Mtoto Analia Sana Je, Kuna Uovu Wowote Uliomfika?

SWALI 

ASALAMA ALAYKUM WARAHAMATULLAHI WABARAKATU.

SWALI LANGU NI KUWA KUNASABABU GANI INAYOMSABABISHA MTOTO MDOGO WA MWAKA MMOJA KULIA SANA USIKU JE KUNA KITU KIBAYA ATAKUA AMEONA AU NDOTO.NA NI DUA IPI NNAWEZA KUSOMA YA KINGA  

 

 


 

 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Jambo la kwanza tunapenda kukunasihi ni kuwa umpeleke mtoto kwa tabibu wa masikio kwani huenda ikawa ana maumivu sikioni yanayomsababisha kulia sana, na hii imeshatokea kwa watoto fulani wakilia sana nyakati za usiku na wazazi hawakuweza kutambua tatizo hadi kumpeleka kwa tabibu na kujulikana kuwa ni maumivu ya masikio.  

Jambo la pili, inapasa uzingatie na ufuate yafuatayo:

1.     Hakikisha kwamba katika nyumba na haswa chumba chake anacholala hakuna picha za watu, au wanyama au vinyago, au picha za aina yoyote za viumbe kwani Malaika huwa hawaingii katika nyumba iliyotundikwa picha. Amesema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth ndefu inayoelezea:

((...إن البيت الذي فيه الصور لا تدخله الملائكة ))

      ((Hakika Malaika hawaingii nyumba ambayo ina picha)).

       [Al-Bukhaariy, Muslim na wengineo]

 

2.    Mkinge mtoto kwa kumsomea kila siku du'aa ifuatayo ambayo alikuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akiwasomea wajukuu wake Al-Hasan na Al-Husayn:

 

أُعيـذُكُمـا بِكَلِـماتِ اللهِ التّـامَّة، مِنْ كُلِّ شَيْـطانٍ وَهـامَّة، وَمِنْ كُـلِّ  عَـيْنٍ لامَّـة

 

U'iydhukuma Bikalimaati-Llahit-Taammati min kulli shaytwaanin wa haammah, wa min kulli 'aynin laamah.
 

"Nawakinga kwa maneno ya Allaah yaliyotimia Awakinge kutokana na kila shaytwaan na uvamizi na kila jicho lenye kudhuru"

Lakini kwa vile ni mtoto mmoja ikiwa wa kiume utasema:

U'iydhuka na kama ni mtoto wa kike utasema U'iydhuki badala ya U'iydhukuma

 

3.      Msomee Suratul Ikhlaasw (Qul-Huwa Allaahu Ahad) na Al-Mu'awidhataan (Qul-A'uudhu Birabbil-Falaq na Qul A'uudhu Birabbin-naas), Aayatul Kursiy na Aayah mbili za mwisho za Suratul Baqarah kama ilivyoelezewa katika Kitabu cha Hiswn Al-Muslim kama ni kinga ya mtu anapokwenda kulala. Ingia katika kiungo kifuatacho upate maelezo zaidi.

 

Duaa ya wasiwasi usingizini au kusikia uoga na mafazaiko

 

4.     Soma Suratul Baqarah nyumbani kwenu kwani ni kinga pia ya mashaytwaan kama alivyosema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

عن أبي هريرة رضي الله عنه أن رسول الله صلى الله عليه وسلم قال:))لا تجعلوا بيوتكم قبورًا فإن البيت الذي تقرأ فيه سورة البقرة لا يدخله الشيطان)) صحيح الجامع

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema ((Msifanye nyumba zenu makaburi kwani nyumba inayosomwa Suratul-Baqarah haingii Shaytwaan)) [Sahiyh Al-Jaami'i]

 

5.     Msome nyiradi za asubuhi na jioni za kuingia katika nyumba na kutoka zinazipatikana katika kitabu cha Hiswnul Muslim zote zidumishwe ili kuhifadhi nyumba na viumbe viovu.

6.       Mjitahidi sana  kusoma Qur-aan nyumbani kwenu, msifungulie muziki katika Radio, Televisheni na aina yoyote ya muziki, kwani hayo ndiyo yanayowavutia mashaytwaan katika nyumba.     

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amuepushe mtoto huyo na kila ovu na amrudishe katika hali yake ya utulivu. Aamiyn. 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share