Nywele Za Bandia Nini Hukmu Yake?

 

Nini Hukumu Ya Nywele Za Bandia?

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Asalaam aleykum,

Naomba kufahamishwa zaidi juu ya nywele za bandia.Siku hizi zipo nyuzi za sweta ambazo hutumika kusukia nywele, hizi si nywele wala si nywele za bandia lakini hufanya nywele zikaonekana ndefu je vipi hukumu yake?

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Kubandika nywele za bandia ni katika maovu aliyotuhadharisha Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)    Humlaani mwanamke anayefanya hivyo kama ilivyo katika Hadiyth ifuatayo:

 

Mwanamke wa Ki-Answaari aliyemuozesha binti yake ambaye nywele zake zilianza kung'ooka.  Mwanamke huyo wa Ki-Answaari alikuja kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  na kumtajia kwamba "Mumewe (mume wa mwanangu) ameona kwamba nimwachie avae nywele za bandia."  Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Usifanye hivyo kwani Allaah  Huteremsha laana Yake kwa wanawake kama hao wanaoongeza nywele za bandia))   [Al-Bukhaariy (7:133)  Hadiyth ya Aaishah Radhwiya Allaahu ’anhaa]  

 

 

Makatazo katika Hadiyth hiyo yamekuja kwa ujumla kuharamishwa kuvaa  nywele  za bandia au kuunga nywele    kwa hiyo hata kama zinazotumika sio nywele hasa bali ni nyuzi au chochote kingine, hukumu inabakia ni hiyo hiyo nayo ni kuharamishwa kufanya hivyo na adhabu yake ni kupata laana kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), na laana maana yake ni kuwa mbali na rahmah za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).

 

Bila ya shaka hakuna atakaye kupata laana ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa hiyo dada zetu wajaribu kujiepusha na maovu kama haya  na waridhike na maumbile Aliyowajaalia Rabb wao.

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

 

 

Share