Shaykh Fawzaan: Tafsiyr Zipi Za Qur-aan Zenye Kuaminika?

 

Tafsiyr Zipi Za Qur-aan Zenye Kuaminika?

 

Shaykh Swaalih bin Fawzaan Al-Fawzaan (Hafidhwahu Allaah)

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Tafsiyr ziko nyingi, Je Tafsiyr zipi unatunasihi kusoma?

 

 

JIBU:

 

Hakuna shaka kwamba Tafsiyr ziko nyingi Himdi zote ni za Allaah, na hii ni miongoni mwa neema za Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Na Tafsiyr zimetofautiana; miongoni mwake kuna ambazo zina sharh kwa upana zaidi na kuna zingine ambazo ni mukhtasari. Pia kuna ambazo hazina makosa, na kuna ambazo kuna makosa ndani yake khasa kuhusiana na mas-alah ya ‘Aqiydah.

 

Ninaloshauri kwa ndugu zangu miongoni mwa vijana, ni Tafsiyr ya Ibn Kathiyr kwa sababu ni Tafsiyr tukufu kabisa na ambayo inatumia njia bora kabisa na manhaj (ya kufasiri Qur-aan) japokuwa imefupishwa. Hiyo kwa sababu inafasiri kwanza Qur-aan kwa Qur-aan, kisha kwa Sunnah ya Nabiy, kisha kauli za Salaf, kwa muktadha wa lugha ya Kiarabu, lugha ambayo imeteremshiwa kwayo Wahyi. Kwa hiyo ni Tafsiyr iliyowafikiwa, inayokubalika na yenye uhakika.  

 

Vile vile kuna Tafsiyr ya Al-Baghawiy na Tafsiyr ya Al-Haafidwh Ibn Jariyr Atw-Twabariy ambazo zimefahamisha kwa upana na ni Tafsiyr zilizokamilka.  Vitabu hivi vya tafsiyr ndivyo vya kuaminika.

 

Vile vile kuna Tafsiyr ya Shaykh ‘Abdur-Rahmaan As-Sa’dy, ambayo ni Tafsiyr ‘adhimu, na yenye maelezo mepesi na ambayo imejaa ‘ilmu kubwa.

 

 Ama vitabu vinginevyo vya Tafsiyr, vyaweza kuwa vizuri kwa upande mmoja, lakini vina makossa khasa kuhusiana na mas-alah ya ‘Aqiydah. Wala haipasi yeyote kusoma aina hizi za tafsiyr isipokuwa mtu ambaye ana ustadi wa ‘ilmu kiasi kwamba anaweza kuchukua mazuri yake na akaacha makosa yake. Lakini ambaye ndio kwanza anaanza kusoma, hatoweza kufanya hivyo kwa hiyo lazima asome kutoka Tafsiyr ambazo hazina khatari wala makosa kama vile Tafsiyr ya Ibn Kathiyr, Tafsiyr ya Al-Baghaawiy, na Tafsiyr ya Al-Haafidhw Ibn Jariyr. Vitabu vyote hivi ni vya thamani na vizuri kabisa. Himdi zote ni za Allaah.

 

[Mawqi' Ar-Rasmiy li Ma'aaliy Shaykh Ad-Duktuwr Fawzaan]

 

 

Share