Allaah!  Na hakika ima sisi au nyinyi, bila shaka tuko juu ya uongofu au katika upotofu bayana.[7]

 

 

 

قُل لَّا تُسْأَلُونَ عَمَّا أَجْرَمْنَا وَلَا نُسْأَلُ عَمَّا تَعْمَلُونَ ﴿٢٥﴾

25. Sema: Hamtoulizwa kuhusu ule uhalifu tulioufanya, na wala hatutoulizwa kwa yale mnayoyatenda.

 

 

 

قُلْ يَجْمَعُ بَيْنَنَا رَبُّنَا ثُمَّ يَفْتَحُ بَيْنَنَا بِالْحَقِّ وَهُوَ الْفَتَّاحُ الْعَلِيمُ ﴿٢٦﴾

26. Sema: Rabb wetu Atatukusanya, kisha Atahukumu baina yetu kwa haki, Naye Ndiye Hakimu, Mjuzi wa yote.

 

 

 

قُلْ أَرُونِيَ الَّذِينَ أَلْحَقْتُم بِهِ شُرَكَاءَ ۖ كَلَّا ۚ بَلْ هُوَ اللَّـهُ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ ﴿٢٧﴾

27. Sema: Nionyesheni wale mliowaunganisha Naye kuwa washirika. Laa hasha! Bali Yeye Ndiye Allaah Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Hikmah wa yote.

 

 

 

وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا كَافَّةً لِّلنَّاسِ بَشِيرًا وَنَذِيرًا وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٢٨﴾

28. Na Hatukukutuma (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) isipokuwa kwa watu wote uwe mbashiriaji na muonyaji, lakini watu wengi hawajui.[8]

 

 

 

وَيَقُولُونَ مَتَىٰ هَـٰذَا الْوَعْدُ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ ﴿٢٩﴾

29. Na wanasema: Ni lini hiyo ahadi (ya Qiyaamah), mkiwa ni wasemao kweli?[9]

 

 

 

قُل لَّكُم مِّيعَادُ يَوْمٍ لَّا تَسْتَأْخِرُونَ عَنْهُ سَاعَةً وَلَا تَسْتَقْدِمُونَ ﴿٣٠﴾

30. Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Mnayo miadi ya Siku ambayo hamtoiakhirisha saa, na wala hamtakadimisha.

 

 

 

وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا لَن نُّؤْمِنَ بِهَـٰذَا الْقُرْآنِ وَلَا بِالَّذِي بَيْنَ يَدَيْهِ ۗ وَلَوْ تَرَىٰ إِذِ الظَّالِمُونَ مَوْقُوفُونَ عِندَ رَبِّهِمْ يَرْجِعُ بَعْضُهُمْ إِلَىٰ بَعْضٍ الْقَوْلَ يَقُولُ الَّذِينَ اسْتُضْعِفُوا لِلَّذِينَ اسْتَكْبَرُوا لَوْلَا أَنتُمْ لَكُنَّا مُؤْمِنِينَ ﴿٣١﴾

31. Na wale waliokufuru wakasema: Hatutoiamini Qur-aan hii, na wala yale yaliyokuwa kabla yake. Na lau ungeliona pale madhalimu watakaposimamishwa mbele ya Rabb wao, wakirejesheana wenyewe kwa wenyewe maneno. Watasema wale waliodhoofishwa kuwaambia wale waliotakabari: Lau isingelikuwa nyinyi, bila shaka tungelikuwa Waumini.

 

 

 

قَالَ الَّذِينَ اسْتَكْبَرُوا لِلَّذِينَ اسْتُضْعِفُوا أَنَحْنُ صَدَدْنَاكُمْ عَنِ الْهُدَىٰ بَعْدَ إِذْ جَاءَكُم ۖ بَلْ كُنتُم مُّجْرِمِينَ ﴿٣٢﴾

32. Na watasema wale waliotakabari kuwaambia wale waliodhoofishwa: Je, kwani sisi ndio tuliokuzuieni na mwongozo baada ya kukujieni? Bali nyinyi mlikuwa wahalifu.

 

 

 

وَقَالَ الَّذِينَ اسْتُضْعِفُوا لِلَّذِينَ اسْتَكْبَرُوا بَلْ مَكْرُ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ إِذْ تَأْمُرُونَنَا أَن نَّكْفُرَ بِاللَّـهِ وَنَجْعَلَ لَهُ أَندَادًا ۚ وَأَسَرُّوا النَّدَامَةَ لَمَّا رَأَوُا الْعَذَابَ وَجَعَلْنَا الْأَغْلَالَ فِي أَعْنَاقِ الَّذِينَ كَفَرُوا ۚ هَلْ يُجْزَوْنَ إِلَّا مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿٣٣﴾

33. Na watasema waliodhoofishwa kuwaambia wale waliotakabari: Bali ni njama (zenu) za usiku na mchana, mlipotuamrisha tumkufuru Allaah na tumfanyie wa kumsawazisha Naye. Na wataficha (au watafichua) majuto watakapoiona adhabu. Na Tutaweka minyororo shingoni mwa wale waliokufuru. Je, wanalipwa isipokuwa yale waliyokuwa wakiyatenda?

 

 

 

وَمَا أَرْسَلْنَا فِي قَرْيَةٍ مِّن نَّذِيرٍ إِلَّا قَالَ مُتْرَفُوهَا إِنَّا بِمَا أُرْسِلْتُم بِهِ كَافِرُونَ ﴿٣٤﴾

34. Na Hatukupeleka katika mji wowote ule mwonyaji yeyote isipokuwa walisema wastareheshwa wake (wa mji) kwa anasa za dunia: Hakika sisi kwa yale mliotumwa nayo ni wenye kuyakanusha.

 

 

 

وَقَالُوا نَحْنُ أَكْثَرُ أَمْوَالًا وَأَوْلَادًا وَمَا نَحْنُ بِمُعَذَّبِينَ ﴿٣٥﴾

35. Na wakasema: Sisi tuna mali nyingi zaidi na watoto, na sisi hatutaadhibiwa.

 

 

 

قُلْ إِنَّ رَبِّي يَبْسُطُ الرِّزْقَ لِمَن يَشَاءُ وَيَقْدِرُ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٣٦﴾

36. Sema: Hakika Rabb wangu Anamkunjulia riziki Amtakaye na Humkadiria kwa kipimo (Amtakaye), lakini watu wengi hawajui.

 

 

 

وَمَا أَمْوَالُكُمْ وَلَا أَوْلَادُكُم بِالَّتِي تُقَرِّبُكُمْ عِندَنَا زُلْفَىٰ إِلَّا مَنْ آمَنَ وَعَمِلَ صَالِحًا فَأُولَـٰئِكَ لَهُمْ جَزَاءُ الضِّعْفِ بِمَا عَمِلُوا وَهُمْ فِي الْغُرُفَاتِ آمِنُونَ ﴿٣٧﴾

37. Na si mali zenu wala watoto wenu ambavyo vitakukurubisheni Kwetu muwe karibu isipokuwa yule aliyeamini na akatenda mema, basi hao watapata malipo maradufu kutokana na yale waliyoyatenda, nao watakuwa katika maghorofa (Jannah) wenye amani.

 

 

 

وَالَّذِينَ يَسْعَوْنَ فِي آيَاتِنَا مُعَاجِزِينَ أُولَـٰئِكَ فِي الْعَذَابِ مُحْضَرُونَ ﴿٣٨﴾

38. Na wale wanaofanya bidii katika Aayaat (na Ishara) Zetu watake kuzibatilisha, hao watahudhurishwa kwenye adhabu.

 

 

 

قُلْ إِنَّ رَبِّي يَبْسُطُ الرِّزْقَ لِمَن يَشَاءُ مِنْ عِبَادِهِ وَيَقْدِرُ لَهُ ۚ وَمَا أَنفَقْتُم مِّن شَيْءٍ فَهُوَ يُخْلِفُهُ ۖ وَهُوَ خَيْرُ الرَّازِقِينَ ﴿٣٩﴾

39. Sema: Hakika Rabb wangu Anamkunjulia riziki Amtakaye kati ya Waja Wake na Humkadiria kwa kipimo (Amtakaye). Na kitu chochote mtoacho, basi Yeye Atakilipa, Naye Ni Mbora wa wenye kuruzuku.

 

 

 

وَيَوْمَ يَحْشُرُهُمْ جَمِيعًا ثُمَّ يَقُولُ لِلْمَلَائِكَةِ أَهَـٰؤُلَاءِ إِيَّاكُمْ كَانُوا يَعْبُدُونَ ﴿٤٠﴾

40. Na Siku Atakayowakusanya wote, kisha Atawaambia Malaika: Je, hawa ndio waliokuwa wakikuabuduni?  

 

 

 

قَالُوا سُبْحَانَكَ أَنتَ وَلِيُّنَا مِن دُونِهِم ۖ بَلْ كَانُوا يَعْبُدُونَ الْجِنَّ ۖ أَكْثَرُهُم بِهِم مُّؤْمِنُونَ ﴿٤١﴾

41. Watasema: Subhaanak! (Utakasifu ni Wako). Wewe Ni Waliyy[10] wetu, sio hao! Bali walikuwa wakiabudu majini, wengi wao wakiwaamini.

 

 

 

فَالْيَوْمَ لَا يَمْلِكُ بَعْضُكُمْ لِبَعْضٍ نَّفْعًا وَلَا ضَرًّا وَنَقُولُ لِلَّذِينَ ظَلَمُوا ذُوقُوا عَذَابَ النَّارِ الَّتِي كُنتُم بِهَا تُكَذِّبُونَ ﴿٤٢﴾

42. Basi leo hawatoweza baadhi yenu kuwapatia wenziwenu manufaa yoyote na wala madhara yoyote, na Tutawaambia wale waliodhulumu: Onjeni adhabu ya moto ambao mlikuwa mkiukadhibisha.

 

 

 

وَإِذَا تُتْلَىٰ عَلَيْهِمْ آيَاتُنَا بَيِّنَاتٍ قَالُوا مَا هَـٰذَا إِلَّا رَجُلٌ يُرِيدُ أَن يَصُدَّكُمْ عَمَّا كَانَ يَعْبُدُ آبَاؤُكُمْ وَقَالُوا مَا هَـٰذَا إِلَّا إِفْكٌ مُّفْتَرًى ۚ وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا لِلْحَقِّ لَمَّا جَاءَهُمْ إِنْ هَـٰذَا إِلَّا سِحْرٌ مُّبِينٌ ﴿٤٣﴾

43. Na wanaposomewa Aayaat Zetu bayana, husema: Huyu (Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) si chochote isipokuwa mtu anataka akuzuieni na yale waliyokuwa wakiyaabudu baba zenu. Na husema: Hii (Qur-aan) si chochote isipokuwa uzushi uliotungwa. Na wale waliokufuru wakasema kuhusu haki ilipowajia: Hii si chochote isipokuwa ni sihiri bayana.[11]

 

 

 

وَمَا آتَيْنَاهُم مِّن كُتُبٍ يَدْرُسُونَهَا ۖ وَمَا أَرْسَلْنَا إِلَيْهِمْ قَبْلَكَ مِن نَّذِيرٍ ﴿٤٤﴾

44. Na wala Hatukuwapa kitabu chochote wakisomacho, na wala Hatukuwapelekea kabla yako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) mwonyaji yeyote.

 

 

 

وَكَذَّبَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ وَمَا بَلَغُوا مِعْشَارَ مَا آتَيْنَاهُمْ فَكَذَّبُوا رُسُلِي ۖ فَكَيْفَ كَانَ نَكِيرِ ﴿٤٥﴾

45. Na walikadhibisha wale wa kabla yao, na (hawa Maquraysh) hawakufikia sehemu moja ya kumi katika yale Tuliyowapa[12] kisha wakakadhibisha Rusuli Wangu. Basi kulikuwa vipi Kukana Kwangu!

 

 

 

قُلْ إِنَّمَا أَعِظُكُم بِوَاحِدَةٍ ۖ أَن تَقُومُوا لِلَّـهِ مَثْنَىٰ وَفُرَادَىٰ ثُمَّ تَتَفَكَّرُوا ۚ مَا بِصَاحِبِكُم مِّن جِنَّةٍ ۚ إِنْ هُوَ إِلَّا نَذِيرٌ لَّكُم بَيْنَ يَدَيْ عَذَابٍ شَدِيدٍ ﴿٤٦﴾

46. Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Hakika nakuwaidhini kwa jambo moja tu!  Msimame kwa ajili ya Allaah wawili wawili, au mmoja mmoja kisha mtafakari. Sahibu yenu si mwendawazimu! Yeye si chochote isipokuwa mwonyaji kwenu, kabla ya kufika adhabu kali.

 

 

 

قُلْ مَا سَأَلْتُكُم مِّنْ أَجْرٍ فَهُوَ لَكُمْ ۖ إِنْ أَجْرِيَ إِلَّا عَلَى اللَّـهِ ۖ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ شَهِيدٌ ﴿٤٧﴾

47. Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Ujira wowote kama nimekuombeni basi huo ni wenu. Sina ujira ila kwa Allaah tu. Naye juu ya kila kitu Ni Shahidi.

 

 

 

قُلْ إِنَّ رَبِّي يَقْذِفُ بِالْحَقِّ عَلَّامُ الْغُيُوبِ ﴿٤٨﴾

48. Sema: Hakika Rabb wangu Anateremsha haki, Ni Mjuzi Mno wa ghaibu. 

 

 

 

قُلْ جَاءَ الْحَقُّ وَمَا يُبْدِئُ الْبَاطِلُ وَمَا يُعِيدُ ﴿٤٩﴾

49. Sema: Haki imekuja, na ubatilifu hausimamishi (tena chochote), na wala haurudishi (kitu).[13]

 

 

 

قُلْ إِن ضَلَلْتُ فَإِنَّمَا أَضِلُّ عَلَىٰ نَفْسِي ۖ وَإِنِ اهْتَدَيْتُ فَبِمَا يُوحِي إِلَيَّ رَبِّي ۚ إِنَّهُ سَمِيعٌ قَرِيبٌ ﴿٥٠﴾

50. Sema: Ikiwa nimepotoka, basi hakika nimepotoka kwa khasara ya nafsi yangu, na ikiwa nimehidika, basi ni kwa yale Aliyonifunulia Wahy Rabb wangu. Hakika Yeye Ni Mwenye Kusikia yote, Yu Karibu.

 

 

 

وَلَوْ تَرَىٰ إِذْ فَزِعُوا فَلَا فَوْتَ وَأُخِذُوا مِن مَّكَانٍ قَرِيبٍ ﴿٥١﴾

51. Na lau ungeliona watakapofazaika kwa khofu, basi hakuna kukwepa, na watachukuliwa kutoka mahali pa karibu.

 

 

 

وَقَالُوا آمَنَّا بِهِ وَأَنَّىٰ لَهُمُ التَّنَاوُشُ مِن مَّكَانٍ بَعِيدٍ ﴿٥٢﴾

52. Na watasema: (Sasa) Tumemwamini Allaah! Lakini wataweza wapi kuipata (imaan) kutoka mahali mbali?

 

 

 

وَقَدْ كَفَرُوا بِهِ مِن قَبْلُ ۖ وَيَقْذِفُونَ بِالْغَيْبِ مِن مَّكَانٍ بَعِيدٍ ﴿٥٣﴾

53. Na kwa yakini walikwishaikanusha kabla, na wanavurumisha ghaibu kwa dhana kutoka mahali mbali.

 

 

 

وَحِيلَ بَيْنَهُمْ وَبَيْنَ مَا يَشْتَهُونَ كَمَا فُعِلَ بِأَشْيَاعِهِم مِّن قَبْلُ ۚ إِنَّهُمْ كَانُوا فِي شَكٍّ مُّرِيبٍ ﴿٥٤﴾

54. Na kizuizi kitawekwa baina yao na baina ya yale wanayoyatamani, kama walivyofanyiwa wenzao kabla. Hakika wao walikuwa katika shaka yenye kutia wasiwasi. 

 

 

 

[1] Hakuna Kinachofichika Kwa Allaah (سبحانه وتعالى), Kiwe Cha Dhahiri Au Cha Siri, Kikubwa Au Kidogo:

 

Rejea Al-An’aam (6:59) kwenye faida na maelezo bayana. Na rejea pia Ghaafir (40:19) kwenye maelezo na rejea mbalimbali. Rejea pia Luqmaan (31:16).

 

[2] Washirikina Na Makafiri Hawakuamini Kufufuliwa:

 

Rejea Al-Israa (17:49).

 

[3] Washirikina Kumpachika Sifa Ovu Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم):

 

Rejea Al-Furqaan (25:4) kwenye maelezo bayana.

 

[4] Fadhila Za Nabiy Daawuwd (عليه السّلام):

 

Yaani: Hakika Tulimneemesha Mja Wetu na Rasuli Wetu Daawuwd (عليه السّلام), na Tukampa fadhila katika ilimu yenye manufaa, na matendo mema, na neema za kidini na za kidunia. Na miongoni mwa Neema Zake (Allaah) juu yake, ni pale Allaah (سبحانه وتعالى) Alipomhusishia Amri Yake kwa viumbe kama vile milima, wanyama, na ndege, kwamba vikariri pamoja nae na viitikie sambamba na anavyoleta yeye tasbiyh na tahmiyd ya Rabbi wao. Na katika hili, neema hii inajipambanua yenyewe kwake, pale lilipokuwa jambo hili ni katika mambo maalumu ambayo hayakuwa kwa yeyote kabla yake wala baada yake, na kwamba hilo linakua ni jambo la kumpa nguvu zaidi yeye na mwenginewe katika kumsabbih (Allaah) pindi wanapoviona hivi viumbe visivyo hai na wanyama, vinaitikia kwa Kumsabbih Rabb wake, na Kumtukuza, na Kumhimidi.  Jambo hilo limekuwa ni miongoni mwa vitu vinavyohamasisha juu ya kumtaja Allaah (سبحانه وتعالى).   

 

Na miongoni mwa yenye kufanikisha neema hizo, ni kwamba hilo (la kuitikiwa na viumbe hivyo) kama walivyosema wengi miongoni mwa ‘Ulamaa, ni kutokana na utamu wa sauti ya Daawuwd, kwani Allaah (سبحانه وتعالى) Alimpa sauti nzuri aliyowazidi kwayo wengine. Na alikuwa anapokariri Tasbiyh (Subhaana-Allaah) na Tahliyl (laa ilaaha illa-Allaah) na Tahmiyd (AlhamduliLlaah) kwa sauti hiyo laini yenye huzuni na yenye kugonga (moyo), humgonga kila anayeisikia, katika watu na majini, hata ndege na milima, na vikamtakasa kwa kumhimidi Rabb wao.

 

Na miongoni mwa neema nyingine ndani ya neema hizo, ni kumfanya apate malipo ya viumbe hivyo vinapomsabbih Allaah kwa kuwa yeye ni sababu ya hilo, na vyenyewe vinasabbih kwa kumfuata yeye.

 

Kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى):

وَأَلَنَّا لَهُ الْحَدِيدَ ﴿١٠﴾

“Na Tukamlainishia chuma”

 

Amesema Hasan Al-Baswriy, Qataadah, Al-A’mash na wengineo: “Alikuwa hahitaji kukiingiza chuma motoni wala kukipiga kwa nyundo, bali alikuwa anakikunja kwa mkono wake mfano wa nyuzi.”  [Tafsiyr Ibn Kathiyr]

 

[5] Shukurani Za Daawuwd (عليه السّلام) :

 

Kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى):

اعْمَلُوا آلَ دَاوُودَ شُكْرًا ۚ وَقَلِيلٌ مِّنْ عِبَادِيَ الشَّكُورُ ﴿١٣﴾

“Tendeni enyi familia ya Daawuwd kwa shukurani! Na wachache miongoni mwa Waja Wangu ni wenye kushukuru.”

 

Shukrani ni kukiri na kutambua moyoni Neema za Allaah (سبحانه وتعالى), kuzipokea hali ya kuwa mtu anazihitajia, kuzitumia katika utii wa Allaah (سبحانه وتعالى), na kuzihifadhi zisitumike katika maasi. [Tafsiyr As-Sa’diy]

 

Na katika kushukuru Neema za Allaah (سبحانه وتعالى), ni kutekeleza ibaada kwa wingi kutokana na uwezo, nguvu, na wasaa aliojaaliwa mtu na Allaah (سبحانه وتعالى). Na mfano wa shukurani za Nabiy Daawuwd (عليه السّلام), ni baadhi ya ibaada zake ambazo zinapendwa zaidi na Allaah (سبحانه وتعالى). Hadiyth ifuatayo inataja ibaada hizo:

 

حَدَّثَنَا قُتَيْبَةُ بْنُ سَعِيدٍ، حَدَّثَنَا سُفْيَانُ، عَنْ عَمْرِو بْنِ دِينَارٍ، عَنْ عَمْرِو بْنِ أَوْسٍ الثَّقَفِيِّ، سَمِعَ عَبْدَ اللَّهِ بْنَ عَمْرٍو، قَالَ قَالَ لِي رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم ‏ "‏ أَحَبُّ الصِّيَامِ إِلَى اللَّهِ صِيَامُ دَاوُدَ، كَانَ يَصُومُ يَوْمًا وَيُفْطِرُ يَوْمًا، وَأَحَبُّ الصَّلاَةِ إِلَى اللَّهِ صَلاَةُ دَاوُدَ، كَانَ يَنَامُ نِصْفَ اللَّيْلِ وَيَقُومُ ثُلُثَهُ وَيَنَامُ سُدُسَهُ ‏"‏‏.‏

 

Amesimulia ‘Abdullaah bin ‘Amruw bin al-‘Aasw (رضي الله عنهما): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Swawm inayopendwa zaidi na Allaah ni Swawm ya Daawuwd; alikuwa akifunga siku moja na akiacha siku moja. Na Swalaah inayopendwa zaidi na Allaah ni Swalaah ya Daawuwd. Alikuwa akilala nusu ya usiku, akiswali thuluthi yake na kulala sudusi (1/6) yake.” [Al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuwd, An-Nasaaiy na Ibn Maajah]

 

[6] Saba-a Na Watu Wake Waliokufuru Neema Za Allaah (سبحانه وتعالى):

 

Kuanzia Aayah hii namba (12) hadi namba (21), zinahusiana na kisa cha Saba-a na watu wake waliokufuru Neema za Allaah (سبحانه وتعالى) :

 

Saba-a ni miongoni mwa wafalme wa Yemen na watu wake. Na Balqiys (au Bilqiys) aliyekwenda kwa Nabiy Sulaymaan (عليه السّلام) na kusilimu, alikuwa ni miongoni mwao. Watu wa Saba-a walikuwa katika neema na hali nzuri katika miji yao na maisha yao, mazao mengi, mashamba makubwa na matunda kwa wingi. Hali kadhaalika walijaaliwa barabara za kuwasahilisha safari baina ya nchi; barabara zenye vituo vya safari, zenye amani na usalama. Allaah (سبحانه وتعالى) Akawapelekea Rusuli wakiwaamrisha wale katika riziki Zake, na wamshukuru kwa kumpwekesha (kwenye ibaada) na kumuabudu Yeye. Basi wakawa katika hali hiyo kadri Alivyopenda Allaah (سبحانه وتعالى). Kisha wakapuuza yale waliyoamrishwa, wakaadhibiwa kwa kupelekewa mafuriko na uhaba wa chakula, na kutawanyika katika miji. Rejea Aayah namba (19)

 

Na Hadiyth ifuatayo imeelezea kuhusu Saba-a:

 

 عن فروة بن مسيك المرادي قال: أتيت النبي ﷺ فذكر في الحديث، فقال رجل: يا رسول الله وما سبأ أرض أو امرأة؟ قالليس بأرض ولا امرأة ولكنه رجل ولد عشرة من العرب، فتيامن منهم ستة سكنوا في اليمن، وتشاءم منهم أربعة يعني سكنوا في الشام، فأما الذين تشاءموا في الشام: فلخم، وجذام، وغسان، وعاملة، وأما الذين تيامنوا: فالأزد، والأشعريون، وحمير، وكندة، ومذحج، وأنمار  رواه الترمذي: 3222، وصححه الألباني صحيح الترمذي:2574 .

 

Amesimulia Farwah Bin Musayk Al-Muraadiy: Nilimuendea Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akataja katika mazungumzo (Saba-a), akasema mtu mmoja: Ee Rasuli wa Allaah!  Ni nini Saba-a? Je ni ardhi au ni mwanamke? Akasema: “Si ardhi wala mwanamke lakini ni mtu ambaye alizaa makabila kumi ya Waarabu. Basi sita miongoni mwao, wakaishi Yemen, na wanne wakaishi Sham. Ama wale walioishi Sham, hao (ni makabila ya) Lakhmu, Judhaam, Ghassaan, na ‘Aamilah. Ama wale ambao waliishi Yemen, (hao ni) Uzdu, Humayr, Kindah, Madh-hij na Anmaar.”  [At-Tirmidhiy na ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh At-Tirmidhiy (2574)]

 

[7] Makundi Mawili Ya Haki Na Upotofu:

 

Haiwezekani watu wote wakawa katika haki au wakawa wote katika upotofu. Lazima wagawike. Kundi la kwanza ni wale walionyooka katika njia ya haki, wakafuata maamrisho ya Allaah (سبحانه وتعالى) na wakafuata na kutekeleza mafunzo sahihi aliyokuja nayo Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) na Salaf Swaalih (Wema waliotangulia). Na kwa kuwajibika na hayo, wakajiepusha na shirki, kufru, bid’ah, unafiki, maasi na kadhalika. Na kundi la pili ni wale waliopotoka wasifuate Amri za Allaah (سبحانه وتعالى) na wakatoka nje ya mafunzo ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم), wakaacha kufuata yaliyo sahihi na wakafuata wapotofu, wakafarikiana humo vikundi kwa vikundi na wakazusha mambo katika Dini.   Makundi haya mawili hayawezi kuwa sawa, lazima moja liwe liko juu ya uongofu, na la pili liwe juu ya upotofu.

 

[8] Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) Ametumwa Kwa Walimwengu Wote; Majini Na Wanaadam:

 

Aayah hii ni dalili mojawapo kuwa Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) Ametumwa kwa walimwengu wote na si kwa Waislamu pekee kwa kuwa Allaah (سبحانه وتعالى) Anaielekeza Kauli Yake kwa watu wote Anaposema:

وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا كَافَّةً لِّلنَّاسِ

 Hatukukutuma (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) isipokuwa kwa watu wote.”  

Na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)  amesema:

وَكَانَ النَّبِيُّ يُبْعَثُ إِلَى قَوْمِهِ خَاصَّةً، وَبُعِثْتُ إِلَى النَّاسِ عَامَّةً

“Na Nabiy alikuwa  akitumwa kwa watu wake pekee, lakini mimi nimetumwa kwa watu wote.” [Hadiyth ya Jaabir bin ‘Abdillaah (رضي الله عنه) - Al-Bukhaariy (5011)]

Na pia amesema (صلى الله عليه وآله وسلم):

وَبُعِثْتُ إِلَى كُلِّ أَحْمَر وَأَسْوَد

“Na nimetumwa kwa (wanaadam) wekundu wote na weusi.” [Muslim] Rejea Al-A’raaf (7:158), Al-Furqaan (25:1).

 

[9] Ada Ya Makafiri Kuuliza Lini Qiyaamah Kitatokea Au Adhabu Kuwafikia:

 

Rejea Yuwnus (10:48).

 

[10] Waliyy: Mlinzi, Rafiki Mwandani, Msaidizi, Msimamizi, Mfadhili:

 

Rejea Faharasa Ya Majina Mazuri Ya Allaah Na Sifa Zake. 

 

[11] Washirikina Kuikanusha Qur-aan Na Kuifanyia Istihzai Na Kuisingizia Kila Aina Ya Sifa Ovu:

 

Rejea Al-Furqaan (25:4) kwenye maelezo bayana.

 

[12] Waliyopewa Makafiri:

 

Neema za umri mrefu, mali nyingi, nguvu na neema nyenginezo. Imesemwa pia waliyopewa ni ilimu, dalili za wazi, hoja na kadhaalika.

 

[13] Haki Itaondoka Na Ubatili Utatoweka:

 

حَدَّثَنَا صَدَقَةُ بْنُ الْفَضْلِ، أَخْبَرَنَا ابْنُ عُيَيْنَةَ، عَنِ ابْنِ أَبِي نَجِيحٍ، عَنْ مُجَاهِدٍ، عَنْ أَبِي مَعْمَرٍ، عَنْ عَبْدِ اللَّهِ ـ رضى الله عنه ـ قَالَ دَخَلَ النَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم مَكَّةَ يَوْمَ الْفَتْحِ وَحَوْلَ الْبَيْتِ سِتُّونَ وَثَلاَثُمِائَةِ نُصُبٍ، فَجَعَلَ يَطْعُنُهَا بِعُودٍ فِي يَدِهِ وَيَقُولُ ‏ "جَاءَ الْحَقُّ وَزَهَقَ الْبَاطِلُ، جَاءَ الْحَقُّ، وَمَا يُبْدِئُ الْبَاطِلُ وَمَا يُعِيدُ"‏‏.‏

 

Amesimulia ‘Abdullaah (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alipoingia Makkah katika Siku ya Fat-h Makkah (ukombozi wa Makkah) palikuweko masanamu mia tatu na sitini yamezungushwa katika Al-Ka’bah. Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akaanza kuyapiga kwa fimbo aliyokuwa ameshika mkononi, huku akisema:

 

جَاءَ الْحَقُّ وَمَا يُبْدِئُ الْبَاطِلُ وَمَا يُعِيدُ ﴿٤٩﴾

“Haki imekuja, na ubatilifu hausimamishi (tena chochote), na wala haurudishi (kitu).” [Saba-a (34:49)]

 

[Al-Bukhaariy, Muslim na wengineo]

 

Rejea pia Al-Israa (17:81).

 

Share