Skip navigation.
Home kabah

Historia Ya Hajarul-Aswad (Jiwe Jeusi)


 

 

SWALI

Asalamu aleikum namshukuru Allah kwa kuweza kutufikisha hatua hii ambayo tunaweza kuwasiliana na waislam wa nchi mbali mbali kuuliza masuala na kujibiwa ujira wenu upo kwa Allah Ishaallah  Suala langu nasikia kuna jiwe jeusi huko Maka limewekwa wapi na linahistoria gani unaweza kunielezea tafadhali Ahsante

 



JIBU:

BismiLLaah wa AlhamduliLLaah was-Swalaatu wa Salaamu ‘alaa Muhammad wa ‘alaa  aalihi wa Aswhaabihil Kiraam, wa ba’ad:

Kuna riwaya nyingi zilizotaja kuhusu Hajarul-Aswad (Jiwe jeusi) na asili yake, lakini nyingi kati ya hizo zina mashaka ya usahihi wake. Na katika Uislam hatutakiwi kutegemea marejeo ambayo hayajapatikana usahihi wake mia kwa mia. Kwa hiyo iliyo sahihi zaidi ni kuwa asili yake limewekwa na Nabii Ibraahiym ('alayhis-salaam) baada ya kumaliza kujenga Ka'abah na kutokana na amri ya Allaah سبحانه وتعالى . Na sababu yake ni kuwa ni alama ya kuanzia kufanya twawaaf katika Ka'abah. Kwa hiyo Muislamu hatakiwi kuambatanisha Utukufu wa Allaah سبحانه وتعالى  na jiwe hilo kama alivyosema 'Umar ibnul-Khatwaab رضي الله عنه alipolibusu

   "إني أعلم أنك حجر لا تضر ولا تنفع ‏ ‏ولولا أني رأيت النبي ‏ ‏صلى الله عليه وسلم ‏ ‏يقبلك ما قبلتك"   البخاري

"Wewe ni jiwe tu ambalo halinufaishi wala kumdhuru mtu, na ingelikuwa sikumona Mtume صلى الله عليه وآله وسلم anakubusu basi nisingelikubusu". [Al-Bukhaariy]

Inavyompasa Muislamu anapojaaliwa kwenda 'Umrah au Hajj anapofanya twawaaf ni kulibusu akiweza, yaani ikiwa hakuna zahma ya watu katika Ka'abah, au kuligusa. Na ikiwa ni zahma kubwa ya watu basi haimpasi Muislamu kusukuma watu kulifikia kwa kujilazimisha hadi alibusu kwani si lazima, bali inatosha kunyanyua mkono wake wa kulia kwa mbali na kusema 'Allaahu Akbar'. Na hii pia ni kufuata Sunnah ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  kama ilivyo dalili katika Hadiyth ifuatayo:

Imetoka kwa Ibn 'Abbaas رضي الله عنه kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alifanya twawaaf akiwa amepanda ngamia wake, na kila mara alipofika kwenye pembe (iliyowekwa jiwe) aliashiria na kusema 'Allaahu Akbar'. [Al-Bukhaariy]

 

Lakini baadhi ya Maulamaa wameona usimulizi wa Hadiyth nyingine kuhusu Hajarul-Aswad kuwa ni sahiyh na ambazo zimetaja umuhimu wa Hajarul-Aswad nazo ni zifuatazo:

Hadiyth ya kwanza:

(( الحجر الأسود من الجنة))  صحيح النسائي   

  ((Hajarul-Aswad ni  kutoka Peponi)) [Sahiyh An-Nasaaiy]

Hadiyth ya pili:

عن ‏ ‏ابن عباس ‏ ‏قال: ‏قال رسول الله ‏ ‏صلى الله عليه وسلم ‏ ((‏نزل الحجر الأسود من الجنة وهو أشد بياضا من اللبن فسودته خطايا بني ‏ ‏آدم)) الترمذي

Kutoka kwa Ibn 'Abbaas رضي الله عنه kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema ((Lilipoteremshwa Hajarul-Aswad kutoka Peponi lilikuwa jeupe kama maziwa, lakini dhambi za Binaadamu zimelifanya kuwa jeusi)) [At-Tirmidhiy]

Hadiyth ya tatu:

 

عن ابن عباس رضي الله عنهما قال : قال رسول الله صلى الله عليه وسلم في الحجر((والله ليبعثنه الله يوم القيامة له عينان يبصر بهما ولسان ينطق به يشهد على من استلمه بحق ))  وروى الترمذي وقال : حديث حسن وابن خزيمة وابن حبان في صحيحيهما

 Kutoka kwa Ibn 'Abbaas رضي الله عنه kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema ((Naapa kwa Allah, Allah Atalileta (Hajarul-Aswad) siku ya Qiyaamah na litakuwa na macho mawili ambayo yataona, na ulimi ambao utazungumza na litashuhudia wale walioligusa kwa ikhlaas)) [At-Tirmidhiy na kasema ni Hadiyth Hasan na Ibn Khuzayma, Ibn Hibbaan katika vitabu vyao]

 Jiwe hilo liko katika pembe moja upande wa  Mashariki/Kusini mwa Ka'abah. Urefu wake kutoka ardhi na takriban mita moja na nusu. Jiwe hilo limefunikwa na chuma cha fedha safi kabisa. Tunaloliona ni karibu na nusu ya jiwe tu, na zaidi ya nusu nyingine imefunikwa ndani hatuioni. Kuna maelezo marefu ya aina mbalimbali kuhusiana na jiwe hilo, lakini haya bila shaka yanatosheleza majibu ya muulizaji.

Na Allah Anajua zaidi