Kutia Mafuta Kulainisha Nywele Au Kupaka Dawa Inafaa?

SWALI:

 

ASSALAMU ALAYKUM. JE KUTIA DAWA NYWELE AU KUTUMIA MAFUTA YA KULAINISHA NYWELE KWA MWANAMKE NI HALALI? NAOMBA UFAFANUZI WA KINA NA KWA MISINGI IPI INAWEZA KUKUBALIKA? Ningelipenda kupata majibu kupitia hii hii alhidaaya.

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani kwa swali lako kuhusu kutia mafuta ili kulainisha nywele au kupaka dawa.

Allaah Aliyetukuka Amemuumba mwanaadamu na Akamuweka katika maumbile yake ya uanaadamu ya kukubaliwa kujirembesha na kujiweka katika hali njema. Ni kwa ajili ya hiyo ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipomuona yule mtu akiwa katika hali ambayo nywele zake hazikuwa zimewekwa vyema alimtaka azikirimu kwa kuzichana, kupaka mafuta na mengineyo.

 

Ama tukianza na mafuta, hujataja mafuta gani unayokusudia, kwani mafuta ya kawaida ni halali kabisa kutia kwenye nywele ikiwa mafuta yenyewe hayakutoka kwa mnyama ambaye ni haramu. Hata hivyo, unapouliza uhalali au uharamu inakuwa ni kwamba una tashwishi ya hilo mbali na kuwa suala hilo halina utata kabisa.

 

Ama kutumia dawa ili kulainisha nywele, ni kuwa madawa mengi hutumiwa kemikali katika kutengeneza dawa hizo. Kemikali mara nyingi zinakuwa na madhara kuliko yale manufaa madogo ya kulainisha hizo nywele. Na kitu chochote ambacho kina madhara, Uislamu umetaka tukiache kwani Allaah Aliyetukuka Anasema:

Wala msijitie kwa mikono yenu katika maangamivu” (al-Baqarah 2: 195).

 

Hivyo, ikiwa pia mafuta ya nywele yatakuwa ni yenye kutiwa kemikali (mkorogo) ili nywele hizo zipate kulainika utumiaji wa mafuta hayo utakuwa na mushkeli. Hivyo, ni vyema na bora kuwa mtu atumie mafuta na zile dawa ambazo zimetengenezwa na miti bila ya kutiwa hizo kemikali.

 

 

Tafadhali bonyeza viungo vifuatavyo upate manufaa zaidi:

 

 

Kuweka Madawa Ya Nywele Na Kuvaa Nywele Za Bandia

 

Mwanamke Kupaka Dawa Ya Nywele

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share