Kisa Cha "Ni Dada Yangu Nuurah"

 

Imefasiriwa na: Ummu 'Abdul-Wahaab

 

 

Mashavu yake yalikuwa yamenywea na kuchujuka na kuambatana na mifupa. Hayo hayakumsitisha yeye kabisa katika ibada zake, kwani huwezi kumkuta kakaa tu bure bila ya kusoma Qur-aan. Daima hukesha kwa ajili ya sala zake za binafsi katika chumba ambacho baba kamtayarishia. Hurukuu, husujudu, na hunyanyua mikono yake katika sala. Hivyo ndivyo alivyo tangu jua linapochomoza hadi kutua na hurudia tena.  Ilikuwa ni kichokesho kwa wengine.

 

 

Kwa upande wangu sikuvutiwa na kitu ila mitindo katika magazeti na vitabu vya visa. Wakati wote niliifanya nafsi yangu iwe kwenye kuangalia video hadi ikawa safari za kwenda sehemu ya kukodia kanda kuwa ndio biashara yangu. Kama isemwavyo, pindi linapokuwa jambo ni tabia, watu huweza kukutofautisha kutokana na jambo hilo. Nilipuuza majukumu yangu na hufanya uvivu kwenye sala.

 

Siku moja wakati wa usiku, nilizima video baada ya kuangalia kwa masaa matatu mfululizo. Sauti nyororo ya adhana ilipaa hewani katika kimya kile cha usiku. Niliteleza pole pole kwenye blankenti langu.

 

Sauti yake ilisikika toka kwenye chumba chake.

 

“Ndio? Unahitajia chochote Nuurah?”

 

Kama vile mfano sindano yenye ncha kali, alitoboa mipangilio yangu.

 

"Usilale kabla ya kusali sala ya Alfajiri!”

 

“Ahh …Kuna saa nzima kabla ya Alfajiri! Hiyo ilikuwa ni adhana ya mwazo tu!”

 

Kwa mifunyo yake ya kimapenzi, aliniita niwe karibu yake. Daima hivyo ndivyo alivyokuwa, pamoja na kuwa ugonjwa mkali uliotikisa imani yake uliomshika ulimlaza kitandani kwake.

 

“Hannaan unaweza kuja kukaa pembeni yangu.”

 

Sikuweza kukataa wito wake wowote, kwa vile ungeweza kugusa utakatifu na ukunjufu wake.

 

“Ndio, Nuurah?”

 

“Tafadhali kaa hapa.”

 

“ Sawa nnakaa. Una jambo gani?”

 

Alianza kusoma kwa sauti nzuri:

 (( كُلُّ نَفْسٍ ذَآئِقَةُ الْمَوْتِ وَإِنَّمَا تُوَفَّوْنَ أُجُورَكُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ))

 ((Kila nafsi itaonja mauti. Na bila ya shaka mtapewa ujira wenu kamili Siku ya Qiyaama)) [Al-'Imraan:185]

 

Alisita huku akiwaza. Kisha akaniuliza, “Unaamini mauti?”

 

“Bila ya shaka  nayaamini.”

 

“Unaamini kwamba utakuwa na jukumu kwa yale yote unayoyatenda, ikiwa ni madogo au makubwa?”

 

“Ndio naamini, lakini Allah ni Mwenye Kusamehe na ni Mwenye Kurehemu na nna umri mrefu unanisubiri.”

 

“Nyamaza Hannaan …huogopi mauti wewe ambayo huja ghafla?  Muangalie Hind, alikuwa mdogo kuliko wewe, lakini alikufa kwa ajali ya gari. Ndivyo hivyo hivyo yalivyotokea kwa wengine, na wengine. Mauti ni kipofua-umri na umri wako hauwezi kuwa na kipimo mpaka ufe.

 

Kiza cha chumba kilifunika ngozi yangu kwa woga. “Naogopa kiza na wewe sasa unanifanya niogope mauti? Unafikiri nitapataje usingizi sasa! Nilifikiri uliahidi kuwa unakwenda na sisi katika mapumziko ya msimu wa joto.”

 

Mgongano! Sauti yake ilivunjika na moyo wake ukatetemeka. “Huenda nikenda safari ndefu mwaka huu Hannaan, sehemu nyengineyo. Labda! Sisi sote uhai wetu upo mikononi mwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na sisi ni Milki Yake.”

 

Macho yangu yalinilengalenga na machozi yalinititririka kwenye mashavu yangu. Nilifikiria ugonjwa wa dada yangu, kwani madaktari waliwahi kumjulisha baba kwa faragha kuwa hakuna matumaini makubwa kwa Nuurah kuweza kuishi bila ya maradhi. Lakini yeye mwenyewe hakujulishwa hayo. Sasa nani alimjulisha? Au aliwezaje kuwa na hisia za kujua ukweli?

 

“Unawaza nini Hannaan?” Sauti yake ilikuwa kali. “Unafikiri nasema hivi kwa sababu naumwa?  Aah!....Aah! Kwa kweli, huenda nikaishi sana kuliko yule ambaye haumwi. Na wewe Hannaan, unajua utaishi kwa muda gani? Miaka ishirini, labda? Arobaini? Kisha nini?”

 

Kwenye kiza kile aliufikia mkono wangu akaubana kwa utaratibu. “Hakuna tofauti kati yetu; sote tutaondoka katika ulimwengu huu na kwenda kuishi kwenye Pepo au kuangamia mwenye Moto. Sikiliza maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):

((فَمَن زُحْزِحَ عَنِ النَّارِ وَأُدْخِلَ الْجَنَّةَ فَقَدْ فَازَ وَما الْحَيَاةُ الدُّنْيَا إِلاَّ مَتَاعُ الْغُرُورِ))

((Na atakayeepushwa na Moto na akatiwa Peponi basi huyo amefuzu. Na maisha ya dunia si kitu ila ni starehe ya udanganyifu)) [Al-'Imraan:185]

  

Niliondoka kwenye chumba cha dada yangu nikiwa nimepigwa na bumbuwazi, maneno yake yalikuwa yakisikika kwenye masikio yangu: "Allah Atakulinda Hannaan.  Usisahau kusali"

 

Saa mbili asubuhi mlango wangu uligongwa. Kwa kawaida siamki wakati huu. Kilio! Mbabaiko! "Ewe Allah! kitu gani kimetokea?"

 

Hali ya Nuurah ilikuwa mbaya baada ya sala ya Alfajiri, alichukuliwa kwa haraka kupelekwa hospitali.  "Inna liLLlaahi wa innaa Ilayhi raaji'uun" (Hakika sisi sote ni waja wa Allah na kwa hakika marejeo yetu ni Kwake).

 

Hakukuwa tena na safari ya mapumziko ya msimu wa joto.  Ilikwishaandikwa kwamba nitabakia nyumbani.

 

Baada ya muda …..

Ilikuwa saa saba za mchana mama alipopiga simu hospitali. “Ndio. Unaweza kuja sasa kumuona.” Sauti ya baba ilibadilika, mama aliweza kuhisi kuwa kuna jambo ambalo limetokea.  Tuliondoka haraka sana.

 

Iko wapi ile njia ambayo nilizowea kuipita na kudhania kuwa ni fupi? Kwanini imekuwa ndefu sana leo?  Uko wapi ule mlolongo wa magari ambao ulikuwa ukinipa fursa ya kukatisha kulia na kushoto? "Hebu ondokeni upande wetu tunaopita". Mama alikuwa akitikisa kichwa chake na mikono yake huku analia na kumuombea du'aa Nuurah.

 

Tuliwasili kwenye mlango mkuu wa kuingilia hospitali. Tulimkuta mtu mmoja akiwa anahuzunika. Mwengine alikuwa amepatwa na ajali na watatu wao macho yake yametulia tuli hayatikisiki! Huwezi kusema kuwa ni yuhai au amekwisha kufa.

 

Tulizikiuka ngazi kuelekea ghorofa aliyokuwa Nuurah. Alikuwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi.

 

Muuguzi alitukaribia. “Acha nikupelekeni alipo.” Tulipokuwa tunapita kwenye ujia kuelekea kule alipo, Muuguzi alielezea jinsi ya uzuri wa msichana Nuurah. Alimuhakikishia mama kuwa hali ya Nuurah ilikuwa ina afadhali kulinganisha na alivyokuwa asubuhi.

 

"Samahani!"  "Sio zaidi ya mtu mmoja kwa wakati!"  Kilikuwa ni chumba cha wagonjwa mahututi. Kupitia kidirisha kidogo cha mlango na uwazi wa mapazia meupe, niliyafuma macho ya dada yangu. Mama alisimama pembezoni mwake. Baada ya dakika mbili, mama alikuja nje huku akishindwa kukizuia kilio chake.

 

"Unaweza kuingia na kumsalimia lakini kwa sharti ya kuwa hutozungumza nae kwa muda mrefu". Hivyo ndivyo walivyonambia mimi.  "Dakika mbili zinatosha".

 

"Unajisikiaje Nuurah? Ulikuwa hujambo jana usiku dada yangu, kitu gani kimetokea?"

 

Tulishikana mikono, alinibinya mikono yangu lakini si kwa kunidhuru. "Hata hivi sasa, AlhamduliLLah, naendelea vizuri".

 

"AlhamduliLLaah".  Lakini …mikono yako ibaridi sana!

 

Nilikaa pembezoni mwa kitanda chake na kuweka vidole vyangu kwenye vifundo vyake vya miguu. Alivirusha vidole vyangu. "Samahani ... nimekuumiza?"

 

"Hapana! Ila nimekumbuka maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):

 ((وَالْتَفَّتِ السَّاقُ بِالسَّاقِ))

((Na utapoambatishwa muundi kwa muundi)) [Al-Qiyaamah:29] [Mguu mmoja utakunjwa juu ya mwengine (katika sanda)]

 

"…… Hannaan niombee du'aa. Hivi punde tu huenda nikakutana na siku ya kwanza ya maisha ya Akhera. Ni safari ndefu na sikutayarisha vya kutosha sanduku langu kwa amali njema".

 

Machozi yalitoroka kwenye macho yangu kukimbilia kwenye mashavu yangu. Nililia na yeye aliungana na mimi tukalia pamoja. Michirizi ya machozi yalitawanyika kwenye mashavu ya dada yangu ambapo nilimshikilia kwa mikono yangu  yote miwili. Baba aliingiwa na wasiwasi sana kwa jinsi nilivyolia kwa sababu sikuwahi kulia kama vile kabla yake.

 

Nilipokuwa nyumbani, juu kwenye chumba changu, nililiangalia jua likitua kwenye siku ya huzuni. Kimya kilichanganyika katika njia za ndani ya nyumba yetu. Ndugu na jamaa walikuja katika chumba changu. Watu wengi walihudhuria na sauti zilisikika zikichanganyika kutoka sehemu ya chini ya nyumba yetu. Kitu kimoja tu ndicho kilichosikika kwa uwazi wakati ule……..  Nuurah alikwishafariki!

 

Nilishindwa kutofautisha ni nani aliyeingia na nani aliyetoka.  Sikuweza kukumbuka walichokisema.  Ewe Allah, nilikuwa wapi? Nini kiliendelea? Sikuweza hata kulia tena!

 

Baadaye, walinielezea kitu gani kilitokea. Baba alinishika mkono kunipeleka kwenda kumuaga dada yangu kwa mara ya mwisho, nilikibusu kichwa cha Nuurah.

 

Hata hivyo nakumbuka kitu kimoja, kumuona dada yangu alivyolala kwenye kile kitanda, kitanda ambacho ndicho alichofia juu yake. Naikumbuka Aayah aliyoisoma:

 

((وَالْتَفَّتِ السَّاقُ بِالسَّاقِ))

 

((Na utapoambatishwa muundi kwa muundi)) [Al-Qiyaamah:29] [Mguu mmoja utakunjwa juu ya mwengine (katika sanda)]

 

 

Na nilikuwa nnaijuia vizuri ukweli wa Aayah inayofuata:

 

((إِلَى رَبِّكَ يَوْمَئِذٍ الْمَسَاقُ))

 

((Siku hiyo ndiyo kuchungwa kupelekwa kwa Mola wako) [Al-Qiyaamah:30]

 

Nilinyatia usiku ule kuelekea chumba chake cha kusalia. Nikapigwa na bumbuwazi nilipoyatazama makabati na vioo ambayo yalikuwa kimya. Nilimthamini yule ambaye alishirikiana na mimi katika tumbo la mama yangu. Ni dada yangu Nuurah ambaye alikuwa ni pacha wangu!

 

Namkumbuka yule ambaye alikuwa akizibadilisha huzuni zangu. Ni yeye ambaye alikuwa akinifariji wakati wa shida.  Namkumbuka yule ambaye alikuwa akiniombea muongozo na aliyatumia machozi yake mengi katika katika nyusiku nyingi akinielezea kuhusu mauti na kuhesabiwa. Huenda Allah atatuokoa sote.

 

Usiku wa leo ni usiku wake wa mwanzo ambao Nuurah atautumia kwenye kaburi. "Ewe Allah, Mrehemu na Mtilie nuru kaburi lake"

 

Hii ilikuwa ni Qur-aan yake, msala wake, na kanzu ya wardi ambayo aliniambia ataificha mpaka atakapoolewa ili aje amvalie mumewe.

 

Nilimkumbuka dada yangu na nililia siku zote kwa ajili ya kumkosa. Nilimuomba Allah Anirehemu, Anitakabalie du’aa zangu na Anisamehe.  Nilimuomba Allah Ampe Qawluth-thaabit (kauli thabiti kuweza kujibu maswali ya Malaika; Munkar na Nakiyr) katika kaburi lake kama alivyozoea kusema katika du'aa zake.

 

Nilisita kwa wakati ule, nikajiuliza: "Je! Ingelikuwa ni mimi niliyekufa?  Ningelielekea upande gani?"  Woga ulinivaa na machozi yakaanza kunitoka tena.

 

Allahu Akbar, Allahu Akbar …!

 

Sauti nyororo ya adhana ya kwanza ilipaa hewani kutoka msikitini. Uzuri ulioje kusikia sauti ya adhana wakati ule. Nilitulizana kimya nikawa nayakariri maneno ya muadhini. Nilivaa nguo zangu za kusalia nikasali sala ya Alfajiri. Nilisali kama kwamba ilikuwa ni sala yangu ya mwisho, sala ya kuaga, kama Nuurah alivyofanya. Alfajiri ilikuwa ni sala yake ya mwisho.

 

Kutoka sasa mpaka mwisho wa maisha yangu, ikiwa nitaamka asubuhi, basi sitojihesabu tena kuwa nitakuwa hai ifikapo jioni, na itapokaingia jioni (vile vile) sitojihesabu kama nitakuwa hai ifikapo asubuhi. Sisi sote tunakwenda safari aliyokwenda Nuurah. Je! Tumejitayarisha vipi na safari hiyo?

((اللَّهُ نُورُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ مَثَلُ نُورِهِ كَمِشْكَاةٍ فِيهَا مِصْبَاحٌ الْمِصْبَاحُ فِي زُجَاجَةٍ الزُّجَاجَةُ كَأَنَّهَا كَوْكَبٌ دُرِّيٌّ يُوقَدُ مِن شَجَرَةٍ مُّبَارَكَةٍ زَيْتُونِةٍ لَّا شَرْقِيَّةٍ وَلَا غَرْبِيَّةٍ يَكَادُ زَيْتُهَا يُضِيءُ وَلَوْ لَمْ تَمْسَسْهُ نَارٌ نُّورٌ عَلَى نُورٍ يَهْدِي اللَّهُ لِنُورِهِ مَن يَشَاء وَيَضْرِبُ اللَّهُ الْأَمْثَالَ لِلنَّاسِ وَاللَّهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ))

 

((Allah ni Nuru ya Mbingu na Ardhi. Mfano wa Nuru Yake ni kama shubaka lenye kuwekwa ndani yake taa. Taa ile imo katika tungi. Tungi lile ni kama nyota inayomeremeta, inayo washwa kwa mafuta yanayotoka katika mti uliobarikiwa, mzaituni. Si wa Mashariki wala Magharibi. Yanakaribia mafuta yake kung'aa wenyewe ingawa moto haujayagusa - Nuru juu ya Nuru. Allah  Humuongoa kwenye Nuru Yake Amtakaye. Na Allah Huwapigia watu mifano. Na Allah ni Mwenye kujua kila kitu)) [An-Nuur:35]

 

AL HIDAAYA intaoa mafunzo yanayopatikana katika kisa hiki:

 

1-      Kuacha mambo ya upuuzi na kujitayarisha na safari ndefu ya Akhera kwa kuwa na taqwa (ucha Mungu) kufanya amali nyingi njema.

2-     Kuthamini mapenzi ya undugu wakati tuko hai kabla ya mauti ya mmoja wetu.

3-      Kupokea nasiha za dini tunapopewa na sio kuzipuuza.

4-      Kujifunza maana na tafsiyr ya Qur-aan ili kujua mafunzo yaliyokuwemo humo na kuweza kuyatumia katika kupeana nasiha iwe kama ukumbusho na mazingatio ya maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala),   kwani huenda Aayah moja tu ikamzindua mtu akatanabahi na kutafakari akatambua haki.

5-       Kuombeana du'aa.

6-      Nafsi haijui lini itarudi kwa Mola wake. Hatujui wapi tutafia. Mauti hayana mdogo wala mkubwa, wala hayana ugonjwa au uzima kama alivyosema mshairi:

 

تزود من التقوى فإنك لا تدري                   

Zidisha taqwa kwani hujui

إذا جن عليك ليل هل تعيش إلى الفجر

usiku utakapokufunika, je, utaishi hadi Alfajiri?

فكم من صحيح مات بغير علة                

Kwani wangapi waliokuwa na siha zao wamekufa bila ya maradhi

  وكم من سقيم عاش حينا من الدهري

Na wangapi walio wagonjwa wameishi miaka?  

وكم من صغار يرتجى طولة عمرهم               

Na Wangapi miongoni mwa wadogo wana matumaini ya maisha marefu

وقد دخلت أجسادهم ظلمة القبر

Na miili yao imekwishaingia katika kiza cha kaburi

 فكم من فتى يمسي ويصبح ضاحكا       
Na vijana wangapi wameamka huku wanacheka

 

       وقد نسجت أكفانه وهو لايدري

Na hali sanda yake inashonwa (inaandaliwa) naye hajui

 

 

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala Atuongoze sote katika kutambua kuwa mauti hayana budi ila kumfikia kila mmoja wetu, ili tuwe daima katika kujitayarisha kukutana na Mola wetu kwa kutenda mema mengi. Aamiyn.

 

  

 

Share