Maamkizi Ya Ramadhwaan Nini Hukmu Yake

 

Maamkizi Ya Ramadhwaan Nini Hukmu Yake?

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Nini hukumu ya kupeana pongezi kwa kuanza mwezi wa Ramadhwaan kwa kusema “Kullu ‘aam wa antum bikhayr" (kwa maana sawa na "Zirudie Ramadhwaan nyingi za furaha")  (ni maamkizi ya mila za Kiarabu za kupeana pongezi katika siku kama za 'Iyd na kadhalika)

 

 

JIBU:

 

Hakuna maneno maalum ya maamkizi ya Kiislamu yaliyopokelewa kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wala Maswahaba zake kwa ajili ya mwezi wa Ramadhwaan.

 

Hata hivyo wanasema ‘Ulamaa kuwa hakuna makatazo kupeana pongezi kwa maneno yanayotumika katika mila za Waislamu kama kusema 'Taqabballa Allaahu minnaa wa minkum' au 'Ramadhwaan Mubaarak' au 'Kullu ‘aam wa antum bikhayr' na maneno mengine ambayo hayana maana zilizokatazwa katika Uislamu.

 

Lakini baadhi ya ‘Ulamaa hawapendelei kuleta maamkizi kabla ya Ramadhwaan, mfano Imaam Ahmad bin Hanbal yeye hapendi kuanza kutoa maamkizi hayo lakini akiamkiwa kwa maamkizi hayo ya Ramadhwaan huitika kwani kuitika kumesisitizwa.

 

Imaam Ibn 'Uthaymiyn (Rahimahu-Allaah) anasema kuwa haipendezi na si sawa kutumia maamkizi yaliyozoeleka sana ya 'Ramadhwaan Kariym' kwani Ramadhwaan si inayoifanya mwezi huu kuwa ndio Kariym, bali hilo hufanywa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Hivyo anasema, ni bora kusema 'Ramadhwaan Mubaarak'.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share