039 - Az-Zumar

 

 

 

   الزُّمَر

Az-Zumar: 039

 

 

 

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

 

تَنزِيلُ الْكِتَابِ مِنَ اللَّـهِ الْعَزِيزِ الْحَكِيمِ ﴿١﴾

1. Ni uteremsho wa Kitabu hiki kutoka kwa Allaah Mwenye Enzi na Nguvu Asiyeshindika, Mwenye hikmah wa yote.

 

 

 

إِنَّا أَنزَلْنَا إِلَيْكَ الْكِتَابَ بِالْحَقِّ فَاعْبُدِ اللَّـهَ مُخْلِصًا لَّهُ الدِّينَ ﴿٢﴾

2. Hakika Sisi Tumekuteremshia Kitabu hiki kwa haki, basi mwabudu Allaah kwa kumtakasia Dini Yeye.

 

 

 

 

أَلَا لِلَّـهِ الدِّينُ الْخَالِصُ ۚ وَالَّذِينَ اتَّخَذُوا مِن دُونِهِ أَوْلِيَاءَ مَا نَعْبُدُهُمْ إِلَّا لِيُقَرِّبُونَا إِلَى اللَّـهِ زُلْفَىٰ إِنَّ اللَّـهَ يَحْكُمُ بَيْنَهُمْ فِي مَا هُمْ فِيهِ يَخْتَلِفُونَ ۗ إِنَّ اللَّـهَ لَا يَهْدِي مَنْ هُوَ كَاذِبٌ كَفَّارٌ ﴿٣﴾

3. Tanabahi! Ni ya Allaah Pekee Dini iliyotakasika. Na wale waliojichukulia badala Yake walinzi (wakisema): Hatuwaabudu isipokuwa ili wapate kutukurubisha karibu kabisa kwa Allaah. Hakika Allaah Atahukumu baina yao katika yale wanayokhitilafiana nayo. Hakika Allaah Hamhidi aliye mkadhibishaji, kafiri mkubwa.

 

 

 

لَّوْ أَرَادَ اللَّـهُ أَن يَتَّخِذَ وَلَدًا لَّاصْطَفَىٰ مِمَّا يَخْلُقُ مَا يَشَاءُ ۚ سُبْحَانَهُ ۖ هُوَ اللَّـهُ الْوَاحِدُ الْقَهَّارُ ﴿٤﴾

4. Lau Angelitaka Allaah kujichukulia mwana, Angelikhitari Amtakaye miongoni mwa Aliowaumba. Subhaanah! (Utakasifu ni Wake), Yeye Ndiye Allaah Mmoja Pekee, Asiyepingika.

 

 

خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ بِالْحَقِّ ۖ يُكَوِّرُ اللَّيْلَ عَلَى النَّهَارِ وَيُكَوِّرُ النَّهَارَ عَلَى اللَّيْلِ ۖ وَسَخَّرَ الشَّمْسَ وَالْقَمَرَ ۖ كُلٌّ يَجْرِي لِأَجَلٍ مُّسَمًّى ۗ أَلَا هُوَ الْعَزِيزُ الْغَفَّارُ ﴿٥﴾

5. Ameumba mbingu na ardhi kwa haki. Anaufunika usiku juu ya mchana, na Anafunika mchana juu ya usiku. Na Ametiisha jua na mwezi; kila kimoja kinakwenda mpaka muda maalumu uliokadiriwa. Tanabahi! Yeye Ndiye Mwenye Enzi na Nguvu Asiyeshindika, Mwingi wa Kughufuria.

 

 

 

خَلَقَكُم مِّن نَّفْسٍ وَاحِدَةٍ ثُمَّ جَعَلَ مِنْهَا زَوْجَهَا وَأَنزَلَ لَكُم مِّنَ الْأَنْعَامِ ثَمَانِيَةَ أَزْوَاجٍ ۚ يَخْلُقُكُمْ فِي بُطُونِ أُمَّهَاتِكُمْ خَلْقًا مِّن بَعْدِ خَلْقٍ فِي ظُلُمَاتٍ ثَلَاثٍ ۚ ذَٰلِكُمُ اللَّـهُ رَبُّكُمْ لَهُ الْمُلْكُ ۖ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۖ فَأَنَّىٰ تُصْرَفُونَ ﴿٦﴾

6. Amekuumbeni kutokana na nafsi moja, kisha Akamfanya kutokana nayo mkewe, na Akakuteremshieni katika wanyama wa mifugo jozi nane. Anakuumbeni matumboni mwa mama zenu umbo baada ya umbo, katika viza vitatu. Huyo Ndiye Allaah Rabb wenu Mwenye Ufalme, hakuna Muabudiwa wa haki ila Yeye. Basi vipi mnageuzwa?

 

 

 

إِن تَكْفُرُوا فَإِنَّ اللَّـهَ غَنِيٌّ عَنكُمْ ۖ وَلَا يَرْضَىٰ لِعِبَادِهِ الْكُفْرَ ۖ وَإِن تَشْكُرُوا يَرْضَهُ لَكُمْ ۗ وَلَا تَزِرُ وَازِرَةٌ وِزْرَ أُخْرَىٰ ۗ ثُمَّ إِلَىٰ رَبِّكُم مَّرْجِعُكُمْ فَيُنَبِّئُكُم بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ ۚ إِنَّهُ عَلِيمٌ بِذَاتِ الصُّدُورِ ﴿٧﴾

7. Mkikufuru, basi hakika Allaah Ni Mkwasi kwenu (Hawahitajieni kwa lolote), na wala Haridhii kufuru kwa Waja Wake. Na mkishukuru, basi Huridhika nanyi. Na wala mbebaji mzigo (wa dhambi) hatobeba mzigo wa mwengine. Kisha kwa Rabbi wenu ndio marejeo yenu, Atakujulisheni yale mliyokuwa mkiyatenda. Hakika Yeye Ni Mjuzi wa yaliyomo vifuani.

 

 

وَإِذَا مَسَّ الْإِنسَانَ ضُرٌّ دَعَا رَبَّهُ مُنِيبًا إِلَيْهِ ثُمَّ إِذَا خَوَّلَهُ نِعْمَةً مِّنْهُ نَسِيَ مَا كَانَ يَدْعُو إِلَيْهِ مِن قَبْلُ وَجَعَلَ لِلَّـهِ أَندَادًا لِّيُضِلَّ عَن سَبِيلِهِ ۚ قُلْ تَمَتَّعْ بِكُفْرِكَ قَلِيلًا ۖ إِنَّكَ مِنْ أَصْحَابِ النَّارِ ﴿٨﴾

8. Na inapomgusa binaadamu dhara, humwomba Rabb wake huku akijisogeza Kwake, kisha Akimruzuku Neema kutoka Kwake, husahau yale aliyokuwa akimwomba kabla, na kumfanyia Allaah wanaolingana Naye, ili apotoshe (watu) kutoka Njia Yake. Sema: Starehe kwa kufuru yako kidogo tu, hakika wewe ni miongoni mwa watu wa motoni.  

 

 

 

أَمَّنْ هُوَ قَانِتٌ آنَاءَ اللَّيْلِ سَاجِدًا وَقَائِمًا يَحْذَرُ الْآخِرَةَ وَيَرْجُو رَحْمَةَ رَبِّهِ ۗ قُلْ هَلْ يَسْتَوِي الَّذِينَ يَعْلَمُونَ وَالَّذِينَ لَا يَعْلَمُونَ ۗ إِنَّمَا يَتَذَكَّرُ أُولُو الْأَلْبَابِ ﴿٩﴾

9. Je, yule anayeshikamana na ‘ibaadah nyakati za usiku akisujudu na kusimama (kuswali), ilhali anatahadhari na Aakhirah, na anataraji Rahmah ya Rabb wake (ni sawa na aliye kinyume chake?). Sema: Je, wanalingana sawa wale wanaojua na wale wasiojua? Hakika wanakumbuka wenye akili tu.

 

 

 

قُلْ يَا عِبَادِ الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا رَبَّكُمْ ۚ لِلَّذِينَ أَحْسَنُوا فِي هَـٰذِهِ الدُّنْيَا حَسَنَةٌ ۗ وَأَرْضُ اللَّـهِ وَاسِعَةٌ ۗ إِنَّمَا يُوَفَّى الصَّابِرُونَ أَجْرَهُم بِغَيْرِ حِسَابٍ ﴿١٠﴾

10. Sema: Enyi Waja Wangu ambao mmeamini, mcheni Rabb wenu. Kwa wale waliofanya mazuri katika dunia hii watapata mazuri. Na Ardhi ya Allaah ni pana. Hakika wanaosubiri watalipwa kikamilifu ujira wao bila ya hesabu.

 

 

قُلْ إِنِّي أُمِرْتُ أَنْ أَعْبُدَ اللَّـهَ مُخْلِصًا لَّهُ الدِّينَ ﴿١١﴾

11. Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Hakika mimi nimeamrishwa nimwabudu Allaah nikiwa mwenye kumtakasia Dini Yeye.

 

 

وَأُمِرْتُ لِأَنْ أَكُونَ أَوَّلَ الْمُسْلِمِينَ ﴿١٢﴾

12. Na nimeamrishwa kuwa niwe wa kwanza wa Waislamu. 

 

 

 

قُلْ إِنِّي أَخَافُ إِنْ عَصَيْتُ رَبِّي عَذَابَ يَوْمٍ عَظِيمٍ ﴿١٣﴾

13. Sema: Hakika nikimuasi Rabb wangu, nina khofu adhabu ya Siku iliyo kuu kabisa.

 

 

قُلِ اللَّـهَ أَعْبُدُ مُخْلِصًا لَّهُ دِينِي ﴿١٤﴾

14. Sema: Allaah Pekee namwabudu nikimtakasia Yeye tu Dini yangu. 

 

 

 

فَاعْبُدُوا مَا شِئْتُم مِّن دُونِهِ ۗ قُلْ إِنَّ الْخَاسِرِينَ الَّذِينَ خَسِرُوا أَنفُسَهُمْ وَأَهْلِيهِمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۗ أَلَا ذَٰلِكَ هُوَ الْخُسْرَانُ الْمُبِينُ ﴿١٥﴾

15. Basi abuduni mnayotaka badala Yake. Sema: Hakika waliokhasirika ni wale waliokhasiri nafsi zao na ahli zao Siku ya Qiyaamah. Tanabahi!  Hiyo ndio khasara bayana.

 

 

 

لَهُم مِّن فَوْقِهِمْ ظُلَلٌ مِّنَ النَّارِ وَمِن تَحْتِهِمْ ظُلَلٌ ۚ ذَٰلِكَ يُخَوِّفُ اللَّـهُ بِهِ عِبَادَهُ ۚ يَا عِبَادِ فَاتَّقُونِ ﴿١٦﴾

16. Watawekewa kutoka juu yao matabaka ya moto, na chini yao matabaka. Kwa hayo, Allaah Anakhofisha Waja Wake. Enyi Waja Wangu! Basi Nikhofuni.

 

 

 

وَالَّذِينَ اجْتَنَبُوا الطَّاغُوتَ أَن يَعْبُدُوهَا وَأَنَابُوا إِلَى اللَّـهِ لَهُمُ الْبُشْرَىٰ ۚ فَبَشِّرْ عِبَادِ ﴿١٧﴾

17. Na wale waliojiepusha na kuabudu twaghuti na wakarejea kwa Allaah, watapata bishara njema. Basi wabashirie Waja Wangu.

 

 

 

الَّذِينَ يَسْتَمِعُونَ الْقَوْلَ فَيَتَّبِعُونَ أَحْسَنَهُ ۚ أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ هَدَاهُمُ اللَّـهُ ۖ وَأُولَـٰئِكَ هُمْ أُولُو الْأَلْبَابِ ﴿١٨﴾

18. Wale wanaosikiliza kwa makini maneno, wakafuata yaliyo mazuri yake zaidi, hao ndio wale Aliowahidi Allaah, na hao ndio wenye akili.

 

 

 

أَفَمَنْ حَقَّ عَلَيْهِ كَلِمَةُ الْعَذَابِ أَفَأَنتَ تُنقِذُ مَن فِي النَّارِ ﴿١٩﴾

19. Je, yule liliyemthibitikia neno la adhabu, je, basi wewe utaweza kumuokoa aliyemo katika moto?

 

 

 

لَـٰكِنِ الَّذِينَ اتَّقَوْا رَبَّهُمْ لَهُمْ غُرَفٌ مِّن فَوْقِهَا غُرَفٌ مَّبْنِيَّةٌ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ ۖ وَعْدَ اللَّـهِ ۖ لَا يُخْلِفُ اللَّـهُ الْمِيعَادَ ﴿٢٠﴾

20. Lakini wale waliomcha Rabb wao, watapata maghorofa yaliyojengwa juu yake maghorofa, yanapita chini yake mito.  Ni Ahadi ya Allaah. Allaah Hakhalifu miadi.

 

 

 

أَلَمْ تَرَ أَنَّ اللَّـهَ أَنزَلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَسَلَكَهُ يَنَابِيعَ فِي الْأَرْضِ ثُمَّ يُخْرِجُ بِهِ زَرْعًا مُّخْتَلِفًا أَلْوَانُهُ ثُمَّ يَهِيجُ فَتَرَاهُ مُصْفَرًّا ثُمَّ يَجْعَلُهُ حُطَامًا ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَذِكْرَىٰ لِأُولِي الْأَلْبَابِ ﴿٢١﴾

21. Je, huoni kwamba Allaah Anateremsha kutoka mbinguni maji, Akayapitisha chemchemu katika ardhi, kisha Anatoa kwayo mimea ya rangi mbalimbali, kisha hunyauka, basi utayaona ni manjano, kisha Huyafanya mabua yaliyonyauka na kupondekapondeka?  Hakika katika hayo bila shaka kuna ukumbusho kwa wenye akili.

 

 

 

أَفَمَن شَرَحَ اللَّـهُ صَدْرَهُ لِلْإِسْلَامِ فَهُوَ عَلَىٰ نُورٍ مِّن رَّبِّهِ ۚ فَوَيْلٌ لِّلْقَاسِيَةِ قُلُوبُهُم مِّن ذِكْرِ اللَّـهِ ۚ أُولَـٰئِكَ فِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ ﴿٢٢﴾

22. Je, ambaye Allaah Amemkunjulia kifua chake kwa Uislamu naye yuko juu ya Nuru kutoka kwa Rabb wake (ni sawa na aliyekinyume chake?). Basi ole wao wenye nyoyo zinazo susuwaa kwa sababu ya kutajwa Allaah. Hao wamo katika upotofu bayana.

 

 

 

اللَّـهُ نَزَّلَ أَحْسَنَ الْحَدِيثِ كِتَابًا مُّتَشَابِهًا مَّثَانِيَ تَقْشَعِرُّ مِنْهُ جُلُودُ الَّذِينَ يَخْشَوْنَ رَبَّهُمْ ثُمَّ تَلِينُ جُلُودُهُمْ وَقُلُوبُهُمْ إِلَىٰ ذِكْرِ اللَّـهِ ۚ ذَٰلِكَ هُدَى اللَّـهِ يَهْدِي بِهِ مَن يَشَاءُ ۚ وَمَن يُضْلِلِ اللَّـهُ فَمَا لَهُ مِنْ هَادٍ ﴿٢٣﴾

23. Allaah Ameteremsha habari nzuri kabisa. Ni Kitabu ambacho ibara zake zinashabihiana, zinazokaririwa kila mara. Zinasisimuka kwazo ngozi za wale wanaomkhofu Rabb wao, kisha zinalainika ngozi zao na nyoyo zao kwa kudhukuriwa Allaah. Huo ndio Mwongozo wa Allaah, Humhidi kwao Amtakaye. Na ambaye Allaah Amempotoa basi hana wa kumuongoa.

 

 

 

أَفَمَن يَتَّقِي بِوَجْهِهِ سُوءَ الْعَذَابِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۚ وَقِيلَ لِلظَّالِمِينَ ذُوقُوا مَا كُنتُمْ تَكْسِبُونَ ﴿٢٤﴾

24. Je, yule anayekinga kwa uso wake adhabu mbaya Siku ya Qiyaamah (ni sawa na atayesalimika nao?). Na madhalimu wataambiwa: Onjeni yale mliyokuwa mkiyachuma.

 

 

 

كَذَّبَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ فَأَتَاهُمُ الْعَذَابُ مِنْ حَيْثُ لَا يَشْعُرُونَ ﴿٢٥﴾

25. Wamekadhibisha wale wa kabla yao, basi ikawajia adhabu kutoka mahali wasipotambua.

 

 

 

 

فَأَذَاقَهُمُ اللَّـهُ الْخِزْيَ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ۖ وَلَعَذَابُ الْآخِرَةِ أَكْبَرُ ۚ لَوْ كَانُوا يَعْلَمُونَ ﴿٢٦﴾

26. Allaah Akawaonjesha hizaya katika uhai wa dunia. Na bila shaka adhabu ya Aakhirah ni kubwa zaidi, lau kama wangelikuwa wanajua.

 

 

 

وَلَقَدْ ضَرَبْنَا لِلنَّاسِ فِي هَـٰذَا الْقُرْآنِ مِن كُلِّ مَثَلٍ لَّعَلَّهُمْ يَتَذَكَّرُونَ ﴿٢٧﴾

27. Na kwa yakini Tumewapigia watu mifano ya kila aina katika hii Qur-aan ili wapate kukumbuka.

 

 

 

قُرْآنًا عَرَبِيًّا غَيْرَ ذِي عِوَجٍ لَّعَلَّهُمْ يَتَّقُونَ ﴿٢٨﴾

28. Qur-aan ya Kiarabu isiyo na kombo ili wapate kuwa na taqwa.

 

 

 

ضَرَبَ اللَّـهُ مَثَلًا رَّجُلًا فِيهِ شُرَكَاءُ مُتَشَاكِسُونَ وَرَجُلًا سَلَمًا لِّرَجُلٍ هَلْ يَسْتَوِيَانِ مَثَلًا ۚ الْحَمْدُ لِلَّـهِ ۚ بَلْ أَكْثَرُهُمْ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٢٩﴾

29. Allaah Amepiga mfano wa mtu aliye chini ya washirika wagombanao, na mtu mwengine aliye pweke na bwana mmoja tu. Je, wanalingana sawa kwa hali zao? AlhamduliLLaah (Himidi Anastahiki Allaah). Bali wengi wao hawajui.

 

 

إِنَّكَ مَيِّتٌ وَإِنَّهُم مَّيِّتُونَ ﴿٣٠﴾

30. Hakika wewe (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) utakufa nao pia watakufa.

 

 

 

ثُمَّ إِنَّكُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ عِندَ رَبِّكُمْ تَخْتَصِمُونَ ﴿٣١﴾

31. Kisha hakika nyinyi Siku ya Qiyaamah mtazozana mbele ya Rabb wenu.

 

 

 

فَمَنْ أَظْلَمُ مِمَّن كَذَبَ عَلَى اللَّـهِ وَكَذَّبَ بِالصِّدْقِ إِذْ جَاءَهُ ۚ أَلَيْسَ فِي جَهَنَّمَ مَثْوًى لِّلْكَافِرِينَ﴿٣٢﴾

32. Basi ni nani dhalimu zaidi kuliko yule aliyemsingizia uongo Allaah, na akaukadhibisha ukweli ulipomjia? Je, kwani sio katika Jahannam makazi kwa ajili ya makafiri?

 

 

 

وَالَّذِي جَاءَ بِالصِّدْقِ وَصَدَّقَ بِهِ ۙ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُتَّقُونَ﴿٣٣﴾

33. Na yule aliyekuja na ukweli na akausadikisha, hao ndio wenye taqwa.

 

 

 

لَهُم مَّا يَشَاءُونَ عِندَ رَبِّهِمْ ۚ ذَٰلِكَ جَزَاءُ الْمُحْسِنِينَ﴿٣٤﴾

34. Watapata yale wayatakayo kwa Rabb wao. Hiyo ndio jazaa ya wafanyao ihsaan.

 

 

 

لِيُكَفِّرَ اللَّـهُ عَنْهُمْ أَسْوَأَ الَّذِي عَمِلُوا وَيَجْزِيَهُمْ أَجْرَهُم بِأَحْسَنِ الَّذِي كَانُوا يَعْمَلُونَ﴿٣٥﴾

35. Ili Allaah Awafutie ukomo wa uovu walioutenda, na Awalipe ujira wao kwa ukomo wa ihsaan ambao walikuwa wakitenda.

 

 

 

أَلَيْسَ اللَّـهُ بِكَافٍ عَبْدَهُ ۖ وَيُخَوِّفُونَكَ بِالَّذِينَ مِن دُونِهِ ۚ وَمَن يُضْلِلِ اللَّـهُ فَمَا لَهُ مِنْ هَادٍ﴿٣٦﴾

36. Je, kwani Allaah Si Mwenye Kumtosheleza Mja Wake? Na eti wanakutisha na wale wasiokuwa Yeye. Na ambaye Allaah Amempotoa basi hana wa kumhidi.

 

 

وَمَن يَهْدِ اللَّـهُ فَمَا لَهُ مِن مُّضِلٍّ ۗ أَلَيْسَ اللَّـهُ بِعَزِيزٍ ذِي انتِقَامٍ﴿٣٧﴾

37. Na ambaye Allaah Amemhidi, basi hapana wa kumpotoa. Je, kwani Allaah Si Mwenye Enzi na Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Kulipiza?

 

 

 

وَلَئِن سَأَلْتَهُم مَّنْ خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ لَيَقُولُنَّ اللَّـهُ ۚ قُلْ أَفَرَأَيْتُم مَّا تَدْعُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ إِنْ أَرَادَنِيَ اللَّـهُ بِضُرٍّ هَلْ هُنَّ كَاشِفَاتُ ضُرِّهِ أَوْ أَرَادَنِي بِرَحْمَةٍ هَلْ هُنَّ مُمْسِكَاتُ رَحْمَتِهِ ۚ قُلْ حَسْبِيَ اللَّـهُ ۖ عَلَيْهِ يَتَوَكَّلُ الْمُتَوَكِّلُونَ﴿٣٨﴾

38. Na ukiwauliza: Ni nani aliyeumba mbingu na ardhi? Bila shaka watasema: Allaah. Sema: Je, mnaonaje wale mnaowaomba badala ya Allaah, ikiwa Allaah Atanikusudia dhara, je, wao wataweza kuondosha Dhara Yake? Au Akinikusudia Rahmah je, wao wataweza kuizuia Rahmah Yake? Sema: Ananitosheleza Allaah, Kwake watawakali wenye kutawakali.

 

 

قُلْ يَا قَوْمِ اعْمَلُوا عَلَىٰ مَكَانَتِكُمْ إِنِّي عَامِلٌ ۖ فَسَوْفَ تَعْلَمُونَ﴿٣٩﴾

39. Sema: Enyi watu wangu! Tendeni kwa namna zenu, hakika nami natenda. Basi karibuni mtakuja kujua.

 

 

مَن يَأْتِيهِ عَذَابٌ يُخْزِيهِ وَيَحِلُّ عَلَيْهِ عَذَابٌ مُّقِيمٌ﴿٤٠﴾

40. Ni nani itakayemfikia adhabu itakayomhizi, na itamshukia adhabu ya kudumu.

 

 

 

إِنَّا أَنزَلْنَا عَلَيْكَ الْكِتَابَ لِلنَّاسِ بِالْحَقِّ ۖ فَمَنِ اهْتَدَىٰ فَلِنَفْسِهِ ۖ وَمَن ضَلَّ فَإِنَّمَا يَضِلُّ عَلَيْهَا ۖ وَمَا أَنتَ عَلَيْهِم بِوَكِيلٍ﴿٤١﴾

41. Hakika Sisi Tumekuteremshia Kitabu kwa ajili ya watu kwa haki. Basi atakayehidika, ni kwa ajili ya nafsi yake. Na atakayepotoka, basi hakika anapotoka dhidi yake, na wewe si mdhamini wao.

 

 

 

اللَّـهُ يَتَوَفَّى الْأَنفُسَ حِينَ مَوْتِهَا وَالَّتِي لَمْ تَمُتْ فِي مَنَامِهَا ۖ فَيُمْسِكُ الَّتِي قَضَىٰ عَلَيْهَا الْمَوْتَ وَيُرْسِلُ الْأُخْرَىٰ إِلَىٰ أَجَلٍ مُّسَمًّى ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ﴿٤٢﴾

42. Allaah Huzichukua roho wakati wa kufa kwake, na zile zisizokufa katika usingizi wake, kisha Huzizuia ambazo Amezikidhia mauti, na Huzirudisha nyingine mpaka muda maalumu uliokadiriwa. Hakika katika hayo bila shaka kuna ishara kwa watu wanaotafakari.

 

 

أَمِ اتَّخَذُوا مِن دُونِ اللَّـهِ شُفَعَاءَ ۚ قُلْ أَوَلَوْ كَانُوا لَا يَمْلِكُونَ شَيْئًا وَلَا يَعْقِلُونَ﴿٤٣﴾

43. Je, wamejichukulia badala ya Allaah waombezi?  Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Je, japokuwa hawana uwezo wa kumiliki chochote na wala hawana akili?

 

 

قُل لِّلَّـهِ الشَّفَاعَةُ جَمِيعًا ۖ لَّهُ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۖ ثُمَّ إِلَيْهِ تُرْجَعُونَ﴿٤٤﴾

44. Sema: Uombezi wote ni wa Allaah Pekee. Ana Ufalme wa mbingu na ardhi, kisha Kwake mtarejeshwa.

 

 

وَإِذَا ذُكِرَ اللَّـهُ وَحْدَهُ اشْمَأَزَّتْ قُلُوبُ الَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِالْآخِرَةِ ۖ وَإِذَا ذُكِرَ الَّذِينَ مِن دُونِهِ إِذَا هُمْ يَسْتَبْشِرُونَ﴿٤٥﴾

45.  Na anapotajwa Allaah Pekee, nyoyo za wale wasioamini Aakhirah hunyweya kwa ghadhabu na kukengeuka, na wanapotajwa wengineo pasi Naye, tahamaki wanafurahia.

 

 

قُلِ اللَّـهُمَّ فَاطِرَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ عَالِمَ الْغَيْبِ وَالشَّهَادَةِ أَنتَ تَحْكُمُ بَيْنَ عِبَادِكَ فِي مَا كَانُوا فِيهِ يَخْتَلِفُونَ﴿٤٦﴾

46. Sema: Ee Allaah! Muanzilishi wa mbingu na ardhi, Mjuzi wa ghaibu na dhahiri, Wewe Utahukumu baina ya Waja Wako katika yale ambayo walikuwa wakikhitilafiana.

 

 

 

وَلَوْ أَنَّ لِلَّذِينَ ظَلَمُوا مَا فِي الْأَرْضِ جَمِيعًا وَمِثْلَهُ مَعَهُ لَافْتَدَوْا بِهِ مِن سُوءِ الْعَذَابِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۚ وَبَدَا لَهُم مِّنَ اللَّـهِ مَا لَمْ يَكُونُوا يَحْتَسِبُونَ﴿٤٧﴾

47. Na kama wale waliodhulumu wangelikuwa na vile vyote vilivyomo ardhini na pamoja navyo mfano wake, bila shaka wangelivitoa waokoke kutokana na adhabu mbaya ya Siku ya Qiyaamah. Na yatawafichukia kutoka kwa Allaah ambayo hawakuwa wanatarajia.  

 

 

 

وَبَدَا لَهُمْ سَيِّئَاتُ مَا كَسَبُوا وَحَاقَ بِهِم مَّا كَانُوا بِهِ يَسْتَهْزِئُونَ﴿٤٨﴾

48. Na yatawafichukia maovu ya yale waliyoyachuma, na yatawazunguka yale waliyokuwa wakiyafanyia istihzai. 

 

 

 

فَإِذَا مَسَّ الْإِنسَانَ ضُرٌّ دَعَانَا ثُمَّ إِذَا خَوَّلْنَاهُ نِعْمَةً مِّنَّا قَالَ إِنَّمَا أُوتِيتُهُ عَلَىٰ عِلْمٍ ۚ بَلْ هِيَ فِتْنَةٌ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَهُمْ لَا يَعْلَمُونَ﴿٤٩﴾

49. Na inapomgusa binaadamu dhara, hutuomba, kisha Tunapomtunukia Neema kutoka Kwetu husema: Hakika nimepewa hayo kwa sababu ya ilimu yangu. Bali hayo ni jaribio, lakini wengi wao hawajui.

 

 

 

قَدْ قَالَهَا الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ فَمَا أَغْنَىٰ عَنْهُم مَّا كَانُوا يَكْسِبُونَ﴿٥٠﴾

50. Wamekwishayasema hayo wale wa kabla yao, basi hayakuwafaa yale waliyokuwa wakiyachuma.

 

 

 

فَأَصَابَهُمْ سَيِّئَاتُ مَا كَسَبُوا ۚ وَالَّذِينَ ظَلَمُوا مِنْ هَـٰؤُلَاءِ سَيُصِيبُهُمْ سَيِّئَاتُ مَا كَسَبُوا وَمَا هُم بِمُعْجِزِينَ﴿٥١﴾

51. Yakawasibu maovu ya yale waliyoyachuma. Na wale waliodhulumu katika hawa, yatawasibu maovu ya yale waliyoyachuma, nao si wenye kushinda.

 

 

 

أَوَلَمْ يَعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ يَبْسُطُ الرِّزْقَ لِمَن يَشَاءُ وَيَقْدِرُ ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ﴿٥٢﴾

52. Je, hawajui kwamba Allaah Anamkunjulia riziki Amtakaye na Humkadiria kwa kipimo (Amtakaye). Hakika katika hayo mna ishara kwa watu wanaoamini.

 

 

 

قُلْ يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ أَسْرَفُوا عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ لَا تَقْنَطُوا مِن رَّحْمَةِ اللَّـهِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ جَمِيعًا ۚ إِنَّهُ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ﴿٥٣﴾

53. Sema: Enyi Waja Wangu ambao wamepindukia mipaka juu ya nafsi zao: Msikate tamaa na Rahmah ya Allaah, hakika Allaah Anaghufuria dhambi zote. Hakika Yeye Ndiye Mwenye Kughufuria, Mwenye Kurehemu.

 

 

وَأَنِيبُوا إِلَىٰ رَبِّكُمْ وَأَسْلِمُوا لَهُ مِن قَبْلِ أَن يَأْتِيَكُمُ الْعَذَابُ ثُمَّ لَا تُنصَرُونَ﴿٥٤﴾

54. Na rudini kwa Rabb wenu (kwa tawbah na matendo mema) na jisalimisheni Kwake kabla haijakufikieni adhabu, kisha hamtonusuriwa.

 

 

 

وَاتَّبِعُوا أَحْسَنَ مَا أُنزِلَ إِلَيْكُم مِّن رَّبِّكُم مِّن قَبْلِ أَن يَأْتِيَكُمُ الْعَذَابُ بَغْتَةً وَأَنتُمْ لَا تَشْعُرُونَ﴿٥٥﴾

55. Na fuateni yaliyo mazuri zaidi ambayo mmeteremshiwa kutoka kwa Rabb wenu kabla haijakufikieni adhabu ghafla na hali nyinyi hamhisi.

 

 

 

أَن تَقُولَ نَفْسٌ يَا حَسْرَتَىٰ عَلَىٰ مَا فَرَّطتُ فِي جَنبِ اللَّـهِ وَإِن كُنتُ لَمِنَ السَّاخِرِينَ﴿٥٦﴾

56. Isije nafsi ikasema: Ee majuto yangu kwa yale niliyokusuru katika upande wa Allaah! Na hakika nilikuwa miongoni mwa wenye kufanya masikhara.

 

 

أَوْ تَقُولَ لَوْ أَنَّ اللَّـهَ هَدَانِي لَكُنتُ مِنَ الْمُتَّقِينَ﴿٥٧﴾

57. Au iseme: Lau Allaah Angelinihidi, bila shaka ningelikuwa miongoni mwa wenye taqwa.

 

 

 

أَوْ تَقُولَ حِينَ تَرَى الْعَذَابَ لَوْ أَنَّ لِي كَرَّةً فَأَكُونَ مِنَ الْمُحْسِنِينَ﴿٥٨﴾

58. Au iseme pale itakapoiona adhabu: Lau ningelikuwa na fursa ya kurudi (duniani) basi ningekuwa miongoni mwa wafanyao ihsaan.

 

 

بَلَىٰ قَدْ جَاءَتْكَ آيَاتِي فَكَذَّبْتَ بِهَا وَاسْتَكْبَرْتَ وَكُنتَ مِنَ الْكَافِرِينَ﴿٥٩﴾

59. (Ataambiwa) Lakini ndio! Kwa yakini zilikujia Aayaat Zangu ukazikadhibisha, na ukatakabari na ukawa miongoni mwa makafiri.

 

 

 

وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ تَرَى الَّذِينَ كَذَبُوا عَلَى اللَّـهِ وُجُوهُهُم مُّسْوَدَّةٌ ۚ أَلَيْسَ فِي جَهَنَّمَ مَثْوًى لِّلْمُتَكَبِّرِينَ﴿٦٠﴾

60. Na Siku ya Qiyaamah utawaona wale waliomsingizia uongo Allaah, nyuso zao zimesawajika. Je, kwani si katika Jahannam ndio makazi kwa ajili ya wanaotakabari?

 

 

وَيُنَجِّي اللَّـهُ الَّذِينَ اتَّقَوْا بِمَفَازَتِهِمْ لَا يَمَسُّهُمُ السُّوءُ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ﴿٦١﴾

61. Na Allaah Atawaokoa wale waliokuwa na taqwa kwa sababu ya kufuzu kwao, halitowagusa ovu, na wala hawatohuzunika.

 

 

 

اللَّـهُ خَالِقُ كُلِّ شَيْءٍ ۖ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ وَكِيلٌ﴿٦٢﴾

62. Allaah Ni Muumbaji wa kila kitu, Naye juu ya kila kitu Ni Mdhamini.

 

 

 

لَّهُ مَقَالِيدُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۗ وَالَّذِينَ كَفَرُوا بِآيَاتِ اللَّـهِ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْخَاسِرُونَ﴿٦٣﴾

63.  Anazo funguo za mbingu na ardhi. Na wale waliozikanusha Aayaat na Ishara za Allaah hao ndio waliokhasirika.

 

 

 

قُلْ أَفَغَيْرَ اللَّـهِ تَأْمُرُونِّي أَعْبُدُ أَيُّهَا الْجَاهِلُونَ﴿٦٤﴾

64. Sema: Je, mnaniamrisha nimuabudu ghairi ya Allaah enyi majahili?

 

 

 

وَلَقَدْ أُوحِيَ إِلَيْكَ وَإِلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكَ لَئِنْ أَشْرَكْتَ لَيَحْبَطَنَّ عَمَلُكَ وَلَتَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ﴿٦٥﴾

65. Kwa yakini umefunuliwa Wahy na wale walio kabla yako kwamba: Ukifanya shirki bila shaka zitaporomoka ‘amali zako, na kwa hakika utakuwa miongoni mwa waliokhasirika.

 

 

بَلِ اللَّـهَ فَاعْبُدْ وَكُن مِّنَ الشَّاكِرِينَ﴿٦٦﴾

66. Bali Allaah Pekee mwabudu, na kuwa miongoni mwa wenye kushukuru.

 

 

 

وَمَا قَدَرُوا اللَّـهَ حَقَّ قَدْرِهِ وَالْأَرْضُ جَمِيعًا قَبْضَتُهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَالسَّمَاوَاتُ مَطْوِيَّاتٌ بِيَمِينِهِ ۚ سُبْحَانَهُ وَتَعَالَىٰ عَمَّا يُشْرِكُونَ﴿٦٧﴾

67. Na hawakumkadiria Allaah kama inavyostahiki kumkadiria. Na hali ardhi yote Ataikamata Mkononi Mwake Siku ya Qiyaamah, na mbingu zitakunjwa kwa Mkono Wake wa kulia. Subhaanahu wa Ta’aalaa (Utakasifu ni wa Allaah na Ametukuka kwa ‘Uluwa) kutokana na yale yote wanayomshirikisha.

 

 

 

وَنُفِخَ فِي الصُّورِ فَصَعِقَ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَمَن فِي الْأَرْضِ إِلَّا مَن شَاءَ اللَّـهُ ۖ ثُمَّ نُفِخَ فِيهِ أُخْرَىٰ فَإِذَا هُمْ قِيَامٌ يَنظُرُونَ﴿٦٨﴾

68. Na itapulizwa katika baragumu. Watakufa kwa mshtuko walioko mbinguni na ardhini isipokua Amtakaye Allaah. Kisha litapulizwa humo jengine, tahamaki hao wanasimama wakitazama.

 

 

وَأَشْرَقَتِ الْأَرْضُ بِنُورِ رَبِّهَا وَوُضِعَ الْكِتَابُ وَجِيءَ بِالنَّبِيِّينَ وَالشُّهَدَاءِ وَقُضِيَ بَيْنَهُم بِالْحَقِّ وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ﴿٦٩﴾

69. Na ardhi itang’ara kwa Nuru ya Rabb wake, na Kitabu (cha ‘amali) kitawekwa, na wataletwa Manabii na Mashahidi, na patahukumiwa baina yao kwa haki, nao hawatodhulumiwa.

 

 

 

وَوُفِّيَتْ كُلُّ نَفْسٍ مَّا عَمِلَتْ وَهُوَ أَعْلَمُ بِمَا يَفْعَلُونَ﴿٧٠﴾

70. Na kila nafsi italipwa kikamilifu kwa yale iliyoyatenda, Naye Anajua zaidi wanayoyafanya (duniani).

 

 

 

وَسِيقَ الَّذِينَ كَفَرُوا إِلَىٰ جَهَنَّمَ زُمَرًا ۖ حَتَّىٰ إِذَا جَاءُوهَا فُتِحَتْ أَبْوَابُهَا وَقَالَ لَهُمْ خَزَنَتُهَا أَلَمْ يَأْتِكُمْ رُسُلٌ مِّنكُمْ يَتْلُونَ عَلَيْكُمْ آيَاتِ رَبِّكُمْ وَيُنذِرُونَكُمْ لِقَاءَ يَوْمِكُمْ هَـٰذَا ۚ قَالُوا بَلَىٰ وَلَـٰكِنْ حَقَّتْ كَلِمَةُ الْعَذَابِ عَلَى الْكَافِرِينَ﴿٧١﴾

71. Na wataswagwa wale waliokufuru kuelekea Jahannam makundi-makundi, mpaka watakapoifikia, itafunguliwa milango yake, na walinzi wake watawaambia: Je, hawajakufikieni Rusuli miongoni mwenu, wakikusomeeni Aayaat za Rabb wenu, na wakikuonyeni kukutana na Siku yenu hii? Watasema: Ndio (walitufikia)!  Lakini neno la adhabu limethibiti juu ya makafiri.

 

 

قِيلَ ادْخُلُوا أَبْوَابَ جَهَنَّمَ خَالِدِينَ فِيهَا ۖ فَبِئْسَ مَثْوَى الْمُتَكَبِّرِينَ﴿٧٢﴾

72. Itasemwa: Ingieni milango ya Jahannam, mdumu humo. Basi ubaya ulioje makazi ya wanaotakabari!   

 

 

وَسِيقَ الَّذِينَ اتَّقَوْا رَبَّهُمْ إِلَى الْجَنَّةِ زُمَرًا ۖ حَتَّىٰ إِذَا جَاءُوهَا وَفُتِحَتْ أَبْوَابُهَا وَقَالَ لَهُمْ خَزَنَتُهَا سَلَامٌ عَلَيْكُمْ طِبْتُمْ فَادْخُلُوهَا خَالِدِينَ﴿٧٣﴾

73. Na wataongozwa wale waliomcha Rabb wao kuelekea Jannah makundi-makundi, mpaka watakapoifikia na milango yake ishafunguliwa, na walinzi wake watawaambia: Salaamun ‘Alaykum! (Amani iwe juu yenu), furahini na iingieni, mdumu milele.

 

 

 

وَقَالُوا الْحَمْدُ لِلَّـهِ الَّذِي صَدَقَنَا وَعْدَهُ وَأَوْرَثَنَا الْأَرْضَ نَتَبَوَّأُ مِنَ الْجَنَّةِ حَيْثُ نَشَاءُ ۖ فَنِعْمَ أَجْرُ الْعَامِلِينَ﴿٧٤﴾

74. Watasema: AlhamduliLLaahi (Himidi Anastahiki Allaah) Ambaye Ametuhakikishia kweli Ahadi Yake, na Ameturithisha ardhi tunakaa popote katika Jannah tutakapo. Basi uzuri ulioje ujira wa watendao!  

 

 

 

وَتَرَى الْمَلَائِكَةَ حَافِّينَ مِنْ حَوْلِ الْعَرْشِ يُسَبِّحُونَ بِحَمْدِ رَبِّهِمْ ۖ وَقُضِيَ بَيْنَهُم بِالْحَقِّ وَقِيلَ الْحَمْدُ لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ﴿٧٥﴾

75. Na utawaona Malaika wakizunguka pembezoni mwa ‘Arsh, wanasabbih na kumhimidi Rabb wao. Na itahukumiwa baina yao kwa haki, na itasemwa: AlhamduliLLaahi (Himidi Anastahiki Allaah), Rabb wa walimwengu.

 

 

 

 

 

 

Share