Kisa Cha Msichana Wa Chuo Kikuu Misr Na Hijaab

 

Kisa Cha Msichana Wa Chuo Kikuu Misr Na Hijaab

 

Imefasiriwa Na: Alhidaaya.com

 

 

Alhidaaya.com

 

 

Sifa zote njema anastahiki Allaah peke Yake, Swalaah na salamu zimshukie Rasuli wake ambaye baada yake hakuna Nabiy, familia yake na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) mpaka Siku ya Mwisho.

 

Ama baada ya hayo, njozi yangu kuu ilikuwa ni kuingia katika Chuo Kikuu. Nilikuwa natamani sana wakati ule ambao nitakuwa msichana wa Chuo Kikuu. Nitastarehe kwa kudura hii kubwa kwa ile heshima anayopatiwa msichana wa Chuo. Dini yangu ilikuwa na upungufu mkuu na Swalaah zilikuwa zinanipita pamoja na Ibadah nyinginezo, yote haya yalikuwa ni mambo ya kawaida. Pamoja na haya yote nilikuwa radhi kwa hii kudura ya kutekeleza ile sehemu ndogo ya dini.

 

Nilikuwa nikiwatizama wale walioshika dini kwa mtizamo wa kuwatweza. Nilikuwa nawaona wao ni watu waliobaki nyuma na wasiopenda maendeleo. Na hivyo wao wanasimama msimamo wa kukataa kila kipya cha kisasa.

 

Nilikuwa nafadhilisha rai za wenye kusahilisha ambao nilikuwa nazisikia kutoka kwa Mashaykh kwenye idhaa na runinga. Nikazijaalia kuwa hizo ni dalili kwangu kwa yale niliyokuwa nayo kwa yale makosa na munkar (maovu).

 

Hakika nilikuwa nimechoshwa na kukerwa na makatazo na amri ambazo zilikuwa zinatufunga katika madrasah (shule). Nilikuwa natamani kupata ziada katika uhuru, sehemu ya kuanzia na kuondoshewa vikwazo.

 

Katika Chuo nitavaa ninavyotaka na kufanya ninayotaka. Bila shaka ilikuwa dhiki na kuchoshwa na nasiha za madrasah na sheria zao. Usiweke nguo yako kwenye viganja vya mkono… Usivae aina hii ya nguo… Tahadhari na kuvaa nguo fupi…Ondoa (usitumie) aina yeyote ya vipodozi usoni mwako. Hivyo ni juu ya mwanadamu asubiri mpaka atakapofikia lengo lake, naam (ndio) nitasubiri.

 

Nilikuwa nafikiria sana huku nikingojea siku ambayo nitamaliza kwayo na kujitoa katika vikwazo hivi. Ninataka kuwa msichana ambaye nina rai zangu mwenyewe na fikira hasa na maazimio yangu yaliyo huru.
 

Nilifaulu sekondari na matokeo yangu yalikuwa yananiwezesha kuingia Chuo kikuu. Hatimaye njozi yangu imepatikana niliokuwa naitamani kila wakati. Mwishowe nitakuwa na rai na wala sitalazimizishwa kufuata rai za wengine.

 

Mwaka wa masomo ulianza nami nikaanza kutafuta rafiki msichana ili tubadilishane hisia za nafsi. Awe anaishi kwa hamu ile ile ninayoishi mimi. Rafiki zangu wawe wamefunguka kimawazo na wa kisasa na wawe wanauona ule uhuru ambao ninauona mimi. Nilijuana na baadhi ya marafiki na nikajenga pamoja nao uhusiano usiotikisika na ambao ni imara. Mazungumzo yetu yalikuwa yakizunguka katika mambo ya kipuuzi, hivyo kuashiria upuuzi wetu na mambo ya kijuu juu (bila kuwa na maana yeyote) mitindo ya kisasa na fasheni na nguo za fahari kupita kiasi, vitu vya urembo, vipindi vya televisheni, sinema, vipindi vya kuendelea (musalsalaat), nyimbo za video za kisasa, kusengenya, istihzai na mambo mengi ya aina hii.

 

Baba yangu alikuwa ameshughulika sana katika biashara na kaka zangu wote walikuwa katika njia hiyo hiyo. Sikusikia kutoka kwao kabisa maneno ya nasiha. Nilikuwa naishi katika ulimwengu mwengine kabisa ambao niliukumbatia kwa nafsi yangu na wala sikutaka kujiondoa kwayo. Sikuwa ni mwenye kufanya kitu chochote kimakosa katika kipindi nilipokuwa pamoja na marafiki zangu.

 

Siku moja nilipokuwa ninamgojea dereva kwenye mlango wa Chuo, alinikabili msichana. Inavyoonekana ni kwamba yeye anamili (au mwanajumuiya) wa mfumo uleule ambao mama yangu na nyanya yangu wanamili. Nguo yake ilikuwa imemsitiri sana na hakuna kitu kilichoonekana.

 

Alinisalimia kisha akaninyoshea mkono ambao ulikuwa na glavu. Nilimnyoshea mkono kisha nikauondosha kwa haraka. Nikamwambia: “Kama kwamba unataka kitu?” Akasema: “Kwa hakika ee dada yangu! Nguo yako ndio imenivutia, hivyo kutaka kuuliza modeli yake”.

 

Nikamuambia kwa kujiamini: “Ufaransa, hii ni katika modeli mpya kabisa iliyoingia madukani”. Akasema: “Je, unadhani ya kwamba kwa kuwa nguo hiyo imetengenezwa Ufaransa inafaa kuvaliwa na Waislamu? Naje, inafuata kanuni zilizowekwa na Uislamu?” Nikasema: “Ni kanuni au maagizo gani unayokusudia?” Akasema: “Je, hujui ya kwamba vazi la Kiislamu la kike lina sharti za kisheria, miongoni mwa hizo ni: kufunika mwili mzima, lisiwe lenyewe ni pambo, lisiwe ni lenye kuonyesha maungo, liwe ni pana na wala si lenye kubana, lisifanane na vazi la mwanamume wala vazi la makafiri, na wala lisiwe vazi la kujionyesha. Na nguo yako inakwenda kinyume na mengi katika haya masharti. Nalo limejaa mapambo na kufumwa kwa vito, linabana na kuonyesha pia. Nalo linashabihiana na vazi la kikafiri, kwa kuwa linadhihirisha mikono yako”.

 

Nikasema: “Inatosha, inatosha, haya yanatosha. Nyinyi daima mnachukua rai za wenye kushadidisha (kufanya ugumu) na wapo ‘ulamaa ambao wameruhusu kuvaa nguo mfano wa hizi”. Akasema: “Suala ee dada yangu! Si kufuata kauli ya fulani au fulani, kwani haki haijui watu. Na kwa kila mmoja yanachukuliwa maneno yake na kurudishwa isipokuwa kauli za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Na hakika amesema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ‘Watu aina mbili katika ummah wangu ni watu wa motoni ambao bado sijawaona. Watu ambao wana viboko mfano wa mkia wa ng’ombe huku wakiwapiga nayo watu na wanawake wamevaa lakini wapo uchi wakiwa wamemili katika matamanio. Hawa hawataingia Jannah (Peponi) wala kusikia harufu yake japokuwa harufu yake inasikika masafa kadha na kadha” [Imepokewa na Imam Ahmad na Muslim].

 
Wamesema wanachuoni: “Yeyote atakayevaa mfano wa nguo hizi zako basi anachukuliwa ni katika hii aina ya pili iliyotajwa katika hii Hadiyth”.

 

Na pia amesema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Mwanamke yeyote atakayepaka manukato kisha akatoka kuelekea Msikitini, haikubaliwi Swalaah yake mpaka aoge” [bn Maajah].

 

Na haya manukato yako ni mazuri ambayo yamenivutia kwako. Itakuwaje kwa vijana na wanaume? Ee dada yangu! Hijabu ni utohara, haya, wacha fadhila na vazi la mwanamke ambalo linamlinda na macho ya wezi wenye tamaa ya kuendea yale yasiyohalalishwa kwao. Hijabu ee dada yangu… Hapo nilimkatiza kwa nguvu huku nikisema: “Inatosha inatosha, tumemaliza. Nitafanya utafiti kwa mambo haya baadae”. Kisha nikajitenga kando kidogo, wala sikuathirika sana kwa msimamo huu. Nilikuwa nimemuandalia jumla ya msimamo ambayo nilikuwa nimeitoa katika madrasa yangu kwa walimu wangu (wa kike) na baadhi ya wanafunzi mfano wa huyo msichana.

 

Katika moja ya vikao vyetu katika mgahawa “cafeteria” pamoja na rafiki zangu, tulikuwa tukiendelea na hadithi zetu tofauti. Na vikawa vicheko vyetu ni kwa sauti kubwa na tulikuwa tumeweka karibu yetu tepu (radio) ndogo na tukaweka nyimbo miongoni mwa zile tulizokuwa tukizipenda sana. Na mara hii ilionekana kuwa sauti ya tepu ilikuwa kubwa. Akaja kwetu msichana na kututolea salamu (Assalamu ‘Alaykum) na akataka tupunguze sauti ili apate kuzungumza na sisi.

 

Tukapunguza sauti. Alikuwa msichana mrembo sana na mavazi yake yalionyesha utamu (ustaarabu) wa hali ya juu lakini pamoja na hilo halikuwa na mapambo wala la kuvutia wala la kujionyesha. Hata hivyo lilikuwa zuri sana na pia mpangilio baina ya rangi ulikuwa mzuri. Nilikuwa nangoja mazungumzo ya huyu msichana ambaye alinistaajabisha uzuri wake na vazi lake.

 

Akaanza kwanza kabisa kutulaumu juu ya kusikiliza nyimbo (muziki) na kutunasihi kusikiliza Qur-aan na kaseti za (mawaidha) zenye faida. Nilistaajabu sana kwa mazungumzo ya huyu msichana mrembo wa kisasa kuhusu mambo hayo aliyotuambia. Lakini niliathirika mara hii katika kuhifadhi utulivu na kutafuta maalumati yangu ya dini ya zamani. Nikamwambia: “Sisi tunasikiliza Qur-aan mara nyingine, lakini hili halitukatazi sisi kusikiliza muziki na nyimbo”.

 

Akasema: “Qur-aan na nyimbo haziyumkini kukaa kwenye moyo mmoja .. Bali ikimakinika mojawapo katika moyo, huiondoa ile nyingine mara moja”. Nikasema: “Hii ni rai yako wewe. Na haifai kuilazimisha rai yako kwa wengine. Nasi tunaipenda Qur-aan na nyimbo pia”.

 

Akasema: “Ili nipate kuthibitisha usahihi wa maneno yangu ningependa yeyote miongoni mwenu anieleze: Ni lini mara ya mwisho kutafuta idhaa ya Qur-aan Tukufu ili apate kusikiliza Qur-aan au kusikiliza kanda ya Qur-aan?” Sote tukanyamaza kimya na pamoja na hayo sauti ya kiburi, majivuno, majisifu na ghera ilikuwa ikipanda ndani yetu.

 

Akasema mmoja wetu: “Si juu yako kutufanyia hesabu kwa yale tunayofanya. Nasi hatupo katika kitengo cha Sheria mpaka uje na nasaha hizo”.

 

Akasema: “Na je, haya masomo ya Kiislamu yapo katika vitengo vya sheria pekee na wengine wanaweza kufanya wanayotaka?” Nikasema: “Sivyo hivyo, huyo (msichana) hakukusudia hilo. Analokusudia ni kuwa nyimbo sio haramu kwani hakuna dalili ya kuharamisha”. Akasema: “Bali kuna dalili nyingi, katika hizo ni kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

وَمِنَ النَّاسِ مَن يَشْتَرِي لَهْوَ الْحَدِيثِ لِيُضِلَّ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ بِغَيْرِ عِلْمٍ وَيَتَّخِذَهَا هُزُوًا ۚ أُولَـٰئِكَ لَهُمْ عَذَابٌ مُّهِينٌ ﴿٦﴾

Na miongoni mwa watu, yuko ambaye hununua maneno ya upuuzi ili apoteze (watu) njia ya Allaah bila elimu, na huichukulia mzaha. Hao watapata adhabu ya kudhalilisha. [Luqmaan:  6]

Amesema Ibn Mas’uud (Radhwiya Allaahu ‘anhu): Maneno ya upuuzi ni nyimbo.

 

Na amesema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Zitakuja zama katika ummah wangu ambapo watu watahalalisha zinaa na kuvaa hariri na kutumia khamri (vileo) na ala za muziki” [Al-Bukhaariy]. Na Ma‘azif ni muziki na nyimbo.

 

Walipoona marafiki zangu ya kuwa sisi hatuwezi kupambana naye (kwa hoja) alisema mmoja wao: “Tuache mazungumzo na hawa wakaidi (na wenye akili finyu)”. Kisha nilimuelekea huku nikisema: “Umetukatisha mazungumzo yetu na ninaona kuwa nasaha yako imeisha, hivyo tuache sasa na uende na shughuli zako”.

Akasema: “Samahani sana kwa kuwakatisha mazungumzo yenu, lakini msisahau ya kwamba vitendo hivi vyenu vinakwenda kinyume na nidhamu ya chuo”. Baada ya hapo aliomba ruhusa na kuondoka.

 

Sikupendelea kabisa kukutana tena na huyu msichana mrembo mwenye nidhamu kwa mfano wa njia yake aliyotumia ambayo ni kavu ambayo ilidhihirisha udhaifu wetu mbele ya hoja zake zenye nguvu. Ilikuwa ninapenda kumdhihirishia katika majadiliano na kumthibitishia rai yangu kuwa muziki si haramu. Lakini nitafanya vipi ikiwa yeye ametoa dalili kutoka katika ayaah na hadiyth kuharamishwa kwa muziki? Mkono wa mmoja wa rafiki yangu ulisogea ili kuongeza sauti ya nyimbo kwa kuirudisha kama ilivyokuwa mbeleni. Kicheko kikachukua nafasi mara nyingine tena.

 

Na katika moja wa siku alinikuta tena huyu msichana chuoni. Alikuja na kunisalimia na akawa anataka kuomba msamaha, lakini nikaanza mimi kuomba msamaha kwa yale yaliyotokea na kufanywa na marafiki zangu. Ikadhihiri katika mazungumzo kuwa yeye husoma katika kitengo kile kile ninachosoma mimi. Nikaona ajabu kwa hilo, nami nikasema: “Kwa hakika nilikuwa ninakuhesabu kuwa unasoma katika moja wapo ya vitengo vya sheria”. Akasema: “Na kwa nini iwe hivyo?” Nikasema: “Kwa kuwa utamaduni na elimu yako ya kisheria iko juu. Kwani hilo haliathiri daraja yako ya masomo?”

 

Akasema: “Hilo haliathiri kabisa, kwani mimi ninachunga wakati wangu. Na hakika nimezidi kufuata nidhamu kwa kujua umuhimu wa wakati. Na kwa munasaba mimi najua lugha ya Kiingereza na elimu ya uhasibu ‘Accountancy’. Na masomo haya ndiyo muhimu kabisa katika kitengo chetu. Pia ninawafafanulia baadhi ya wanafunzi (wasichana). Ukihitaji chochote katika hilo (ya kusaidiwa) basi mimi niko tayari kabisa”

 

Hapo nilimuangalia kwa maajabu na nikaifanya nafsi yangu kuwa ndogo, kwa ule uhakika ya kuwa yeye anafundisha wenziwe Kiingereza na uhasibu! Na sisi tunakaa kufanya dhihaka na kusikiliza nyimbo. Je, huu ndio usasa ambao nilikuwa nauota na kuutamani?

 

Nilihisi ya kwamba msichana huyu ananipatia umuhimu kwa njia ya kipekee. Na yeye alikuwa anataka kufanya urafiki na mimi. Lakini vipi nitafanya mahusiano na yeye akiwa daima anazungumza kuhusu halali na haramu?

 

Hili linanifanya mimi kuhisi ya kwamba bado nipo katika shule ya kati (Middle School) au sekondari. Muache huyo kwani ni miongoni mwa wale wanaoshadidisha (kukaza na kufanya mambo magumu katika dini) na wala hawajui ya kwamba zama zimebadilika na hapana budi kwa mwanadamu kuishi na wakati ambao yeye yupo. Inatosha kubaki nyuma kwa muziki ulio mkuu na ukamilifu .. usasa.. utamaduni.. maendeleo. Haya yote si ule udhahiri wa kisasa ambao tunaishi ndani yake isipokuwa ni mavazi ya suruali zilizobana na sketi za kike na viatu vya kiume na nyuso zinazofanana na wanasarakasi kwa kurembwa!

 

Ama yeye (msichana aliyeshika dini) anasoma Kiingereza na Elimu ya uhasibu. Hakika yeye amenizidi katika utamaduni na hivyo hivyo ameshika vilivyo masomo ya dini yake. Yeye amechanganya baina ya mazuri mawili. Ni nini haya ninayosema? Je, nimeathirika na huyu msichana kwa kiwango hichi? Je, rai yangu huru ipo wapi? Na pia yangu ya kipekee.. na uhuru wangu ambao nilikuwa nikiutafuta daima? Sivyo, sivyo.. hapana budi kumalizana na huyu msichana ili asiyamalize maisha yangu ya uhuru na starehe.

 

Niliahidi ya kwamba baada ya hapo nisimuone tena wala asinione. Na nilipokuwa ninamuona kutoka mbali nilikuwa ninageuza njia nyingine ili asinione. Na mahusiano yangu na marafiki zangu yakabaki vilevile. Isipokuwa sura ya huyo msichana, utamaduni wake binafsi na utamduni wake wa hali ya juu wa sampuli tofauti na usasa wake ulio wazi kabisa, ulikuwa bado ukinipitia katika akili yangu baina ya kila muda fulani.

 

Ilifika wakati wa uhakika. Nami nilikuwa mgonjwa, maradhi yaliyokuwa magumu na kwa sababu hiyo nikalalishwa hospitali na nikabaki kwa muda mrefu. Nilikuwa na hamu kuonana na rafiki zangu ili kupata habari za mwisho za chuo na masomo yaliyonipita.

 

Baada ya wiki ndio alikuja mmoja wa wale rafiki zangu na akanipasha habari ya udhuru uliotolewa na wale waliobakia kwa kushindwa kuja kunizuru. Nikamuomba anitolee kopi ya masomo yote yaliyonipita, naye akaniahidi hilo. Nikawa ninangoja hiyo mihadhara ‘lectures’ kwa hamu kubwa bila ya kuwa subira lakini hakuna hata rafiki yangu mmoja aliyefika kunizuru hata baada ya kumuomba yule wa mwanzo anitolee kopi ya mihadhara.

 

Je, kuna faida gani ya urafiki ikiwa hauzai matunda wakati wa shida? Je, rafiki si ni yule akufaaye wakati wa dhiki?  Nikangojea wiki nyingine lakini bila ya kupata chochote.

 

Baada ya siku mbili nilijulishwa ya kwamba kuna msichana amekuja kunitembelea hospitali nami nikadhania ya kwamba ni mmoja wa wale rafiki zangu ambaye amekuja na ile mihadhara niliyomuagizia. Nikamtaka muuguzi ‘nurse’ amuingize.

 

Akaingia yule msichana aliyejadiliana nami katika masuala ya hijabu kwenye geti la chuo kikuu. Nikaona ajabu kwa ziara yake. Huyu alijuaje ya kwamba mimi ni mgonjwa na niko hospitalini? Na pale alipotoa niqabu na kukaa ubavuni mwangu nilifahamu ya kwamba yeye pia ndiye yule yule msichana aliyetupatia nasaha kwenye cafeteria.

 

Naye ni msichana yule yule ambaye anasoma nami kitengo kimoja. Naye ni yule ambaye nilimuonea ajabu kwa urembo wake na utamaduni wake na uchaguzi wake mzuri wa mavazi. Haiba yake pia ilikuwa ni yenye nguvu na kuvutia.

 

Nilikuwa si mwenye kusadiki kuwa huyu msichana wa kisasa amekaa mbele yangu na amevaa haya mavazi yenye kusitiri kabisa. Nikamuuliza: “Wewe ndiye wewe?”  Akasema: “Ndio, kwa hakika niliwauliza marafiki zako kuhusu wewe, nao wakanieleza ya kwamba wewe ni mgonjwa. Nikawataka wanieleze jina la hospitali na namba ya chumba chako ili nije kukuzuru. Kwani katika kuwazuru wagonjwa kuna thawabu (ujira) mkubwa”. Nikamwambia: “Kwa hakika mimi sijui nitakushukuru vipi kwa hisia zako hizi nzuri. Na ninataka kukuomba msamaha kwa yote yaliyotokea kutoka kwangu”. Akasema: “Hayo si juu yako, muhimu wa yote ni utoke hapa salama salimini kwani mitihani ipo mlangoni (karibu)”.

 

Kisha akatoa kutoka katika mkoba wake makaratasi mengi na akaniambia, “Hizi ni nyaraka za mihadhara uliyokosa na utapata mwisho wa kila muhadhara ufupisho wake. Nami nitakuja kukuzuru tena – In shaa Allaah – baada ya wiki na nikuletee mihadhara mipya”.

 

Hapo sikuweza tena kuizuia nafsi yangu kulia, huku nikikumbuka shida yangu naye na vikwazo vyangu kwake kwenye mlango wa chuo na pia katika cafeteria. Na pamoja na hayo anaamiliana nami kwa aina ya ukunjufu wamoyo, urafiki, mahaba na huruma.

 

Nikakumbuka marafiki zangu ambao kwamba walifanya ubakhili kunizuru au hata kunijulia hali kwa simu. Hapo fikira zangu na sura yangu ya uhuru, maendeleo na usasa zilibadilika kabisa.

 

·    Sasa nimefahamu ya kuwa uhuru si kuacha zile desturi (ada) na misingi mitukufu.

·   Hakika sasa nimefahamu ya kuwa usasa si kukataa dini na maadili na kung’ang’ania fikira na tamaduni ambazo zipo mbali sana na dini yetu.

·   Hakika sasa nimefahamu ya kuwa uhuru si katika Kuzuia ukaidi wa nafsi na ni kukosekana unyenyekevu wa matarajio na kujisalimisha kwa wasiwasi.

·  Hakika sasa nimefahamu ya kuwa Uislamu umemdhaminia mwanamke uhuru wake na kumpatia haki zake ambazo humpatia yeye usalama wa maisha yake ya heshima chini ya kivuli cha uongofu wa mfumo wake wa elimu.

 

Nilimwambia: “Nimetambua sasa kuwa nimeshindwa… na nimetia nia ya kwamba kuanzia sasa nitaanza kubadilisha maisha yangu kulingana na shari’ah ya Allaah Aliyetukuka, ili niwe msichana mzuri kama wewe”. Akasema na huku uso wake umebadilika kwa tabasamu yenye mwangaza: “Ee dada yangu! Hakuna katika mahusiano yetu mshindi na mshindwa.

 
Muhimu ni kuwa sisi sote tufike kwenye bara ya usalama na amani na kufuzu kwa hakika na ufanisi wa milele”. Nikasema:

“Ndio, hili ndilo muhimu”.

Share