Kisa Cha Mtoto Aliyekuwa Akiswali Jamaa'ah Msikitini

Kisa Cha Mtoto Aliyekuwa Akiswali Jamaa Msikitini

 

Alhidaaya.com

 

 

 

BismiLaah wa AlhamduliLLaah was-Swalaatu wa Salaamu ‘alaa Muhammad wa ‘alaa  aalihi wa Aswhaabihil Kiraam, wa ba’ad:

 

Kisa hichi cha tukio la kweli ni kuhusu mtoto mdogo aliyekuwa katika darasa la pili (tunampa jina la ‘Abdullaah) ambaye mama yake alifanya jitihada kubwa kumlea malezi ya dini ainukie katika Ridhaa ya Allaah (Subhaanah wa Ta'aalaa). Alimfundisha umuhimu wa Swalaah tano na khaswa umuhimu wa kuswali Swalaah ya Alfajiri Msikitini.

 

 

Mtoto alikuwa na juhudi ya kwenda Msikitini ingawa baba yake hakuwa akifanya hivyo, bali alikuwa akilala wakati mtoto huyo akienda kuswali Swalaah ya Jamaa Msikitini.

 

Siku moja wakati yuko darasani, mwalimu aliamua kutoa adhabu ya kuwachapa wanafunzi wote darasani kwa sababu fulani. Akaanza kuwachapa wanafunzi mmoja mmoja hadi alipomfikia ‘Abdullaah. Mwalimu akamuambia ‘Abdullaah afungue mikono yake ili amchape kwa rula (mstari wa mita).

 

Mjadala ulikuwa kama ifuatavyo:

 

 

Mwalimu:      

Fungua mikono yako nikuchape.

 

 

‘Abdullaah:                        

Hapana! Huwezi kunipiga mimi.

 

Mwalimu:                           

(Akaanza kuhamaki)Fungua mikono yako ee ‘Abdullaah nikuchape!

 

 

‘Abdullaah:            

Nakuambia huwezi kunipiga mimi!

 

 

Mwalimu:                           

Akapandisha sauti kwa ukali: Husikii nakuambia fungua mikono yako nikuchape?

 

 

‘Abdullaah:                        

Wa-Allaahi huwezi kunichapa mimi! Wa-Allaahi huwezi kunichapa mimi!

 

 

Mwalimu:                           

(Akipigwa mshangao mkubwa) Unasema nini ee ‘Abdullaah? NNitakuchapa mimi popote kama hutaki kufungua mikono yako!

 

 

‘Abdullaah:                        

Nimekuambia mwalimu kuwa huwezi kunichapa mimi, hebu jaribu kunichapa kama unataka.

 

 

Mwalimu:                          

(Hali hii ikamfanya mwalimu apigwe na bumbuwazi asiweze kumchapa na badala yake kutaka kujua kwanza sababu ya kusema hivyo) Kwa nini unasema hivyo ee ‘Abdullaah?

 

 

‘Abdullaah:                       

Je, kwani hukusikia Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliyosema kuwa ((Yeyote atakayeswali Swalaah ya Alfajiri atabakia katika himaya ya Allaah?)) Na mimi nimeswali Swalaah ya Jamaa  Alfajiri Msikitini, kwa hiyo niko katika himaya (kuhifadhiwa) ya Allaah. Na vile vile sikufanya kosa lolote la wewe kuniadhibu.”

 

Mwalimu akasimama akiwa ameshangazwa na maneno ya ‘Abdullaah na huku akaingiwa na unyenyekevu kwa Allaah (Subhaanah wa Ta'aalaa). Akatoka na kwenda kumuelezea mkuu wa shule ili aitwe baba yake ‘Abdullaah ili apewe hongera kwa kumpa mwanawe malezi mema ya kumzoesha kwenda kuswali Swalaah za Jamaa Msikitini.

 

Lakini masikitiko ni kwamba alipokuja baba yake ‘Abdullaah ilikuwa ni mshangao kwa kila mmoja. Kwani walitambua kuwa baba huyo hakuwa ni mtu wa kujali malezi ya mtoto wake. Kila mmoja akamuuliza: "Wewe kweli ni baba yake ‘Abdullaah?" Akajibu: "Ndiyo".

 

Wakamuuliza ‘Abdullaah: "Huyu kweli ni baba yako ee ‘Abdullaah?" Akajibu: 'Ndio lakini yeye haji kuswali Swalaah za Jamaa na mimi Msikitini".

 

Mwalimu akamuelezea baba yake ‘Abdullaah yaliyojiri darasani. Baba yake ‘Abdullaah akaguswa sana na kisa cha mwanawe, na ikawa ni sababu ya yeye kurudi kwa Allaah (Subhaanah wa Ta'aalaa) na tokea siku hiyo akawa ni mwenye kuswali Swalaah zote za Jamaa Msikitini.

 

 

Subhaanah Allaah! Tazama jinsi gani Swalaah inaweza kutuathiri sisi na kutufundisha kuwa tusimkhofu mtu yeyote ila tumkhofu Allaah (Subhaanah wa Ta'aalaa). Hakika Swalaah ni chanzo cha nguvu kwa Muumini, ni mwangaza unaomuongoza mtu katika njia iliyonyooka.  

 

Enyi ndugu Waislamu, msisahau kwamba maneno ya mwisho ya Nabiy wetu (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kabla ya kuaga dunia hii, yalikuwa ni nasaha kwetu tusiache Swalaah kwani ni mawasiliano na Rabb wetu Mtukufu. Swalaah inayo majibu ya Du'aa zetu, Swalaah ina Nuru katika nyuso zetu, Swalaah ni hifadhi yetu kutokana na machafu na maovu, Swalaah ni kisaidizi chetu katika migogoro na ni Nuru katika makaburi yetu.

 

Watu wengi wamo katika khofu, wasiwasi na dhiki, wanakosa raha kwani hawana utulivu wa nyoyo. Na ukiwazingatia watu kama hawa utaona kwamba ni wale wanaoacha Swalaah na ni wenye kushughulika zaidi na dunia. Vipi mtu hataki kumuabudu Rabb wake Ambaye Ndiye Anayemjaalia kuwa na umri na afya ya kuweza kuishi? Bila ya kumuomba Rabb wake Azidi kumpa umri na afya atawezaje mtu kuendeleza maisha yake?

 

Utaona mtu anaweka kengele ya saa Alfajiri kwa ajili ya kuwahi kazini, na sio kwa ajili ya Swalaah, hivyo ameona kuwa kazi kwake ni bora kuliko kumuabudu Rabb wake Ambaye Akitaka Anaweza Amfanyishe asiweze hata kwenda huko kazini kwa kumpa ugonjwa au maafa au mauti. Basi umezingatia hilo ee Muislamu usiyeswali?   

 

Tukumbuke kuwa jambo la kwanza tutakaloulizwa siku ya Qiyaamah ni Swalaah zetu. Ikiwa tumezitimiza zinavyopasa basi mambo mengine yatakuwa salama.    Kwa hiyo na tujitahidi kuzitimiza Swalaah zetu na kuwakumbusha na kuwahimiza watoto wetu, ndugu zetu, jamaa zetu wote katika familia, na ndugu zetu Waislamu umuhimu wa Swalaah.

 

 

 

Share