067-Aayah Na Mafunzo: Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Ametimiza Risalah

Aayah Na Mafunzo

Al-Maaidah

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Ametimiza Risalah

 

 

 

يَا أَيُّهَا الرَّسُولُ بَلِّغْ مَا أُنزِلَ إِلَيْكَ مِن رَّبِّكَ ۖ وَإِن لَّمْ تَفْعَلْ فَمَا بَلَّغْتَ رِسَالَتَهُ ۚ وَاللَّـهُ يَعْصِمُكَ مِنَ النَّاسِ ۗ إِنَّ اللَّـهَ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الْكَافِرِينَ ﴿٦٧﴾

67. Ee Rasuli! Balighisha yale yaliyoteremshwa kwako kutoka kwa Rabb wako. Na usipofanya, basi utakuwa hukubalighisha ujumbe Wake. Na Allaah Atakuhifadhi dhidi ya watu. Hakika Allaah Haongoi watu makafiri.

 

Mafunzo:

 

Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) ametimiza Risala: Hakika Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) aliifikisha na kuitangaza Dini ya Allaah (سبحانه وتعالى) na akaieneza da’wah yake mpaka ikawafikia majini na watu.  Na akawafundisha yote aliyoyaweka Allaah (سبحانه وتعالى) kuwa ni shariy’ah. Akausimamia uwajibu huu kwa nguvu zote, na Allaah (سبحانه وتعالى) Hakumfisha mpaka Alipoinyoosha kupitia yeye dini iliyopindishwa na Akayafungua kupitia yeye macho yenye upofu na kuzifungua nyoyo zilizokuwa zimefunikwa na ujinga.

 

 

Sababun-Nuzuwl: Kuhusu kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى): “Na Allaah Atakuhifadhi dhidi ya watu.” Imeteremka pale Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) aliposhuka chini ya kivuli cha mti na akalitundika panga lake juu ya huo mti kisha akasinzia. Bedui mmoja akamjia akiwa katika hali ya usingizi, akalikamata panga la Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kisha akamuamsha, akamwambia huku amelishika panga lake juu: Nani ana uwezo wa kunizuia nisikuue? Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akamjibu yule bedui: “Allaah Ndiye mwenye uwezo wa kukuzuia.” Hapo ikateremka kauli hii ya Allaah (سبحانه وتعالى): “Na Allaah Atakuhifadhi dhidi ya watu.” (5: 67)  [Amehadithia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) - Ameipokea Ibn Hibbaan].

 

 

Share