Kufungua Hoteli (Mgahawa) Ramadhwaan Inajuzu?

SWALI:

Assalaam alaikum,

Swali langu linakuja kwenye uhalali wa kutoa huduma za kuuza chakula mchana wa mwezi Mtukufu wa ramadhani. Kama inafaa kutoa huduma hii naomba unipatie dalili zake ili nipate mwangaza zaidi juu ya jambo hili, na kama haifai naomba unifahamishe hukmu ya watu hawa wanaotoa huduma ya chakula mchana wa ramadhani kwa sababu za kuhudumia wagonjwa, wasafiri, wanawake walio katika tarehe zao na hata wasiokuwa waislam.

Nitafurahi iwapo nitajibiwa kabla ya mwezi wa ramadhani kwa faida ya walio wengi.

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema anastahiki Allah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum)  na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa wote wenye kuchangia au kuuliza maswali. Kuhusu hili jambo ni kuwa inategemea hali ilivyo na sehemu iliyopo kazi hiyo na hasa wakati wa Ramadhaan. Ni yakini kuwa ikiwa tupo katika Dola ya Kiislamu yenye kuhukumiwa na Shari'ah tukufu, utawala huo hautaruhusu wenye mahoteli ua mikahawa/migahawa kuuza vyakula wakati wa mchana katika mwezi Mtukufu wa Ramadhaan. Sababu ni kuwa kufanya huko kunaweza kuwashawishi Waislamu kuweza kuingia katika hoteli hizo na kula.

 

Mpaka wakati huu wetu wa leo tunaona kuwa miji ambayo Waislamu ni wengi hasa katika mwambao wa pwani wa Afrika Mashariki ikifika Ramadhaan watu hufunga mahoteli na mikahawa yao kwa ajili ya ukarabati au hufungua karibu na magharibi. Hii ni ada au desturi ('Urf) ambayo imechukuliwa kama chimbuko la kishari'ah na Maimaam wakubwa kama Imaam Abu Haniyfah na Maalik. Na desturi kama hii imeshikiliwa na hata wafuasi wengi wa Shaafi'iy katika sehemu hiyo tuliyoitaja hapo juu.

 

Hali nyengine ni kuwa mtu ni mfanyakazi hiyo lakini yupo katika mji au nchi ambao Waislamu ni kidogo kuliko wsaiokuwa Waislamu. Hapa kunaweza kupatikana kama hali mbili. Ya kwanza ni kuwa ikiwa mtu mwenyewe ni muweza basi ni bora afunge hoteli au mkahawa/mgahawa wake mpaka Ramadhaan imalizike. Ikiwa mfanya biashara mwenyewe hajiwezi na hilo ndio tegemeo lake la kuweza kujikimu na kuiweka familia yake katika hali nzuri basi anaweza kufungua hoteli au mkahawa/mgahawa wake jioni wakati wa futari kwa kuuzia Waislamu futari. Na hilo ni bora kwake zaidi.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 
Share