Vuno Chungu - Kisa Cha Khaalid

 

Vuno Chungu – Kisa Cha Khalid

 

Imetarjumiwa Na:   Ummu 'Abdil-Wahhaab

 

 

Alhidaaya.com

 

 

Nilikuwa ni mwalimu wa somo la Qur’aan katika halaqah (darsa duara) kwenye eneo letu. Ilikuwa wakati baada ya swalaah ya Maghrib, nilipomuona kijana wa kiume ambae ungelimuona ungelisema labda ana umri wa miaka kumi na tano hivi. Alikuwa ameshikilia Qur’aan ndogo ya mfukoni na amekaa peke yake anaisoma – hapana, kumbe alikuwa haisomi bali alikuwa anajaribu kujifanya aonekane kuwa anaisoma.

 

Tena alikuwa akitutupia jicho la chinichini kwa aibu, ana hamu ya kujua nini tunafanya. Ungelimuona ungelijua kwamba anafanya bidii ya kujua nini tunachozungumzia.

 

Kila yanapogongana macho yangu na yake, alikuwa akigeuza kichwa chake na kuendelea na kisomo chake kama kwamba alikuwa hana nia ya kutazama upande huu (wetu).

 

Siku baada ya siku, alikuwa akikaa katika desturi ile ile na kufanya vilevile. Mwishowe siku moja baada ya swalaah ya Isha, niliamua kumkabili.

 

“As Salaamu `Alaykum, jina langu ni Salmaan, ninasomesha darsa duara la Qur’aan msikiti huu.”

 

‘Na mimi naitwa Khalid.’

 

Ajabu, alijibu kwa haraka sana, kama kwamba alikuwa akisubiri kwa muda mrefu kuulizwa.

 

“Unasoma wapi Khalid?”

‘Darasa la nane ….na……ninapenda Qur’aan sana.’

Ajabu sana, kwa nini alizidisha maelezo haya yote ya mwisho?

Kwa kujiamini nikamuuliza, “sikiliza Khalid, unaweza kupata nafasi baada ya swalaah ya Maghrib? Tungependelea ujiunge na sisi katika darasa.”

 

‘Nini eeh? Ni Qur’aan? Ni Halaqah? Sawa … Kwa nini nisije (furaha ilimjaa). Nitahudhuria, In shaa Allah.’

 

Usiku ule sikuweza kufikiria chochote zaidi ya yule kijana jinsi ya utulivu ulivyomzunguka kwenye tabia yake. Usingizi haukuweza kuja.

 

Nilifanya juhudi ya kuitafsiri jawabu ya kile nilichokiona na kukisikia, lakini sikuambulia kitu. Ubeti wa shairi ulinijia katika mawazo yangu: ‘siku zijazo zitafunua vilivyofichikana / na habari zitatokea pale ambapo usingeweza kupaona.’

 

Niligeuka upande wangu wa kulia na nikatelezesha mkono wangu wa kulia chini ya shavu langu. Ee Allaah, nimesalimisha nafsi yangu Kwako na nnaelekeza matendo yangu juu Yako.

 

***Ametakasika Allaah, siku zilikuwa zinakwenda, Khalid sasa alikuwa ni wa kawaida katika  darasa la kujifunza Qur’aan kwenye halaqah, mwenye juhudi na hodari wa kuhifadhi. Alikuwa ni rafiki wa kila mtu na kila mtu alifanya urafiki nae. Huwezi kumkuta bila ya Qur’aan kwenye mkono wake, wala kwenye safu yoyote ya swalaah isipokuwa safu ya mbele. Kulikuwa hakuna jambo baya juu yake isipokuwa mara kwa mara hukosa makini. Kuna baadhi ya wakati macho yake huelekea kuwa ni kwenye fikra nzito. Mara nyingine tulijua kwamba kimwili huwa yupo na sisi, lakini nafsi yake huwa yupo sehemu nyingine kabisa, ana hisia za ulimwengu mwengine.

 

Mara kwa mara ninamzindua, alichokuwa akikifanya ni kujibu kwa kumumunya, na huwa yeye ni wa mwanzo kukiri kuwa anachojibu huwa ni cha kutunga na si kweli.

 

Siku moja usiku baada ya darasa, nilitembea na yeye katika ufukwe. Labda siri yake kubwa alonayo huenda ikapata nafasi muafaka na kuweza kutoa joto na maumivu alonayo.

 

Tuliwasili kwenye ufukwe tukawa tunaangalia mawimbi. Mwezi mpevu ulikuwa ushatoweka.

 

Mandhari ngeni. Kiza cha usiku kilikitambua kiza cha bahari kutokana na muangaza mdogo wa mwezi baina yao.

 

Mwanga huo mdogo wa mwezi, uliovamia viza viwili hivyo, ulijikuta umekaa katika hali ya kutahayari kama nilivyo mimi pembeni ya Khalid.

 

Miale ya ukimya wa mwezi ilitulia kwenye ukimya wa mawimbi ya bahari. Nilisimama nyuma ya kijana yule mkimya. Mandhari ilikuwa kimya.

 

Kisha punde!

 

Yote yale yalikatishwa ghafla na muanguko wa yule kijana (alikaa kitako kwa ghafla), akiuvujisha moyo wake kwa machozi. Niliamua nisiingilie hisia zake anazozitoa, labda ladha ya chumvi iliyomo kwenye machozi yake yangemsaidia kumpumzisha na kusafisha dhiki zake.

 

Baada ya muda mfupi alijisemea, `Nnakupendeni nyote …. Nnaipenda Qur’aan… na wote wanoipenda Qur’aan. Nnawapenda ndugu wenye msimamo, uadilifu na udugu wa kweli.

 

‘Lakini….baba yangu….ni baba yangu.’

“Baba yako? Ana jambo gani baba yako Khalid?”

 

‘Baba yangu kila wakati ananitahadharisha nisiingiliane na nyie. Anaogopa. Anakuchukieni nyote. Kila mara anajaribu kunishawishi ili na mimi nikuchukieni pia. Nafasi yoyote anayoipata, anajaribu kuthibitisha madai yake kwa visa na simulizi.

 

‘Lakini …Nilipokuoneni mkisoma Qur’aan kwenye Halaqah, niliona kitu tofauti kabisa. Niliona nuru katika nyuso zenu, nuru katika nguo zenu, nuru katika maneno yenu, hata mlipokuwa kimya vile vile niliweza kuiona nuru hata baada yake.

 

‘Nilikuwa na shaka na simulizi za baba yangu na ndio sababu nilikaa baada ya swalaah ya Magharibi ili nikutazameni, nilijisingizia kuwa nimo kwenye mzunguko (wa kusoma), nikijaribu kushiriki katika nuru hiyo.

 

Nna ….. Nnakumbuka Ustaadh Salmaan …. Nnakumbuka wakati uliponijia baada ya swalaah ya Ishaa. Niliusubiri wakati ule kwa muda mrefu (utokee). Wakati nilipoanza madarasa, nafsi yangu ilijifunga yenyewe kwenye ulimwengu wa kujitakasa pamoja na nafsi zenu. Ilikuwa ni vigumu kwangu nilipoanza kusoma kwenye halaqah. Sikuweza kulala, usiku na mchana ilinijia Qur’aan. Baba yangu aligundua mabadiliko ya mwenendo wangu. Alibaini kwa njia moja au nyengine kwamba nilikwisha jiunga na masomo ya halaqah na sasa niko pamoja na “magaidi.”

 

‘Ilikuwa usiku wa kiza…..

‘Tunamsubiri baba arudi nyumbani kutoka duka la kahawa, kama ilivyo kawaida yake, ili tuweze kula chakula cha usiku kwa pamoja.

 

‘Aliingia nyumbani akiwa na uso wa ghadhabu na uliogeuka kwa hasira.

 

‘Sote tulikaa pamoja kwenye mkeka wa kulia chakula. Kimya kilituwa kwenye kikao chetu kama kawaida, tulikuwa tunaogopa kusema akiwepo.

 

‘Aliukatisha ukimya kwa mngurumo na sauti ya ghafla. “Nimesikia kwamba umejiunga na mafundamentalisti (akikusudia magaidi).

 

‘Nilipiga wekundu. Ulimi wangu ulifungika na kuanguka. Maneno ndani ya kinywa changu yalinijia kwa pamoja. Lakini, hakusubiri jawabu …

 

‘Alilivuta birika la chai kwa ghafla na kulirusha usoni mwangu kunidhuru.

 

‘Chumba kilizunguka na rangi zote ziliungana pamoja mbele ya macho yangu. Nilishindwa kutofautisha dari na kuta, nikaanguka.

 

‘Mama yangu akanishika.

 

‘Nguo imaji iliyowekwa kwenye paji langu la uso ndio iliyonikumbusha wapi nilipo.

 

Sauti mbaya ilimgeukia mama yangu, “Mwache peke yake, au utakuwa kama yeye.”

 

‘Nilitambaa kutoka kwenye mapaja ya mama yangu na huku nnalia (kwa khofu) nikielekea chumbani kwangu. Alinifuata kwenye ujia wa vyumba huku akinitukana.

 

‘Hakukuwa kuna siku aliyoacha kunipiga kwa aina moja au nyingine ya kipigo. Matusi, mateke, kunirushia chochote kilichokuwa karibu na mkono wake. Mwishowe mwili wangu ulitetemeka kwa khofu, rangi (alama) za kutisha zilijiunda mwili mzima. Nilimchukia.

 

‘Siku moja wakati tukiwa tumekaa kwenye mkeka kwa ajili ya chakula, alisema, “ondoka, usile na sisi.”

 

‘Kabla sijainuka vizuri, alinirukia ghafla na kunipiga teke kwa nyuma, ikasababisha niangukie kwenye vyombo.

 

‘Wakati huo nilipokuwa nimelala chini, ilibidi nijifanye kuwa na mimi ni mkubwa kuliko yeye na nikajibishana nae…..

 

‘Ipo siku nitakurejeshea. Nitakupiga kama unavyonipiga, nitakutukana kama unavyonitukana.

 

‘Nitakua mkubwa na mwenye nguvu. Na wewe utazeeka na utadhoofika.

 

‘Tena … nitakutendea kama ulivyonitendea. Nitakulipa.

 

‘Baada ya hapo, niliondoka nyumbani na nikakimbilia mbali. Nilikimbia, potelea mbali, sikujali tena.

 

‘Nikaipata njia ya kuelekea ufukweni. Ilinisaidia kuniondolea kiasi fulani ya huzuni. Nilishikilia Qur’aan yangu ndogo (ya mfukoni) na nilianza kuisoma mpaka ikafikia hali ya kuwa siwezi tena kuendelea zaidi kwa sababu ya wingi wa kilio changu.’

 

Na hapa, machozi yaliyokuwa hayana hatia yaliendelea kunidondoka, machozi yaliyokuwa yaking’ara kwa mwangaza wa mwezi mfano wake yalikuwa ni kama lulu iliyowekwa kwenye mwangaza wa taa. Sikuweza kusema kitu, mshangao uliukamata ulimi wangu.

 

Je, niwe na hofu juu ya unyama wa baba yangu, ambaye moyo wake haukujua chochote kuhusu rehma?  Au nishangazwe na ustahamilivu wa kijana ambaye Allaah kisha Mtakia ulinzi na Kumtia imani.

 

Au, nishtushwe na yote mawili, ambapo kiungo cha baba na mtoto kimekwisha vunjika, kupelekea uhusiano wake kubadilika ukawa kama wa simba na chui, au mbwa mwitu na mbweha.

 

Nilimshikilia mikono yake yenye ujoto na kumfuta machozi yalokuwa kwenye mashavu yake. Nilimhakikishia, nikamuombea, na nikamshauri kurejesha utii kwa baba yake. Nilimwambia awe mstahamilivu na kwamba hayupo peke yake. Nilimuahidi kuwa nitakutana na baba yake, nitazungumza naye ili arudishe huruma juu yake.

 

*** Tukio lile lilipita kwa muda na kadiri ya siku zilivyokuwa zikipita. Nilijaribu kufikiria njia za kuifungua kesi ya Khalid na baba yake. Vipi ningeliweza kuzungumza nae. Vipi ningelimuendea kwa kumtuliza? Ili niwe muwazi, vipi ikiwa nitaenda na kugonga mlango wake? Mwishowe nilikusanya ushujaa wangu, nikajifanyia mazoezi ya yale niliyoyapanga ili kusuluhisha mgogoro …. Aah, mkutano…. ungelikuwa siku ile ile saa kumi na moja.

 

 

Wakati ulipowadia, niliondoka kuelekea nyumbani kwa kina Khalid huku nikiwa na ushauri wangu na maswali kwa ajili ya baba yake, yakining’inia kwenye mifuko yangu.

 

Nilipiga kengele ya mlango. Vidole vyangu vya mikono vilikuwa vikitetemeka na magoti yangu yalikuwa yanayayuka. Mlango ulifunguliwa. Hapo, kilichosimama kwenye kivuli kilikuwa na midomo iliyokunjika na mishipa ya damu ipigayo kwa hasira.

 

Nilijaribu kuanzia kwa kudhihirisha tabasamu. Huenda ikakunjua mikunjo ya uso wake kabla hata hatujaanza.

 

Alinikamata ukosi kwa ghafla na kunivutia upande wake. Wewe ni yule fundamentalisti ambaye unamsomesha Khalid msikitini, siye wewe?’

 

“sawa … aah … ndie.”

 

‘Ee Allaah Nisaidie, ikiwa nitakuona unatembea na yeye tena basi nitakuvunja miguu yako. Khalid hatokuja tena katika darasa lako.’

 

Tena, akakusanya mate yote kwenye kinywa chake akanitemea kwenye uso wangu. Mlango ukafungwa kwa nguvu nyuma yangu.

 

Polepole nikakunjua karatasi ya kufutia iliyokuwa kwenye mfuko wangu, nikapangusa kile ambacho amenitunukia, na nikateremka ngazi huku nikijiliwaza nafsi yangu. Rasuli wa Allah – swalla Allahu ’alayhi wa aalihi wa sallam – alitaabika sana kuliko hivi. Walimwita muongo, walimtukana, walimpiga mawe akavuja damu mpaka miguuni.  Walimvunja meno yake na kumuekea mzoga kwenye mgongo wake na walimlazimisha aihame nyumba yake.

 

*** Siku baada ya siku. Mwezi baada ya mwezi. Hakukuwa na alama ya Khalid. Baba yake alimkataza kuondoka nyumbani (kwao), hata kwa ajili ya swalaah ya jamaa. Alitukataza hata sisi kuonana au kukutana nae. Tulimuombea dua Khalid … mpaka ikafikia tukamsahau kabisa. Miaka ikapita. Siku moja usiku, baada ya swalaah ya ‘Ishaa’, kivuli kilipita nyuma yangu ndani ya msikiti, mkono uliochukiza ambao niliuzoweya uliwekwa juu ya bega langu.  Ni mkono ule ule ambao ulionishika (na kubana ukosi wangu) miaka mingi iliyopita Ni uso ule ule, na mikunjo ile ile na kinywa kile kile ambacho kilinitunukia (kilinitemea mate) kitu ambacho sikuwa wakutunukiwa.

 

Lakini … kulikuwa na mabadiliko. Uso wa ujinga ulikwisha tawanyika. Mishipa ya damu yenye hasira ilikwisha nyweya, imedodoweka na kutulia. Mwili wake ulionekana umechoka kwa wingi wa maumivu na mzozo, umedhoofika kwa huzuni na majonzi.

 

“Habari yako?” Nilimbusu kipaji chake na kumkaribisha. Tulikwenda kwenye kona ya msikiti. Alishindwa kuvumilia akafikia kwenye paja langu huku analia kwa kwikwi.

 

Ametakasika Allaah, sikufikiria kwamba yule simba siku moja angeliweza kuwa mtoto wa paka.

 

Sema. Kuna nini (baya)? Vipi Khalid?

 

‘Khalid!’ Hili jina lilikuwa kama mithili ya mchimbaji anachimba ndani ya moyo wake, na kuutikisa na kuuvunja kabisa. Kichwa chake kiliinamia chini.

 

‘Khalid siye tena yule kijana ambae ulikuwa ukimjua. Khalid sio tena mkarimu, mpole na kijana mnyenyekevu.

 

‘Baada ya kuacha darasa lako (halaqah ya Qur’an), alifanya urafiki na vijana waovu, tangu alipokuwa mdogo alikuwa akipenda kuingiliana na watu. Na (hao vijana waovu) wakampata pale kwenye wakati vijana wanapofikia umri wa kupenda kuwa mitaani nje ya nyumba zao, katika ule umri wanaotawaliwa na majivuno na mizaha.

 

‘Alianzia kwa kuvuta sigara. Nilimtukana, nilimpiga.  Haikusaidia, mwili wake ulikulia katika mazoea ya kupata vipigo, masikio yake yakawa yamezoea kusikia matusi.

 

‘Alikuwa mkubwa haraka. Alianza kukaa nao (vijana wabaya) hadi usiku wote, hakuwa akirudi nyumbani ila kumepambazuka. Alifukuzwa skuli.

 

‘Baadhi ya usiku alikuwa akiturudia akiwa na mazungumzo yasiyo ya kawaida, uso wake umesawajika, ulimi wake ukibabaika, mikono yake ikitetemeka.

 

‘Ni mwili ule ule uliokuwa wenye nguvu, umetimia, na nyororo, ulitoweka. Nini kilichobakia ni mifupa iliyodhoofika. Uso halisi uliganda (ulimkauka) kwa jinsi alivyobadilika. Ulikuwa umefifia na mchafu. Ni povu chafu lilikosa maelekezo na dhambi zilizoganda juu yake.

 

‘Macho yake ya kawaida na yenye haya yalibadilika. Yalipiga wekundu mithili ya moto kama kwamba kila kitu alichokunywa au kula vilionekana mara moja katika macho yake, kama ni adhabu ya maisha ya hapa kabla ya baadae.

 

‘Uadui na kutokwa na heshima vilichukua nafasi ya ile aibu na woga aliyokuwa nayo, Ulaini na heshima ya moyo wake mdogo uliondoka, na nafasi yake ikatawaliwa na kituo kigumu (moyo) kama jiwe au mgumu zaidi ya jiwe.

 

‘Mara chache sana katika siku hupita bila ya kutokea jambo. Huwa ananitukana, ananisukuma au ananipiga. Hebu fikiri, mtoto wangu mwenyewe. Mimi ni baba yake, na bado ananipiga mimi.’

 

Baada ya kuyatoa yote hayo, macho yake yalikuwa yamerowa na machungu. Lakini, aliongezea kwa haraka, ‘nakuomba Salman, mtembelee Khalid. Mchukue, unazo baraka zangu, mlango uwazi.

 

‘Mpitie baadhi ya wakati. Anakupenda. Muandikishe kwenye darsa duara la kusoma Qur’aan. Anaweza kwenda na wewe kwenye safari za masomo. Sina pingamizi. Kwa kweli, mimi nnapendelea hata kumruhusu kuishi kwenye nyumba yako na kulala huko huko pia.

 

‘Jambo la muhimu ni kwamba, Salmaan … jambo la muhimu ni kwamba Khalid arudi katika mwenendo aliokuwa nao.

 

‘Nnakuomba ee kijana, nitakubusu mikono yako, nitaipa ujoto miguu yako, nnakuomba na nnakuomba …’

Hakuweza kujizuiya, alilia na huku akikwamwa na pumzi, akiyakumbuka majonzi na maumivu. Nilimruhusu amalize kila kitu alichotaka kusema.

 

Baadae nilimjuulisha …

 

“Ijapokuwa yamepita hayo, ngoja na mimi nijaribu. Ndugu, wewe uliipanda mbegu hii. Na hili ndilo vuno lake.” 

 

******* 

Nyongeza Ya Al Hidaaya

 

Kisa hiki kizuri chenye kusikitisha kilichojaa mazingatio makubwa kutoka kwa Al Akh Muhammad Ash-Shariyf, kinatupa mafundisho ya kutohukumu na kuchukia mambo ya kheri, ima kwa ujinga, au kwa kupotoshwa na vyombo vya habari. Hali kama hii ya baba yake Khaalid, ni hali iliyopo kwa ndugu zetu wengi kwenye jamii yetu haswa iliyopo Umagharibini (nchi za Ulaya na Marekani).

 

Tumesikia visa vingapi vya mabint kukemewa kwa kuvaa hijaab eti wanajizeesha, na wanapovaa 'niqaab' ndio kabisa wanaambiwa washakuwa 'siasa kali', mafundamentalisti, na wana mielekeo ya kigaidi!! Na hali ni hivyo hivyo kwa vijana wa kiume, baadhi ya wazazi wao na ndugu zao wakiona kijana keshaanza kuweka ndevu, basi tuhuma mtindo mmoja, kama kisa cha mama mmoja kukamata mkasi na kumkamata kijana wake mtu mzima na kutaka kumkata ndevu kwa nguvu kwa madai anafanana na magaidi!!

 

Leo, kheri kama za Khaalid alizokuwa nazo za kupenda dini yake na kuitafuta bila kusukumwa na wazazi, ni kheri kila mzazi au mlezi mwenye mapenzi na Uislam anazitafuta, kwani ni vijana wangapi leo hii wasiotaka masomo ya dini? Ni vijana wangapi yakija masuala ya skuli anakuwa mwepesi, haihitaji kuamshwa wala kukumbushwa? Lakini yakija masuala ya madrasah utaona hila na mbinu zizukazo za kukwepa na kudharurika!

 

Neema hizo si rahisi kuzipata haswa kila zama zinavyosogea, neema hizo zipupiwe na wazazi kabla hayajaja majuto kama ya babake Khaalid.

 

Tujenge mapenzi na dini yetu, na tuwapende wasimamizi wa dini na kuwaheshimu. Tusidanganywe na vyombo vya habari ambayo hivi sasa ndio mwongozo wa Ulimwengu, ndio fikra za watu, na ndio dini kwa wengi...SubhaanaAllaah! Fitna ya vyombo vya habari ni kubwa mno kwa zama zetu, na kunatosha kutazama habari kwenye ma-televisheni kwa mtu wa kawaida kuichukia dini yake kwa propaganda zinazopikwa kila siku kukicha!

 

Tusije kuwa kama baba yake Khaalid aliyepotosha maana ya halaqah ya Qur'an na kuita ugaidi, na washiriki wake akawaita magaidi kama tunavyoona vyombo vya habari vinavyofasiri Madrassah hivi sasa, na mwisho wake kuanzwa Madrassah kufungiwa na serikali zao katika nchi mbalimbali za Waislam! Tusije kuwa kama Allaah Alivyosema:

 

إِنَّ الَّذِينَ يُلْحِدُونَ فِي آيَاتِنَا لَا يَخْفَوْنَ عَلَيْنَا ۗ أَفَمَن يُلْقَىٰ فِي النَّارِ خَيْرٌ أَم مَّن يَأْتِي آمِنًا يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۚ اعْمَلُوا مَا شِئْتُمْ ۖ إِنَّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ﴿٤٠﴾ إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا بِالذِّكْرِ لَمَّا جَاءَهُمْ ۖ وَإِنَّهُ لَكِتَابٌ عَزِيزٌ﴿٤١﴾ لَّا يَأْتِيهِ الْبَاطِلُ مِن بَيْنِ يَدَيْهِ وَلَا مِنْ خَلْفِهِ ۖ تَنزِيلٌ مِّنْ حَكِيمٍ حَمِيدٍ﴿٤٢﴾

Hakika wale wanaozipotosha Aayaat Zetu hawawezi kujificha kwetu. Je, basi yule atakayetupwa katika moto ni bora au yule atakayekuja akiwa katika amani Siku ya Qiyaamah? Tendeni mpendavyo; hakika Yeye ni Mwenye kuona yote myatendayo. Tendeni mpendavyo; hakika Yeye ni Mwenye kuona yote myatendayo. Hakika wale waliokanusha Ukumbusho ulipowajia (wataangamia). Na hakika hicho ni Kitabu chenye utukufu na udhibiti. Hakitokifikia ubatili mbele yake, na wala nyuma yake; ni uteremsho kutokakwa Mwenye hikmah wa yote, Mwenye kustahiki kuhimidiwa kwa yote. [Fusw-swilat: 40-42]

 

Ee Allaah Tulinde na fitna hizi tuzijuazo na zile tusizozijua. Na Utupe mapenzi ya dini yetu, na Uwape wazazi wetu mapenzi hayo na ujaze mioyo yetu imaan, na wala Usiigeuze wala Kuipoteza. Aamiyn

 

 

Share