Wajibu Na Shuruti Za Hajj

    Wajibu Na Shuruti Za Hajj

 

Allah Amewaamrisha waja Wake kuitekeleza ibada ya Hijja kwenye Nyumba Tukufu, na kuwalipa malipo mema kutokana na ibada hiyo. Yeyote mwenye kuitekeleza Hijja kwenye Nyumba hiyo (Ka'abah) na akawa hakumkaribia mkewe kwa matamanio ya nafsi yake, wala hakutenda dhambi yoyote, basi atatoka kwenye ibada hiyo hali ya kuwa hana dhambi yoyote mfano wake ni kama mtoto mchanga ambaye ndio kwanza amezaliwa na mama yake. Hijja iliyokubaliwa (Al-Hajj Al-Mabruur) malipo yake si chochote ila ni Pepo.

Enyi watu! Muogopeni Allah na jitahidini kuutekeleza wajibu wa Hijja, ambao Allah Amekuamrisheni juu yenu. Allah amesema:

((إِنَّ أَوَّلَ بَيْتٍ وُضِعَ لِلنَّاسِ لَلَّذِي بِبَكَّةَ مُبَارَكًا وَهُدًى لِّلْعَالَمِينَ ))

(( فِيهِ آيَاتٌ بَيِّنَاتٌ مَّقَامُ إِبْرَاهِيمَ وَمَن دَخَلَهُ كَانَ آمِنًا وَلِلّهِ عَلَى النَّاسِ حِجُّ الْبَيْتِ مَنِ اسْتَطَاعَ إِلَيْهِ سَبِيلاً وَمَن كَفَرَ فَإِنَّ الله غَنِيٌّ عَنِ الْعَالَمِينَ))

((Hakika Nyumba ya kwanza waliowekewa watu kwa ibada ni ile iliyoko Bakka, iliyobarikiwa na yenye uongofu kwa walimwengu wote))

 

 ((Ndani yake zipo Ishara zilizo wazi - masimamio ya Ibraahiym, na mwenye kuingia humo anakuwa katika amani. Na kwa ajili ya Allah imewajibikia watu wahiji kwenye Nyumba hiyo, kwa yule awezae njia ya kwendea. Na atakayekanusha basi Allah si mhitaji kwa walimwengu)) [Al-'Imraan: 96-97]

  

Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Uislaam ni kushuhudia ya kwamba Hapana Mola anaestahiki kuabudiwa kwa haki ila Allah na Muhammad ni Mjumbe wa Allah, kusimamisha sala, kutoa Zakaah, kufunga mwezi wa Ramadhaan, na kuhiji kwenye Nyumba Tukufu kwa mwenye uwezo)) [Muslim] 

Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema Uislaam umejengeka kutokana na hizi nguzo tano na endapo yoyote miongoni mwa nguzo hizi tano ikikosekana basi, Uislaam hautimii. ‘Umar Ibnul-Khattaab (Radhiya Allahu 'anhu) amesema; "Nilikuwa karibu nitume wajumbe katika miji kuchunguza wale walio na uwezo wa kufanya Hijjah lakini hawafanyi, ili niwaamrishe walipe kodi, hao si Waislamu, hao si Waislamu".

Wajibu wa Hijja umethibitishwa katika Kitabu cha Allah na Sunnah za Mjumbe wa Allah (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na vile vile kwenye makubaliano ya wanavyuoni wa Kiislaam. Mtu yeyote anaepinga wajibu huu, huyo hana dini, na yeyote anaeacha wajibu huu eti kwa sababu ya kutojali, japo kuwa mtu huyo anaamini, huwa yupo kwenye ukingo wa ukafiri.

Baada ya kubainisha (kuainisha) Wajibu wa Hijja, Allah Anasema

(( فِيهِ آيَاتٌ بَيِّنَاتٌ مَّقَامُ إِبْرَاهِيمَ وَمَن دَخَلَهُ كَانَ آمِنًا وَلِلّهِ عَلَى النَّاسِ حِجُّ الْبَيْتِ مَنِ اسْتَطَاعَ إِلَيْهِ سَبِيلاً وَمَن كَفَرَ فَإِنَّ الله غَنِيٌّ عَنِ الْعَالَمِينَ))

((Ndani yake zipo Ishara zilizo wazi - masimamio ya Ibraahiym, na mwenye kuingia humo anakuwa katika amani. Na kwa ajili ya Allah imewajibikia watu wahiji kwenye Nyumba hiyo, kwa yule awezae njia ya kwendea. Na atakaye kanusha basi Allah si mhitaji kwa walimwengu)) [Al-'Imraan: 97]

Huwaje kwa Muislamu akajihisi kasalimika hali ya kuwa kaipuuza Hijja na ilhali ana uwezo wa kuitekeleza kiafya na kifedha, na anafahamu kuwa Hijja ni wajibu, na ni moja miongoni mwa nguzo za Kiislaamu?

Huwaje kwa Muislaamu kujizuia fedha kuzitumia kwa ajili ya Hijja, na hali ya kuwa anazitumia fedha hizo kwa mambo ya anasa za kidunia?

Huwaje kwa Muislaamu akajihifadhi kutokana na uchovu wa Hijja, lakini anajitahidi kwenye mambo (ya kipuuzi) ya kidunia?

Huwaje mtu akawa mvivu katika kuitekeleza Hijja, hali ya kuwa ibada hii imeamrishwa mara moja tu katika uhai wake?

Huwaje mtu akaakhirisha kuitekeza Hijja, na ilhali hajui kuwa uhai wake utafikia angalau siku moja ijayo au la?

Hivyo, Muogopeni Allah enyi waja, na timizeni wajibu wa Hijja ambao umeamrishwa juu yenu, tekelezeni kwa dhati ya kumpenda Yeye, yakubalini maamrisho Yake na fanyeni hima na hamu ya kumtii Yeye, ikiwa nyinyi ni waumini wa kweli.  Allah Anasema:

((وَمَا كَانَ لِمُؤْمِنٍ وَلَا مُؤْمِنَةٍ إِذَا قَضَى اللَّهُ وَرَسُولُهُ أَمْرًا أَن يَكُونَ لَهُمُ الْخِيَرَةُ مِنْ أَمْرِهِمْ وَمَن يَعْصِ اللَّهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا مُّبِينًا))

((Haiwi kwa Muumini mwanamume wala Muumini mwanamke kuwa na khiari katika jambo, Allah na Mtume Wake wanapokata shauri katika jambo lao. Na mwenye kumuasi Allah na Mtume Wake basi hakika amepotea upotofu ulio wazi)) [al-Ahzaab:36]

Ikiwa Muumini ataitekeleza ibada ya Hijja mara moja tu baada ya kufikia balegh, basi itatosheleza na atakuwa ameutimiza msingi muhimu wa Uislaamu. Hatotakiwa tena kutekeleza Hijja wala Umrah baada ya hapo, isipokuwa ikiwa kama aliweka nadhiri ya kutekeleza moja kati yake, basi atawajibika kuitekeleza nadhiri yake kama tulivyofundishwa na Mtume wetu (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth ifuatayo:  

Kutoka kwa mama wa waumini 'Aaishah (Radhiya Allahu 'anhaa kwamba Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Yeyote atakayeweka nadhiri ya kumtii Allah basi amtii. Na yeyote atakayeweka nadhiri kumuasi Allah basi asimuasi)) [Al-Bukhaariy]

 

Share